Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 - Ofisi ya Waziri Mkuu

Hon. Vedastus Mathayo Manyinyi

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Musoma Mjini

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 - Ofisi ya Waziri Mkuu

MHE. VEDASTUS M. MANYINYI: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante kwa kunipa nafasi na mimi niweze kuchangia katika hii hotuba ya bajeti ya Ofisi ya Waziri Mkuu.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza naomba nichukue nafasi hii kumpongeza Mheshimiwa Rais kwa kazi nzuri ambayo ameendelea kuifanya yeye na wasaidizi wake kwa maana ya Makamu wa Rais, Waziri Mkuu pamoja na viongozi wote wa Serikali. Mambo haya kusema kweli yako wazi kwa maana ya maendeleo ambayo yameendelea kufanyika hasa katika kuboresha huduma za jamii.

Mheshimiwa Naibu Spika, labda nizungumzie kwanza ushahidi huo katika Jimbo langu la Musoma, kwamba ni kwa kiasi gani katika kipindi hiki kifupi huduma za jamii zimeendelea kuboreshwa sana. Leo unapozungumza upande wa elimu, nakumbuka Mheshimiwa Rais aliposema kwamba sasa elimu itatolewa bure, kiwango cha uandikishwaji wa watoto kimekuwa kikubwa sana na mpaka kimepelekea darasa la kwanza kwenye shule mbalimbali wanaenda mpaka watoto 800 kwa darasa moja badala ya yale madarasa matatu. Hiyo yote inaonesha ni kwa kiasi gani wanafunzi wengi zaidi wamejiunga katika elimu ya msingi.

Mheshimiwa Naibu Spika, hata unapozungumza habari ya afya, mfano mwaka jana tu achana na miaka mingine tumepata shilingi milioni 400 kwa ajili ya huduma ya afya lakini tumepata zaidi ya shilingi bilioni 3 kwa ajili ya Hospitali yetu ya Rufaa. Kwa hiyo, hayo yote ni matokeo ya uongozi mzuri na kuwajali wananchi ndiyo maana yameendelea kujitokeza.

Mheshimiwa Naibu Spika, hali kadhalika, hata upande wa habari ya maji, kwa Musoma Mjini tulikuwa na tatizo kubwa la maji lakini leo shida kubwa tuliyonayo ni tatizo la mabomba kupasuka shauri ya pressure ya maji. Kwa hiyo, hii yote inaonesha ni kwa kiasi gani Serikali ya Chama cha Mapinduzi imeendelea kushughulikia matatizo ya wananchi. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kama hiyo haitoshi nakumbuka katika hiki cha miaka miwili pale kwangu nimepata shilingi bilioni 12 kwa ajili ya barabara, lakini hata kwa mwaka huu tu nimepata shilingi bilioni 4. Hata ile Kamati ya Bunge iliyokuja Mjini Musoma nadhani iliweza kuona maana ilizitembelea zile barabara iliona ni kwa kiasi gani ule Mji wetu wa Musoma umekuwa mzuri kwa ujenzi wa barabara za kiwango cha lami. Kwa hiyo, ndiyo maana tunasema tuna kila aina ya sababu ya kuishukuru na kuipongeza Serikali kwa kazi kubwa na nzuri ambayo imefanyika.

Mheshimiwa Naibu Spika, kama Mbunge wa Jimbo la Musoma nimeona nizungumzie tu yale ya pale mjini zaidi ya yale makubwa ambayo yanaonekana katika nchi nzima. Mfano leo ukipita wakati wa usiku kwenye maeneo mengi utadhani kama ni mjini kwa sababu karibu kata na miji inazo taa kwa maana kwamba umeme umesambaa.

Mheshimiwa Naibu Spika, leo kwetu sisi kama nchi matumizi yetu ya umeme ni wastani wa MW 1,100 lakini umeme ambao unazalishwa sio chini ya MW 1,600. Kwa hiyo, hii tu inaonyesha ni kwa kiasi gani tumejitahidi lakini Serikali ina jukumu la kuhakikisha ule umeme unasambaa katika maeneo mengine ambayo bado hayajapata umeme.

