Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Itilima
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
1
Ministries
nil
MHE. NJALU D. SILANGA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Kwanza nianze kumshukuru Waziri wa Viwanda na Biashara kwa hotuba yake nzuri ambayo imeelekeza changamoto za Watanzania. Nitaanza na ku-declare interest kwa maana ya kwamba ni mmiliki wa kiwanda.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tunapozungumzia viwanda tunazungumzia viwanda vya aina gani? Sisi wakulima wa pamba tunakotoka tulikuwa na viwanda 77 leo vimebaki 40 na hivi 40 na vyenyewe vipo katika hali tete. Nini mpango wa Serikali kuvisaidia viwanda hivi ili viweze kufanya kazi? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ukizungumza na ukifuatilia suala la viwanda kwanza malighafi yenyewe haipo ni kwa sababu Serikali haijaweka kipaumbele kwa mazao yanayozalishwa hapa nchini ili yaweze kuwa na bei kubwa. Kwa mfano, pale Morogoro tunacho Kiwanda cha Ngozi baada ya Serikali kuzuia ngozi zetu zisisafirishwe bei zimeshuka. Leo bei ya kilo moja ya ngozi ya ng‟ombe ni shilingi 400 lakini enzi zile wakati wanasafirisha ilikuwa ni shilingi 1,500, ya mbuzi ilikuwa shilingi 1,000, ya kondoo ilikuwa shilingi 800, leo unazungumzia ya kondoo shilingi 100 kwa kilo na ya mbuzi unazungumzia shilingi 200, kwa jinsi hii tunalindaje viwanda vyetu vya ndani? Ifike mahali sasa Serikali ijaribu kuangalia kwa undani na kwa umakini zaidi ili kuhakikisha mali tunayoizalisha hapa nchini inakuwa na viwanda vya kuzalisha vizuri zaidi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile ione ni jinsi gani ya kuongeza bei, hili jambo kwa kweli linanipa taabu. Unakuta mazao yetu ya ndani kodi inaongezwa, mfano kama pamba. Mashudu yana kodi, mafuta yana kodi lakini mali inayotoka nje inakuwa haina kodi, unategemea hii mali itapanda kwa utaratibu upi? Ukizungumzia zao la pamba, zao la pamba linajumuisha vitu vingi, utachukua mapumba yale makapi, utachukua mbegu zake utauza lakini kwa hali iliyopo ukigusa kila kitu kina kodi kwa sababu sisi soko la nje hatuli-control hatuwezi kuongeza bei na mkulima bei yake ikiongezeka ni sehemu ya kichecheo kwa wakulima kuweza kuzalisha kwa mwaka unaofuata. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, taarifa ya Wizara ya Kilimo imezungumza, kwa mwaka 2004 nchi ilizalisha robota 700,000 lakini leo tunazungumzia uzalishaji wa tani 150,000, ni tayari nchi imeingia hasara kwa aina gani? Tumekosa dola lakini vilevile tumekosa ajira kwa vijana wetu. Mimi niiombe sana Serikali, Waziri atenge muda wa kukutana na wenye viwanda hawa ili aweze kuzungumza nao wamwambie ni changamoto za aina gani wanazokabiliana nazo. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, haiwezekani nchi inazungumza kila siku masuala ya viwanda lakini bado kuna watu ambao wana viwanda lakini wameshindwa kuviendesha kwa sababu ya mambo mengi. Tuna kiwanda pale Arusha kipya na kizuri kabisa lakini kimeshindwa kufanya kazi. Hata huyu Mchina ambaye yuko pale Shinyanga amefungua Kiwanda cha Nyuzi pamoja na Kiwanda cha Oil Mill haviwezi kufanya kazi kwa sababu ya malighafi na gharama inakuwa kubwa. Kwa hiyo, ifike mahali tuangalie ni jinsi gani tunataka kuwasaidia Watanzania lakini tuangalie ni jinsi gani tunataka tusimamie mazao yetu ya ndani ili kuyaongezea thamani ili wakulima wetu waweze kupata bei zilizokuwa nzuri.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ni mambo mengi ambayo yanasababisha tushindwe kusonga mbele. Ukiangalia mfano mwaka huu tumekosa pamba na mtu anayehusika na viwanda anapaswa sana kusimama kwa sababu ni sehemu yake ili viwanda vyake viweze kufanya kazi. Mwaka huu tuna maeneo mengi ambayo yamesababishiwa hasara na baadhi ya wataalam wa TPRI kwa sababu ya kuleta dawa mabovu hivyo hatuna pamba ya kutosha. Hili jambo lazima Waziri wa Viwanda aliangalie kwa umakini zaidi na kuhakikisha wanakuwa wamoja ili wasukume gurudumu la maendeleo kuhakikisha nchi yetu tunaipeleka mahali tunakokusudia. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, tuna changamoto nyingine kwenye suala la viwanda. Viwanda vyetu lazima tukubali, kwanza suala la umeme bado halijakaa vizuri, lazima ongezeko la umeme wa kutosha liwepo. Kiwanda unakiendesha ndani ya miezi miwili, lakini ndani ya miezi hiyo miwili utalipa miezi mitatu inayofuata, kama ni bili ya shilingi milioni 100 utalipa miezi mitatu mfululizo, tayari pale yule mwenye kiwanda hawezi kuendelea atasimama tu hivyo hivyo na mwisho wa siku nchi yetu itaingia kwenye matatizo makubwa sana.
