Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 - Ofisi ya Waziri Mkuu

Hon. Mahmoud Hassan Mgimwa

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Mufindi Kaskazini

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 - Ofisi ya Waziri Mkuu

MHE. MAHMOUD H. MGIMWA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nachukua fursa hii kumpongeza sana Mheshimiwa Waziri Mkuu kwa kazi nzuri ya kizalendo anayoifanya katika nchi yetu. Mchango wangu utajikita katika maeneo matatu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza ni afya. Jimbo la Mufindi Kaskazini lina Tarafa nne, lakini kwa masikitiko makubwa tuna kituo kimoja kinachofanya kazi cha Ifwagi. Nakupongeza wewe binafsi pamoja na Mheshimiwa Rais Dkt. John Pombe Magufuli kwa kutupatia shilingi milioni 400 kwa ajili ya Kituo cha Afya cha Ifwagi na sasa kiko katika hatua za mwisho, lakini Tarafa tatu zilizobaki hazina Kituo cha Afya. Naomba nichukue nafasi hii kuiomba Serikali itusaidie kupata Kituo cha Afya kimoja kwa kila Tarafa nasi wananchi tuko tayari kusaidia katika shughuli za maendeleo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pili ni miundombinu ya barabara. Kumekuwa na tatizo kubwa la miundombinu katika Jimbo la Mufindi Kaskazini. Barabara hazipitiki kabisa; Barabara ya Mtili – Ifwagi – Mdeburo – Ihenu – Mpanga – Tazara – Mrimba. Barabara ya Tambaranyimbo – Uyele – Ikwaha - Kwa Twanga haipitiki kabisa na TARURA ni tatizo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nakuomba sana kupitia Waziri mwenye dhamana ya TAMISEMI aingilie kati barabara ya Kinyanambo A – Isalavenu –Igombavanu, Sadani – Madibira - Rugisa ipo kwenye Ilani ya Uchaguzi ya CCM toka mwaka 2000/2005, 2005/2010, 2010/2015, 2015/2020 lakini haijajengwa hata kilometa moja ya lami. Ni vyema sasa Serikali ikasema ili tuweze kuwaambia wananchi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, la tatu ni kuhusu miundombinu ya maji. Ni vyema sasa Serikali ikakubaliana na Wabunge kwa kuingiza tozo ya shilingi 50 ambayo sisi tuna uhakika ikiongezwa itapunguza kwa kiasi kikubwa tatizo la maji hapa nchini.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naunga mkono hoja.