Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 - Ofisi ya Waziri Mkuu

Hon. Victor Kilasile Mwambalaswa

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Lupa

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 - Ofisi ya Waziri Mkuu

MHE. VICTOR K. MWAMBALASWA: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru sana kwa kunipa nafasi na mimi niweze kuchangia hoja hii iliyo mbele yetu. Napenda kumpongeza sana Mheshimiwa Waziri Mkuu kwa hotuba yake hii nzuri sana, ya kitaalamu. Pia napenda niwapongeze Mawaziri wa Nchi, Mheshimiwa Jenista Mhagama na Mheshimiwa Angellah Kairuki, Naibu Mawaziri Mheshimiwa Antony Mavunde na Mheshimiwa Stella Ikupa, Makatibu Wakuu Bibi Maimuna Tarishi, Bwana Andrew Massawe na Bibi Dorothy Mwaluko, hotuba yenu hii ni ya kitaalamu sana, hongereni sana. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa ruhusa yako, naomba kunukuu sehemu chache sana, ukurasa wa sita ambapo hotuba inasema: “Mheshimiwa Spika, katika mpango wa maendeleo na bajeti ya 2019/2020, Serikali itaendelea kutekeleza Mradi wa Umeme wa Maji yam to Rufiji, ujenzi wa miundombinu ya reli ya kisasa, barabara pamoja na kukuza sekta ya anga. Utekelezaji wa miradi hiyo ya miundombinu wezeshi ya kiuchumi una lengo la kufungamanisha ukuaji wa sekta hizo na sekta nyingine hasa hasa za biashara, kilimo na utalii”.

Mheshimiwa Naibu Spika, kukuza sekta za miundombinu ni kukuza uchumi. Nchi ya Tanzania imebahatika kuwa na bandari nyingi na tumezungukwa na nchi nyingi ambazo hazina bandari. Tumezungukwa na nchi za Malawi, Zambia, Congo hasa upande wa Mashariki, Burundi, Rwanda na Uganda na Jamhuri ya Kati ambazo hazina bandari. Kwa hiyo, bahati hii ambayo ametupa Mwenyezi Mungu kuwa na bandari tuitumie vizuri.

Mheshimiwa Naibu Spika, nimefurahishwa sana kwamba Serikali sasa inaboresha bandari zote, imeanza na bandari ya Dar es Salaam, inakwenda bandari ya Tanga na bandari ya Mtwara na kujenga bandari mpya hapo Bagamoyo. Tunapozitumia bandari hizi, tujue kwamba kuna wenzetu nao ambao wana bandari, Msumbiji wana bandari ya Beira, Afrika Kusini wana bandari ya Durban kubwa sana, Angola kuna bandari ya Luanda, zote hizi zinaangalia nchi hizi ambazo ziko landlocked. Kwa hiyo, naomba tunapoziboresha bandari zetu tujue kwamba kuna ushindani wa kibiashara, wataalamu wetu wahakikishe wanaweka vivutio vizuri vya kuweza kuzivutia nchi hizi zije kupitisha mizigo yao kwenye bandari zetu kuliko bandari za wenzetu, tulitilie maanani sana suala hilo. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, ukichukua reli ya kati, hii mpya ambayo inajengwa ya Standard Gauge, tulikuwa tunakazania sana kutoka Dar es Salaam, Tabora, Isaka kwenda mpaka Kigali ambako na nchi ya Rwanda nayo inajenga kipande kile kule na hii inayokwenda mpaka Kigali inalenga mizigo ya Rwanda, Uganda na Jamhuri ya Kati. Nchi ya Burundi ina madini ya platinum zaidi ya tani milioni 6,7,8, sasa reli yetu tukitoa Uvinza, Msongati tuongee na nchi ya Burundi na yenyewe ijenge kutoka Bujumbura kuja Msongati, tuongee na nchi ya Congo ijenge reli kama hii kutoka bandari ya Uvira ije mpaka Bujumbura ili tuweze tuweze kuidaka ile mizigo ya Congo kwani ina madini mengi sana. Tukiacha sisi wenzetu wa Angola watajenga reli kutoka Rwanda kuja Lubumbashi au Lusaka.

Kwa hiyo, naomba sana tulenge mizigo ya Congo, Burundi na Jamhuri ya Kati kwa sababu reli yetu hii ya Standard Gauge itakapokuwa tayari ina uwezo wa kubeba tani karibu milioni 20 za mizigo kwa mwaka, naomba tulenge kuelekea huko.

Mheshimiwa Naibu Spika, pamoja na reli hii ya kati ya Standard Gauge, nimefurahishwa sana bado Serikali inaendelea kuikarabati hii reli ambayo ipo sasa hivi ya Metre Gauge. Kwa hiyo, hapa kati tutakuwa na reli mbili, Reli ya Standard Gauge na Metre Gauge. Mwaka jana nilisema kwamba tunaponunua rolling stock tuhakikishe tunanunua rolling stock ambayo unaweza ukatumia kwa reli zote mbili.

Mheshimiwa Naibu Spika, pia tuna reli yetu ya TAZARA, yenyewe haihitaji kuboreshwa katika miundombinu mingi, inahitaji umeme tu. Reli ya TAZARA yenyewe ni Cap Gauge inaoana na reli za Afrika Kusini na Zambia. Naomba na hii reli tuiboreshe kwa kuiwekea umeme ili reli zetu zote tatu, Standard Gauge, Metre Gauge na hii Cap Gauge zifanye kazi za kuhudumia nchi ambazo ziko Landlocked.

Mheshimiwa Naibu Spika, pamoja na hayo naipongeza sana Serikali kwamba imenunua meli mbili au tatu kwenye Ziwa Nyasa ambazo zinafanya biashara nzuri sana ya kusafirisha binadamu na mizigo katika nchi ya Tanzania, Malawi na Msumbiji. Naomba sasa pale Inyara tuweke bandari kavu na vilevile Serikali ifikirie kujenga sasa reli kutoka hapo Inyara kuelekea bandari ya Itungi ili tuweze kuihudumia nchi ya Malawi.

Mheshimiwa Naibu Spika, mchango wangu ulikuwa ni huo tu katika hotuba hii, naunga mkono hoja. (Makofi)