Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 - Ofisi ya Waziri Mkuu

Hon. Alex Raphael Gashaza

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Ngara

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 - Ofisi ya Waziri Mkuu

MHE. ALEX R. GASHAZA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa nafasi ili niweze kuchangia kwenye hotuba ya Waziri Mkuu na mchango wangu utajikita zaidi katika sekta ya uwekezaji. Kabla sijaanza kutoa mchango wangu, nichukue nafasi hii kwanza kupongeza jitihada zinazofanywa na Serikali ya Awamu ya Tano chini ya Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli kwa ajili ya kuwaletea maendeleo Watanzania. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ni ukweli usiopingika kwamba nchi yetu imepiga hatua hususani katika sekta hii ya uwekezaji na ndiyo maana hata taarifa mbalimbali zinaonyesha kwamba Tanzania tumepiga hatua. Kwa mfano, Africa investment Index inaonyesha jinsi gani ambavyo Tanzania tumepiga hatua na kufikia namba 13 katika nchi 54 za Afrika. Pia ukiangalia hata katika taarifa ya Where to Investment in Africa inaonyesha jinsi ambavyo tumepiga hatua hususani katika kuvutia uwekezaji na masoko.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hakuna namna ambavyo tunaweza tukapiga hatua na kufikia uchumi wa kati kupitia sekta ya viwanda kama hatutajipanga vizuri na kuona ni namna gani ambavyo tutaweza kwenda katika uwekezaji huu. Kuna kauli inayosema kwamba, we have to learn from the past for future. Tutakumbuka kwamba baada ya uhuru chini ya Rsis wa kwanza wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Baba wa Taifa, Hayati Mwalimu Nyerere, baada ya uhuru alijikita kuona ni namna gani ambavyo tunaweza sasa tukakimbizana kuinua uchumi wa Tanzania kupitia sekta hii ya viwanda.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naamini zipo changamoto nyingi ambazo tumejifunza baada ya kuona baadhi ya viwanda ambavyo tulikuwa navyo wakati huo vilikumbana na changamoto kadhaa wa kadhaa. Awamu hii ya Tano tunapokuja kuwekeza zaidi na kuweka nguvu katika uwekezaji kwenye sekta ya viwanda kama injini ya maendeleo kufikia uchumi wa kati, naamini tumejifunza changamoto ambazo zilitukwamisha wakati ule. Nimpongeze Rais kwa sababu yeye sasa amekuwa ni mbeba maono mapya katika kuwekeza kwenye sekta hii ya viwanda. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, changamoto tulizokutana nazo baada ya uhuru ni rasilimali watu kwa maana ya wataalam walikuwa wachache, miundombinu ya umeme kwani maeneo yaliyokuwa yameunganishwa kwenye gridi ya Taifa yalikuwa ni machache mno lakini sasa kwa sababu ya maono ambayo anayo Mheshimiwa Rais ndiyo maana tumeanza kujenga msingi ili kuhakikisha kwamba tunapoingia sasa kwenye uwekezaji katika sekta ya viwanda hatukumbani na vikwazo tena. Tunaona jinsi ambavyo amethubutu kuanzisha mradi mkubwa wa umeme (Stiegler’s Gorge) kwenye Bonde la mto Rufiji, tunaona jinsi ambavyo tunaboresha bandari kwa sababu hizi ni fursa ambazo zitatuwezesha sasa kuweza kuingia kwenye uchumi wa kati. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tuna neema kwamba Tanzania kijiografia sehemu kubwa tuko kwenye ufukwe wa bahari ya Hindi na ndiyo maana tukaona ni vyema kuanzisha Maeneo Maalum kwa ajili ya Uwekezaji (EPZ, SEZ) na ndiyo njia pekee ambayo inaweza ikatupeleka kuwa na uchumi wa viwanda. Kwa mfano, nchi za China na India, zimepata uhuru kutoka kwa Wakoloni miaka inayofanana, miaka ya 1949. Baada ya kupata uhuru tu ndani ya miongo sita waliangalia ni namna gani sasa ambavyo uhuru wao watautumia kwa ajili ya kuboresha uchumi wao.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nchi hizi zilianza kuwekeza kwenye Maeneo haya Maalum (EPZ, SEZ) kwa maana ya Export Processing Zones na Social Economic Zones kwa lengo la kutaka kuinua uchumi wao. Hiki ndicho ambacho kimeweza kuwafanya waweze kukimbia kwa haraka. Leo China ni nchi ya pili duniani katika uchumi unaokua kwa kasi. Ni ukweli usiopingika kwamba sasa hivi katika sekta ya viwanda, China inaongoza ikiwa ni pamoja na India. Tukiangalia mifano pia hata ya nchi za Bara la Asia (Indonesia, Malaysia na Korea ya Kusini) nao pia kupitia mifumo hii ya uwekezaji wameweza kupiga hatua kwa haraka. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, niungane na hotuba ya Mheshimiwa Waziri Mkuu na mapendekezo ya Kamati ya Sheria lakini pia na taarifa za Kamati ambazo zipo katika sekta hii kwamba lazima tuweke nguvu sasa katika kuwekeza na lazima tuangalie ni namna gani ya kuweza kuendelea kupanua maeneo haya ya EPZ na SEZ. Maeneo yametengwa, najua yapo na ni machache na bado kumekuwepo na changamoto ambazo zinakabili maeneo haya lakini lazima tuangalie ni namna gani sasa tunavyoweza kuendelea kupanua maeneo lakini pia tukiendelea kuboresha na kuondoa vikwazo vya fidia ili kusudi maeneo haya yaweze kutumika.

