Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Nkasi Kaskazini
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
0
Ministries
nil
MHE. ALLY K. MOHAMED: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana kwa kunipa nafasi nami nipatre kuchangia dakika zangu hizi 10. Kwanza kabisa, naunga mkono hoja kwanza kwa asilimia mia moja. Namshukuru Waziri Mkuu kwa jitihada anazofanya pamoja na Mawaziri wote. Kusema kweli Mawaziri wanapishana kwenye anga za Wilaya na anga za Majimbo. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, namshukuru Mheshimiwa Rais, Wilaya yangu ina miaka 40 lakini ilikuwa haina Hospitali ya Wilaya ila mwaka huu imepata fedha za Hospitali ya Wilaya pamoja na Vituo vya Afya viwili. Tumelalamika miaka na miaka. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine, nataka kuchangia kwenye Tume ya Uchaguzi. Wengi wanazungumzia habari Tume ya Uchaguzi, mimi nazungumzia Tume ya Uchaguzi, ipitie upya Majimbo na Kata. Hatulingani Majimbo. Unakuta Mbunge mmoja ana Kata nne, Kata sita, Kata saba mwingine Kata 28 au 29, anapata mafuta yale yale ya Jimbo, pesa ile ile ya Jimbo, mwingine amekaa tu anazunguka na bajaji na pikipiki anamaliza Jimbo lake. Naomba Tume ya Uchaguzi kabla ya uchaguzi wa Serikali za Mita aipitie Kata upya, kabla ya Uchaguzi Mkuu apitie Majimbo upya. Kama Majimbo hayafai, fyekelea mbali. Nadhani tunaelewana hapo. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nazungumzia habari ya wakulima wa Rukwa. Wakulima wa Rukwa ni wakulima wa mahindi na mahindi yetu hayo ni zao la biashara. Mwaka 2018 wameteseka sana, leo hi nimepata habari DRC Congo mahindi gunia ni shilingi 100,000/= lakini kwetu mahindi ni shilingi 30,000/= vikwazo vimekuwa too much. Vikwazo vimezidi. Mahindi yanatakwenda Kenya vikwazo, yanataka kwenda South Sudan, vikwazo; yanataka kwenda wapi, vikwazo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sisi wakulima wetu mahindi ni kama zao la biashara. Kwanza hamwasaidii mbolea, hamwasaidi kupalilia, hamwasaidii kuvuna, wakivuna mnawawekea vikwazo, kwa vipi? Mwaka huu ndugu zangu sehemu nyingi mnasikia mvua hakuna. Kufa kufaana. Tuache tuuze mahindi tunapotaka, kila mtu ajue. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, wengine wanakalia kucheza bao, kucheza dhumna hawalimi shambani, wanaogopa kwenda kulima, walime wengine mwekewe vikwazo. Vikwazo mwaka huu hatuvitaki Mheshimiwa Waziri Mkuu. Kila mtu ajue lake, tuuze mahindi tunavyotaka na ondoeni vikwazo kuuza mahindi popote tunapoweza. Nyie chukueni ushuru wenu, mambo yaishe.
Mheshimiwa Mwenyekiti, usafiri Ziwa Tanganyika. Tufanye biashara. Ziwa Tanganyika tumezungukwa na nchi ambayo ni tajiri katika Afrika DRC Congo. DRC Congo hawana usafiri. Hivi tukitengeneza meli kubwa iwe inazunguka kutoka Kigoma iende Huvira, Kalemi, Moba, Zambia - Mpulungu, irudie huku kwetu, tutapata na pesa za kigeni. Tusijifungie kati. Congo kama Congo ni nchi tajiri. Tufunguke tufanye biashara DRC Congo. Huwezi kufanya biashara na masikini mwenzako, huwezi kuendelea, miaka yote utakuwa masikini. Tuelekeze nguvu zetu Congo. Congo kuna utajiri mkubwa! Tufanye biashara Congo. Tupeleke ujumbe mkubwa wa wafanyabiashara kule Congo watu wafanye biashara zao, tusifanye vikwazo. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu maji. Kila mara nazungumza kuhusu maji. Hakuna Waziri anayefanya kazi kwa wakati huu kama Mheshimiwa Profesa Mbarawa, amejitahidi sana kutembea kila sehemu. Naomba aongeze ukali, tunaibiwa sana kwenye miradi ya maji. Bwawa la Fili- Namanyere, nimezungumza kila mara hapa, hata ukienda lile bwawa halizidi shilingi milioni 300, Mkandarasi akapewa shilingi milioni 900.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hata ukifanya hesabu za haraka haraka, uchukue grader na excavator zifanye kazi kwa mwezi mmoja thamani yake ni shilingi milioni 78. Hakuweka cement, hajaweka nondo, kachimba tuta; tuta lenyewe mita 100. Kokoto zenyewe hakuweka chochote. Mawe trip 100. Nimepiga hesabu lile bwawa kwa hesabu zangu za haraka haraka iko hapa karatasi, haifiki shilingi milioni 110, yeye kachukua shilingi milioni 900.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa nashauri, kuna mabwawa hapa nikikusomea hapa, ni Nchi nzima. Mabwawa yaliyopo katika nchi hii, karibuni yote yana ufisadi ndani yake. Namwomba Mheshimiwa Profesa Mbarawa aunde Tume Maalum afuatilie bwawa moja hadi moja atagundua wizi wa hali ya juu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Rais anafoka. Siku anakwenda Mheshimiwa Rais ndio anakataa majengo, anakataa mabwawa, miradi ya maji anaikataa. Ndugu zangu, naomba Mawaziri mumsaidie kabla Mheshimiwa Waziri hajaja muanze kuwatumbua watu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nitakusomea idadi ya mabwawa hapa ya nchi nzima ambayo ukiyapitia yote yana ufisadi wa pesa. Yaani ni mengi, ukiyapitia utapata kujua hata kule kwako labda yapo hayo mabwawa. Ni mengi ajabu, yana ukakasi wa wizi, yana matatizo na kila kitu. Naomba Wizara ya Maji iyapitie kabla Mheshimiwa Rais hajaenda akapata matatizo. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna mabwawa ya idadi ambayo yameshajengwa Habia, Itimila, Kawa, Nkasi, Matwiga, Chunya, Mwanjoro kule Mkinga, Kilungadunga - Mkinga, Donda - Mkinga, Loliondo, Mafutela, Selewa -Kilindini na mabwawa kadhaa wa kadhaa. Ni hatari. Tunakusanya kodi kwa walala hoi lakini Wakandarasi wanakwenda kuchukua hela ambao siyo halali.
