Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Biharamulo Magharibi
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
0
Ministries
nil
MHE. OSCAR R. MUKASA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushuru sana. Awali ya yote namshukuru Mwenyenzi Mungu kwa kuturuhusu kufanya hii shughuli leo, lakini nitumie fursa hii kuendelea kuwashukuru wananchi wa Biharamulo kwa kuendelea kunipa imani na kunivumilia kwenye kazi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pili, nataka niipongeze Serikali, Mheshimiwa Rais Dkt. John Pombe Magufuli kwa kazi nzuri anayofanya, lakini kwa maana ya bajeti hii, napenda nimshukuru sana Mheshimiwa Waziri Mkuu kwa kazi anayoifanya, Mheshimiwa Jenister, Mheshimiwa Angellah Kairuki, Manaibu wao; Mheshimiwa Mavunde na Mheshimiwa Ikupa, hongereni sana kwa kazi nzuri. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nitazungumzia mambo mawili; Sekta ya Afya kama iliyoelezwa kwenye kitabu cha hotuba ukurasa 56 mpaka 62, lakini nitagusia kidogo suala la UKIMWI na mwishoni nitaja mambo mawili matatu yanayohusu Biharamulo mahususi ambayo mengine ni dharura na mengine ambayo yamekuwa yanatusumbua kwa muda mrefu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ukurasa wa 56 mpaka 62 wa kitabu cha Mheshimiwa Waziri Mkuu, kinaongelea Sekta ya Afya na kuna mahali kinasema vizuri kabisa kuhusu mafanikio ambayo nimeyapongeza na ninaendelea kuyapongeza. Kwa mfano, miundombinu ya huduma za afya kumeongeza vituo vya tiba kutoka vituo 7,678 mpaka vituo 8,119. Maana yake ni kwamba tunaendelea kupeleka huduma za afya kwenye maeneo ambayo zinaweza kutolewa kwa wananchi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, maoni yangu kwenye hilo, twende mbali zaidi. Ukisoma ukurasa huo wa 56 mpaka 62 ingawa kichwa cha habari kinasema “Afya”, lakini kwa kiwango kikubwa tumejikita kwenye tiba, ambapo tiba tunaihitaji, lakini tunahitaji sana kwenda kwenye afya kwa ujumla. Afya inaanzia kwenye kuzuia/kukinga lakini kuelimisha watu ili hata hayo mahitaji ya Vituo vya Afya na vifaa tiba, hata kama yanaongezeka yasiendelee kuongeza kwa kasi, ifikie mahali sasa tunashughulika na tiba kwa wale ambao wanaumwa, lakini kwa kiwango kikubwa tunazuia watu wasiugue. Kwa namna hiyo tutakuwa tunatumia zaidi pesa yetu inayozalishwa na sekta nyingine za uchumi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nilikuwa naangalia hapa kitabu cha ikama ya Wizara ya Afya wanaita Staffing Level for Ministry of Health and Social Welfare kwa 2014 - 2019 ndiyo kinatumika mpaka sasa. Wameweka pale Staffing Level kwa ngazi ya zahanati.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Ukiangalia pale, karibu asilimia 80 ya watumishi ambao wamewekwa pale kwenye Kituo cha Afya ni watumishi wa tiba. Mtumishi wa Kinga ni mmoja tu, wanamwita Community Health Worker or Social Welfair Assistant ambapo hao wengi wote wa tiba wanaelekezwa kabisa, kwa mfano, Clinical Officer anaambiwa kwa siku ataona wangonjwa 40, Mphamasia anaambiwa kwa siku atafanya prescription 40 na Nesi anaambiwa kwa siku ataona wagonjwa 30. Huyu mtu, Community Health Worker kazi yake anaambiwa to link person between community and the dispensary. Hata ile dhana ya kwamba sasa huyu naye anapaswa tumwekee kipimo kwamba kwa siku atatembelea nyumba kadhaa ahakikishe kuna sehemu ya kunawa mikono, kaya zina vyoo na mambo kama hayo ili nguvu yetu iwe kwenye kinga zaidi kuliko tiba.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Sekta ya Afya ili iweze kuleta majibu kwa maana ya afya kwa ujumla, mapendekezo yangu ni kwamba sasa taratibu tuanze kuondoka kwenye kuwekeza tiba peke yake, tuanze kwenye kinga. Nafahamu kwenye upande wa kinga, kwa mfano, upande wa chanjo tunafanya vizuri sana. Tanzania ni moja ya nchi ambazo zimeshafika zaidi ya asilimia 95 kwenye kuchanjwa watoto wetu. Vile vile kuna kinga za magonjwa mengine kama ya kuhara, magonjwa mengine ambayo yanasabishwa na tabia tu za wananchi kule vijijini, hatujawekeza vya kutosha. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ukiangalia ule mzigo wa magonjwa kwenye zahanati zetu, ukiangalia burden of diseases profile, utakuta kuna sehemu kubwa ni magonjwa ya kuambukiza ambayo yanazuilika. Malaria ni wazi hilo ni tatizo la Kitaifa, lakini unakuta magonjwa ya kuhara kwenye zahanati yanachukua namba mbili ama namba tatu. Kwa hiyo, mzigo ni mkubwa sana, ni magonjwa ambayo ukielimisha watu tu kidogo, akanawa mikono kabla kula, akanawa mikono baada ya kula, akahakikisha kuna choo kizuri, ule mzigo utapungua na ile nguvu ya pesa tutaipeleka kwenye maeneo mengine ambayo ni ya uzalishaji. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, niongelee UKIMWI. Tuna tatizo mpaka sasa kwamba asilimia 93 ya pesa ya mwitikio wa UKIMWI kwenye nchi hii ni kutoka kwa wafadhili. Tumesikia hivi karibuni, wametanga wenzetu Wamarekani kwamba asilimia 23 ya fedha hiyo inaondoka kwa mwaka huu. Ambapo ukiipeleka kwenye thamani ya fedha Kitanzania ni shilingi bilioni 282. Ni fedha nyingi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, siyo vizuri tuendelee kuwa tegemezi, lakini namna nzuri ya kujitoa kwenye utegemezi ni kuanza kuwekeza kwenye mfuko wetu wenyewe, Mfuko wa AIDs Trust Fund. Uwezo huo tunao na mifano tunayo, tumefanya hivyo kwenye REA, tumefanya hivyo kwenye maeneo mengine, tutafute namna kukanza kusimama…
MHE. ALLY K. MOHAMED: Mheshimiwa Mwenyekiti, taarifa.
