Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 - Ofisi ya Waziri Mkuu

Hon. Mary Deo Muro

Sex

Male

Party

CHADEMA

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 - Ofisi ya Waziri Mkuu

MHE. MARY D. MURO: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante kwa kupata nafasi ya kuchangia hotuba iliyopo mezani. Kwanza namshukuru Mungu kwamba nina afya njema, kwa hiyo nitakuwa niko vizuri kuweza kuchangia yale ambayo naona ni muhimu kwa ajili ya Taifa letu.

Mheshimiwa Naibu Spika, napenda kuanza na suala la hifadhi ya jamii. Hifadhi ya jamii mifuko iliunganishwa ya LAPF, GEPF na PPF ikaunda PSSSF. Kwenye kitabu chao ukurasa wa 70 wanahitimisha kwa kusema hatua hii imewezesha kutatua kero za wastaafu ambazo zilidumu kwa muda mrefu lakini ukiangalia kwenye uhalisia ni kwamba wastaafu wengi wanahangaika sana kupata mafao yao. Nina ndugu zangu ambao mpaka leo hii wana mwaka mzima hawajapata mafao. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, Ukiachia hao wastaafu, kuna watoto ambao waliachwa na hao ambao walikuwa ni wafanyakazi na walijiunga katika mifuko hii. Nina watoto yatima ambao ninaishi nao kuanzia Januari mpaka sasa hivi ni mwezi Aprili hajalipiwa ada ya shule. Wakati nafuatilia nimekuta na akina mama wengi sana ambao wanalalamikia suala la watoto wao kutolipiwa ada na sasa watoto wako majumbani hawaendelei na shule. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, sasa ukiangalia wanavyohitimisha kwamba eti kero zimepungua, sijaona kwamba kero zimepungua kwa mifuko hii kuunganishwa labda Serikali ijipange upya kuhakikisha kwamba tatizo hili linapungua. Nafahamu kabisa hii Wizara ina wanawake wengi, Makatibu Wakuu watatu kama sio wawili ni wanawake, Mheshimiwa Waziri wa Nchi ni mwanamke, kwa kiasi nilichokutana na wale wanawake wanahangaika na watoto mitaani huko hawasomi kwa sababu waume zao wamefariki na mifuko hii tangu imeunganishwa watoto hao wanapata shida kulipiwa mafao yao ya elimu, kwa kweli naomba Serikali mkajipange vizuri. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, najua kabisa Mheshimiwa Jenista unasikia na unafahamu jinsi gani akina mama wanateseka katika kuhangaika na hawa watoto. Nakupa mifano hiyo miwili kwamba nina watoto wa ndugu zangu tena kaka yangu ambaye ananiachia ziwa, mpaka sasa hivi tangu mwezi Januari hawajalipiwa ada. Nimejaribu kulipa na mimi napokea posho kama watu wengine nimeshindwa, ina maana hao ambao hawana hata ndugu wa kuwalipia hali yao ikoje? (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, napenda kuhamia sehemu ya Mahakama. Napenda kusema kwamba Mahakama ni mahali ambapo tunatakiwa tupate haki na kama haki na kwa wakati. Ukiangalia jinsi kesi zinavyocheleweshwa Mahakamani imesababisha msongamano mkubwa sana wa mahabusu na ukienda magerezani unakuta hali ni mbaya sana ambayo imesababishwa na ucheleshwaji wa kesi ambazo zingeamuliwa kwa haraka ina maana mahabusu kule magerezani wangepungua. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, hapa tunapanga bajeti ya kulisha watu magerezani ni kwa sababu tumeshindwa kuwa na kesi zinazoenda haraka ili kupunguza mahabusu, ukipunguza wafungwa maana yake umepunguza na bajeti ya Serikali. napenda kuwaambia Serikali kama tunataka kupunguza gharama za kuendesha baadhi ya mambo ni pamoja na kuhakikisha kwamba kesi zinaendeshwa haraka. Kwa kufanya hivyo, tunapunguza gharama za uendeshaji wa Serikali na pia tunaongeza pato kwa sababu kesi zikiisha haraka watu wanaenda kufanya kazi zao walizozizoea. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kitu kingine ambacho nakishangaa sijajua kama msongamano ulioko magerezani na ile mito ndoo ambayo inawekwa kule zote hizo ni adhabu za huyo mtu ambaye amefungwa au ni nini? Haki za binadamu ziko wapi kumfanya mtu aishi na kinyesi? Kwa nini Serikali isitengeneze vyoo hata kama maeneo ya kulala ni finyu lakini vyoo vingetengenezwa kulikoni watu wanalala na vinyesi, haki ya binadamu inakuwa wapi? (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, napenda kuzungumzia habari za UKIMWI. Tunafahamu kabisa UKIMWI ni janga la Taifa na Serikali inajitahidi kuhakikisha kwamba dawa za kufubaza ugonjwa wa UKIMWI zinapatikana lakini watu hawafi kwa sababu ya wadudu wale wa UKIMWI wananchi wengi wanakufa kwa sababu ya magonjwa nyemelezi magonjwa kama Kifua Kikuu, kuharisha na kadhalika ambayo tumekuwa tukisema humu ndani mara nyingi kwamba kama ARV ingekuwa na package ya Septrin, it means wananchi wenye magonjwa nyemelezi wangeweza kupata dawa hizo na wakapona. Kama tunawapa dawa za UKIMWI hatuwapi dawa za magonjwa nyemelezi wagonjwa wengi wanakufa kwa magonjwa nyemelezi na wala sio kwa ugonjwa wa UKIMWI wenyewe. Kwa hiyo, naiomba Serikali ifanye mkakati wa kuweka Septrin kwenye package ya ARV ili mtu anapopewa dawa za ARV apewe na zile za Septrin zitasaidia anapopata magonjwa nyemelezi anatumia zile dawa. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kitu kingine ni tatizo la vituo vya kupimia UKIMWI.