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini tunapowekeza katika uzalishaji wa viwanda ni lazima tuangalie masoko ya vile tunavyovizalisha. Najua kwamba yapo masoko ya aina mbili, soko la ndani na la nje. Tunapokwenda kwenye ushidani wa soko la nje lazima tuangalie ni mazingira gani ambayo yanawezesha masoko ya nje kufanyika.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nachoamini, kama tutakuwa tumeweza kuendelea kutengeneza mazingira bora ya uwekezaji, tukaendelea kuita au ku-attract wawekezaji wenye tija ambao uwekezaji wao huo utatupa faida kwa maana ya kuongeza mitaji, kuwa na akiba ya fedha za kigeni, kutoa ujuzi kwa maana ya kwamba tuta-attract na ujuzi kwa sababu wanatoka kwenye mataifa ambayo yamefanikiwa basi itatuwezesha katika kufanya exportation ya bidhaa zinazozalishwa ndani ya nchi kushindana kwenye soko la nje. Kwa hiyo, lazima yote haya kuyaangalia na kujipanga kuona kwamba sasa ni wawekezaji wa aina gani pia ambao tunawaalika kuwekeza ndani ya nchi yetu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, uwekezaji wa aina yoyote unaoweza kufanyika, uwe uwekezaji kwenye sekta ya viwanda, sekta ya kilimo na sekta ya madini ni lazima tushirikishe idara au sekta mbalimbali. Sekta muhimu katika uwekezaji huu ni pamoja na sekta ya ardhi. Najua kwamba upo mpango wa miaka 20 (2013 - 2033) wa matumizi ya ardhi. Mipango hii inatakiwa iende sambamba kwa sababu kama tutakuwa hatujaweza kutekeleza mpango huu wa matumizi ya ardhi na tukaainisha maeneo ambayo tunahitaji kuwekeza na tuwekeze nini kwa maana ya vipaumbele, tutajikuta tunashindwa kufanikiwa na tunakutana na vikwazo. Ndiyo maana nikasema kwamba lazima tuangalie sasa tunaweka vipaumbele katika uwekezaji upi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pengine ninukuu hotuba ya Mheshimiwa Rais wa Awamu ya Nne kwenye Mkutano wake wa kwanza anahutubia Bunge baada ya uchanguzi wa mwaka 2005. Alijaribu kueleza mafanikio ambayo yamepatikana kutoka na awamu zilizopita. Akasema wakati Awamu ya Pili kulingana na hali ya uchumi ilifikia mahali Mheshimiwa Rais wa Awamu ya Pili, Mzee wetu Mwinyi ikabidi aanze kuruhusu sasa watu waingize mitumba kulingana na hali ya uchumi tukaingia kwenye biashara ya nje. Kwa hiyo, wakati wa kuruhusu Mzee akaitwa Mzee wa Ruksa, akasema kwamba hata nzi na mbu waliingia baada ya kufungua madirisha.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hata sasa naomba niseme kwamba ni vyema tukachukua tahadhari kwa sababu lazima tuwe na vipaumbele kwamba tunataka tuwekeze kwenye nini. Kwa mfano, tunapotaka tusema tuwekeze kwenye viwanda lazima tujue raw material zinapatikana kutoka wapi.

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

MWENYEKITI: Ahsante sana Mheshimiwa kwa mchango wako, muda wako ndiyo huo umeisha.

MHE. ALEX R. GASHAZA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa nafasi na naunga mkono hoja.