Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 - Ofisi ya Waziri Mkuu

Hon. Ritta Enespher Kabati

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 - Ofisi ya Waziri Mkuu

MHE. RITTA E. KABATI: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana kwa kunipa nafasi ili nami niweze kuchangia bajeti iliyoko mezani kwetu.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza kabisa nianze na kuipongeza Serikali hii ya Awamu ya Tano inayoongozwa na Rais wetu, Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli kwa kazi kubwa sana ambayo ameifanya kwa kweli katika nchi yetu na hata imefanya baadhi ya viongozi wetu akiwepo Mheshimiwa Lowassa kurudi CCM, baadhi ya Wabunge wengine wote kurudi CCM na viongozi mbalimbali baada ya kuona kazi nzuri sana na mno inayofanywa na Chama chetu cha Mapinduzi.

Mheshimiwa Naibu Spika, vilevile nimpongeze sana Mheshimiwa Waziri Mkuu kwa kazi yake nzuri. Kwa kweli, amefanya kazi nzuri sana, ametembea karibu nchi nzima kuhakikisha kwamba miradi inakwenda. Pia nawapongeza Mawaziri waliopo katika Ofisi ya Waziri Mkuu; Mheshimiwa Jenista Mhagama, Mheshimiwa Ikupa na Mheshimiwa Naibu Waziri wa Kazi. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, pia nampongeza sana Mheshimiwa Rais kwa kumteua Mheshimiwa Angellah Kairuki kwa kuongeza tena kasi katika ofisi yake kwenye suala la uwekezaji. Ninaamini kabisa uwekezaji sasa unaenda kuinua nchi yetu. Bila kuwekeza, sidhani kama nchi yetu itaweza kusikika hata katika viwanda au katika nyanja zozote. Bila kuwekeza, kuleta wawekezaji, kuweka vivutio vingi na kutoa changamoto nyingi ambazo kwa kweli tulikuwa tunaona kama ni kero sana katika nchi yetu, nchi hii haiwezi kuendelea.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, nashauri kwamba Mheshimiwa Jenista sasa apewe wataalam na ofisi ambayo itasaidia sasa kuondoa ule urasimu ambao ulikuwepo kwa wawekezaji wetu ili waweze sasa kuwekeza na nchi yetu iweze kuongeza ajira na kipato kikubwa kabisa katika nchi yetu.

Mheshimiwa Naibu Spika, vilevile naomba nipongeze sana mambo makubwa yanayofanyika katika Mkoa wetu wa Iringa. Ukarabati wa Kiwanja cha Nduli, kwa kweli Wana- Iringa tunasema Kamwene. Kazi ile ni nzuri sana na mpaka sasa hivi ukarabati ule tarehe 29 nawakaribisha wote, ndege kubwa Bombadier inatua pale Iringa. Kwa hiyo, niwaombe muionje siku hiyo, twende tukatue pale hata Naibu Spika ili mwone kazi na kasi kubwa kabisa inayofanywa na nchi yetu ikiongozwa na Chama cha Mapinduzi. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa sababu, Iringa ni kitovu cha utalii, sasa ukarabati ule uende sambamba na ukarabati wa kiwango cha lami, ile barabara inayokwenda mbuga za wanyama Ruaha Nationa Park kwa sababu, ni mbuga ya pili. Tunaamini kama itajengwa kwa kiwango cha lami, sasa utalii utaongezeka, uchumi wetu wa Iringa na uchumi wa nchi hii kutumia utalii tutaongeza hata watalii wengi sana watakuja, hata wananchi watajiajiri kwa kupitia utalii. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, sasa naiomba Serikali yangu, wale wananchi waliopisha ukarabati ule, basi wapewe fidia zao mapema kabisa. Vilevile uzio ujengwe kwa sababu kuna wanyama wanazunguka, ili kuhakikisha kwamba mambo ni motomoto Iringa. Iringa siyo ile ya wakati ule. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, vilevile nizungumzie kuhusu utafiti. Kwa kweli nchi hii haitaendelea bila kufanya tafiti mbalimbali, kwa sababu, tunavyo vituo vingi sana vya utafiti; TARIRI, COSTECH, NIMRI na NBC. Hivi vituo vina hali mbaya mno. Sasa tutaendeleaje?

