Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Female
Party
CHADEMA
Constituent
Special Seats
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
0
Ministries
nil
MHE. LUCY F. OWENYA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru. Nami nimshukuru Mwenyezi Mungu kwa kunipa pumzi niweze kusimama katika Bunge lako Tukufu na kuchangia hotuba ya Mheshimiwa Waziri Mkuu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kipekee naomba niipongeze hotuba ya Kiongozi wa Kambi ya Upinzani Bungeni, iwapo hakuisoma lakini naamini kwamba Serikali imesoma na mmeona imefanyiwa utafiti wa kutosha, imesheheni ushauri wa kutosha, nategemea mtaifanyia kazi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nizungumzie barabara ambayo nimekuwa nikiizungumzia kila leo, barabara iliyopo Moshi Vijijini kutokea Kibororoni kwenda Kikarara hadi Tuduni. Kweli kwa sasa hivi Serikali imetenga fedha, imetengeneza kwa kiasi fulani, lakini haifiki hata kilomita moja. Tunajua sasa hivi kule Moshi masika inaenda kuanza, kwa hiyo, ni mategemeo yangu barabara ile watatengeneza mitaro na ninaomba bajeti ya mwaka huu basi zile kilomita 10 zilizobaki Serikali itenge fedha iweze kuimaliza kwa sababu nimeshaelezea umuhimu wa barabara ile ni barabara ambayo ni ya kitalii na KINAPA imeitenga ile barabara kwa ajili ya watu mashuhuri ambao watakuwa wanapanda mlima kwa kupitia barabara ya Old Moshi. Kwa hiyo, ni mategemeo yangu sasa bajeti ya mwaka huu barabara ile itatengewa fedha za kutosha ili iweze kumalizika. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nizungumzie TEMESA. Serikali imekuwa ikinunua magari ya kifahari kila mwaka na TEMESA zilijengwa kila mkoa kwa lengo la kuhakikisha kwamba gari zote za Serikali zinatengenezwa kwenye karakana za TEMESA. Mashine zilizoko kule TEMESA kwa sasa hivi zimepitwa na wakati, hazifanyi kazi na magari ya kisasa sasa hivi hayawezi kutambulika na zile mashine zilizoko TEMESA kwa sababu teknolojia sasa hivi ni mambo ya kompyuta. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, nategemea sasa Serikali ili kupunguza matumizi itengeneze zile karakana zilizoko kwenye kila mkoa na kuhakikisha kwamba wanaweka vifaa vya kisasa ili kupunguza matumizi, maana yake sasa hivi unakuta Serikali inatengeneza gari inapeleka gari TEMESA, TEMESA wanachukua wanapeleka kwenye private garage ambazo ni za Wachina, wao wanaenda kupeleka bili inakuwa mara tatu ya bili ambayo ingetengenezwa na TEMESA. Kwa hiyo, naishauri Serikali ipeleke mafundi wetu waende wakasomee jinsi ya kutengeneza haya magari na mlete sasa teknolojia mpya ambazo zitaweza kutumika katika hizo garage ili tuweze kupunguza matumizi kwa Serikali. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, hii inaenda sambamba na karakana iliyoko Kilimanjaro. Kweli tumenunua ndege nyingi na tunahitaji hizo ndege, lakini tukitengeneza ile karakana iliyoko pale KIA ina maana ndege zetu zitaweza kutengenezwa pale pale KIA. Badala ya kupeleka ndege Canada mnaweza mkawaambia wale mafundi kutoka Canada wakaja wakatengeneza ndege pale KIA. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, hili ni jambo ambalo tumekuwa tukilizungumzia mara nyingi sana, tunarudia na kurudia lakini bado Serikali haijaona umuhimu wa kutengeneza ile karakana. Nataka sasa Mheshimiwa Waziri akija atueleze, kwa jinsi gani mmejipanga kuhakikisha kwamba mnaitengeneza ile karakarana kwa sababu sasa hivi kama nchi tumeanza kuwa na ndege zetu wenyewe. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, hili ni pamoja na uwanja wa Moshi Airport. Uwanja wa Moshi Airport idea ilikuwa ni kufanya ule uwanja uwe kwa ajili ya mafunzo ya ma-pilot. Sasa hivi na sisi tunasema tuna ndege nyingi, ule uwanja sasa umesahaulika kabisa. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nilishawahi kuzungumza kipindi kilichopita na ninarudia tena, ule uwanja watu wengi sasa hivi wanalima maharage kule na karanga. Ni aibu. Uwanja ni mzuri kabisa, ulikuwa unatumika, lakini sasa hivi una potholes haufahi kabisa, hata ndege ndogo sidhani kama zinaweza kushuka pale. