Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Female
Party
CHADEMA
Constituent
Nkasi Kaskazini
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
1
Ministries
nil
MHE. AIDA J. KHENANI: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru. Nami namshukuru Mwenyezi Mungu kwa kunipa uhai na kuweza kusimama tena ndani ya Bunge lako Tukufu.
Mheshimiwa Naibu Spika, nitachangia hotuba ya Waziri Mkuu kwenye mambo makuu matatu. Sehemu ya kwanza ni ajira kwa vijana, jambo ambalo imekuwa ni kilio kwa vijana wa Kitanzania. Kwa sasa kumaliza elimu ya chuo kikuu imekuwa ni kama laana kwenye nchi yetu. Mpaka nasimama kuchangia hapa message za vijana waliotuma kwamba hebu waambie watuambie hatma ya sisi tuliomaliza vyuo vikuu toka mwaka 2015 ni nini?
Mheshimiwa Naibu Spika, kwenye suala la ajira ukiangalia ajira inayotokea kwa mwaka hailingani na idadi ya wahitimu kwa mwaka kwenye nchi yetu. Nataka Serikali ije ituambie nini hatma ya vijana hawa wa toka mwaka 2015 mpaka leo? Kwa sababu kitu kingine ambacho kingewasaidia kujiajiri ni upande wa kilimo, suala la kilimo liko hoi bin taabani.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwenye suala hili la ajira kwa vijana sasa kumekuwa na suala la ubaguzi. Kwa sasa watu wanapotafuta ajira kuna maeneo imefikia wanaambiwa waoneshe Kadi yao ya Chama cha Mapinduzi. Naomba suala hili Serikali iliangalie kwa sababu ubaguzi huu hautaishia kwenye chama peke yake, athari za ubaguzi ni kubwa sana, zikianzia kwenye vyama zitakwenda kwenye makabila, zikitoka kwenye ukabila zitakwenda kwenye udini, ni vizuri Serikali ifuatilie jambo hili. Si kwamba limejificha kiasi kwamba hamuoni, kama mlikuwa hamjui mimi nawaambia kwamba kuna hili jambo kwenye suala la ajira sasa watu wanaambiwa wapeleke Kadi za Chama cha Mapinduzi jambo ambalo kwenye Katiba yetu ya nchi halipo. Sasa kama ni utekelezaji wa Ilani ya Chama ya Mapinduzi pia tujue kwamba ajira kwa sasa lazima uwe na kadi ya Chama cha Mapinduzi. (Makofi) [Maneno Haya Siyo Sehemu ya Taarifa Rasmi za Bunge]
Mheshimiwa Naibu Spika, suala la pili ambalo nitaenda kulizungumzia ni suala la kilimo. Tunapozungumzia kilimo, ni lazima tuzungumzie masoko na pembejeo.
NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU (KAZI, VIJANA NA AJIRA): Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusu utaratibu.
NAIBU SPIKA: Mheshimiwa Aida Khenani ukae. Mheshimiwa Antony Mavunde, kanuni iliyovunjwa.
KUHUSU UTARATIBU
NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU (KAZI, VIJANA NA AJIRA): Mheshimiwa Naibu Spika, Kanuni ya 64(1)(a) ambayo inazuia Mbunge kutotoa taarifa ambazo hazina ukweli. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, Mbunge anayezungumza, anatoa taarifa kwamba kuna ubaguzi mkubwa kwenye eneo la ajira na kwamba ni lazima mtu aoneshe kadi ya CCM ndiyo aweze kupata ajira.
Mheshimiwa Naibu Spika, suala hili siyo kweli. Matangazo yote ya ajira, huwa yanatoa vinavyohitajika kwa maana mwombaji awasilishe nini. Kwa hiyo, kwa sababu taratibu zimewekwa vizuri kabisa katika kila ajira ambazo zinatangazwa na mwombaji anatakiwa awasilishe nyaraka ambazo zimesemwa; na katika nyaraka hizo haijawahi kuwemo kadi ya Chama cha Mapinduzi kama kigezo cha mtu kupata ajira; hivyo kwa mujibu wa kanuni; na kwa sababu mimi nimethibisha kwamba siyo kweli, tunamtaka mtoa taarifa aondoe maneno yake au lah, athibitishe mbele ya Bunge lako tukufu na kanuni za Bunge hili ziweze kuchukua hatua. (Makofi)
NAIBU SPIKA: Waheshimiwa Wabunge, amesimama Mheshimiwa Naibu Waziri, Ofisi ya Waziri Mkuu, Ajira na Vijana, akitumia kanuni ya 64(1)(a) inayozungumzia mambo yasiyoruhusiwa Bungeni, lakini amesoma kifungu kidogo cha
(1) kinachosema Mbunge hatatoa ndani ya Bunge taarifa ambazo hazina ukweli. Sasa ukishazungumza kuhusu taarifa ambazo hazina ukweli zinakupeleka kwenye kanuni ya 63 inayohusu kutokusema uongo Bungeni.