MWENYEKITI: Mheshimiwa Keissy, taarifa.
T A A R I F A
MHE. ALLY K. MOHAMED: Mheshimiwa Mwenyekiti, nampa taarifa mzungumzaji kwamba badala ya kuongeza bajeti kwenye UKIMWI ashauri wananchi waache uasherati. (Kicheko)
MWENYEKITI: Mheshimiwa Mukasa.
MHE. OSCAR R. MUKASA: Mheshimiwa Mwenyekiti, hiyo taarifa naiachia kiti, kitaona inaendaje.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tunayo mifano kwamba Tanzania kwenye baadhi ya maeneo tumeendelea kusimama wenyewe na jambo hili la UKIMWI ni jambo ambalo linatoa platform, ni jambo mtambuka ambalo linasababisha magonjwa mengine yote ikiwemo TB, Hepatitis hata Kisukari sasa hivi, mtu ambaye ana tatizo la upungufu wa kinga, anakuwa kwenye hatari kubwa zaidi ya kufariki kutokana na magonjwa mengine kwa sababu ya kuwa na upungufu wa kinga. Jambo ambalo linahusu maisha yetu tena kwa upana huo ni vizuri sana na ni muhimu sana Serikali ikafahamu kwamba tuanze sasa kutafuta namna ya kusimama wenyewe.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nina mambo matatu ya Biharamulo; moja jana jioni Askari wa SUMA JKT wamemuua mwananchi mmoja wa Kijiji wa Mavota kwa tuhuma kwamba aliingia kwenye eneo ambalo hapaswi kuingia. Naomba Serikali, Waziri wa Nishati kama yuko hapa, Waziri wa Ulinzi watusaidie kuangalia hali kama hii, kama inaanza kujitokeza tena, ni kweli hatuwaambii wananchi wetu wavunje sharia, lakini taratibu za kuwadhibiti pale ambapo wanaonekana wamevunja sheria zinafahamika. Huko nyuma jambo hili lilikuwa kubwa sana, tukalikabili likawa limeisha, lakini sasa inaonekana linataka kurudia.
Mheshimiwa Mwenyekiti, niongee habari ya ulinzi na usalama Biharamulo; jana na wiki kadhaa zilizopita yameanza kurudi matukio kwa kasi ya majambazi kuvamia maduka, majambazi kuteka magari, jambo ambalo lilikuwa linatuathiri siku za nyuma kwa sababu ya sisi kuwa mpakani na nchi jirani ambazo zina watu wanaoingia bila utaratibu likawa limedhibitiwa kwa kiwango kikubwa hasa kwa kuweka kikosi maalum pale Nyakanazi, lakini kwa wiki chache zilizopita inaonekana ile hali ya zamani ambayo ni mbaya inaanza kurudi kwa kasi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tunaomba Serikali waangalie jambo hili kwa sababu wananchi wa Biharamulo sasa hali kama ile inavyojirudia kwa kiwango kikubwa, tunashindwa kufanya shughuli zetu za uchumi, tunaishia nguvu zetu zote kuweka kwenye mambo ya kiusalama. Kuna migogoro ya Jeshi na Vijiji, Kijiji cha Rusabya, Kabukome na Kalebezo, nimesikia Mheshimiwa Naibu Waziri wa Ardhi asubuhi analiongelea kwa ujumla, lakini ujumla huo, umekuwa unachukua muda mrefu sana. Tunaomba Serikali, hizo Wizara zimepewa kazi ya kwenda kutazama, hebu tumalize kazi hiyo, kwa sababu kule wananchi kule wamesimama hawafanyi shughuli zao.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru na kwa mara nyingine nampongeza Waziri Mkuu na timu yake, kwa kazi nzuri. (Makofi)