Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 - Ofisi ya Waziri Mkuu

Hon. Fakharia Shomar Khamis

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 - Ofisi ya Waziri Mkuu

MHE. FAKHARIA SHOMARI KHAMIS: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. Kwanza sina budi kumshukuru Mheshimiwa Waziri Mkuu kwa hotuba yake nzuri aliyotoa na ambayo imetoa mwanga kwa Watanzania na wengi walioisikia hotuba yake wanaiunga mkono kama tunavyounga mkono sisi. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, najua ameweza kufanya hivi kwa sababu ana Mawaziri walio mahiri, ana Manaibu Waziri walio mahiri na watendaji wake katika Wizara yake pia ni watendaji walio bora na waliotukukuka na ndio maana akaweza kufanya kitu kizuri kama hiki. Vilevile sina budi kumpongeza Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Makamu wake wa Rais kwa maelekezo yao mema wanayoyatoa na kwa shughuli zao njema za kazi wanazozifanya, inakuwa dira kwa Tanzania. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nataka kuzungumzia huu ukurasa wa 56 unaozungumzia mambo ya afya. Kwa kweli nampongeza Mheshimiwa Waziri Mkuu pale alipoeleza kwamba vituo vya afya vilikuwepo 7,678 na sana vimefika 8,119. Hili ni jambo jema kwa sababu tunaongeza vituo ili kuwasaidia Watanzania kupata afya bora. Hata hivyo, tukae tukijua kuna vituo vinavyotoa dawa hovyo mitaani pharmacy. Vituo hivi unakwenda unasema unataka dawa au unamwambia nini shida yako unayoumwa na unapewa dawa bila kuangalia una cheti ya Daktari au hauna. Unajua kuna dawa nyingine kama akina panadol unaweza ukapewa, hasa hizi za maumivu, ukaeenda kule kwenye hospital pharmacy zao na unaweza ukapewa bila hata kuwa na cheti, lakini kuna zingine lazima uwe na cheti cha Daktari, sio unakwenda unamwambia naumwa kitu fulani na baadaye anakupa dawa.

Mheshimiwa Naibu Spika, sasa hapa panataka elimu itolewe, watupe elimu sisi wananchi, wawape elimu na wale wenye vituo, maana wao wanajali fedha kuliko afya ya mtu. Sasa na hivyo tutawapa matatizo Watanzania ambao wengine hawajui, yeye anajua nikienda hospitali itabidi Daktari nimlipe na nani nimlipe, lakini nikienda pharmacy nitanunua dawa tu, wakati dawa atakayonunua siku nyingine haitamtibu, itampa madhara. Sasa hapa kitu kikubwa ni elimu kutolewa kwetu zote na vilevile kufanya ziara mara kwa mara kuvamia hivi vituo ili wapate uhakika wa hao wanayoyatenda.

Mheshimiwa Naibu Spika, kuna msemo unatumiwa sana, tunaweza au naweza. Huu unamtaka mama mjamzito na baba mwenye mjamzito nyumbani awe anamsaidia mama mjamzito kwenda kliniki na hii lazima pia iwe inapigiwa debe. Mama mjamzito anapokwenda kliniki kupima akienda na baba toka kuanzia mwanzo mpaka atakapojifungua, itasaidia sana baba kujua upungufu wa mama yule. Sasa unaambiwa utumie neno naweza, sasa mnaweza mkikaa baba anasema na mama anasema ili kumfanya kiumbe aliyeko tumboni kupata uhai uliokuwa mwema. Hivyo, hili linataka elimu ili kwa mama inambidi lazima aende lakini kwa baba inakuwa kidogo mbinde kumsindikiza mama, hata handbag yake baba inabidi ambebee maana imeshakuwa mama ana mzigo. Sasa na yeye akienda naye na kambebea ki-handbag chake mapenzi yanazidi.

Mheshimiwa Naibu Spika, nikija ukurasa wa 29 uzalishaji wa mazoa ya biashara, suala hili nampongeza Mheshimwa Rais kwa ziara yake aliyoifanya juzi Mtwara, kaupata ukweli kuondosha upotoshwaji, maana vyombo vya habari vilikuwa vinasema kwamba watu hawajalipwa, Serikali haijawalipa watu inawasumbua kumbe katikati kuna watu walipita njia za mkato wakazinunua korosho wakajifanya wao ndiyo wenye korosho wakauze Serikali ili wao wapate faida. Baada ya kujulikana Mheshimiwa kawasemehe, kawaambia wapite kwenye sheria, wawaone, wawalipe lakini lisiendee. Namshukuru Rais wangu mweledi, ana ufahamu mpana na anatizama tatizo na akalipatia ufumbuzi ili kuwasaidia Watanzania kuondokana na matatizo. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nataka kuongelea ukurasa wa 81 kuhusu Muungano. Kwanza niipongeze Serikali ya Muungano na lazima nipongeze kwa kufuta malimbikizo ya deni ya kodi ya VAT yaliyofikia shilingi bilioni 2.8, hili ni jambo jema, hapa ndiyo Muungano tunapouona. Muungano unazungumza pande zote mbili msaidiane, hii ilikuwa si kusaidia ni wajibu wake umefanya kwa sababu ilikuwa kelele ikipigwa muda mrefu, wameliangalia, wakaona tatizo hakuna, ni haki yao na kuweza kulitekeleza. Kwa hili natoa pongezi kwa Serikali ya Muungano na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kwa kushirikiana hili suala likamalizika kwa amani na usalama. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, sikitiko langu liko mwisho hapa, baadhi ya Ofisi za Muungano Zanzibar zina majengo ya Muungano lakini Wizara ya Mambo ya Nchi za Nje kuanzia mwaka 1964 hadi leo mwaka 2019 halina jengo lake officially walilojenga, jengo wanalotumia ni nyumba iliyokuwa ya Kiongozi wa Upinzani kabla ya Mapinduzi. Jengo la nyumba ukaligeuza ofisi unatupa pesa zako bure kwa sababu halitokubali. Suala hili nimeshalizungumza mara nyingi, naomba Mheshimiwa Waziri alichukue, tunataka jengo la Wizara ya Mambo ya Nchi za Nje Zanzibar kama ilivyojenga Muungano, Polisi, Jeshi, Uhamiaji na Wizara nyingine na wao ni Wizara kubwa…

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

NAIBU SPIKA: Mheshimiwa Fakharia, kengele ya pili.

MHE. FAKHARIA SHOMARI KHAMIS: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante, naunga mkono hoja. (Makofi)