Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 - Ofisi ya Waziri Mkuu

Hon. Augustine Vuma Holle

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Kasulu Vijijini

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 - Ofisi ya Waziri Mkuu

MHE. AUGUSTINE V. HOLLE: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa nafasi hii ya kuchangia kwenye bajeti hii ya Ofisi ya Waziri Mkuu. Mchango wangu utajikita sana kwenye shukurani, maombi, pia na ushauri. Nitaanza na la mwisho.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nianze kushauri kwanza kwenye suala la vibali vya ajira. Nchi yetu hii tunavyojua ni kwamba ina soko dogo sana la ajira. Ajira ni chache lakini tunao vijana wengi ambao hawana ajira. Kwanza nimpongeze Mheshimiwa Jenista na Ofisi yake kwa kazi kubwa ambayo wameifanya kwenye kudhibiti otoaji holela wa vibali vya ajira. Maana hapo katikati vibali hivi vimekuwa vinatolewa kama njugu, sasa sisi kama Taifa tuna uhitaji mkubwa wa ajita kwa sababu kuna vina wengi ambao wako mtaani. Nashangaa kuna watu ambao wanakuja hapa Bungeni kutetea kwamba Serikali izidi kumwaga vibali vya ajira hii kwa wawekezaji mbalimbali. Jambo la ajabu kabisa hili.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nadhani kwa sababu tuna vijana wengi ambao wako mtaani, Mheshimiwa Jenista na ofisi yake waendelee kuminya. Nimpongeze Kamishna wa Ajira, waendelee kuminya, wasitoe vibali hivi kwa wageni ili wananchi wa Tanzania, vijana wengi ambao wako mtaani ambao hawana ajira, waendelee kupata kazi hizi. Hili ni jambo la kwanza. Niseme, kwa sababu tunajua kuna shida, tatizo kubwa la ajira nchini, mimi nitoe ushauri wa Ofisi ya Waziri Mkuu, kwamba iundwe Task Force, yaani Kikosi Kazi, chini ya Ofisi ya Waziri Mkuu, ambacho kitajumuisha wasomi, wajasiriamali na wadau mbalimbali ili kuweza kujadili tatizo hili la ajira nchini na hatimaye waweze kutoa ushauri mzuri kwa Serikali yetu pendwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, najua, Serikali inaendelea na juhudi zake za kuendelea kutoa ajira kwa maelfu…

MHE. ALLY SALEH ALLY: Mheshimiwa Mwenyekiti, taarifa.

MWENYEKITI: Mheshimiwa Vuma, taarifa.

MHE. ALLY SALEH ALLY: Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kumpa taarifa msemaji, hoja iliyopo hapa ni ile sheria inayosema kwamba, mwekezaji ana fursa ya kuleta watu watano wa mwanzo, automatic bila hata akileta mtu wa aina gani, wale ambao watamlindia mali yake. Kwa hiyo, hawa kwa nini wanasumbuliwa ndiyo hoja, napenda kumpa taarifa hiyo, wakati wameshatajwa kwenye sheria.

MWENYEKITI: Ahsante. Mheshimiwa Augustine taarifa hiyo unasemaje?

MHE. AUGUSTINE V. HOLLE: Mheshimiwa Mwenyekiti, siipokei, kwa sababu Kamishna wa Ardhi anaifahamu vizuri kabisa Sera na Sheria yetu, amekuwa anawanyima vibali watu ambao hawana sifa za kupata vibali vya kuajiriwa, kabisa, kwa sababu nina watu ambao nimeshuhudia kwa macho yangu, wenye vigezo, wanapata vibali. Kwa hiyo, wale ambao wananyimwa ni wale ambao hawana vigezo na nashauri Kamishna wa Ardhi aendelee kukaza buti, kwa sababu kuna vijana, kuna wadogo zetu, kuna watoto wengi ambao wako mtaani ambao hawana kazi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kushauri Ofisi ya Mheshimiwa Kairuki, Uwekezaji, kwamba niko Kamati ya PIC tuna Mashirika mengi ya Serikali, tuna mashirika mengi ya Serikali ambayo yana fedha nyingi sana. Badala ya mashirika haya kwenda kujikita kuwekeza kwenye ujenzi wa majengo ya nyumba za kuishi, sijui za biashara, nashauri, washauriwe watu hawa waende kuwekeza kwenye sekta ambazo zitawagusa Watanzania walio wengi sana, hususan kwenye kujenga viwanda.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa mfano, nitoe ushauri mmoja, kwamba katika Awamu hii ya Tano, ambayo tunajua kwamba ni Serikali ya Viwanda, ningeweza kushauri kwamba, Mheshimiwa Waziri akae na Mifuko hii ya Hifadhi ya Jamii, hasa NSSF, PSSPF,waweze kukaa pamoja na kutafuta wadau mbalimbali wengine ambao wataunganisha nguvu pamoja, tupate kiwanda kikubwa cha mbolea katika nchi hii ili tuweze kuondokana na tatizo la kuagiza mbolea kila mwaka kutoka nje ya nchi, ushauri huo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kushauri kwenye suala pia la internship, vijana wengi ambao wanamaliza vyuoni wanakaa mtaani na wakati mwingine wanakosa ajira katika sehemu mbalimbali kwa sababu ya ukosefu wa uzoefu. Sasa nashauri, Serikali iwe na mkakati wa kutoa internship kwa vijana ambao wanamaliza vyuoni.