Sasa ukiisoma kanuni ya 63, huwa inamtaka anayemwambia Mbunge mwingine kwa maana ya mchangiaji kwamba amesema uongo, yeye anatakiwa kusema maelezo yake yanayoonesha kwamba yule Mbunge aliyetangulia kusema kabla yeye hajasimama na kusema kuhusu utaratibu, alikuwa akisema uongo.
Kwa maelezo ambayo ameyatoa Mheshimiwa Naibu Waziri na amesema kuhusu matangazo yanayotolewa na vigezo vinavyowekwa na kwamba kigezo ambacho alikuwa anakitaja Mheshimiwa Mbunge aliyekuwa akichangia hakipo kwenye ajira kama ambavyo yeye amekisema. Sasa kwa masharti ya kanuni inayokataza kusema uongo Bungeni, Mheshimiwa Mbunge anapewa fursa ya kufuta usemi wake ama kuthibitisha.
Kwa hiyo, kwa mujibu wa Kanuni zetu tulizojiwekea nitampa fursa Mheshimiwa Aida Khenani kufuta kauli inayosema ajira Serikalini inataka mtu awe na kadi ya Chama cha Mapinduzi. Mheshimiwa Aida Khenani.
MHE. AIDA J. KHENANI: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru. Ni vizuri tukaacha hofu. Nimesema wakafuatilie, ndiyo jambo nililozungumza, Hansard ziko wazi. Kwa kuwa umeniongoza, nayafuta, ila mimi nimesema na ni wajibu wa Serikali kwenda kufuatilia jambo hilo. Mitandao iko wazi, mambo hayo yako wazi kabisa yanaonekana.
NAIBU SPIKA: Mheshimiwa Khenani, ili Taarifa zetu Rasmi za Bunge zikae vizuri, kama unasema unafuta kama ulivyozungumza, huwezi tena kuendelea kutoa maelezo juu ya jambo hilo hilo ambalo unalifuta. Kwa hiyo, lifute ili taarifa zikae rasmi, halafu uendelee na mchango wako.
MHE. AIDA J. KHENANI: Mheshimiwa Naibu Spika, nimefuta maelezo yangu. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, nitazidi kusema, kama kuna nchi wanalia njaa kwenye Taifa lao, vijana wa Tanzania wanalia na ajira kwenye Taifa lao. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, nitakwenda kwenye suala la kilimo ambalo tunaamini vijana wengi walikimbilia huko kujikita, lakini nako hali ni mbaya kupita kawaida.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwenye suala la kilimo nitazungumzia masoko. Suala la masoko ya mazao mchanganyiko na mazao yote nchini, imekuwa ni shida kubwa sana kwa wakulima na sasa wanajiona ni kama hawana uhalali wa kuendelea na kilimo, hasa wakulima wa zao la mahindi wa Mkoa wangu wa Rukwa.
Mheshimiwa Naibu Spika, nilizungumza mwaka 2018 kwamba kabla ya tamko la Mheshimiwa Waziri Mkuu ndani ya Bunge kukataza wakulima kuuza mazao yao nje ya nchi hali ya mazao yao na bei halisi ilikuwa ni shilingi 75,00/=. Baada ya tamko lile, baadaye akaja kuruhusu wakati huo tayari nchi ambazo zilikuwa zina uhitaji, hazihitaji tena, inakuwa ni hasara kwa mkulima. Ni vyema Serikali kabla ya matamko yake ikafanya kwanza tafiti kuliko kuwapa adhabu wakulima wa nchi hii. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, suala la pembejeo bado ni shida kwa wakulima wetu. Serikali ya Awamu ya Tano, slogan yake ni Serikali ya viwanda. Kwa nini sasa wasiweke kipaumbele cha kujenga viwanda zizalishwe pembejeo hapa ili kupunguza hali ngumu ya bei kwa wakulima wanaopata shida? (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba Ofisi ya Waziri Mkuu watakapokuja watuambie, wana mkakati gani wa kuanzisha viwanda vitakavyotengeneza pembejeo nchini ili kupunguza bei kubwa ya pembejeo ambayo inaenda kuwaumiza wakulima wetu? Bei kubwa ya pembejeo haiendani na hali ya bei ya mazao ambayo wanazalisha. Kwa hiyo, ni vyema, wakipunguza bei ya pembejeo itawasaidia hata uzalishaji wa kulima ambapo kilimo chetu sasa kitakuwa ni chenye tija.