Mheshimiwa Mwenyekiti, akija Rais katika Wilaya ya Nkansi, nitamwomba hata kwa dakika tatu akaangalie bwawa ambalo wanapiga kelele la Mfili akalione kama thamani yake kweli ni shilingi milioni 900. Tumesikia wanakwenda Mawaziri kwenye bwawa, tunamwambia asilipwe hela zake shilingi milioni 300 mpaka wataalam waje kilichunguza hili bwawa lakini walimlipa. Kaenda Mheshimiwa Waziri Kakunda kaenda kusema hili bwawa halifiki shilingi milioni 300. Tupo na RAS pale, tunazuia asilipwe Mkandarasi lakini analipwa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mradi wa maji Kirando walithamini shilingi bilioni 7.4 na cheque imeandikwa Mkandarasi apewe shilingi milioni 800 juu ya meza tukazuia. Wataalam wamekwenda ku-check ule mradi wa mamji utaona ajabu, wamegundua kwamba ni shilingi bilioni 4.6 na Mkandarasi wamempa kwa shilingi bilioni 4.6. Tumekoa shilingi bilioni tatu.
Mheshimiwa Mweyekiti, sasa kama Namanyere ni mradi huu mmoja tu tumekuta tofauti ya shilingi bilioni tatu, miradi mingine ilikuaje katika nchi hii? Mheshimiwa Waziri, msaidieini Mheshimiwa Rais. Mheshimiwa Rais kila akienda, hotuba zake za Mikoa ya kusini huko nimezifuatilia, zote zina mtatizo ya miradi miradi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mfano ndege tu kupaka rangi. Wewe mwenyewe usingepaka rangi ndege. Walitaka kulipua shilingi milioni 300. Sasa kama mbele ya macho Jijini Dar es Salaam wanataka kulipua shilingi milioni 300, kule vijijini karibu na Zaire wanatulipua kiasi gani? Tunasema mpaka povu linatoka, lakini wanakaa maofisini wanaandika mikataba, Mawaziri wanasema hawawasikilizi. Mheshimiwa Prof. Mbarawa anasema mpaka povu linamtoka, Mdogo wangu Mheshimiwa Aweso amekuja kule amesema ufisadi umefanyika lakini hawachukuliwi hatua zozote, wamekaa wamestarehe, wanatuchezea akili tu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa ndugu zangu, tuonyeshe mfano. Tusisubiri mpaka Mheshimiwa Rais anakwenda kwenye miradi ndiyo anawatumbua majipu. Mawaziri fanyeni hiyo kazi. Haiwezekani sisi Wabunge kwa sababu ni wanasiasa tunaropoka, lakini ndugu zangu hesabu haidanganyi. Bei ya bomba inajulikana, bei ya kutengeneza barabara inajulikana, bei ya kila kitu inajulikana, lakini unakuta mikataba tunajiumiza wenyewe. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nchi yetu ni tajiri. Leo tungekuwa tuna uwezo wa kuzikopesha nchi za Ulaya kama Ureno, kama Spain, tuna uwezo wa kuzikopesha, lakini sisi leo ndiyo tunakopa. Ni aibu. Tuna kila kitu katika nchi hii. Tuna utajiri wa ajabu katika nchi hii. Ni sisi wenyewe tunajitafuna. Ni mikataba mibovu ndiyo inatumaliza katika nchi hii. Lazima tuiangalie mikataba. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, tungekuwa na mikataba halali leo nchi yetu ingekuwa na neema, ingeneemeka. Mheshimiwa Rais anafanya kazi mpaka anachoka, lakini wasaidizi ndugu zangu wamekaa maofisini, wanakula AC wanatuharibia nchi. Nimezungumza kila mara, mtu unamwona kabisa anaiba, muda wa mwezi mmoja ana jumba la ghorofa; miezi miwili ana magari matatu. Mshahara wake unafahamika; anatoa wapi hizo hela? Halafu TAKUKURU wanasema wanamchunguza, wanamchunguza kitu gani? Ushahidi upo. Hawa ni kuwatandika tu.
(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)
MWENYEKITI: Ahsante sana Mheshimiwa Keissy.
MHE. ALLY K. MOHAMED: Mheshimiwa Mwenyekiti, naunga mkono hoja. (Makofi)