Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 - Ofisi ya Waziri Mkuu

Hon. Njalu Daudi Silanga

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Itilima

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 - Ofisi ya Waziri Mkuu

MHE. NJALU D. SILANGA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa nafasi na mimi niweze kuchangia hotuba hii ya Waziri Mkuu. Nichukue fursa hii kuwapongeza sana Ofisi ya Waziri Mkuu kwa kazi kubwa na nzuri sana wanayoifanya katika kutekeleza majukumu yao.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nitaanza kutoa pongezi zangu katika Mkoa wetu wa Simiyu hususani Jimbo la Itilima. Serikali ya Awamu ya Tano imeweza kututengea fedha kwa ajili ya ujenzi wa Hospitali ya Wilaya lakini na Hospitali ya Mkoa wa Simiyu. Niwapongeze sana Wizara husika. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la pili, niwapongeze sana Wizara ya Maji kwa kututengea fedha kwa ajili ya ujenzi wa mradi mkubwa wa maji unaotoka Busega kuja Wilayani Bariadi pamoja na Itilima na Meatu kwa ujumla. Shukrani kwa Mheshimiwa Rais kwa kazi nzuri wanazozifanya. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, pongezi zingine ni katika suala zima la ujenzi wa kiwanda cha vifaa tiba. Kiwanda hiki kinajengwa katika Mkoa wetu wa Simiyu, Dutwa ambako ndiko kwenye Jimbo lako. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nichukue fursa hii kuwashauri watu wa Serikali; pamoja na kwamba sisi Mkoa wa Simiyu na Shinyanga ni wazalishaji wakubwa wa pamba lakini tunaozalisha pamba nyingi nchini ni Mkoa wetu wa Simiyu. Katika kiwanda hiki cha vifaatiba teknolojia iendane sambamba na viwanda vilivyopo sasa kuliko kuwa na teknolojia ndogo matokeo yake haiwezi ikakidhi mahitaji ya wakulima wa Kanda ya Ziwa. Kwa hiyo, Serikali ilitazame jambo hili kwa mapana zaidi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini jambo lingine, tunavyo viwanda vya nguo lakini ukitazama uzalishaji wake na uhitaji wa zao la pamba haufanani. Asilimia 80 tunasafirisha, asilimia 20 ndiyo inayobaki hapa nchini lakini hata hiyo asilimia 20 inayobaki ukikaa na hawa watu wa viwanda wana changamoto zao. Naiomba Serikali, badala sasa ya kuwa na mipango mingi, sera nzuri na kadhalika ni vyema Serikali ikutane na hawa watu na ichukue changamoto walizonazo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pale Shinyanga kuna kiwanda cha Serikali ya China kiliwekeza kwa ajili ya kutengeneza nguo lakini leo kiwanda kile kinatengeneza nyuzi, kinapeleka nje halafu ndiyo inarudi malighafi. Kwa hiyo, ni suala kujiuliza kama Serikali kwa nini hawa wawekezaji wetu wanaokuja hapa nchini wanatumia gharama ya kuwekeza viwanda hivi na malighafi iko hapa, kila siku tunasema malighafi tunayo ya kutosha lakini kwa nini iende nje na gharama za uzalishaji zinakuwa kubwa katika maeneo yao, unakuta katika uzalishaji mzima hatupati bei nzuri katika mazao yetu. Jambo hili kama Serikali wakilitazama na kujua changamoto zilizoko naamini kabisa Wizara ya Viwanda na Biashara, Wizara ya Uwekezaji ikikutana na hawa watu wanaweza wakapata majibu mazuri na ni kwa nini mazao yetu hayapandi lakini sasa hivi asilimia kubwa utakutana na changamoto hizo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini jambo lingine; Serikali imekuwa ikiendelea kuweka sera zake nzuri. Tulikuwa na viwanda vya ngozi lakini ngozi wakati ilikuwa ikienda nje kwa maana ya Kenya na sehemu zingine bei zilikuwa kubwa na nzuri sana lakini mkaweka sera ya kwamba viwanda vyetu tuvilinde leo ngozi bei zake ni za kutupa hazieleweki. Kwa hiyo, ni mambo ambayo lazima utafiti wetu ufanyike kwa uhakika zaidi na kufahamu kwa nini tunapoweka hiki bei zinashuka. Katika uwekezaji wetu tunaozungumzia lazima tuangalie mambo muhimu hususani kwenye suala la pamba na viwanda vya ngozi na alizeti. (Makofi)

Waheshimiwa Wabunge, utakubaliana nami kwamba asilimia kubwa ya wawekezaji wetu wanatoka nje na wawekezaji wetu hawa wanatarajia kupata wataalam kutoka nje lakini sera zilizopo zinawabana kuwa na wataalam wa kuwafundisha vijana wetu hapa nchini kwa sababu bureaucracy ni kubwa. Kwa hiyo, hilo nalo wakiliangalia tutatoka kwenye asilimia 20 tutakwenda mpaka kwenye asilimia 50.

