Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 - Ofisi ya Waziri Mkuu

Hon. Zainab Mndolwa Amir

Sex

Female

Party

CUF

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 - Ofisi ya Waziri Mkuu

MHE. ZAINAB M. AMIRI: Mheshimiwa Mwenyekiti, awali ya yote nipongeze hotuba nzuri ya Waziri Mkuu, Mheshimiwa Majaliwa Kassim Majaliwa. Pia, nina mambo ambayo nataka kuishauri Serikali ambayo mengine ni kero kwa wananchi na yanahitaji kufanyiwa kazi ipasavyo na maoni mengine ni kuishauri Serikali ili kuweza kupiga hatua mbele katika kuijenga nchi yetu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, afya; Serikali imejitahidi kujenga hospitali, vituo vya afya na zahanati, maoni yangu nashauri Serikali iweke vifaa tiba katika vituo vya afya na hospitali ili kuweza kuondoa msongamano katika hospitali za rufaa. Katika Hospitali ya Rufaa Temeke, Dar es Salaam ina uchache wa wodi za wagonjwa na majengo mengi ni chakavu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali ijenge wodi za zamani maghorofa, ili kuweza kukidhi mahitaji ya idadi kubwa ya wagonjwa kwa sababu hospitali hii ya Temeke, hupokea wagonjwa kutoka wilaya za jirani za Mkoa wa Pwani kama vile Wilaya ya Mkuranga, pia Wilaya ya Kigamboni. Serikali iwapatie hospitali ya rufaa Temeke mashine ya kufulia mashuka ya wagonjwa, maana kwa sasa yanapelekwa katika hospitali ya Taifa Muhimbili kwa ajili ya kufuliwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia, katika hospitali za rufaa mfano Muhimbili, Mloganzila, Serikali ijenge maeneo maalum ambayo yatatumiwa na ndugu wa wagonjwa wakati wagonjwa wao wanasubiri, siyo wagonjwa wote wanandugu au jamaa katika Mkoa wa Dar es Salaam. Huduma ya kuhifadhi maiti iwe bure, maana mara nyingi tunaona inawakwaza wafiwa kwa kushindwa kulipia maiti zao na hatimaye Serikali inapewa lawama kuwa haina huruma na wananchi, ukizingatia wakati wa uhai wake marehemu alikuwa anachangia pato la Taifa kwa kulipa kodi kupitia huduma mbalimbali alizokuwa anazifanya, kama vile kununua mahitaji yake ya kila siku, kuna kodi za Serikali inachukua. Huduma hii ya kuhifadhi maiti iwe bure.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali ije na sheria ya kuongeza muda wa likizo ya uzazi kwa akinamama wanaojifungua watoto chini ya miezi tisa (njiti) na kwa akinamama waliojaliwa kujifungua watoto zaidi ya mmoja ili kuweza kuwapa muda wa kuwalea watoto wao, maana miezi mitatu wakati mwingine ni michache mno, ukilinganisha na mwanamke aliyejifungua mtoto mmoja na ambaye ametimiza miezi tisa tumboni.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa upande wa biashara na viwanda, nashauri Serikali itoe muda maalum grace period angalau wa miezi mitatu, kisha ndipo waanze kumkadiria mtu ambaye anataka kuanza kufanya biashara na siyo mfumo unaotumika sasa wa kulipa mapato kabla ya mwananchi kuanza biashara yake. Hili si jambo zuri kabisa. Kuna asilimia 15 ambayo wenye viwanda vinavyotumia sukari ya viwandani huilipa waingizapo sukari hiyo nchini, lakini wafanyabiashara hao wanaidai Serikali fedha nyingi sana na wamefanya taratibu zote zinazohitajika ili waweze kujereshewa fedha hizo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali iwalipe wenye viwanda hivyo ambavyo wanadai ili fedha hizo ziweze kuwasaidia kuendesha viwanda vyao, maana suala la kutolipwa kwa wakati kunaathiri uzalishaji katika viwanda vyao. Ni muhimu kwa kuelekea uchumi wa viwanda, kuwalipa kwa wakati na siyo kidogo kidogo kama ifuatavyo Serikali sasa hivi, walipe kwa mkupuo kama wao walivyokuwa wanalipwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika kuijenga nchi yetu ni muhimu Serikali itatue changamoto zote ambazo zipo ndani ya uwezo wake ili kuweza kufikia lengo la kuondoa umaskini kwa Watanzania.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante.