Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 - Ofisi ya Waziri Mkuu

Hon. Amb. Adadi Mohamed Rajabu

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Muheza

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

2

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 - Ofisi ya Waziri Mkuu

MHE. BALOZI ADADI M. RAJAB: Mheshimiwa Naibu Spika, nami nashukuru sana kwa kupata nafasi hii ya kuweza kuchangia hoja hii muhimu sana ya Mheshimiwa Waziri Mkuu. Kwanza, nampongeza sana Mheshimiwa Waziri Mkuu pamoja na Mawaziri wote kwa jinsi Mheshimiwa Waziri Mkuu alivyo- present hoja yake kwa weredi mkubwa sana, kwa sababu ametumia system ya PowerPoint na mambo yote mazuri ambayo alikuwa anayasema tulikuwa tunayaona pale. Kwa hiyo, nampa hongera sana. Nategemea na Waheshimiwa Mawaziri wengine basi na wenyewe wata-present kwa system ya PowerPoint ili tuweze kuona kazi nzuri ambazo zinafanyika. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, pamoja na kazi nzuri ambazo zinafanywa na Serikali ya Awamu ya Tano, tumeona kazi nzuri sana na nyingi sana ambazo hazijawahi kufanyika katika nchi hii katika kipindi kifupi. Tumeona mambo ya kisasa ambayo yanakwenda na ambayo yanafanyika kwa weledi mkubwa sana na miradi mikubwa sana. Sasa pamoja na kazi hiyo, nilitaka kuchangia kwenye sekta zifuatazo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, nitaanza na suala la uchumi. Hivi karibuni Mheshimiwa Rais aliwaelekeza TRA kuangalia uwezekano wa kupunguza mapato kwa sababu kodi ambazo wanatoza ni kubwa sana to the extent kwamba wananchi wa kawaida wanashindwa kulipa kodi na badala yake wanatumia njia mbalimbali za kukwepa kodi au kukimbia nje ya nchi ili mradi tu waweze kuona kwamba watafanya vipi kukwepa kodi?

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, Mheshimiwa Rais aliposema TRA ni lazima waangalie namna gani wanaweza kupunguza kodi, wananchi wasiweze kukimbia kulipa kodi. Hivi karibuni tulikwenda Kampala kuangalia wenzetu wanafanyaje kwenye Treasury Single Account. Kule Kampala pamoja na mambo mengine tulikutana na Watanzania wengi. Watanzania ambao wanatoka hapa wanakwenda Kampala kununua bidhaa na kuzirudisha hapa, bidhaa hizo hizo zimepita kwenye bandari yetu hapa hapa na zimekwenda na baadaye wale wale wanazifuata kuzirudisha hapa. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, sasa hii system kwa kweli ni kitu ambacho Mheshimiwa Rais alikuwa anasema. Kwa sababu hapa ilikuwa ni kama hub, ilikuwa ni kana Dubai, tuna bandari sisi. Walikuwa wanakuja wafanyabiashara wengi, Afrika Kusini, Zimbabwe, Malawi, Zambia, wote walikuwa wanakuja hapa. Sasa wamehama wote, tumewakuta kule. Sasa ni vizuri suala hili likaangaliwa. Tuliongea na Mheshimiwa Waziri wa Fedha kwenye Kamati na aliahidi kutuma watu ili kuangalia kwamba tutaweza kulirekebisha namna gani?

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, ni muhimu sana watu waende kwa sababu tunafanya mambo mazuri sana juu kule, miradi mikubwa sana inafanyika, lakini bado sasa hivi tuangalie namna gani tunaweza kupunguza kodi, namna gani tunaweza kufanya wananchi wetu kulipa kodi bila ya kukimbia au bila kufanya mchezo mwingine. Kwa sababu hapa karibuni tu kule Tanga kuna kiwanda kikubwa sana cha Pembe ambacho ni cha ngano; jamaa kafunga kiwanda kwa sababu ya kukimbia kodi. Kafunga kiwanda na kageuza mambo mengine; kwa mfano, magari yake sasa yanasomba mchanga au kitu kingine chochote. Kwa hiyo, ni suala muhimu sana ambalo naomba liangaliwe kwa undani wake.

Mheshimiwa Naibu Spika, suala la pili ni suala la hizi ndege zetu ambazo zimekuja. Tunategemea ndege hizi zifanye, nimeona faraja sana kwa sababu tulikwenda na Airbus mpaka Kampala na tukaja kuchukuliwa na Airbus hiyo hiyo. Kwa kweli tulipofika KIA ilijaa kabisa ile ndege. Kwa hiyo, ni fahari kubwa kwamba hizi ndege zina umuhimu wake na zitasaidia sana.

