Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 - Ofisi ya Waziri Mkuu

Hon. Rashid Abdallah Shangazi

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Mlalo

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 - Ofisi ya Waziri Mkuu

MHE. RASHID A. SHANGAZI: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana kwa nafasi hii, nami niweze kushiriki katika hoja iliyopo katika Bunge lako tukufu.

Mheshimiwa Naibu Spika, nimefarijika sana kuona Mheshimiwa Waziri wa Fedha yupo hapa, lakini Mheshimiwa Waziri wa Uwekezaji yupo pale kwa sababu mambo ambayo nakusudia kuyazungumza yanagusa sana katika maeneo yao.

Mheshimiwa Naibu Spika, tunapozungumza uchumi wa viwanda kwa maana ya kulipeleka taifa kwenye uchumi wa kati ni lazima tuwe na models ambazo zinatupeleka huko. Hatuwezi tu kuwa na model ya viwanda ambavyo hatuelewi ni viwanda vya namna gani vitatupeleka huko. Kwa maoni yangu nadhani kwa kuwa nchi hii asilimia zaidi ya 70, 75 ni wakulima basi model nzuri itakuwa ni ya viwanda ambavyo vinahusianisha au vinajifungamanisha na kilimo. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, hapa ulizuka mjadala wa kuhusu matumizi ya ndege, lakini inawezekana labda tu ni kwa sababu vitu hivi sisi kama Watanzania tumechelewa kuvitumia na ndiyo maana wakati mwingine hata tukiona mizigo inapanda ndege tunaona kama ni israafu, lakini nataka nikwambie kwamba sehemu mojawapo itakayosaidia kukuza Sekta ya Kilimo ni kuwepo kwa ndege ambazo zinabeba mizigo, hasa mazao haya ambayo ni perishable. Tunapozungumza mazao kama maparachichi, mazao ya kilimo ya matunda, mbogamboga, green beans, French beans, broccoli, coriander, lakini pia na mazao ya maua, haya yanahitaji ndege ili yaweze kufika kwenye masoko kwa haraka sana.

Mheshimiwa Naibu Spika, sasa tatizo kubwa katika nchi yetu ni kwamba hatuna ndege nyingi za mizigo zinazotua katika viwanja vyetu. Sio katika Uwanja wa Ndege wa Dar es Salaam, sio Kilimanjaro wala sio kule Songwe, kidogo kwa watu wa Kaskazini wanatumia Uwanja wa Ndege wa Nairobi kwa kupeleka maua na bidhaa hizi za matunda na mbogamboga.

Mheshimiwa Naibu Spika, sasa niiombe sana Wizara ya Fedha iangalie hapa kwa sababu kuna tatizo moja. Kwanza ni airport charges zetu ziko juu, lakini pia landing fee ya kutua katika viwanja vyetu ziko juu sana. Sambamba na hilo, wakiweza kuangalia pia mafuta ya ndege kwamba angalau yasiwe na tozo nyingi, najua yako zero lakini ingekwenda mbali zaidi kwamba angalau tuyapate kwa bei ya nafuu sana ili yavutie ndege ambazo ni za mizigo ziweze kutua katika viwanja vyetu.

Mheshimiwa Naibu Spika, juzi hapa nilimwona Mheshimiwa Waziri wa Fedha yuko kule Rungwe, nadhani alikuwa na Waziri wa Uwekezaji, wakiwa wanaangalia uwezekano wa kusafirisha maparachichi kupitia Uwanja wa Songwe. Sasa kama tutakuwa na ndege za mizigo zinazoweza kutua katika viwanja vyetu hivi maana yake hii itaongeza thamani ya uzalishaji kwa wakulima wetu. Kwa hiyo hili naomba tulitazame sana.

Mheshimiwa Naibu Spika, la pili katika eneo hilohilo la viwanda, hasa vinavyofungamanishwa na kilimo, ni suala zima la vifungashio. Tanzania bado tuna tatizo la vifungashio, ndiyo maana unakuta maparachichi yanayolimwa Njombe, Iringa na kwingineko yanapelekwa Nairobi yakifika kule yanafungwa katika vifungashio ambavyo ni bora na yanapelekwa kwenye masoko ya Ulaya na Marekani ambapo wanauza kwa bei kubwa zaidi.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, niombe sana Wizara hii iangalie eneo hili, kwamba tutafute wawekezaji ambao watawekeza katika viwanda vya vifungashio ili mazao yetu yanapotoka moja kwa moja kutoka Tanzania yawe yako katika ule ubora ambao unaweza kuyafanya yakashindana kimataifa. Unaweza ukaona mfano maparachichi ambayo tunauziwa hapa Tanzania kwa shilingi labda 1,400, huko kwenye masoko ya dunia inafika mpaka dola kumi, kwa hiyo utaona kwamba ni kiasi gani cha pesa ambacho tunapoteza kwa sababu tu hatuyaandai vizuri wala hatuyawekei mpango madhubuti wa ku-process katika ubora ambao unatakiwa.

