Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Nkasi Kusini
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
0
Ministries
nil
MHE. DESDERIUS J. MIPATA: Mheshimiwa Mwenyekiti, naunga mkono hoja. Nampongeza Waziri Mkuu na Mawaziri walioko chini yake.
Mheshimiwa Mwenyekiti, napongeza kazi nzuri zinazotekelezwa na Serikali yetu ya Awamu ya Tano. Naridhishwa sana namna miradi mingi ya kipaumbele kwa Taifa inavyotekelezwa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi ni Mjumbe wa Kamati ya PIC, tumeweza kutembelea miradi mingi inayotekelezwa kwa kipindi hiki. Miradi hii ni pamoja na SGR ambao ni mradi wa ujenzi wa reli kwa kiwango cha kimataifa. Kazi inaenda vizuri sana na ujenzi unaenda kwa kasi na naamini ifikapo Novemba, 2019 huduma ya usafiri itawezekana kuanza kupatikana kwani hadi Morogoro kazi ni nzuri kabisa (Dar – Morogoro). Nampongeza Rais wetu na watendaji wote wakiongozwa na Mheshimiwa Waziri Mkuu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mradi mwingine ni ujenzi wa Kituo cha Kufua Umeme cha Kinyerezi I and II. Tumeweza kuona vituo vyote na kuona kiasi cha umeme kinachopatikana katika maeneo yote mawili, ni kazi kubwa imefanyika. Tumepata maelezo kuwa kwa sasa MW 1,650 zinapatikana kiasi hiki kinatosheleza mahitaji ya nchi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile kuna utaratibu wa ujenzi wa Mradi wa Kufua Umeme wa Stigler’s Gorge ambapo tutaweza kupata MW 2,100. Kiasi hiki ni kikubwa kuliko hata kiasi cha umeme tulichoweza kufanikiwa kupata tangu tupate uhuru. Kazi hii nayo imeanza katika hatua ya awali, inatia moyo na inaonyesha Mheshimiwa Rais alivyo mtu wa kuthubutu na sina shaka tutafanikiwa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mradi mwingine ni ununuzi wa ndege na ujenzi wa viwanja vya ndege nchini. Nampongeza sana Mheshimiwa Rais adumu na Mungu ampe afya atimize malengo yake ambayo yamepokelewa vizuri sana na Watanzania wote.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mwingine ni miradi ya ujenzi wa vituo vya afya, hospitali za Wilaya na Mikoa. Hizi ni juhudi kubwa kabisa, naipongeza sana Serikali.
Mheshimiwa Mwenyekiti, baada kusema hayo, naomba nichangie mambo ya jimboni kwangu. Naomba Serikali inipe Kituo cha Afya katika Kata za Ninde, Kijiji cha Ninde. Wananchi wamejenga kwa nguvu zao jengo la vyumba 10, naomba tuwaunge mkono.
Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile naomba Kituo cha Afya katika Kata ya Kala. Kata hii iko umbali wa zaidi ya kilometa 150 toka Makao Makuu ya Wilaya. Ni muhimu sana wapatiwe kituo cha afya.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba Vijiji vya Kasapa King’ombe, Mlambo Ng’undwe na Mlalambo mgogoro wao wa mpaka na Lwanfi Game Reserve utatuliwe. Naomba utatuliwe ili wananchi waweze kuishi kwa amani na kuzalisha uchumi kwa manufaa yao na Taifa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna mgogoro wa Shamba la Milundikwa JKT na vijiji vinavyozunguka vya Kasu, Milundikwa, Kisula na Malongwe. Nashauri wananchi waongezewe ardhi ya kulima ili wafanye kazi za kujiletea maendeleo yao na Taifa kwa ujumla.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba vijiji vya Katani, Malongwe, Sintali, Nkana Kasapa na Mkomanchindo viwe vya mwanzo mwanzo kupata umeme ili kuweka vizuri mazingira ya kisiasa na maendeleo jimboni. Naomba umeme uende katika vijiji hivyo kwa awamu hii ya tatu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba Shule ya Sekondari ya Kala miundombinu yake ya nyumba za walimu itazamwe. Pia mabweni ya watoto wa kike hakuna na iko maeneo ya mwambao ambako mwamko wa elimu bado ni duni.
Mheshimiwa Mwenyekiti, barabara ya Namanyere - Ninde naomba ikamilishwe. Daraja la Kizumbi, Kata ya Kizumbi lijengwe kwani maombi yalishaletwa kwa maombi maalum lakini ni muda mrefu halipitiki.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba Kata ya Kala wapate kituo cha Afya. Wananchi wako tayari kutoa nguvu zao kushiriki katika ujenzi huo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, wananchi wa Kata ya Sintali pia hawana maji katika vijiji karibu vyote vinne. Naomba utafiti ufanyike kuona chanzo kizuri cha kusaidia wananchi hawa ambao vijiji vyao viko karibu karibu yaani Sintali, Nkana na Mkomanchindo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mwisho nashauri katika suala la kilimo Serikali ione namna ya kuendelea kutoa ruzuku kwa wakulima wa chini bila hivyo hali inaendelea kuwa mbaya sana katika uzalishaji na kumudu maisha kwa wakulima hawa. Pembejeo zitolewa hata kwa watu wachache.
Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile masoko ya mazao ya wakulima hasa mahindi Mkoa wa Rukwa na mikoa yote inayolima zao hilo yatiliwe maanani vinginevyo wakulima watakata tamaa. Naiomba Serikali yangu ya Chama cha Mapinduzi ilete mageuzi kwenye kilimo kama inavyofanya katika maeneo ya miundombinu mbalimbali kama ujenzi wa SGR, ujenzi wa barabara, viwanja vya ndege, afya na elimu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naona kama Mheshimiwa Magufuli ni zawadi kwa Watanzania toka kwa Mungu. Ana maono na uthubutu na kweli anatatua yale yote yaliyoonekana kushindikana. Kama vile madawa ya kulevya; uzembe wa kazi Serikalini; wizi wa mali ya umma; urasimu na kuchelewesha maamuzi na uonezi hasa kwa watu wa chini. Mungu amzidishie aweze kufikia malengo yake kwa Watanzania.