Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 - Ofisi ya Waziri Mkuu

Hon. Abdallah Ally Mtolea

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Temeke

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 - Ofisi ya Waziri Mkuu

MHE. ABDALLAH A. MTOLEA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kunipa nafasi nami nichangie machache kwenye mjadala ulio mezani asubuhi ya leo. Kwanza nianze kwa kumshukuru Mwenyezi Mungu, mwingi wa rehema kwa kunijalia afya nzuri siku ya leo, lakini niendelee kumwomba anilinde kunipa afya njema mpaka siku nitakayopiga kura ya bajeti ili nami kwa mara ya kwanza niweze kuwatendea haki wananchi kwa kupiga kura ya ndiyo kwenye bajeti hii. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza niipongeze sana Serikali kwa namna ambavyo imemwaga miradi mingi Majimboni kwetu katika kuboresha huduma za jamii. Imeweka fedha nyingi sana kwenye miradi ya afya na huduma za afya kwa kweli zimeboreka kwa kiasi kikubwa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nakumbuka kabla ya Serikali ya Awamu ya Tano kuingia madarakani, ulikuwa ni utaratibu wa kawaida wamama wanapoenda kujifungua, kubeba vifaa vya kujifungulia, kubeba mabeseni na vitu vya namna hiyo, jambo ambalo kwa sasa limekuwa ni historia. Wamama wanakwenda kujifungua, wanapata huduma zote hospitalini na hawachajiwi. Jambo hili limekuwa ni la kihistoria na wananchi wa Temeke wanaishukuru sana Serikali ya Awamu ya Tano kwa namna ambavyo imejikita katika kuboresha huduma za jamii. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, siyo tu kwenye huduma za afya, lakini pili, kwenye uboreshaji wa miundombinu. Nikitolea mfano tu wa huko huko Jimboni kwangu Temeke, kuna ujenzi mkubwa wa miundombinu, achilia mbali daraja la juu (flyover) ambalo limerahisisha sasa foleni zilizokuwa zikiwakabili watu wakati wakwenda Airport, lakini barabara nyingine zinazoungana na zenyewe pia zinaendelea kujengwa. Wakandarasi wako site wanaboresha miundombinu. Tunaipongeza sana Serikali kwa jambo hili lakini Waziri Mkuu na Ofisi yake kwa namna ambavyo wanakuja kusimamia na kuhakikisha kwamba ujenzi na matumizi ya fedha hizi za Serikali unakuwa ni wenye tija. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia niipongeze sana Tume ya Uchaguzi kwa namna ambavyo wamekuwa wanafanya kazi zao vizuri. Tume ya Uchaguzi inafanya kazi zake vizuri na mfano mkubwa ni kwenye chaguzi hizi chache ambazo zimepita hivi karibuni ambavyo wamezisimamia vizuri. Sisi Wandengereko huwa tuna usemi wetu tunasema, “maiti ya Kimakonde haikosi mchawi.” Ni kwa maana pamoja na kazi nzuri mnayoifanya, bado wapo watu ambao wataendelea kuwakosoa. Wanaowakosoa kwa kusema kwamba Tume ya Uchaguzi inapendelea, ni hao hao ambao nanyi mliwahi kuwatangaza na leo ni Wabunge huku. Kwa hiyo, hayo…

MHE. MUSSA B. MBAROUK: Mheshimiwa Mwenyekiti, taarifa.

MWENYEKITI: Tusikie taarifa.

T A A R I F A

MHE. MUSSA B. MBAROUK: Mheshimiwa Mwenyekiti, mzungumzaji anayezungumza, mimi binafsi amenishtua kidogo aliposema maiti ya Mmakonde haikosi mchawi. Nataka ufafanuzi, atufafanulie tafsiri yake ni nini hapo? Ahsante.

MWENYEKITI: Hilo ni swali, mtaeleza huko nje. Endelea Mheshimiwa.

