Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 - Ofisi ya Waziri Mkuu

Hon. Asha Abdullah Juma

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

2

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 - Ofisi ya Waziri Mkuu

MHE. ASHA ABDULLAH JUMA: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru sana kwa kunipa nafasi hii. Naomba nianze na kumshukuru Mwenyezi Mungu ambaye amenipa uwezo na nguvu za kuweza kusimama katika Bunge hili leo, na kuweza kuchangia Hotuba hii ya Bajeti.

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba sana kutoa pongezi za dhati kwa Mheshimiwa Waziri Mkuu, Mheshimiwa Jenista, Mheshimiwa Antony Mavunde, Mheshimiwa Stella, Katibu Mkuu na Watendaji wote wanaoshirikiana katika ofisi hii ya Waziri Mkuu, kwa jinsi walivyoiandaa Bajeti hii na jinsi walivyokuwa wanafanya kazi zao. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, pia naanza kwa kuunga mkono hoja hii ya bajeti. Napenda kutumia nafasi hii katika Bunge lako hili Tukufu kuandikisha masikitiko yangu ya moyoni na ya dhati kabisa kuhusiana na kwamba, ninavyofahamu hili Bunge ni sehemu ya mhimili mkubwa sana na muhimu sana katika ujenzi wa nchi yetu. Ni mahali pa heshima, tunapotakiwa tufanye kazi zetu kwa taratibu na kwa mujibu wa kanuni na sheria zilizopo.

Mheshimiwa Naibu Spika, jambo la kusikitisha sana, kuna Mheshimiwa aliamua kwa kupitia kwenye Bunge hili kwa kinywa kipana kabisa kusema kwamba Rais analalamika lalamika. Nasikitika sana kwamba Mbunge huyu alivyofanya siyo sawa. Mheshimiwa Rais halalamiki, ameapa kusimamia maendeleo na ustawi wa nchi hii kwa kiapo. Kwa hiyo, ni kazi yake kukosoa, kukemea, kuelekeza na kufuatilia. Ndiyo maana unaona mambo yamechukua sura hii yaliyochukua. Sasa napenda jambo hilo lisije likajirudia hapa kusema kiongozi wetu mkubwa, Amiri Jeshi kwamba yeye kazi yake ni kulalamika. Hiyo siyo kazi yake.

Mheshimiwa Naibu Spika, vilevile namwomba sana Rais wetu Mheshimiwa Dkt. Magufuli azidishe na aendelee kuwashughulikia wezi, wabadhirifu, wala rushwa na wale wote wanaokwenda kinyume na maagizo ya maadili ya maelekezo ya Chama chetu na misingi yetu. Chama chetu kwa wale wasiokijua ni Chama cha Mapinduzi, ndiyo ninachokikusudia, ninachokisemea hapa.

Mheshimiwa Naibu Spika, kazi zinazofanyika kwa usimamizi wa Rais wetu huyu zinatambuliwa hata nje ya mipaka yetu. Sasa kama huku ndani kuna mtu hatambui, huyu ndio anapanda mgomba changaraweni hauwezi ukamea. Tabia na dhamira inayooneshwa baadhi ya wenzetu humu kwa lengo la kutoka walikotoka kwamba nia ya kuivuruga Serikali na kuitifua humu sio mahali pake, kama wanataka kuitifua waende wakatifue malundo ya mchanga huko nje na ndio maana Spika juzi aliwaona akawaambia, wakafanye mambo ya huko nje Bunge. Nipende kusisitiza kwamba tukitunze chombo chetu hiki Bunge kama inavyostahili. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, sasa nijielekeze kwenye mchango na napenda kuchangia kwenye Tume ya Uchaguzi. Tume ipo imara na imepangika vizuri na kama mlivyoona kwenye hotuba hapo, imefanya kazi zake kwa vizuri na imeweza kuongeza vituo na kuboresha madaftari ya kupiga kura, kwa hiyo suala kusimamia demokrasia ya uchaguzi limekaa vizuri. Tumeona hapo kuna ongezeko la vituo 27 kwa upande wa Zanzibar, jambo ambalo ni zuri na nahakikisha kwamba Tume yetu hii pia kwa upande wa Zanzibar iko vizuri vile vile hakuna tatizo na demokrasia ya vyama itakwenda vizuri na uchaguzi utasimamiwa vizuri na ni matumaini yangu pia uchaguzi unaokuja wa Serikali za Mitaa utakwenda vizuri.

