Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Mpanda Mjini
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
2
Ministries
nil
MHE. SEBASTIAN S. KAPUFI: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru. Kwanza, nianze kwa kuunga mkono hoja. Nimshukuru Mheshimiwa Waziri Mkuu na Mawaziri wote walioko katika ofisi hii, kitabu kimesheheni mambo mbalimbali na nitajikita katika maeneo machache, eneo la afya pia madini. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, uhakika wa sera zisizoyumba, amani na utulivu, vitu hivi vikiwepo vinatengeneza ustawi wa uchumi. Kama hiyo haitoshi doplomasia ya kiuchumi ndiyo gari tunaloweza kusafiria na likatufikisha katika uchumi wa kati na uchumi wa viwanda. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kwenye kitabu cha hotuba ya Waziri Mkuu katika sekta za uzalishaji kwa maana ya ukurasa wa 27, eneo la utalii ambao ni ukurasa wa 32, eneo linalogusia uendelezaji wa utalii Ukanda wa Kusini kwa maana ya REGROW nimeona linazungumziwa suala zima la uendelezaji wa viwanja vya ndege, ni jambo jema na lenye afya. Kwa kuwa Mkoa wangu wa Katavi uko katika Ukanda huo wa Kusini tunao Uwanja mzuri wa Ndege wa Katavi, bila kuufanya uwanja ule ukafanya kazi habari hii ya kuendeleza ukanda ule kiutalii itakuwa pia haijakaa vizuri. Nendelea kumkumbusha Waziri Mkuu Uwanja wa Katavi, Uwanja wa Mpanda ni mzuri, ni changamoto katika kuibua suala la utalii katika ukanda ule. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kabla sijaenda kwenye eneo la madini natamani kwanza nigusie masuala yanayogusa afya, kwa maana ya kitabu cha Waziri Mkuu tutaikuta ukurasa wa 56, 57, 58, najielekeza katika suala la hospitali. Nafarijika sana nikija katika eneo hilo kwa maana ya Hospitali ya Taifa ya Muhimbili, Hospitali ya Benjamin Mkapa na Hospitali ya Mloganzila.
Mheshimiwa Naibu Spika, eneo hili likitumika vizuri na kwa jinsi ambavyo nchi imejiwekeza kwenye kuimarisha sekta hiyo ya afya, tunakuja kwenye kitu kinachoitwa utalii wa tiba. Tukifanya vizuri, tukiendelea kuimarisha hospitali zetu hizo watu kutoka nchi za jirani iwe ni Malawi, Zambia au Kenya kama ambavyo Watanzania tumekuwa tukitoka hapa tukienda India, tutumie nafasi hii ya kuimarika kwa hospitali zetu kwenda kwenye eneo la utalii wa tiba. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa misingi hiyo siwezi nikashindwa kuzitaja hospitali zote za rufaa. Najua nchi kama nchi imejipanga vizuri na nafahamu mara ya mwisho tuna zaidi ya hospitali zile 67 kwa maana ya Halmashauri mbalimbali lakini kuna hospitali mbalimbali za rufaa ambapo nchi imejipanga kwenda kuzijenga, hospitali hizo ni pamoja na Hospitali ya Mkoa wa Katavi. Rai yangu ni moja, kusema ahsante ni namna ya kuomba tena. Najua tumetengewa takribani shilingi bilioni 1 lakini kwa maana ya bajeti ya zaidi ya shilingi bilioni 9, naomba sana Serikali yangu sikivu uwezekano wowote wa kuona namna ya kupatikana kwa fedha ili badala ya kuwa na muda mrefu wa kujenga hospitali hizo tuwe na muda mfupi na tukamilishe zoezi hilo. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, nikilisema hilo ninamaanisha nini? Niliwahi kusema katika Bunge lako hili Tukufu kwa sisi ambao tuko Mikoa hiyo kama Katavi, kumtoa mgonjwa kutoka Katavi kumpeleka Bugando au Dar es Salaam umbali huu unaweza ukamalizwa kwa kuwa na hospitali ya rufaa pale pale Katavi. Ndiyo maana naendelea kusisitiza ujenzi wa hospitali hizo za rufaa. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, eneo la madini na kama ilivyo ada mimi pia ni mchimbaji mdogomdogo wa madini, naomba hilo lifahamike mbele ya umma huu. Rai yangu katika eneo la madini, tumekuwa tukiongelea habari ya ajira. Nitoe ufafanuzi mdogo, eneo la madini katika muda mfupi na ukizunguka nchi hii ukaangalia eneo la machimbo ya madini ndiko ambako ni maeneo yamekusanya watu wengi. Kukiwa na kitu wanaita gold rush kwa wakati mmoja usishangae kukuta una watu hata 5,000 na zaidi ya hapo. Kwa hiyo, unaweza ukaona jinsi ambavyo eneo la madini limesheheni watu wengi na linatoa nafasi kubwa ya ajira. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, nafahamu kazi nzuri ambayo inafanywa na Rais wetu, najua tarehe 22 Janauri, 2019 alihamasisha na Wizara ikawakusanya wadau wa madini, kazi aliyoifanya Mheshimiwa Rais ni kazi nzuri. Rai yangu naitoa upande wa Wizara ya Madini, wakati tukiendelea kuboresha, unapomboresha mchimbaji mdogo hatima yake atatoka hapo atakuwa mchimbaji wa kati na baadaye anaweza kuwa mchimbaji mkubwa.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, tunapomlenga huyu mchimbaji mdogo hatutarajii abaki kuwa mchimbaji mdogo, kesho atakuwa. Sasa rai yangu ni nini? Kama nchi tuendelee kuandaa watu hawa kwa maana ya elimu. Leo wachimbaji wengi wadogo ikifika sehemu anatakiwa aingie ubia labda na watu wa kutoka nchi za nje, je, kama nchi tumewaandaa vipi watu hawa kwa maana ya elimu ya mikataba, tunafahamu vipi watu hawa katika maeneo ambayo wanayo? (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kuna kitu kinaitwa reserve, labda kwa kupitia GST wanaendeleaje kuwasaidia wachimbaji hawa wakajua hifadhi ya madini waliyonayo kwamba ile inaweza ikawa ni jambo jema la yeye kuingia mikataba? Anapoweza kuingia mkataba asilimia ambazo anaweza akazipata kutokana na eneo lake na hifadhi aliyonayo ya madini pale ni silaha tosha au ni ngao tosha ya kumpa kibali cha kuingia mkataba. Kama watu hawafahamu elimu ya mikataba, wanaishia kudhulumiwa. Naomba elimu hiyo ya mikataba iendelee kutolewa kwa wachimbaji wetu mbalimbali.
(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)