Mheshimiwa Naibu Spika, mahindi kwetu ni siasa, mahindi ni maisha na mahindi ni biashara. Hapa nataka kuzungumzia jambo moja, kwenye korosho fedha zimetoka kwenye Benki ya Kilimo. Sasa mimi sijui kama ile benki imebadilika imekuwa ni Benki ya Korosho. Kama ni mazao mchanganyiko, haya mazao mengine utaratibu ukoje? Ningependa kujua, Serikali ina mkakati gani na mazao mengine? Je, huu utaratibu utakuwa ni wa kila mwaka wa kuchukua pesa kwenye Benki ya Kilimo kwenda kununua mazao ambayo yatakosa soko?
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba niiambie Serikali tu kwamba baba akinunua chakula nyumbani hapongezwi kwa sababu ni wajibu wake. Kwa hiyo, tunategemea Serikali ni wajibu wenu kuhakikisha mnawatengenezea soko wakulima wanchi hii. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, nitakwenda kuzungumzia Uchaguzi wa Serikali za Mitaa. Mpaka leo mimi ni Mwenyekiti wa Serikali ya Mtaa. Jana limejibiwa hapa kwamba Wenyeviti wa Serikali wanalipwa shilingi 20,000 kama posho. Kabla sijamaliza muda wangu wa miaka mitano, nimezungumza hili jambo mara tatu ndani ya Bunge. Hili jambo inategemeana na makusanyo ya Halmashauri, kwa nini Serikali isilete heria hapa ambayo itakuwa uniform kwamba hawa Wenyeviti watalipwa posho kiasi gani? (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kwenye Halmashauri sasa hali ni mbaya na huwezi kufananisha Mwenyekiti wa Sumbawanga Mjini ukamfananisha na Mwenyekiti wa Kinondoni kwa sababu zile Halmashauri za Mjini zitakusanya tofauti na Halmashauri za Vijijini. Sasa kama Serikali ina uwezo wa kutenga fedha kwa ajili ya uchaguzi, kwa nini wasitenge fedha kwa ajili ya kuwalipa posho Wenyeviti wa Serikali? Kama jambo hili halijaandaliwa, ni vizuri kwa ushauri tu, kabla hawajajipanga na uchaguzi, wajipange kwanza ni namna gani wataanza kuwalipa Wenyeviti wa Serikali za Mitaa? Hili jambo…
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. MWITA M. WAITARA): Mheshimiwa Naibu Spika, Taarifa.
NAIBU SPIKA: Mheshimiwa Naibu Waziri, TAMISEMI.
T A A R I F A
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. MWITA M. WAITARA): Mheshimiwa
Naibu Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi. Naomba nimpe taarifa Mheshimiwa Mbunge kwamba kabla uchaguzi wa Serikali za Mitaa haujafanyika, wananchi wenye sifa wanajipanga kwa nafasi ambazo wanahitaji; ama kuwa Mwenyekiti wa Mtaa au wa Kijiji, au wa Kitongoji au Mjumbe wa Serikali ya Kijiji au Serikali ya Mtaa. Utaratibu ni kwamba kazi za Uenyeviti wa Mitaa ni kazi za kujitolea na ni lazima awe na kipato ambacho kinamwingizia maisha yake halali ili aweze kufanya kazi bila kumdhulumu mwananchi na bila kuiba.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, katika mazingira hayo, hata kabla posho haijapangwa, anakuwa anapanga na anakwambia kwa sababu zipi na ataishije?
Mheshimiwa Naibu Spika, taarifa ya pili ni kwamba…
NAIBU SPIKA: Taarifa ni moja Mheshimiwa. Mheshimiwa Aida Khenani, unaipokea taarifa hiyo?
MHE. AIDA J. KHENANI: Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza najua wana muda wa kujibu, sijui ana pressure ya nini; lakini pia alikuwa Mwenyekiti mwenzangu, anajua kwa nini hiyo nafasi ameikosa kwa wakati huu. Kwa hiyo, aniache Mwenyekiti nizungumze kwa sababu nawajua Wenyeviti wenzangu. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, hili suala la ukusanyaji wa mapato linategemea na uwezo wa Watendaji kwa maana ya Wakurugenzi, anaweza kubuni vipi vyanzo vya mapato? Kwa hiyo, hii hali itaweka utofauti mkubwa sana wa Wenyeviti juu ya posho zao. Kama Serikali inaweza kumwamini Mwenyekiti akaandika barua ya kumdhamini mtu, inakuwaje ashindwe kutambua kwamba ana mchango gani ndani ya nchi hii? Ni kiongozi pekee wa Serikali wa Mtaa ambaye hana usiku, hana mchana, hana jua, hana mvua. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, napenda kuwaambia tu Serikali, kama bado hawajatambua mchango wa Wenyeviti, ni bora wafute suala hili la uchaguzi wa Serikali za Mitaa, wabaki wabaki Madiwani tu ambao wanapata posho. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. (Makofi)