Mheshimiwa Naibu Spika, tunaelekea kwenye uchumi wa viwanda, bila kuboresha mambo ya utafiti, bila kutenga pesa ya utafiki katika hivi vituo ili tafiti mbalimbali katika nchi hii ziweze kufanyika, hatutakwenda. Nchi za wenzetu zinaendelea kwa sababu wanafanya tafiti za kutosha. Tunaona tunapata pesa za kigeni, lakini wao wanalenga tunataka kufanya tafiti tulani. Nchi yetu bado hatujajipanga kuweka pesa ya kutosha kwenye utafiti. Unaona karibu 90% inaenda kwenye ya mbegu. Asilimia 90 tunaagiza mbegu kutoka nje wakati tunacho Kituo cha Utafiti cha Mbegu nzuri, nasi tumekwenda, wanashindwa tu kupata pesa. Kuna changamoto kubwa sana kwenye vituo hivi vya tafiti.

Mheshimiwa Naibu Spika, naiomba Serikali yetu kwa kweli sasa ione umuhimu mkubwa kabisa wa kuhakikisha tunatenga fedha za utafiti. Kwa tulishasema katika Mpango wa Maendeleo kwamba 1% ya bajeti tutenge kwa ajili ya tafiti mbalimbali hapa nchini. Kwa hiyo, naomba hii iwe ni lazima itengwe ili tufanye utafiti wa kutosha ili uchumi wa viwanda uende vizuri. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nielezee kitu kingine kuhusu barabara zetu za kiuchumi. Barabara za kiuchumi kwa kweli naomba zipatiwe kipaumbele cha kutosha. Kwa sababu barabara nyingi sana za Mkoa wetu wa Iringa ambazo ndiyo uchumi mkubwa; na nafikiri tunaenda kwenye viwanda na kule ndiyo kuna malighafi za kutosha, bado sasa hivi hazipitiki.

Mheshimiwa Naibu Spika, nitoe tu mfano mmoja, kwa sababu najua nitakuja kuchangia kwenye mambo ya barabara; utakuta pale Mufindi kuna Barabara ile ya Mtirili – Ifwagi – Mdabulo – Ihanu – Mpanga TAZARA mpaka Mlimba huko kwenda kule kwa Mheshimiwa Susan Kiwanga. Hii barabara ni muhimu sana, lakini hapa ninapozungumza sasa hivi ile barabara haipitiki kabisa. Malori yamekwama, wananchi hawafanyi shughuli zozote. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, ziko barabara nyingi sana za Iringa ambazo kwa kweli ni za kiuchumi kabisa ambazo hazipitiki. Naomba hizi ziangaliwe na ikiwezekana tuzijenge kwa kiwango ambacho magari yaweze kupita yasilale barabarani, maana uchumi ndiyo unazidi kuharibika.

Mheshimiwa Naibu Spika, kitu kingine ambacho nilitaka kuzungumzia pia kuhusiana na tozo katika viwanda vyetu, Mheshimiwa hizi tozo zimekuwa nyingi. Tumekuwa tukiuliza sana maswali hapa Bungeni, tozo zimekuwa nyingi mpaka wakati mwingine zinafika hata 28 kwenye viwanda vyetu. Sasa tunaelekea kwenye uchumi wa viwanda, lakini viwanda vinakufa kabla hata havijaanza kwa sababu, watu wakifikiria tozo nyingi sana karibu 28. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, katika usindikaji wa maziwa, nakipongeza sana kiwanda chetu cha ASAS pale Iringa, kinafanya kazi nzuri, kimetoa ajira nyingi sana, lakini tozo zimekuwa shida. Unakuta kwamba hata zile flavour za maziwa kila flavour inalipiwa. Sasa ifike sehemu jamani Serikali iangalie. Kwanza tusaidie viwanda vyetu vikue, kwa sababu viwanda vikikua, tukipata ajira nyingi, pato litaongezeka kwa kiasi kikubwa na hapo ndiyo tutakuta kweli kazi inakwenda vizuri zaidi. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, sasa hivi tulikuwa tumeenda kwenye ziara, kwa kweli wamempongeza sana Mheshimiwa Rais. Ziara yetu ya Kamati ya Kilimo, Mifugo na Maji, tumepata pongezi nyingi sana kwa wananchi, lakini kuna changamoto ambazo zipo kwa mfano kwenye miradi ya maji.