MHE. ABDALLAH A. MTOLEA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru. Sasa ombi langu kwa Tume ya Uchaguzi, nilikuwa nataka sasa iende mbali zaidi. kwa kuwa imefanikiwa katika usimamizi wa taratibu za uchaguzi, iende mbali kuhakikisha kwamba utekelezaji wa mambo ambayo viongozi waliochaguliwa unaendelezwa hata baada ya wao kumaliza muda wake. Kwa mfano, tunapopata viongozi mahiri kama Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli, ambaye anaanzisha vitu vingi vikubwa, tena vyenye tija kwa Taifa ambavyo vingine vitakuwa bado havijakamilika wakati muda wa miaka 10 unakwisha, ni vizuri Tume ya Uchaguzi ikaandaa mfumo ambapo atakayekuja sasa madarakani naye asianze na vitu vipya, aendeleze yaliyopo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, leo tunazungumzia kuweka Makao Makuu Dodoma. Mpango huu ni endelevu, nyumba na Ofisi za Serikali zinaendelea kujengwa, zipo zitakazokamilika na zipo ambazo zitakuwa hazijakamilika mpaka Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli anaondoka madarakani. Sasa tusipoweka mfumo mzuri kwamba anayekuja naye aendelee mle mle, maana yake anaweza akaja mwingine akaanzisha vitu vipya. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kweli tumeweka sheria ya kuifanya Dodoma kuwa Makao Makuu, lakini sheria zinabadilika, maana yake afadhali lingekuwa ni jambo la kikatiba, utaratibu wake kidogo ni mgumu, lakini sheria zinaweza zikaja amendments zikabadilisha tukarudi tena Dar es Salaam. Jambo hili litakuwa ni hasara kubwa kwa Taifa. Sasa ni vizuri mambo haya yakawekewa utaratibu mzuri.

MHE. FRANK G. MWAKAJOKA: Mheshimiwa Mwenyekiti, taarifa.

MWENYEKITI: Mheshimiwa Mtolea, taarifa.

T A A R I F A

MHE. FRANK G. MWAKAJOKA: Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kumpa taarifa Mheshimiwa Mtolea kwa ushauri ambao ametoa kwenye Tume ya Taifa ya Uchaguzi kwamba angependa sana kuwe na utaratibu ambao utawafanya viongozi ambao amesema mahiri baadaye na wao vitu ambavyo wamevianzisha ili viendelee. Akumbuke kwamba hata waliomtangulia Mheshimiwa Dkt. Magufuli viko walivyovianzisha naye aliviacha. Kwa mfano, miradi ya gesi ambayo Serikali ya nchi hii ilizunguka nchi nzima kuwaambia Watanzania kwamba sasa gesi ikishapatikana tutakuwa hatuna tena tatizo la umeme katika Taifa hili…

MWENYEKITI: Mheshimiwa Mwakajoka!

MHE. FRANK G. MWAKAJOKA: …lakini ameacha na sasa hivi tuna mradi wa Stiegler’s Gorge unaendelea.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante.

MWENYEKITI: Mheshimiwa Mtolea.

MHE. ABDALLAH A. MTOLEA: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba niipuuze hiyo taarifa kama ambavyo nampuuzia na yeye mwenyewe. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyetiki, ninachozungumza ni kwamba, tunahitaji mambo ya msingi, mambo makubwa ambayo yameanzishwa hivi sasa ambayo kila Mtanzania anayaona na anakubali kwamba yana tija kwa kizazi hiki na kizazi kijacho yaweze kuendelezwa. Yasiishie pale ambapo Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli atamaliza muda wake. Kama tunashindwa kumwongezea muda yeye aendelee, basi tuwe na mfumo ambayo Ofisi kwa maana ya Rais kama taasisi itaendeleza yale ambayo aliyaanzisha. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, huu si muda wa sisi kwenda mbele na kurudi nyuma tena, tumeshapiga mark time kwa muda mrefu. Sasa hivi tumepata mtu ambaye ametuonesha njia, ni vizuri tukaenda nae. Watu kama Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli hawazaliwi kila wakati, akipita huyu, inaweza kupita miaka 50 au miaka 100 tusipate mtu mwenye maono ya namna hii. Kwa hiyo ni vizuri tukaona kwamba, haya maono yake... (Makofi)

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)