Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 - Ofisi ya Waziri Mkuu

Hon. Maulid Said Abdallah Mtulia

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Kinondoni

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 - Ofisi ya Waziri Mkuu

MHE. MAULID S. MTULIA: Mheshimiwa Naibu Spika, awali ya yote, nianze kwa kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa kunijaalia uzima na kusimama kwenye Bunge lako Tukufu. Pili, nitoe shukrani zangu za dhati kabisa kwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Dkt. John Pombe Joseph Magufuli kwa namna anavyoliendesha Taifa letu kwa weledi mkubwa sana. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, hotuba ya Waziri Mkuu nimeisikiliza na kwa kweli ilikuwa hotuba nzuri yenye mwelekeo na yenye matumaini. Nianze na ukurasa wa 66 hasa kwa kaka yangu pale Mheshimiwa Mavunde kwa maana nazungumzia vijana na ajira. Sisi watu wa Kinondoni tunakupongeza sana, lakini katika kipengele ambacho amenivutia sana ni kile cha kuhakikisha anatoa ajira kwa vijana; vijana wanapata ajira na mafunzo na hasa mafunzo ya kilimo cha kitalu nyumba. Nasi Kinondoni kwa maana ya Manispaa tumejenga kituo Mabwepande, vijana wanakwenda kusoma.

Mheshimiwa Naibu Spika, tuna jambo moja tu naomba Mheshimiwa Waziri atusaidie pale, atuletee angalau madarasa mawili kwa ajili ya vijana wanaotoka mbali waje kukaa pale na inaweza ikasaidia kwa watu wa Temeke, Ubungo, Ilala na Kigamboni. Vijana wote wa Dar es Salaam watakuja kujifunza pale kwa sababu kutakuwa na mabweni kwa ajili ya wasichana na wavulana. Akitufanyia hilo, kaka yangu Mheshimiwa Mavunde atakuwa ametusaidia sisi pamoja na Jiji la Dar es Salaam na kwa ujumla wake atakuwa ameisaidia sana nchi.

Mheshimiwa Naibu Spika, katika Ofisi ya Waziri Mkuu kuna walemavu. Kwa kweli natamani sana kama Serikali ikija na ruzuku kwa ajili ya walemavu kwa sababu maisha ni mapambano. Kama sisi wengine tunapambana tukiwa tupo timilifu, wenzetu wanaopambana na viungo pungufu maana yake uwanja siyo fair. Kama tumetoa mkopo kwa ajili ya wanawake na vijana ambao ni wazima, haiwezekani na walemavu tukatoa mkopo kwa condition hiyo hiyo, kwa sababu hawa ni watu wenye upungufu. Kwa upungufu huu lazima tutafute namna ya ku-subsidize.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, natamani sana Serikali ije na ruzuku kwa ajili ya walemavu, ije na vifaa kwa ajili ya walemavu wa kutembea kama vile baiskeli, magongo, vifaa vya kuongeza usikivu na kila namna. Lazima walemavu hao tuonyeshe kama jamii tunawajali na tunajua kwamba wenzetu wapo kwenye mapambano haya wakiwa na upungufu. Uwanja uko fair.

Mheshimiwa Naibu Spika, niende kwenye uwekezaji. Kuna uwekezaji wa watu, kuna uwekezaji kwa maana ya ndani na uwekezaji wa nje. Nina hamu kubwa sana tuzungumzie uwekezaji wetu wa ndani. Kwanza naipongeza Serikali yangu kwa kuhakikisha imekuja na miradi mkakati mikubwa, tukianza na mradi wa standard gauge. Huu mradi ni mradi mkubwa na mtu yeyote anayeubeza mradi huu kwa kweli tutakosa kumwelewa. Hata leo mradi unakwenda una miaka; wewe mpaka leo unakuja kuubeza mradi huu maana yake utakuwa unajipotezea muda. Huu mradi ni mzuri. Vile vile tuna mradi wetu wa umeme, ACT na tuna miradi mingi. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, katika miradi hii, tuje na mkakati wa kuona ni namna gani miradi hii inaweza kuwajenga Watanzania? Mfano, tunajenga reli kutoka Dar es Salaam – Mwanza – Kigoma – Rwanda na Burundi wameomba wanataka nao tufike. Haiwezekani tukajenga kwa kutumia Kampuni ya Kituruki tu, lazima tuwe na ajenda. Baada ya Waturuki kuondoka, transformation of knowledge inapatikana? Haiwezekani tena wakiwa Congo wanataka kujenga reli kama ile, wakamtafute tena Mturuki, wanatakiwa waje Tanzania wawakute Watanzania wapo tayari kwa ajili ya kujenga reli.