Mheshimiwa Naibu Spika, unakuta katika miradi ya maji kwanza vibali vya kutoa vile vifaa kwa ajili ya kufanyia kazi havitoki kwa wakati. Kwa mfano, tulienda kwenye mradi ule wa maji Arusha. Ule mradi tayari maji yameshatobolewa pale Moshi, lakini sasa ili waanze kufanya ile kazi, bado hawajapewa vibali. Mizigo iko bandarini imekaa karibu wanasema kwamba ni miezi mitatu sasa.

Mheshimiwa Naibu Spika, nasema hivi, hii miradi ni ya kwetu, Serikali ya kwetu, hebu wekeni mpango mzuri kuhakikisha kwamba vitu vikija kwa mfano labda hawa wenzetu ambao wamekata huu ukandarasi, basi vifaa vyao vitolewe haraka sana bandarini ili iweze kusaidia miradi iende kwa haraka ili gharama za kutengeneza hii miradi ziwe kwa kiasi cha chini. Tunapochelewesha hii miradi kwa ajili tu ya kuchelewesha vifaa bandarini sidhani kama inaleta picha nzuri sana. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, walisema pia vibali vya kazi vya wataalamu wao vinachelewa kutoka. Kwa hiyo, hilo nalo liangaliwe kwa haraka zaidi.

Mheshimiwa Naibu Spika, vile vile nisisahau, sisi ni walemavu watarajiwa. Nizungumzie watu wenye ulemavu. Mheshimiwa Ikupa nakupongeza sana, umefanya kazi nzuri sana, mpaka Iringa umefika, lakini kwa kweli kuna tatizo ambalo liko. Watoto wenye ulemavu wanapoenda kwenye hizi shule, zamani walikuwa wanapatiwa nauli. Sasa matokeo yake watoto wanabaki kwenye mashule hawarudi kwa wazazi wao. Wazazi wao wengi hawana uwezo.

Mheshimiwa Naibu Spika, naiomba Serikali iweke utaratibu wa kuwasaidia hawa watoto wenye ulemavu ili mara wanapofunga shule, basi warudi kwa wazazi wao. Hili ni tatizo kubwa, naomba Serikali iliangalie kwa umuhimu wake.

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba nimpongeze Kamal Steel, kwa kweli, namshukuru Mheshimiwa Ikupa, alitualika tukaenda kwenye kiwanda cha Kamal. Amekuwa akisaidia sana, ameweka kiwanda kwa ajili ya kutengeneza viungo. Kama watu hawafahamu hapa, basi Kamal anafanya hiyo kazi na kwa kweli, ametoa viungo vingi sana vya bandia; na hata Mkoa wangu wa Iringa wameguswa, kwa sababu, pale tuna karibu watu wanaohitaji kama 100. Kwa hiyo, ameshatoa.

Mheshimiwa Naibu Spika, namshukuru pia Mengi naye ametoa mchango, amewapatia mtaji watu wenye ulemavu waliopatiwa na Kamal shilingi laki mbili, mbili. Kwa hiyo, Mr. Mengi pia tunamshukuru kwa kuwasaidia watu wenye ulemavu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kweli, naomba pia nikupongeze, lakini niipongeze Tanzania yetu kwa michezo. Sasa hivi tuko mbali sana kimichezo na tupongeze hili kombe la AFCON kwamba angalau na sisi sasa tuko juu sana kimichezo. Tuendelee kusaidiana, tuendelee kushirikiana na kuhakikisha kwamba nchi yetu inapiga hatua kubwa kabisa katika michezo.

Mheshimiwa Spika, nina imani kabisa nchi hii tutaanza kutengeneza vipaji kwa watoto wetu, tutapata nchi ambayo itakuwa inatangazika kimichezo. Nafikiri kimichezo tunaweza…

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

NAIBU SPIKA: Mheshimiwa kengele ya pili imeshagonga. Naamini hutakosa kwenye mchango wa kuwachangia Yanga, maana umesisitiza watu tuchangie timu. Kwa hiyo, utaenda kuchangia Yanga. (Kicheko)

MHE. RITTA E. KABATI: Mheshimiwa Naibu Spika, ndiyo. Yanga unajua rangi zake ndiyo zitanifanya na mimi pia nichangie, lakini…

NAIBU SPIKA: Ahsante sana Mheshimiwa. (Makofi/ Kicheko)