Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 - Ofisi ya Waziri Mkuu

Hon. Sabreena Hamza Sungura

Sex

Female

Party

CHADEMA

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 - Ofisi ya Waziri Mkuu

MHE. SABREENA H. SUNGURA: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru kwa kunipa nafasi ya kuweza kuchangia katika bajeti iliyopo mbele yetu. Kwanza kabisa, napenda kuchukua fursa hii kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa kunipa uhai na afya bora.

Mheshimiwa Naibu Spika, pia napenda kuchukua fursa hii kuwapa pole viongozi wangu tukiongozwa na Kiongozi wa Upinzani Bungeni kwa kufungwa takribani miezi minne wakiwa mahabusu na kukosa dhamana hali iliyopelekea kwa kweli Kambi yetu kuyumba na wanachama kuhuzunika takribani nchi nzima kwa kitendo kama hicho. Nawapa pole sana nawaombea Mwenyezi Mungu aweze kuwapa subira. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, napenda pia kuchukua fursa hii kukishukuru Kiti chako, nikianza na Mheshimiwa Spika lakini na wewe mwenyewe na Mawaziri na Wabunge mbalimbali ambao kwa namna moja au nyingine walipata kunijulia hali pale nilipopata hitilafu ya kiafya. Nawashukuru sana na Mwenyezi Mungu awabariki. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba sasa nijielekeze kwenye mchango wangu. Wananchi wa Mkoa wa Kigoma wamenituma na wanahoji kwamba katika Mpango wa Maendeleo kulikuwa na suala zima la ununuzi wa meli ya uvuvi katika Ziwa Tanganyika lakini wameshangaa miaka inaenda meli hii bado haijaweza kununuliwa wakati ni kitu ambacho kipo kwenye mpango. Kwa hiyo, wanaomba kwenye bajeti ya mwaka huu basi meli hii iweze kupatikana ili sasa wananchi waweze kupata fursa mbalimbali kutokana na suala zima la uvuvi. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, suala la pili ambalo napenda kuzungumzia na napenda kutoa shukrani kwani kwenye ziara ya Waziri Mkuu alivyokuja Kigoma kwa kuendeleza zao letu la mchikichi na kuanzisha Kituo cha Utafiti katika Mji Mdogo pale Kihinga na kuwezesha kupandikiza miti takribani 4,000 ikiwa na lengo la kwenda mpaka miche 5,000,00. Tunaomba Serikali isiishie hapo iweze kutusaidia kutafuta wawekezaji ili waweze kuwekeza hususani katika Bonde la Mto Luiche kwa kuwa watu wengi sana wana nia ya kuendeleza kilimo hicho lakini issue ni masuala ya kifedha. Pia watusaidie kwa Benki yetu ya Kilimo iwawezeshe wananchi kwa masharti nafuu kabisa waweze kupata mikopo na waweze kuitumia fursa hii adhimu ambayo imeletwa katika mkoa wetu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, pia tungeomba wawekezaji wa zao la mhogo. Nimesikia China ni wanunuzi wazuri sana wa zao mihogo na Mkoa wa Kigoma tumekuwa tukilima sana zao hili. Tunaomba Serikali itusaidie na sisi kupata wawekezaji na wanunuzi kwenye zao hili ili angalau wananchi wetu waweze kuendeleza kilimo hiki ambacho kitakuja kuwa na tija kwa mkoa na kwa taifa kwa jumla. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, wafanyabiashara wa Mkoa wa Kigoma na Tanzania kwa ujumla wamekuwa na malalamiko mengi kuhusiana na masuala mazima ya biashara. Wanasema biashara imekuwa na mlolongo mrefu. Ili mtu aweze kufungua biashara yake na ku-establish na ikakaa kwenye mstari mlolongo wa vitu vingi sana vinahitajika. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa mfano, mtu anataka kutoa ajira kwa vijana, anataka kufungua ofisi, anahitajika alipe Pay As You Earn, Income Tax, OSHA, kwenye Manispaa katika Halmashauri zetu, Workers Compensation Fund, bado kuna mifuko mingi, NSSF na kadhalika atoe michango na Withholding Tax. Kwa hiyo, kumekuwa kuna mlolongo wa vitu vingi, mambo ya fire na kadhalika, ambapo ni mtu anajitahidi kutengeneza ajira mambo yote haya anatakiwa alipie. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, suala hili kwa namna moja ama nyingine ni kikwazo kwa wafanyabiashara wetu. Kwa wale wanaotoka nje pia, wanatakiwa wa-obtain Certificate of Incentive kupitia pale TIC, tumekuwa na mlolongo wa vitu vingi. Nashauri Watanzania wa kawaida na wenyewe wasaidiwe, kama ilivyowekwa One Stop Center basi na Watanzania wa kawaida wanapotaka kuanzisha biashara zao mazingira yawe rahisi mtu akienda sehemu moja aweze kupata vitu vyote kwa wakati na aweze kufanya biashara zake ili aweze kupata kitu ambacho kitasaidia Taifa na yeye mwenyewe na familia yake kwa ujumla. