Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 - Ofisi ya Waziri Mkuu

Hon. Cosato David Chumi

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Mafinga Mjini

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 - Ofisi ya Waziri Mkuu

MHE. COSATO D. CHUMI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru kwa kunipa nafasi na nilikuwa nateta hapa na dada yangu Mheshimiwa Rita, tukasema kwamba, kuna siri katika mafanikio ya hii ofisi. Siri yenyewe nimeona katika watendaji wakuu wa hii ofisi wako hapa saba na ndugu yangu Mheshimiwa Mavunde, lakini katika hawa saba watano ni akinamama, kwa hiyo, kweli, akinamama wanaweza. Mimi ni mtoto wa mama, nalelewa na sasa hivi na mke wangu ni mama, kwa hiyo, akinamama wanaweza. (Makofi)

MBUNGE FULANI: Umeona, una mabinti wangapi?

MHE. COSATO D. CHUMI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nina binti mmoja na yeye najua atanilea wakati ukifika.

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema haya, kwa haraka kabisa kwanza napenda kupongeza jambo moja kubwa ambalo Serikali na Mheshimiwa Rais amelifanya, nalo ni kutupa Waziri ambaye maalum kabisa atahusika na masuala mazima ya uwekezaji. Pia, napongeza hatua za Serikali kuamua chombo kinachohusika na uwekezaji kwa maana ya TIC kukiweka chini ya Ofisi ya Waziri Mkuu. Nadhani hii itarahisisha utekelezaji wa mipango mbalimbali ambayo Serikali imejiwekea katika kuvutia wawekezaji.

