Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Kibaha Vijijini
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
0
Ministries
nil
MHE. HAMOUD A. JUMAA: Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kuchukua fursa hii kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa kuniwezesha kufika mahali hapa nami kuchangia hoja hii muhimu iliyopo mbele yetu. Vilevile nichukue fursa hii kumpongeza Mheshimiwa Waziri Mkuu kwa utendaji kazi mzuri katika kuisimamia Serikali.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hotuba hii ya Ofisi ya Waziri Mkuu inatuonyesha mapitio na mwelekeo wa kazi za Serikali na Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Fedha ya Ofisi ya Waziri Mkuu na Ofisi ya Bunge kwa mwaka 2019/2020. Hotuba hii inakwenda kutekeleza Ilani ya Uchaguzi ya Chama cha Mapinduzi kama ilivyoanishwa hasa katika kuleta maendeleo kwa wananchi na kukamilisha miradi mbalimbali ya kimaendeleo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nijikite katika kuchangia hotuba hii kwa kuanza na kuipongeza Serikali ya Chama cha Mapinduzi ikiongozwa na Mheshimiwa Rais wetu, Dkt. John Pombe Mafuguli, kwa kazi nzuri zilizofanywa na zinazoendelea kutekelezwa. Mapendekezo ya bajeti ya Serikali ya mwaka 2019/2020 yamezingatia Mpango wa Maendeleo wa Taifa 2019/2020 ambao ni wa nne katika mfululizo wa mipango ya kila mwaka ya kutekeleza Mpango wa Taifa wa Miaka Mitano 2016/2017 – 2020/2021. Dhima ya Mpango huo ni kujenga uchumi wa viwanda ili kuchochea mageuzi ya uchumi na maendeleo ya watu wa Taifa hili. Aidha, mpango huu unatekelezwa sanjari na maelekezo ya Ilani ya Uchaguzi ya Chama cha Mapinduzi (CCM) ya mwaka 2015 – 2020.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ahadi za Mheshimiwa Rais wakati wa kampeni za Uchaguzi Mkuu wa mwaka wa 2015 na zile alizozitoa katika hotuba yake ya kuzindua Bunge hili mwezi Novemba, 2015. Naipongeza Serikali kwa kuendelea kuona vipaumbele vya Mpango wa mwaka 2019/2020 ni kuendelea kuimarisha msingi wa uchumi wa viwanda, kufungamanisha ukuaji wa uchumi na maendeleo ya watu, kuendelea kuboresha mazingira wezeshi kwa uendeshaji wa biashara na uwekezaji na kuimarisha usimamizi wa utekelezaji wa mpango.
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika Mpango wa Maendeleo na Bajeti ya mwaka 2019/2020, Serikali imeendelea kutekeleza Mradi wa Umeme wa Maji wa Mto Rufiji (Stiegler’s Gorge). Ni jambo kubwa sana na la kupongezwa na si kubezwa kwani tumeshuhudia baadhi ya wapinga maendeleo wakija na hoja mbalimbali za kupinga mpango huu. Aidha, naipongeza Serikali kwa ujenzi wa miundombinu ya reli ya kisasa (SGR), barabara pamoja na kukuza sekta ya anga. Utekelezaji wa miradi hiyo ya miundombinu wezeshi ya kiuchumi una lengo la kufungamanisha ukuaji wa sekta hizo na sekta nyingine hususan za biashara, kilimo na utalii.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kama nilivyokwishatangulia kusema hapo awali kwa kuipongeza Serikali katika miradi yake mbalimbali ya miundombinu na mingineyo, lakini kumekuwa na changamoto mbalimbali katika miradi hii ambazo mara zote Serikali imezichukulia kama fursa katika kuzitatua. Mradi wa ujenzi wa barabara njia nne (4) ambao kwa hivi sasa unaendelea ni mradi utakaoleta mapinduzi makubwa sana ila napenda kuishauri Serikali mradi huu ujengwe na kufika hadi Ruvu na kuendelea mpaka Mizani Vigwaza. Kwa kufanya hivyo kutasaidia sana kuleta mafanikio makubwa kwa eneo husika ambalo litaongezwa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tuna Mamlaka za Mji lakini kwa muda mrefu imekosa Mkurugenzi. Naomba katika mwaka huu wa fedha basi Serikali yangu sikivu iweze kutatua changamoto hii kwani kukosekana kwa Mkurugenzi kunazorotesha baadhi ya shughuli za Mamlaka hasa katika kuhudumia wananchi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, aidha, napenda kuishukuru Serikali kwa kutupatia fedha kiasi cha Sh.2,745,425,524 kwa ajili ya ujenzi wa Jengo la Ofisi ya Halmashauri. Jengo hili liko katika hatua za mwisho kumalizika. Jengo hili litasaidia sana kupunguza changamoto iliyokuwa inatukabili ya kufuata huduma mbali.
Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile nitoe shukrani zangu za dhati kwa Waziri Mkuu, Mheshimiwa Kassim Majaliwa kwa kutoa mchango wake kiasi cha Sh.1,500,000 aliyotupatia kuchangia ujenzi wa uzio wa Kituo chetu cha Afya Mlandizi. Tunamshukuru sana.
Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kuipongeza Serikali ya Awamu ya Tano kwa kuwa na dhamira ya kujenga uchumi wa viwanda sambasamba na kuhakikisha upatikanaji wa nishati ya umeme wa kutosha na wa uhakika na nafuu. Kwa kutambua hilo, Serikali yetu inaendelea kutekeleza miradi mikubwa ya uzalishaji wa umeme yenye lengo la kuhakikisha Tanzania inakuwa nchi ya uchumi wa kati unaochochewa na ukuaji wa viwanda ifikapo mwaka 2025, hizi ni hatua nzuri na zenye mlengo chanya.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hata hivyo, hatua kubwa ya uwekaji saini mkataba wa ujenzi wa Mradi wa Bwawa la Kuzalisha Umeme wa MW 2,100 kati ya Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) na Kampuni ya JV Arab Contractors & Elsewedy Electric ya Misri ni hatua nzuri na ya kimaendeleo. Mradi huo unaotarajiwa kukamilika 2021/2022 utawezesha ujenzi wa uchumi wa viwanda kwa kuhakikisha upatikanaji wa umeme tena wa bei nafuu na hivyo kukamilisha kivitendo dhana nzima ya mabadiliko na kipaumbele cha kuifanya Tanzania ya viwanda, kwani nishati ya umeme ndio chachu ya kuvutia uwekezaji.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa taarifa tu katika sekta hii ya nishati hadi kufikia mwishoni wa Februari, 2019 uwezo wa jumla wa mitambo ya kuzalisha umeme nchini umeongezeka kutoka MW 1,205 mwaka 2015 hadi kufikia MW 1,614 mwaka 2019. Ongezeko hilo limepelekea kuwa na umeme wa ziada wa wastani wa zaidi ya MW 300 ambao utatuwezesha sasa nchi kama nchi kuwa na uhakika wa umeme.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hatua ya Serikali ya kutekeleza kwa mafanikio makubwa Mpango wa Usambazaji wa Umeme Vijijini umekuwa wa mafanikio makubwa sana hasa kwa sisi tunaotoka maeneo ya vijijini kwani kwetu tatizo la ukosefu wa umeme lilikuwa ni changamoto kubwa sana. Kwa ujumla katika mwaka 2018/2019, vijiji 1,782 vimeunganishwa na umeme. Aidha, tangu kuanza kwa usambazaji wa umeme vijijini, tayari vijiji 5,746 vimeunganishwa umeme kati ya vijiji 12,268 vilivyopo nchini, sawa na takribani asilimia 47 ya vijiji vyote. Nalisema hili pasipo shaka yoyote kwani katika vijiji hivyo pia vipo vya Jimboni kwangu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naunga mkono hoja.