Mheshimiwa Mwenyekiti, najua huwa tuna utaratibu, tuna mipango kwamba baada ya mwaka mmoja tunaajiri watu kadhaa, baada ya miaka mitano tutaajiri vijana kadhaa. Sasa ushauri wangu ni kwamba, vijana wanapokuwa wamemaliza vyuo vikuu, basi tuwe na utaratibu kabla haujafika wakati wa kuwaajiri, tuwachukue tuwaweke sehemu mbalimbali katika ofisi za Serikali, kwenye mashule, mahospitali na sehemu nyingine, waende wakajifunze kuchapa kazi ili wasiwe tu na elimu bali pia wawe na uzoefu wa kufanya kazi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, vijana wengi wako tayari kujitolea, kwa sababu wanajua kwamba kwenye kujitolea wanapata uzoefu na hatimaye wanakuwa na nafasi ya kupata kazi hata kwenye sekta binafsi kwa sababu wanakuwa na uzoefu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, maombi, Halmashauri ya Wilaya ya Kasulu, tumepanga, kwa sababu Makao Makuu ya Halmashauri yako kwenye Halmashauri ya Kasulu Mji, kwa mzee wangu Nsanzugwako pale. Naomba Serikalini, kwamba eneo la kujenga Makao Makuu ya Halmashauri, tunalo tayari, pale Kata ya Nyamnyusi, kwa hiyo, niombe fedha kwa ajili ya ujenzi wa halmashauri ili kwamba tuweze kutoka Kasulu Mjini, twende sehemu yetu kwa maana ya kuwafuata wananchi na kuwapelekea huduma zaidi karibu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna Chuo cha Ufundi cha Nyamidahu, hiki chuo tumejengewa na World Vision, wamejenga chuo kizuri kina mabweni, kina madarasa, kina furnitures, lakini sasa hakina vyoo, hakina umeme na miundombinu midogomidogo. Kwa hiyo, niombe Serikali kwamba ikichukue chuo hiki, ikimalizie, kwa sababu kina zaidi ya miaka mitatu toka kikamilike ili kiweze kuanza kutumika kuwanufaisha wananchi wa Jimbo la Kasulu Vijijini. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ombi lingine, kwa sababu tunaendelea na miradi ya umeme miwili, kwenye Jimbo la Kasulu Vijijini na Mkoa wa Kigoma kwa ujumla, tunaendelea na REA, lakini na ujio wa Gridi ya Taifa. Najua kwenye gridi ya Taifa, evaluation imefikia asilimia 90, na mwezi wa Sita kwa maelezo niliyonayo, kwamba watakuwa wamemaliza tayari evaluation. Wananchi wa Mkoa wa Kigoma wamesubiri kwa muda mrefu sana ujio wa umeme wa gridi ya Taifa, kwa hiyo, niombe chonde chonde evaluation itakapokamilika, kwenye bajeti hii ambayo tunaipitisha muda si mrefu, ya mwezi wa Sita, basi wananchi wa Kigoma tuhakikishe kwenye bajeti hii wanapata umeme wa gridi ya Taifa kwa sababu tumesubiri muda mrefu sana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia nipende kuomba pia, tumepata vibali vya miradi ya maji, miradi ya Nyamnyusi, Titye na Lalambe kule, zaidi ya bilioni sita, tumepata vibali vya kutangaza tenda hizi. Niombe tutakapopata mkandarasi kusiwepo na ucheleweshwaji wa fedha kutoka Serikalini kwa ajili ya mkandarasi huyu ili kuhakikisha kwamba mradi unakamilika kwa wakati na wananchi waweze kunufaika.

Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kuishukuru Serikali, kuna vitu vingi sana ambavyo imefanya kwenye Jimbo la Kasulu Vijijini. Tumepata milioni 500 kwa ajili ya ujenzi wa kituo cha afya cha Nyamidaho, tumepata milioni 500 kwa ajili ya ujenzi wa kituo cha afya cha Rusesa Uboreshaji, tumepata milioni 500 ujenzi wa kituo cha afya cha Nyakitonto, tumepata bilioni moja na milioni mia tano kwa ajili ya ujenzi ya hospitali mpya ya Wilaya kwenye Kata ya Nyamnyusi. Napenda kuishukuru sana Serikali, kwa kweli kazi kubwa imefanyika, kazi kubwa mno. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwenye elimu, juzi tumepata fedha milioni mia tatu kwa ajili ya ujenzi wa mabweni na kupanua Sekondari ya Kasangezi. Tumepata fedha tumemalizia shule ya Asante Nyerere, imeanza tumesajili, tumepata fedha tumemalizia shule ya Sekondari Kitanga imeanza tayari, lakini pia tumepeleka milioni 48 kwenye shule ya msingi Shunga. Kwa kweli kazi kubwa inafanyika, na niwaambieni, mwaka 2020, Magufuli Kasulu yeye aje apunge mkono tu atashinda. (Makofi/Kicheko/Vigelegele)

MWENYEKITI: Mheshimiwa Vuma ahsante sana.

MHE. AUGUSTINE V. HOLLE: Mheshimiwa Mwenyekiti, naunga mkono hoja.