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Waziri atakapokuja kujibu hapa atuelezee sasa wana mikakati gani ya kuhakikisha kwamba Moshi Airport inatengenezwa na iwe kwa ajili ya mafunzo ya ma-pilot? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, pale Kilimanjaro tuna zile mbio za Kilimanjaro Marathon. Mbio hizi zimekuwa zikikua mwaka hadi mwaka. Mfano, mwaka 2014 walikuwa wakimbiaji karibu 4,000; mwaka 2015 wakapanda zaidi wakafika 7,000; mwaka 2018 wamefika 9,000; na mwaka huu
2019 wako zaidi ya 12,000. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, mbio hizi zinafanyika katika uwanja wa Ushirika na uwanja huu unalemewa kwa sababu watu ni wengi. Pale Moshi tuna ule uwanja wa Kim Memorial. Uwanja ule una michezo zaidi ya saba, lakini pale kuna soko la mitumba. Sijakataa watu wa mitumba wawe pale, wanaweza wakawepo pale mkawatengea sehemu lakini bado ile sehemu kubwa iliyobaki ikatumika kwa ajili ya michezo. Kama tunavyosema michezo ni afya, lakini watu wa Kilimanjaro hatuna mahali pa kufanya michezo na tunajua magonjwa ya kuambukiza sasa hivi yamekuwa ni mengi na magonjwa ya kuambukiza tunaweza tukajikinga nayo kwa kufanya mazoezi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, ni mategemeo yangu sasa Serikali itatusaidia watu wa Kilimanjaro ule uwanja uweze kutumika sasa maana mwaka unaokuja sasa 2020 ina maana hizi mbio kwa sababu zimezidi kujitangaza watu wanaweza wakafika hata 15,000 na wakifika hivyo, siyo kwamba wanakuja kukimbia tu, wanaleta biashara Moshi, hoteli zinajaa mpaka Arusha na wakija siyo kwamba wanakimbia tu, wanapanda mlima, wanaenda safari, kwa hiyo, inaongeza pato la Taifa katika nchi yetu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nizungumzie kidogo kuhusu uwekezaji. Kiongozi wa Kambi ya Upinzani katika katika hotuba yake ukurasa wa 30 amezungumzia vizuri sana kuhusu uwekezaji. Sasa hivi imekuwa ni kero kwa mtu kuja kuwekeza Tanzania. Kodi ni nyingi sana. Ameainisha hapa kodi zote ambazo zinatakiwa mtu alipe akija kufanya biashara Tanzania.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba ku-declare, mimi pia ni mfanyabiashara. Wafanyabiashara wengi wanafunga biashara kwa sasa hivi, kisa tu kodi. Hawakatai kulipa kodi, lakini zile kodi basi ziwe rafiki. Unakuta mfano, OSHA; OSHA yenyewe unakuta inampa mtu bili ya shilingi zaidi ya shilingi 2,400,000, hujaenda TBS; hujalipa withholding tax; hujalipa income tax; kodi ni nyingi mno. Hebu jaribuni kufanya hizi kodi ziwe rafiki na mtapata kodi nyingi zaidi na Serikali itapata mapato zaidi. Kwa namna hii, ukienda kuangalia ni wafanyabiashara wangapi wamefunga biashara, ni wengi sana. Kwa hiyo, nafikiri kuna haja ya kuja kuleta sheria hapa na kubadilisha sheria zetu za kodi ndiyo solution pekee ambayo tunaweza tukabadilisha mfumo wetu wa kodi hapa Tanzania. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nizungumzie kidogo kuhusu kilimo. Tunasema kilimo ni uti wa mgongo, maneno mengi tu yamekuja. Tunajua kwamba asilimia zaidi ya 80 ya Watanzania ni wakulima, lakini katika hotuba ya Kambi ya Upinzani tumeeleza wazi kabisa 2016/2018 Serikali ilitakiwa itenge shilingi 150,253,000,000/= kwa ajili ya fedha za maendeleo, lakini hadi Machi, 2018 zimetoka tu shilingi bilioni 16.5 sawa na asilimia 11. Hivyo zaidi ya asilimia 89 ya fedha za maendeleo kwa ajili ya kilimo hazikutoka. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa kama kweli tunataka kuendeleza wakulima wetu, tunasema tunataka Tanzania ya Viwanda, bila kilimo hivyo viwanda tutavitoa wapi? Unakuta tunahitaji watafiti, tunahitaji mbegu ambazo ni za kisasa. Kwa fedha hizi ambazo Serikali imetoa, sioni ni jinsi gani ambayo tunaweza tukaendeleza kilimo hiki. (Makofi)
(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)