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini sio hivyo tu, naona pia jitihada nyingi ambazo Serikali inazifanya ikiwa ni pamoja na kutengeneza miundombinu wezeshi. Tunaona kuna mradi mkubwa utakaokuja wa umeme, yote hii ni kuhakikisha kwamba, uchumi wa viwanda kwa sababu, uchumi wa viwanda bila kuwa na nishati ya uhakika hatuwezi kuufikia. Kwa hiyo, jitihada hizi bila shaka kila mmoja anayo sababu ya kuzipongeza, tunasema kwamba, mnyonge mnyongeni, haki yake mpeni. Naamini kabisa kwa Serikali kuamua kuwa na Waziri maalum ambaye atahusika na mambo ya uwekezaji, changamoto nyingi ambazo wawekezaji wale ambao tunawavutia wanakutana nazo, lakini pia na wawekezaji wa ndani, zitaenda kupata ufumbuzi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na hayo ninao ushauri kwa Serikali; suala la kwanza nashauri kwamba, pia tuweze kuangalia magumu gani au vitu gani ambavyo ni changamoto katika ku-slow down masuala mazima ya uwekezaji. Kwa mfano, naona kabisa tunayo hii Wizara na tunaye Waziri na tunacho hiki chombo cha TIC, lakini kuna maeneo chombo hiki hakina mamlaka ya kufanya maamuzi. Kwa hiyo, niiombe na kuishauri Serikali tuamue kwa wakati, tumekuwa na shida ya kuamua kwa wakati na hata Mheshimiwa Rais mara kadhaa amesema ni afadhali uamue ukosee ufanye marekebisho mbele ya safari kuliko kutoamua kwa wakati.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nitatoa mfano; kule kwetu Mafinga tuna kampuni ambayo imekusudia kuajiri vijana 1,000 kwa ajili ya kuvuna gundi kwenye Msitu wa Sao Hill. Pengine watu mnaweza mkashangaa kwamba, watu wengi wanadhani kwamba, miti ni kwa ajili tu ya mbao, lakini katika miti pia unaweza ukavuna gundi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kampuni hii inavuna gundi ma-container kwa ma-container na inasafisirisha kupeleka China, lakini sasa wanataka wajenge kiwanda ili ile processing iweze kufanyikia pale Mafinga. Maana yake ni kwamba, ajira zitaongezeka, lakini ninapozungumza sasa hivi kuna kitu kinaitwa National Land Allocation Committee, ni miezi nane wale wawekezaji bado hawajapata hati ili kuwawezesha kuanza kufanya kazi. Huu natoa ni mfano mmoja tu, lakini unaweza kuona kuna mambo mengi ambayo jitihada hizi zote ambazo zinafanywa na Serikali, kama vyombo mbalimbali ambavyo kwa namna moja au nyingine vina-cut across kwenye suala la uwekezaji, hatuwezi kupiga hatua mbele. Maana yake ni kwamba, Mheshimiwa Mama Angella Kairuki na vyombo vyake watabaki tu kuratibu, lakini kama vyombo vingine havifanyi maamuzi kwa wakati hatuwezi kupiga hatua. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, hapa pengine ningependa kabisa kuzungumza kuhusu taasisi mbalimbali ambazo zinafanya kazi ya udhibiti, yaani hizi regulatory authorities. Nitatoa tu mfano vyombo kama OSHA, NEMC, TBS, WMA nikiwa na maana wale Wakala wa Vipimo, SUMATRA na
kadhalika. Ningeshauri vyombo hivi ifike wakati vijielekeze katika kufanya kazi ya ku-facilitate kuliko ku-ambush wawekezaji. Vijielekeze katika kutoa elimu kabla ya kufanya ambush na kufanya masuala ya kupiga ma-penalt. Kwa kufanya hivyo maana yake ni kwamba tutakuwa kweli yale mazingira bora ya uwekezaji ambayo yanaendana na uwekezaji katika miundombinu kama umeme, barabara na kadhalika yataweza kufanya wawekezaji kweli waje na wawe wenye tija. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kufanya hivyo maana yake ni kwamba tutakuwa kweli yale mazingira bora ya uwekezaji ambayo yanaendana na uwekezaji katika miundombinu kama umeme, barabara na kadhalika yataweza kufanya wawekezaji kweli waje na wawe wenye tija. Kama hiyo haitoshi, niombe na kushauri pia wakati tuna- focus kuvutia wawekezaji kutoka nje tuangalie pia na wale ambao tayari wameshawekeza wanakutana na changamoto gani wanakutana nazo ambazo pengine tukiweza kuwaondolea zitawasaidia wao kupiga hatua na hivyo kuongeza ajira lakini kuongeza pato la uchumi katika taifa letu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, hata hivyo, natoa rai kwa Serikali na hasa kwa wenzetu wa Kazi na Ajira, uwekezaji huu lazima uendane na ku-reflect welfare ya wafanyakazi katika maeneo yale ambayo wanafanya kazi. Hapa nazungumzia kulipwa kwao, masuala mazima ya hifadhi ya jamii na bima za afya. Nitatoa mfano na hili nimelisema mara nyingi, pale Mafinga tuna wawekezaji hasa wa kigeni hawajali na ku- observe na ku-comply kwenye sheria za kazi. Hawaruhusu vyama vya wafanyakazi, hawalipi bima za afya na hawatoi michango ya wafanyakazi katika mifuko ya hifadhi ya jamii. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, naendelea kutoa rai kwa Mheshimiwa Mavunde naomba ufanye ziara katika Mji wa Mafinga ambako viwanda vipo kwa wingi sana uweze kujionea hali halisi. Pamoja na Mheshimiwa DC na RC kufanya ziara lakini bado nashauri wewe pia ufanye ziara. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, suala la pili kutoka mwisho ni chakula. Natoa ushauri, kutokana na bei ya mahindi kushuka sana, wakulima wa maeneo ambayo chakula kinalimwa kwa wingi kidogo walikata tamaa, hawajalima kama inavyotakiwa na tunaona una hali kidogo ya ukame katika baadhi ya maeneo. Kwa hiyo, nishauri Serikali kupitia Hifadhi ya Chakula inunue chakula cha kutosha iweze kuhifadhi ambapo baadaye itakuja kuuza kwa bei nafuu kwenye maeneo ambayo yatakuwa hayana chakula. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nitakuwa sijatenda haki kama sitazungumzia barabara. Tuna chombo tumeanzisha kinaitwa TARURA, Waheshimiwa Wabunge na Serikali kwa ujumla, kama hatutaiwezesha TARURA kuwa na fedha za kutosha, nilisema mwaka jana tunaweza tukawa na TARURA hata 100, bila fedha za kutosha katika chombo hiki barabara hazitajengwa kama tulivyokusudia. Kweli Serikali imejielekeza katika barabara za kuunganisha mikoa na imefanya kazi nzuri sana lakini sasa nashauri wakati umefika tujielekeze kwenye hizi barabara ambazo zinabeba mazao kutoka vijijini na kuleta kwenye barabara kuu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kama mimi pale Mafinga kwa kweli barabara wakati huu wa mvua yaani ni changamoto kubwa sana. Kwa hiyo, naona suluhisho pekee ni TARURA kuwezeshwa kuwa na fedha za kutosha ili kuweza kutengeneza barabara hizo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, la mwisho, napongeza kwa Tanzania ku-qualify kwenda AFCON. Nimesema mara kadhaa, michezo ni biashara, uchumi na ni ajira. Tutumie fursa hii tunapokwenda Egypt lakini pia tutumie fursa na Waziri Mkuu amesema ya U-17, wenzetu wa TFF na Baraza la Michezo watusaidie kuratibu katika namna ambayo kufanyika kwa mashindano hayo hapa nchini kutakuwa ni neema kwa wananchi wetu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia kuwe na management nzuri ya namna ya kuingia pale uwanjani hasa Uwanja wa Taifa kwa sababu hamasa ni kubwa, watu wanajitolea kwa wingi kuja uwanjani lakini mtu anafika uwanjani anapoteza saa nzima anaingia uwanjani bado dakika kumi. Ni suala tu la ku-manage ili kusudi watu wanapokuja uwanjani viingilio vinapatikana lakini pia hamasa inakuwa kubwa na wananchi wananufaika. (Makofi)

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)