Mheshimiwa Naibu Spika, mfano kama huu uende kwenye viwanja vya ndege. Tuna mpango wa kujenga viwanja vya ndege vya kanda vingi kweli. Viwanda vya Songwe, Dodoma, Iringa, Mtwara na Lindi. Tuna viwanja vingi tunajenga. Hivi viwanja tunavyovijenga tutakwenda na viwanja vya mikoa, haiwezekani mpaka leo hatuna kampuni hata moja ambayo tunailea kwamba wakati viwanja hivi tunajenga kwa kutumia Wakandarasi wa nje, tukimaliza tukianza viwanja vyetu vya mikoa Watanzania wawe wana uwezo wa kujenga hivi viwanja wao wenyewe na hiyo ndiyo transformation of knowledge. Hili hatuwezi tukafanyiwa na mtu, lazima tuwe na mkakati nalo.

Mheshimiwa Naibu Spika, leo tunapeleka umeme vijijini, makampuni tunayotumia mengi katika vijiji vingi; hivi kweli tukimaliza mradi wa umeme vijijini Watanzania washindwe kwenda kufanya oparesheni za miradi ya umeme kwa ajili ya nchi ya Burundi, Congo na nchi nyingine? Tuendelee tu kuwa sisi kazi yetu ni kutumika!

Mheshimiwa Naibu Spika, mtazamo wangu kwa miradi yote mikubwa tunayoweka fedha nyingi, lazima tuje na mpango wa kuhakikisha elimu inabaki ili Watanzania waende mbele.

Mheshimiwa Naibu Spika, jambo lingine, sisi tunajenga reli, lakini tuna mradi wetu wa kimkakati wa Mchuchuma na Liganga. Ni mradi wa muda mrefu. Mchuchuma na Liganga umesimama. Ukiangalia, kuna changamoto. Changamoto ya kwanza, mbia aliyekuja kampuni ile ya Kichina ambayo yuko na NDC hakuja na capital ya kutosha. Mradi unataka capital ya shilingi bilioni tatu yeye amesema anaweza akaja na capital ya dola milioni 600. Kwa maana hiyo, anataka atumie mradi wetu kama collateral kwa kukopa hela benki. Huo ukawa mgogoro wa kwanza.

Mheshimiwa Naibu Spika, mgogoro wa pili, umeme utakaozalishwa kutoka pale Mchuchuma, Megawatt 600, 250 itumike kwenye kiwanda, 300 iingie kwenye grid ya Taifa; na ile inayoingia kwenye grid ya Taifa, anataka Megawatt moja atuuzie kwa senti 12 mpaka senti 15 ambayo ni ghali. Umeme wa gesi tunanunua kwa senti 6 na TANESCO wanauza kwa senti 11. Ukiangalia hapo unaona mgogoro mwingine.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa migogoro hii yote, ndiyo tusitoke? Kwa sababu tukiweza kutengeneza kiwanda cha Liganga, tukatoa chuma cha pua tungeweza kutumia kujenga kama mataruma. Vilevile tunapokwenda kwenye ulimwengu wa Tanzania ya Viwanda, visiwe viwanda vya juice tu, viwe viwanda vya chuma.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, mawazo yangu ni kwamba lazima Serikali ikae na hawa wabia wetu na NDC tutatue huu mgogoro, kwa sababu hiki kiwanda kwetu kina umuhimu mkubwa sana. Chini ya kile chuma kumechanganyika na madini muhimu sana. Kuna madini yanaitwa vanadium na titanium; ni madini muhimu na ghali kuliko hicho chuma, lakini inapatikana tu baada ya kuchimba chuma.

Mheshimiwa Naibu Spika, hata ile reli ya kusini ambayo tunataka kuijenga Mtwara mpaka kwenda Songwe ni reli ambayo inategemea mzigo huu mkubwa utakaotoka Mchuchuma na Liganga. Kwa hiyo, tusipopatana na tukaja na suluhisho, maana yake ile reli ya kusini itabaki kuwa ni ndoto.

Mheshimiwa Naibu Spika, imefika mahali Serikali sasa, nimeona kwenye mpango tumetenga fedha kwa ajili ya fidia, lakini kulipa fidia peke yake haitoshi. Namwombe dada yangu Mheshimiwa Angellah, namuamini sana, alichukue hili kama ni jambo la msingi ambalo anaweza akalisaidia Taifa, akatusaidia na sisi pia. Kwa maana mradi huu ukifanikiwa utakuwa ni mradi mkakati wa kuhakikisha kweli tunakwenda kwenye Tanzania ya viwanda na siyo viwanda vya juice na maji tu.

Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya kusema hayo, nakushukuru sana ahsante. (Makofi)