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini duniani kote, Mheshimiwa mama Kilango wiki iliyopita alitoa mchango wake mzuri sana akatoa mfano wa Bangladesh. Ni-declare interest mimi ni mwekezaji na bahati nzuri mwaka 2008 tulikwenda kutembelea Bangladesh, karibu asilimia 70 ya watu wa India wanaishi kwa ajili ya viwanda lakini sisi Tanzania tunavyo viwanda na malighafi kwa nini hatuendelei? Ni swali kwa Serikali kwa nini viwanda hivi haviendelei? Kwa hiyo, lazima wafanye utafiti wa kujua kwa nini viwanda vinavyoanzishwa hapa nchini havi-perform kwa sababu zipi na nini kifanyike? Watuletee tutoe ushauri ambao unawezekana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kiko kiwanda pale Arusha, Mheshimiwa Jambo alishafunga tangu mwaka 2007 hakijafanya kazi. Ukimuuliza sababu za msingi anazokutana nazo anasema gharama ni kubwa. Kwa hiyo, Wizara ya Uwekezaji, Viwanda na Biashara wakutane na hawa wadau wawaulize wala siyo kutuma Email au kupiga simu wawaulize kwa nini viwanda vyetu hivi havi-perform na kwa nini bei zake zinakuwa ndogo? Utashangaa bei iliyoko soko la dunia inalingana na mtu anayenunua pamba Shinyanga, Morogoro, Dar es salaam tena la kwake linakuwa chini ukimuuliza anasema gharama ni kubwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, liko jambo moja Waheshimiwa Wabunge wanasema kilo moja ya pamba inazalisha masharti matatu, kilo tatu za pamba ndiyo kilo moja ya mahindi. Kwa hiyo, tunapozungumzia kilo moja ya pamba ina maana ni kilo tatu za mahindi lakini siyo pamba tu hiyo hiyo, kuna malighafi ambayo inatarajiwa kutoka nje ili sasa kuunganisha ili vipatikane hivyo vitu ambavyo vinatajwa mara kwa mara.

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini jambo lingine ni suala la umeme. Tunashukuru Serikali imekuwa na mipango mizuri, sasa mipango hii isiendelee kubaki kwenye makaratasi iteremke kwa wahusika kule ili gharama zipungue ili watu hawa waweze kupata profit kwenye maeneo yao. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, changamoto kubwa, narudia kusema na mwaka jana nilitoa mchango wangu, ukiwasha kiwanda bili yako kama ni ya shilingi milioni 30 au 50 utalipa kwa miezi mitatu mfululizo hata kama umezima kiwanda, kwa hiyo, jambo hili ni la kutazama sana. Siamini wenzangu Mheshimiwa Mawaziri kama walishafanya analysis hizo. Ukiwasha kiwanda leo ukaendesha ndani ya mwezi mmoja utalipa mfululizo miezi mitatu KVA. Mambo kama haya yanatengeneza mazingira watu kuona kwaba uwekezaji hauna faida lakini naamini kabisa kama nchi tunazalisha mazao ya kutosha yote haya tukiyachukua kwa pamoja tunaweza tukafanikiwa na tukapiga hatua kubwa katika suala zima la uwekezaji. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, niendelee kuipongeza Serikali ya Awamu ya Tano imejipambanua kwa mambo mazuri makubwa sana hususani kwa wananchi wangu wa Itilima na Mkoa mzima wa Simiyu mambo yaliyofanyika ni makubwa. Naiomba Serikali sasa iongeze speed katika ujenzi wa kiwanda cha vifaatiba pale Dutwa ili mazao yetu yaendelee kupata bei kubwa na nzuri zaidi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya mchango wangu huo, naunga mkono hoja, ahsante sana. (Makofi)