Mheshimiwa Naibu Spika, juzi nilisafiri nilipofika pale Airport saa 12.00 wakati na-board, ukiangalia ule uwanja wa ndege umepambwa kwa ndege za Air Tanzania. Katika siku za nyuma ulikuwa unakuta hata kile kibao kile kimoja tu cha Air Tanzania kilikuwa hakiwezi kuonekana. Haya yote ni mambo makubwa tuna kila aina ya sababu ya kuyasemea wala hatuhitaji kumung’unya maneno. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba wajitahidi sana kama ambavyo speed kubwa imeelekea kwenye hii reli ya mwendo kasi, mwaka jana nilisema na mwaka huu nasema, pale reli itakapofika Morogoro tu basi na vichwa pamoja na mabehewa vianze kutembea ambayo yatakuwa yanaleta abiria pale na abiria kuanzia saa 1.00 wanachukuliwa kutokea pale. Matokeo yake kila Mtanzania atakuwa siku hiyo ametoka Dar es Salaam na atalala nyumbani kwake.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa bahati mbaya sana leo watu wa Kanda ya Ziwa wakiondoka Dar es Salaam lazima walale njiani kwa sababu ya urefu wa barabara. Kwa hiyo, tunadhani kwamba kwa kufanya hivyo, ndivyo Serikali inavyoendelea kushughulikia matatizo ya wananchi wake ili waendelee kuishi kwa amani na raha mustarehe.

Mheshimiwa Naibu Spika, pamoja na hayo mafanikio mengi maana nilidhani nizungumzie machache lakini niendelee kuzungumzia changamoto ambazo bado zinawasumbua Watanzania lakini na watu wa Jimboni kwangu, wa Jimbo la Musoma. Kwangu mimi pale Musoma Mjini sasa yamebaki matatizo mawili makubwa. Tatizo la kwanza Mheshimiwa Waziri Mkuu analifahamu vizuri, niendele tu kumkumbusha na hili sasa badala ya kumkumbusha wale wananchi nitawaleta katika Bunge kwake waje wamuone yeye mwenyewe.

Mheshimiwa Naibu Spika, wako wafanyakazi waliokuwa wa Kiwanda cha Mutex ambao malipo yao nimekuwa nikiyasemea kila leo lakini hayo malipo yamekuja kufanyika ambapo kile kiwango walichokitaa ambacho hawakupewa miaka ishirini iliyopita leo wamekuja kupewa tena nusu ya hicho. Kwa hiyo, hilo kwa kweli kwa wale wananchi ni kero kubwa, ni kero ambayo inawasumbua na kwa sababu Serikali imeahidi kulishughulikia kwa muda mrefu na mpaka leo haijalishughulikia nitawaleta wenyewe waje kuzungumza na Mheshimiwa Waziri Mkuu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, lakini la pili ni suala la kiwanja cha ndege. Tuliomba kiwanja cha ndege na Mheshimiwa Rais aliridhia na tathmini ya fidia ilishafanyika lakini mpaka leo wananchi hawajalipwa na kuna sintofahamu kama kiwanja kitajengwa au hakitajengwa. Naiomba Serikali iseme kama hakijengwi tufute zile alama za ‘X’ ili wananchi waendelee na maisha yao kama kinajengwa basi fidia ilipwe ili ule uwanja uweze kujengwa. Kwa hiyo, hilo nalo nategemea katika kikao hiki au Ofisi ya Mheshimiwa Waziri Mkuu itakapokuwa inajibu italijibu suala hilo ili wananchi waweze kupata taarifa za uhakika. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, la mwisho ni tatizo la ajira. Pamoja na juhudi zote ambazo tumeendelea kuzifanya za kuongeza viwanda lakini tunatambua kwamba ajira pekee au sehemu pekee itakayopunguza tatizo la ajira ni Wizara ya Kilimo. Kwa hiyo, mimi bado sijaona kama Serikali imeweka vipi nguvu kwenye Wizara ya Kilimo katika kupunguza tatizo la ajira.

Mheshimiwa Naibu Spika, njia pekee ni kuhakikisha kwamba tunaweka nguvu kubwa kwenye kilimo cha umwagiliaji. Leo ukienda katika Kanda ya Ziwa na hata katika hizi Kanda zingine, Manyara au Arusha maeneo mengi sasa leo ni kiangazi na vyakula vimekufa. Hiyo inaonesha kabisa kwamba kama tungekuwa na kilimo cha umwagiliaji nguvu zile walizozitumia wananchi leo lisingekuwa tatizo. Wananchi wamelima, mvua hazikupatikana matokeo yake yale mazao yao yanakufa. Hii inaonesha moja kwa moja kwamba yawezekana mwaka huu kutakuwa na njaa kubwa, si kwamba wananchi hawakulima ni kwa sababu mazao yao yamekufa kwa sababu ya kiangazi.

Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru sana naomba kuunga mkono hoja. (Makofi)