Mheshimiwa Naibu Spika, tunataka kutoa idhari kweli Tume yetu ya Uchaguzi ipo vizuri na ipo imara kwa sababu mimi ni moja kati ya wale waliobahatika kwenda changuzi zinavyofanyika nchi zingine, huko inakuwa hali si hali. Tume ya ya Uchaguzi ni mashaka, tume si tume kwa mujibu wa maadili na itifaki hatuwezi kusema ni wapi na nini, lakini sisi tushukuru tume yetu ipo vizuri sana. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, sasa naomba nijielekeze kwenye Ofisi ya Msajili, Ofisi hii ya Msajili kwa sasa badala ya kupitisha ile Sheria Na.5 kuifanyia marekebisho ile ya mwaka 95, naona hali itakuwa nzuri zaidi kwa sababu itapata meno ya kudhibiti wa hivyo wale ambao wamekusudia kufanya vurugu ya aina yoyote, ofisi hii ya msajili ipo tayari kwa ajili yao. Dhamira ya kuhakikisha kwamba hesabu za chama zinaangaliwa vizuri masuala yote yanayohusiana na demokrasia ya vyama vingi kwa msajili kwa imara hizo alizopata itakuwa vizuri. Kwa hiyo napenda kusema kwamba fungu alilopewa Msajili kama kuna namna yoyote ya kuweza kumwongezea, basi aongezewe.

Mheshimiwa Naibu Spika, eneo lingine ninalotaka kuzungumzia ni mahakama, kama tunavyojua huu mhimili ni muhimu sana na unahitaji kuimarishwa zaidi kwa kuwekewa nyenzo za kufanyia kazi. Kuimarisha mfumo wa utoaji haki ni jambo la lazima. Tumeona katika hotuba hii ya Mheshimiwa Waziri Mkuu mashauri kadhaa yameweza kufanyiwa kazi na vile vile tumeweza kuelezwa na kuona kwamba kuna ongezeko la Majaji wa Mahakama ya Rufaa na kuweza vile vile kuweka haya mabadiliko yote. Sasa unapoweza kupata Majaji ushauri wangu ni kwamba lazima uende sambamba na uboreshwaji wa majengo ya mahakama yenyewe.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kadri mahitaji yanapoongezeka majengo vile vile ya mahakama inabidi yaongezeke. Napongeza sana kazi zinazofanywa na hasa Kitengo cha Kusimamia Majengo ya Mahakama, hiki kitengo kimefanya kazi nzuri sana, sisi tuliopata bahati ya kukagua majengo haya tumeweza kuona majengo ya kileo kabisa ya Mahakama ya Rufaa kule Mara na kule Kigoma, kwa kweli Kitengo hiki kinafanya kazi nzuri sana. Kuna sehemu nyingi ambazo bado majengo ya mahakama hayajafikia, lakini tunaamini kwamba fungu likiwekwa hawa watu watapata spidi ya kumaliza kazi ambayo imepangwa na nyingine ambayo itaweza kuzuka. Kwa hiyo upande wa mahakama kwa kweli umejiweka vizuri sana. Naomba kama kuna ziada ya fedha hapo waweze kuongezewa.

Mheshimiwa Naibu Spika, nataka sasa kuzungumzia kilimo cha mchikichi, japokuwa kilipata msito kidogo, kilisita kwa sababu kilianzishwa siku nyingi, lakini kama watu wengine walivyosema kuchelewa sio tatizo, nia ni ile kuhakikisha unataka kufika kule unakokwenda. Kwa hali tuliyoiona ya Kigoma na sehemu nyingine na sehemu nyingi za Tanzania, hii miche inaweza kustawi sana na tukapata mazao mazuri sana. Vile vile lazima twende sambamba na viwanda vya kuchakata hizi chikichi. Tumeweza kuona wananchi kule Kigoma wanajitahidi sana kutumia matunda haya ya chikichi katika kujipatia kipato zaidi kwa kutengeneza sabuni na vitu vingine. Lakini vifaa wanavyotumia bado duni. Kwa hiyo Serikali ingefaa kuwaona watu hawa ambao wengi ni wanawake wanaojishughulisha kwa ujasiliamali kwa kutumia zao hili ili waweze kufanya shughuli zao kitaalam zaidi na kuleta tija zaidi.

Mheshimiwa Naibu Spika, pamoja na zao hilo la chikichi kwa mikoa kama Kigoma lakini naweza hapa kuingizia tu kwamba bado barabara kule haijakaa vizuri, inabidi litupwe jicho la ziada kuweka barabara kule.

Mheshimiwa Naibu Spika, jambo lingine ambalo nalipenda na linanikosha sana ni hili la wazo la kuanzisha SGR - Standard Gauge Railway na ninapoona kwamba itakapofika 2019 itakuwa imeshafika Morogoro, basi inanipa matumaini kwamba inaweza kufika Kigoma hatimaye Mwanza na kwingine na kwa kupitia kwenye reli hiyo ndio pale ambapo uchumi wa maeneo ya pembezoni utaweza kukua kwa sababu watu watasafirisha huku na huku bidhaa zao. Kwa hiyo, hili wazo ambalo champion wetu Rais Jemedari Mkuu amelivalia njuga, napenda nimpongeze linakwenda vizuri sana.

NAIBU SPIKA: Ahsante Mheshimwa, kengele ya pili imegonga.

MHE. ASHA ABDULLAH JUMA: Mheshimiwa Naibu Spika, naunga mkono hoja.