Mheshimiwa Naibu Spika, katika taarifa ya Mheshimiwa Waziri Mkuu sikuona akitaja uwanja wa ndege wa Tanga. Tunategemea nasi tupate ndege ya Bombardier iweze kushuka pale. Sasa nategemea wakati Wizara itakapokuja kutoa taarifa zake, basi itaona kwamba Tanga sasa hivi kwa sababu ya umuhimu wake, wawekezaji wengi wanakuja, basi nasi tuweze kupata ndege ambayo itakuwa pale Tanga. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, suala la tatu ambalo nataka kuchangia ni wawekezaji. Ni kweli ukiangalia kwenye taarifa ya Mheshimiwa Waziri Mkuu kwenye World Investment Report ya mwaka 2018, sisi tunafanya vizuri sana hapa Afrika Mashariki. Pamoja na kufanya vizuri, inabidi tuangalie kituo chetu hiki cha TIC. Tunategemea TIC tumeita ni lakini ni lazima tuhakikishe kwamba ni kweli real One Stop Center kwa ajili ya kuwaweka hawa wawekezaji ili mwekezaji akifika pale, hana sababu ya kuzunguka kwenda mahali pengine popote. Ni kuhakikisha kweli vibali vyote, leseni na vibali vyote vya kuishi nchini vinapatikana bila matatizo yoyote. Bila kufanya hivyo, itakuwa ni delays ambazo hazina umuhimu. Mara nyingi sana wanapofanya assessment hasa za mambo ya corruption na uboreshaji wanaangalia hizi systems, wawekezaji wanakuwa handled namna gani? Unatoa leseni kwa muda gani? unachelewesha kwa muda gani? Je, kuna land bank pale kwenye kituo chetu? Kwa sababu mwekezaji hawezi akaja ukamwambia basi nenda katafute ardhi sehemu nyingine, kuna huyu jamaa uende ukaongee naye. No, inatakiwa akija pale kweli ni One Stop Center, anakutana na kila kitu; kama ni ardhi anaoneshwa, unataka hapa au hapa? Basi yeye ni juu yake kuangalia kwamba anataka sehemu gani?

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, ni muhimu sana kurekebisha vitu kama hivyo. Ni muhimu kwenye Wizara ya Mambo ya nchi za Nje ikafungua kitengo kabisa. Sasa hivi Mabalozi nje kule wamehamasishwa sana na wanatafuta wawekezaji kwa bidii sana. Sasa itakuwa wawekezaji wanatafutwa, wanakuja pale, halafu Foreign Affairs wanakuwa hawana kitengo au department maalum ya kuwashughulikia au kupokea wawekezaji, badala yake Balozi atoke nje aje nao mpaka hapa, aanze kuzunguka kwenda huko.

Mheshimiwa Naibu Spika, ni jukumu ya Foreign Affairs kuweka mazingira mazuri na ni jukumu la TIC kuweka mazingira mazuri. Ninaamini kabisa kwa sababu imekuwa ni Wizara maalum, basi Wizara hiyo itashughulikia mambo haya yaweze kwenda vizuri tuweze kupata wawekezaji wazuri zaidi. Ni vizuri ndege yetu hii Dreamliner sasa ikaanza kufanya kazi, kwa sababu itategemea kwa sababu hakuna mwekezaji ambaye anafurahia kwenda na direct flight. Hakuna mtalii ambaye anafurahia kupata ndege ya direct flight badala kuingia kwenye transit kwenye Miji mingine.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, ni vizuri hizi ndege zianze kufanya kazi tuweze kupata watalii wengi na tuweze kupata wawekezaji ambao ni wazuri.

Mheshimiwa Naibu Spika, la mwisho ambalo nilitaka kuchangia ni suala maji. Maji hasa Muheza ni siasa. Juzi juzi Kamati walikwenda kule na wenyewe watanisaidia kudhihirisha kwamba tuna tatizo kubwa la maji Muheza na tuna tatizo kubwa la maji sehemu mbalimbali hapa nchini. Kuna mradi ule wa shilingi bilioni 500 ambao ofcourse nitakuja kuongelea nikipata nafasi kwenye Wizara ya Maji. Suala hilo tunamsubiri Mkandarasi Mshauri (Consultant) kutoka India. Sasa tumekuwa tunamsubiri na taratibu nyingine, sasa sijui ni miezi mingapi.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, naomba Wizara ya Maji, kama ni kumsubiri, kwa nini tusitume mtu mara moja kwenda India na kurudi na hivyo vitu ambavyo vimebakia?

Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya kusema hayo, naunga mkono hoja, ahsante sana. (Makofi)