T A A R I F A

NAIBU WAZIRI WA MADINI: Mheshimiwa Naibu Spika, taarifa.

NAIBU SPIKA: Mheshimiwa Mary Muro kuna taarifa.

NAIBU WAZIRI WA MADINI: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba tu kumpa taarifa Mheshimiwa anayechangia hivi sasa kwamba si kila mgonjwa anayepewa dawa za ARV anahitaji kupewa Septrin. Tunachotaka kushauri wagonjwa wote au watu wote wanaopata huduma ya ARV ni vizuri wanapojisikia tofauti waende kwenye vituo vyao kwa ajili ya kutibiwa, watapewa dawa zingine kwa sababu watakuwa wanapewa zile kule lakini sio lazima package ya ARV apewe na Septrin.

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kumpa taarifa hiyo. (Makofi)

NAIBU SPIKA: Mheshimiwa Mary Muro, unaipokea taarifa hiyo.

MHE. MARY D. MURO: Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza ningeomba wasubiri baadae watajibu, lingine ni kwamba vituo vilivyo vingi watu wanapewa sawa dawa za ARV lakini wanapokuwa na magonjwa ya nyemelezi hakuna Septrin. Sasa tunaweza tukawauwa hawa watu kwa kukosa Septrin na sio ARV. ARV zinapatikana na ugonjwa wa UKIMWI shida ni magonjwa nyemelezi na wala sio ugonjwa wa UKIMWI wenyewe.

Mheshimiwa Naibu Spika, napenda kuongea vituo vya kupimia UKIMWI. Kuna vituo vichache vya kupimia UKIMWI halafu viko mbali kwa hiyo havifikiki. Nashauri Serikali ijitahidi kuongeza vituo vya kupimia UKIMWI. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, pia kuna tatizo la viral load mashine, nashauri Serikali ijipange at least kila mkoa uwe na viral load mashine kwa sababu unakuta vipimo vile vinapelekwa mbali njiani vinakutana na shida kadha wa kadha tunaweza tusipate really matokeo kwa sababu ya ule ubebaji labda unatoka Njombe kwenda Mbeya au utoke sehemu moja na kupeleka sehemu nyingine ambayo ni mbali. Sehemu fulani Serikali imesema imejitahidi kununua dawa na kujenga vituo basi ijitahidi kuongeza na hizo viral load mashine. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, napenda kuongelea suala la kodi ya mapato. Ni kweli Watanzania wanaishi kwenye wakati mgumu sana kwa sababu ukienda ofisi za Kodi ya Mapato unaweza ukashinda siku nzima unahangaikia kitu kimoja. Haijulikani kama wafanyakazi ni wachache au ndiyo system ilivyo? I ile hali ambayo inaonekana katika Ofisi za Kodi ya Mapato inasababisha watu wengine kukata tama. Kama Serikali ina nia ya kukusanya mapato iongeze watendaji ili kurahisisha kazi. Ni mara nyingi sana mimi nimefika pale nimekuta watu wanagongana tu kwenye corridor, kila sehemu kumejaa. Sasa watu hawa wanatuletea pesa na wao wanaisaidia Serikali kukusanya mapato, kama watendaji ni wachache ina maana wanahangaika siku nzima na wanapoteza muda wa kufanya kazi zingine na Serikali inakosa mapato. (Makofi)

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

NAIBU SPIKA: Kengele ya pili ilishagonga Mheshimiwa, ahsante sana. (Makofi)