Mheshimiwa Naibu Spika, suala lingine linalojifungamanisha pia katika kilimo ni suala zima la majokofu ama hizi cold boxes za kusafirishia haya mazao. Mazao ya mbogamboga, matunda, yanahitaji kupata ubaridi wa kutosha kutoka kule kwenye mashamba kwenda katika hivyo viwanja tunavyozungumza au kwenda katika masoko. Katika eneo hili unakuta kwamba wakulima hawawezi kuyasafirisha yakiwa katika hali ya ubaridi. Kwa hiyo niiombe sana Wizara ya Fedha wakati tunatoa misamaha kwenye vifaa vingine vinavyosaidia kwenye uwekezaji katika kilimo kama matrekta na pembejeo nyingine, hebu tuangalie na hili suala la cooler boxes na cold rooms ambazo zinasaidia sana wakati wa usafirishaji wa haya mazao.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa wale ambao wamepata bahati ya kuwa na miradi ile ya MIVARF katika maeneo yao watakuwa ni mashahidi kwamba MIVARF wameweza kujenga cold rooms ambazo zinaweza kubeba mazao hata kwa tani 15 mpaka 20, lakini tatizo lipo kwenye kuyatoa kule kwenye vijiji kuyaleta kwenye vile vituo ambavyo ni post harvest centers, pale lazima wananchi wetu waweze kupata incentive kwenye kodi ili waweze kuwa na hivi vifaa na waweze kuongeza uzalishaji.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwenye kilimo bado tuna uwezo sasa wa kuhakikisha kwamba tunapata viwanda ambavyo vinakwenda kuongeza thamani kwa maana ya kupata pembejeo na madawa pamoja na viuadudu katika mazingira yetu hapahapa, lakini pia sambamba na uzalishaji wa mbegu. Tatizo la mbegu limekuwa ni tatizo kubwa sana kwa sababu mbegu zetu nyingi zinatafitiwa kutoka nje. Kwa hiyo niombe sana Serikali iongeze pesa katika vituo vyetu vya utafiti ili kutokana na mabadiliko haya ya tabianchi ambayo yameendelea kuikumba nchi yetu wananchi waendelee kubadilisha aina ya mazao kwa sababu bado mpaka sasa hivi wananchi wengi wanapanda mazao mengi kwa mazoea lakini kiuhalisia kwa kweli hayana ubora ule ambao unaweza ukashindana katika soko.

Mheshimiwa Naibu Spika, eneo lingine ambalo nataka kulizungumzia ni la madawa; juzi Kamati ya PAC tulitembelea Bohari Kuu ya Madawa (MSD) na tukakutana na wenzetu wa Nchi za Kusini mwa Afrika (SADC), karibu nchi 16 walikuja pale kufunga mkataba na MSD ili iweze kuagiza madawa kwa niaba ya hizo nchi 16 na kufanya deliveries.

Hata hivyo, changamoto kubwa ni kwamba hapa ndani uwezo wa viwanda vya ndani katika soko la madawa ni asilimia nne peke yake na bado napo kuna tatizo la kwamba hatuna viwanda vya kutosha vya madawa, hata dripu tunaagiza nadhani kutoka Uganda.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo nimwombe sana Mheshimiwa Waziri mwenye dhamana hii ya uwekezaji kwamba sasa tujaribu kupata incentive nzuri kwa ajili ya kuhamasisha viwanda vya madawa vijengwe hapa nchini ili tuweze sasa kupata hili soko la Kusini mwa Afrika. Kama nchi 16 leo zinachukua madawa kutoka Bohari Kuu ya Madawa maana yake ni kwamba hayo madawa yangekuwa yanazalishwa hapa nchini moja kwa moja hii ingekuwa ni faida kwetu, lakini leo MSD anageuka tu kama agent wa kuagiza kwa makampuni mengine ya nje.

Mheshimiwa Naibu Spika, la mwisho kabisa ni kwa Bandari ya Dar es Salaam; bado Bandari yetu na Mamlaka ya Mapato Tanzania sio rafiki sana kwa uwekezaji, kuna mambo mengi ambayo yanafanyika pale kila siku tunarudi nyuma, kila siku wanaanzisha mambo mapya. Kwa hiyo tunapozungumza suala zima la uwekezaji ni lazima Serikali nzima iwe inazungumza, Wizara zote zizungumze na kuwe na connection kwamba mizigo inapotoka nje inapofika katika bandari zetu ichukue muda mfupi na iweze kwenda kule ambako inakusudiwa. Kama tutakuwa tuna bandari ambayo inachelewesha mizigo, basi hata ile dhana nzima ya kwamba nchi yetu inavutia wawekezaji itakuwa haifanyi kazi.

Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru sana kwa muda wako. (Makofi)