Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 - Ofisi ya Waziri Mkuu

Hon. Ahmed Juma Ngwali

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Ziwani

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 - Ofisi ya Waziri Mkuu

MHE. AHMED JUMA NGWALI: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza nashukuru kwa kunipa fursa hii. Nianze hoja yangu na Kituo cha Uwekezaji cha TIC. Kituo cha Uwekezaji cha TIC kilianzishwa kwa malengo maalum ya kuisaidia nchi katika uwekezaji; kuratibu, kusimamia lakini kuishauri Serikali katika maeneo mbalimbali ili nchi hii katika uwekezaji iende mbele.

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la kusikitisha ni kwamba leo wawekezaji wamekuwa wapo katika taabu sana. Utamkuta Mkuu wa Mkoa, Mkuu wa Wilaya, OSHA, Afisa wa TBS na Afisa wa TFDA, wote hao wana mamlaka ya kumkamata mwekezaji wakaita vyombo vya habari wakamwonesha hadharani.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mwekezaji yule ameleta pesa zake nchini, amewekeza, ameajiri Watanzania; hebu Serikali mtuambie, ninyi mnaona fahari gani? Mnaona sifa gani? Serikali inapata faida gani kumwonesha mwekezaji kama jambazi au mtu ambaye hana maana yoyote? Mtu huyu ameajiri watu chungu nzima na Serikali ipo na watu hawa wanaendelea kufanya mambo mabaya kama hivyo na wanaachiwa tu, hakuna hatua yoyote inayochukuliwa. Hilo ni jambo la kwanza. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la pili, naomba Serikali kwenye jambo hili mlikomeshe, likome kabisa, kwa sababu hali ya wawekezaji nchini; hebu niwaeleweshe kwamba wawekezaji ni jamii moja. Mnapomfanyia mmoja tu, dunia nzima inapata taarifa na wanaambiana. Ushindani wa kibiashara uliokuwepo sasa hivi katika nchi jirani, ninyi mnaujua. Kwa hiyo, siyo jambo jema, ni jambo la aibu kwa nchi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la tatu ni Kituo cha TIC. Kile kituo cha TIC cha huduma kwa pamoja (One Stop Center) kimewekwa pale kwa ajili ya kusaidia wawekezaji, lakini kile kituo Maafisa waliopelekwa katika eneo lile kwenye kile kituo, hawana mamlaka ya kumaliza hayo matatizo ya wawekezaji.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa mfano, ukitazama Sheria hii ya Tanzania Investment Act ya mwaka 1997 kifungu Na. 24 kinawapa mamlaka TIC kwa mradi uliosajiliwa pale, watano waruhusiwe waingie kufanya kazi katika hiyo kampuni. Wao wana hiyo sheria, lakini Sheria ya Kazi, The Non- Citizen Development Regulation Act, hii inasema sasa yule anaruhusiwa watu watano automatically, tena kwa mradi fulani, siyo kampuni. Sasa huyu Kamishna wa Kazi kumpatia hicho kibali sasa cha kufanya kazi inachukua miezi sita, miezi saba, jambo ambalo hizo sheria zina-contradict. Kwa nini ikiwa TIC sheria imeruhusu, halafu huyu mpaka sasa kuomba kwake anapata shida na mara nyingi zinakuwa rejection na TIC ndiyo wanaosimamia hiyo shughuli?

Mheshimiwa Mwenyekiti, hapo hapo kwenye Kituo cha Uwekezaji, Sheria ya Immigration Act ya mwaka 1995, naye Kamishna wa Immigration lazima atoe kibali cha resident permit. Mwekezaji lazima awe na vibali viwili, lakini hao TIC wenyewe, ukienda kwenye kile kituo cha huduma kwa pamoja huwakuti wala hawana mamlaka. Hivyo nini maana ya kuwepo hicho kituo cha pamoja? Maana yake ni nini? Suala la vibali, tuseme ukweli, nanyi Serikali mnajua vibali vya kazi imekuwa tatizo, shida kubwa sana katika nchi hii. Kama wawekezaji ni wezi, haiwezekani. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kama haitoshi, Serikali inawachukulia wawekezaji, yaani mwekezaji anaonekana kama kaja katika nchi kuchukua mali za nchi. Mwekezaji siyo hivyo ilivyo jamani. Mheshimiwa Mavunde sasa hivi Kamishna wa Kazi amekuwa mungu mtu kabisa, imekuwa tatizo kubwa. Sawa, hilo tuliache, lakini katika uwekezaji tuna tatizo lingine ambalo lazima tulioneshe hapa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna mabadiliko ya mara kwa mara ya vivutio vya uwekezaji. Wizara ya Fedha kama Wizara ya Fedha wanajua wanafanya nini kwa wawekezaji. Kwa mfano, ukipitia bajeti ya mwaka 2009/2010 Serikali ilifuta ile capital goods ikapelekea idadi ya miradi kushuka kutoka miradi 871 mwaka 2008 mpaka kufika miradi 500 mwaka 2010.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Wizara ya Fedha katika bajeti ya mwaka 2012/2013 ilipunguza kiasi cha Ushuru wa Forodha kutoka asilimia 100 hadi asilimia 90 na pia ikapunguza VAT kutoka asilimia 100 mpaka 45. Katika bajeti 2013/2014 Serikali ilipunguza kiasi cha msamaha wa Ushuru wa Forodha kutoka asilimia 90 mpaka 75. Mambo hayo yote Wizara ya Fedha, vivutio vile vikiwa haviwekwi kwa mpangilio vikawa vya kudumu, mnawasumbua wawekezaji. Wawekezaji wanasumbuka sana. Mwekezaji anakuja kuwekeza leo katika nchi katika vivutio hivi, baada ya mwaka mmoja mnaondoa, hiyo siyo sahihi. Mnafanya vitu vya ajabu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nipendekeze kitu kimoja. Mheshimiwa Waziri alete sheria hapa Bungeni, ile TIC iwe mamlaka. Ikiwa authority, inaweza kutusaidia. Mnapoleta sheria, Maafisa wa TIC wakawa ni Maafisa wenye kuweza kuamua, ndiyo tutakapokuwa na maana, lakini ikiwa mtaendelea na utaratibu ambao upo sasa, hakuna chochote mtakachokifanya kikawa. Hakuna uwekezaji.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nasema ikiwa sheria hizi zitaendelea kuwa kama zilivyokaa kwa namna hii, kama hamjaleta sheria hapa Bungeni tukaibadilisha kuwa mamlaka kama ilivyokuwa Rwanda, Burundi na Kenya, haiwezekani. Maana yake hata tukifika hapa kuja kuzungumza haya maneno, inakuwa mambo yametufika.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ufanyaji biashara na sijui msaada gani hasa Kituo cha Uwekezaji kinatoa kwa wawekezaji wa ndani. Serikali, kwa mfano Wizara ya Maji, inazuia watu wanaosafirisha mchanga kwa ajili ya kuuza wasifanye kazi usiku lakini kuingiza material mchana mjini, foleni yake unaijua. Mkandarasi anahitaji cubic meters 2,000 kwa siku, local investor ana uwezo kutokana na hali ya Dar es Salaam ilivyo na sehemu nyingine kupeleka cubic meters 100. Kuna nchi gani watu wanazuiwa kupeleka material usiku, kufanya kazi usiku jamani? Sisi tunaiga wapi ufanyaji wa biashara? (Makofi)

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

MHE. AHMED JUMA NGWALI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru. (Makofi)