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, napenda kuzungumzia suala zima la dhamana lakini pia na mlundikano wa mahabusu katika magereza yetu. Tumekuwa na mlundikano wa mahabusu wengi kwenye magereza zetu bila sababu za msingi. Police bail imekuwa ni shida katika nchi hii na kumekuwa kuna mchezo watu hawapewi dhamana kwa makusudi tu wakisingizia kwamba haya ni maagizo kutoka juu lakini wakati mwingine hakuna maagizo yoyote kutoka juu, huko juu ni wapi, ni mbinguni? (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, urasimu tu unafanyika huku chini mtu anaamua kusema kwamba ni maagizo kutoka juu. Mimi siamini kama kuna sehemu yoyote ambayo ni juu kuna watu wapo kwa ajili ya kuwakandamiza watu wengine. Nashauri Serikali iweze kuingilia kati ili haki za dhamana ziweze kupatikana na mahabusu waweze kupungua katika magereza zetu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, unaweza kushangaa mtu kama Kiongozi wa Upinzani Bungeni ni Mbunge ana dhamana ya wananchi, ana familia, ana mali, amewekeza katika nchi hii, unamnyima dhamana mtu huyu akikimbia atakwenda wapi? Kwa hiyo, tuwawezeshe watu wetu basi ili Watanzania angalau na wenyewe wawe miongoni mwa watu wanaoishi katika nchi za watu wenye furaha. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, suala lingine ni kuhusu Wakuu wetu wa Mikoa na Wakuu wa Wilaya, hii amri ya kuwafunga watu saa 24 mpaka 48 ni mbaya na inaingilia mamlaka ya vyombo vingine ambavyo vimewekwa kwa mujibu wa Katiba. Unaweza kukuta baadhi ya maeneo Daktari amefanya tu jambo la kawaida ambalo lingeweza kuzungumzwa ama hatua zikachukuliwa kwa mujibu wa sheria lakini unakuta kosa limefanyika na Mkuu wa Wilaya au Mkuu wa Mkoa anatoa amri ya kumfunga Daktari ndani saa 48 lakini kumbe kule theater kulikuwa na wagonjwa hata 5, 6, 7, 8 ambao wanatakiwa wafanyiwe upasuaji. Kwa hiyo, unakuta ni administrative decision ndogo imefanyika lakini ukienda kuangalia huko ndani zaidi inaathiri watu wengi sana. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, Mzee wangu Mheshimiwa Mkuchika hapa alisema, Serikali haiwezi kuwa kama nyumba ya kambale kila mtu awe na sharubu, kwamba kila mtu awe na haki ya kamata, funga, fanya hivi fanya hivi. Kama tumepeana maeneo ya kusimamia, wewe simamia haki, simamia kufungwa, simamia ulinzi, simamia hiki; basi kila mtu afanye kazi ambayo inamhusu. Kwa kweli hili suala la kuwapa mamlaka wenzetu kufunga watu saa 24 - 48, nafikiri siyo sahihi na ikiwezekana Serikali iweze kuleta sheria hapa tufanye amendment ili kuondoa hiki kipengele kwa sababu wananchi wamekuwa wakikilamikia sana. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, suala lingine ambalo napenda kuchangia ni posho za Madiwani. Halmashauri yangu ya Buhigwe wamekuwa wakilalamika takribani zaidi ya mwaka hawalipwi posho zao. Sisi hapa ni Wabunge hata tukifanya semina tu mtu akakosa kulipwa nafsi inahaha kama vile sijui amekosa kitu gani katika ulimwengu. Sasa tuwaangalie wenzetu hawa ambao mtu anafanya kazi miezi sita, mwaka mzima, ni Diwani na hawana shughuli za maana za kufanya huko lakini wanakosa hela ndogo ambayo ingewasaidia. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, mimi sishangai hii hama hama ya watu kutoka chama kimoja kwenda chama kingine ni kwa sababu ya ukata. Hakuna shujaa wa njaa, mtu yeyote akipata njaa ikamzidia lazima atasalimu amri. Kwa hiyo, unaweza kukuta kuna wimbi la watu kuhama kumbe njaa na yenyewe imekuwa ni sababu. (Makofi/Kicheko)

Mheshimiwa Naibu Spika, nashauri Serikali iweze kuwasaidia basi Madiwani wetu ambao sehemu mbalimbali nchini wanadai waweze kupatiwa…

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

T A A R I F A

NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. MWITA M. WAITARA): Mheshimiwa Naibu Spika, taarifa.

NAIBU SPIKA: Mheshimiwa Waitara, muda wake ulikuwa umeisha tayari, utapata fursa ya kujibu. (Makofi/ Kicheko)

MHE. SABREENA H. SUNGURA: Mheshimiwa Naibu Spika...

NAIBU SPIKA: Mheshimiwa Sabreena, muda wako ulikuwa umekwisha, kengele ilishagonga, kwa hiyo, umeshamaliza muda wako. (Makofi)