Niiombe sana Wizara inayohusiana na jambo hili ilishughulikie kwa umakini zaidi na kuona jinsi gani sasa tunasonga mbele na kauli mbiu ya Mheshimiwa Rais inayosisitizia suala la viwanda. Viwanda vina changamoto na lazima Mheshimiwa Waziri aingie ndani zaidi, ajifunze zaidi najua ni mtaalam na jinsi anavyojibu yuko shapu kama Mbunge wa Kishapu akiweka mambo yake vizuri tunaweza tukapiga hatua kubwa sana lakini bila kufanya hivyo tutazungmza hapa miaka mitano itaisha na viwanda havitaenda ni kwa sababu mambo hayako wazi tunaelewa kabisa. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, wenzetu walioendelea, kuna nchi kama Bangladesh, ina sehemu tu ya viwanda, kiwanda kimoja kina wafanyakazi 25,000, kila kitu kipo na masaa yote kinafanya kazi lakini sisi Tanzania hapa hatujajipanga vizuri. Hata hivyo, kwa kasi hii ya Awamu ya Tano naamini imejiwekea utaratibu mzuri. Niwaombe sana Waziri wa Kiwanda pamoja na Waziri wa Nishati na Madini muweke kasi kwenye mambo ya umeme kwa sababu viwanda vyetu vina fail, vinaunguza vitu kutokana na mambo mengi. Yote haya tukiyazingatia na kuyachukulia maanani tutapiga hatua na nchi yetu itabadilika. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ni mambo magumu sana ambayo tunayaona lakini mambo mepesi sana tukishirikiana na wananchi wetu, tunavyo viwanda vya SIDO. Mfano mimi kwenye Jimbo langu pale Luguru, maana Mwenyekiti wewe ni Mtemi kule, kuna Kiwanda cha SIDO kipo siku nyingi tu. Kile tayari kikitengenezewa utaratibu kinafanya kazi maana majengo tunayo zile teknolojia zipo zinabadilika kila siku tu ni kwenda kutoa zilizokuwepo unaweka mitambo mingine kazi inaendelea, lakini bado sasa tunazunguka na tunazungumza sana. Kama tunataka vijana wawe na ajira ni pamoja na vitu kama hivi tukiviwekea kipaumbele tunaweza tukapiga hatua na nchi yetu tukaipelekea pale panapokusudiwa. (Makofi)
Suala lingine ni alizeti. Sasa hivi pamba inaenda inashuka lakini alizeti sasa nayo imeingia kwenye soko. Nimuombe Waziri wa Viwanda ajaribu kuangalia na kutoa ushauri kwenye Wizara ya Kilimo kwa sababu ni wamoja wanaweza wakaungana wakafanya kazi ya pamoja ili kusudi kuhakikisha Taifa letu sasa linapiga hatua. Kwenye alizeti, niishauri Serikali tuna mifumo kwenye nchi hii mingi sana, mkiingiza bodi na kadhalika tayari lile soko litashuka. Leo mwenzangu wa Singida amezungumzia ni walimaji wazuri sana ni kwa sababu hakuna bodi pale ukiingiza tu bodi lazima patakuwa na tatizo, itaanza kushuka na kadhalika. Tuyaangalie sana hizi bodi wakati mwingine yanaliingiza Taifa kwenye matatizo na migongano isiyokuwa na maana.
Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema haya naunga mkono hoja kwa asilimia mia moja, ahsante sana.