Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 - Ofisi ya Waziri Mkuu

Hon. Omari Mohamed Kigua

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Kilindi

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 - Ofisi ya Waziri Mkuu

MHE. OMARI M. KIGUA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nichukue fursa hii kumpongeza Mheshimiwa Waziri Mkuu pamoja na Mawaziri wake wawili Mheshimiwa Jenista Mhagama na Mheshimiwa Kairuki pamoja na Naibu Mawaziri wawili katika ofisi hii kwa hotuba nzuri.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nitaomba kuchangia eneo la sekta ya uwekezaji ambalo ni sehemu muhimu kwa mustakabali wa maendeleo ya nchi yetu. Kitengo cha Uwekezaji ni muda mrefu kimekuwa kikilalamikiwa sana kwa kuchelewesha uwekezaji kwa wawekezaji wa ndani na nje na kubwa zaidi ni urasimu kwa watendaji kutochukua maamuzi kwa wakati.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kubwa ambalo napenda kumsahuri Waziri mwenye dhamana kwenye Ofisi hii kwanza ni kwa watendaji kubadilika kifikra, wasifanye kazi kwa mazoea. Hili litawezekana kwa kutambua umuhimu wa ofisi kwamba ni nyeti na ikitekeleza majukumu yake ipasavyo nchini hii itasongo mbele katika kuvutia wawekezaji.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna umuhimu wa kutazama na kupitia kuona kama sheria za uwekezaji zilizopo kama zinachangia katika kurudisha nyuma uwekezaji. Kama hivyo ndivyo ni vema zikaletwa hapa Bungeni tuzifanyie mabadiliko lakini hili litawezekana kama tathmini itafanywa na Ofisi hii.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tumeshuhudia Waheshimiwa Wabunge wakichangia humu kwamba wawekezaji wengi wanakimbilia nchi jirani wakati fursa nyingi zipo hapa nchini. Naomba Waziri mwenye dhamana aliambie Bunge sababu hasa ni nini? Nashauri kiwepo kitengo katika Ofisi ya Waziri Mkuu cha kufanya tathmini na stadi ya mara kwa mara labda kila baada ya miezi sita ambayo itakuwa inatoa tathmini ya mafanikio, changamoto na wapi uwekezaji umekua. Hii itasaidia kwa kiasi kikubwa kuleta ufanisi wa kitengo hiki.

Mheshimiwa Mwenyekiti, eneo lingine ambalo napenda kutoa mawazo yangu ni ajira hususani kwa vijana. Idadi ya vijana wasiokuwa na ajira inazidi kuongezeka. Kwa sasa tuna vyuo vingi na vinazalisha vijana wengi wa kada mbalimbali lakini pia wapo ambao hawajabahatika kuendelea na masuala ya elimu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nashauri elimu ya ufundi hususani ya VETA ipewe kipaumbele, kila wilaya lazima iwe na chuo cha VETA. Hii itatoa fursa kwa vijana wetu kujifunza stadi mbalimbali na itapunguza changamoto ya ajira. Pia ni vema ofisi hii ikawa na utaratibu wa kuhakikisha vijana wanapata elimu ya ujasiriamali na iratibu na upatikanaji wa mikopo midogo midogo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, asilimia 4 ambayo inatozwa na Halmashauri zetu kutokana na mapato ya ndani kamwe haiwezi kusaidia vijana kujiwezesha kuwa na miradi kwa sababu Halmashauri nyingi uwezo wa mapato umepungua na hata zile zenye uwezo huo watendaji wengi hawatimizi takwa hili la kisheria. Tusipokuwa makini kulitazama kundi hili muhimu la vijana kwa jicho la tatu hakika siku za usoni Serikali itakuwa katika wakati mgumu wa kutatua changamoto za vijana.