Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 - Ofisi ya Waziri Mkuu

Hon. Fatma Hassan Toufiq

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

2

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 - Ofisi ya Waziri Mkuu

MHE. FATMA H. TOUFIQ: Mheshimiwa Mwenyekiti, nampongeza Mheshimiwa Kassim M. Majaliwa. Waziri wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa hotuba iliyosheheni taarifa muhimu za utekelezaji kwa vitendo Ilani ya Uchaguzi na pia kuandaa bajeti yenye dhamira ya dhati ya kuleta maendeleo ya nchi yetu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nawapongeza Mawaziri wote, Naibu Mawaziri pamoja na watendaji wote walioshiriki kuandaa taarifa ya bajeti hii. Wananchi wamejenga maboma mengi ya zahanati na wamefikia hatua mbalimbali na wamekuwa wakihitaji msaada kutoka Serikalini ili kukamilisha maboma hayo kwa ajili ya kupunguza mwendo kwenda kupata huduma za afya. Natoa rai katika bajeti hii Serikali iweke fedha kwa ajili ya kukamilisha baadhi ya zahanati. Aidha, nashauri uwepo mpango maalum wa Serikali na kujiwekea ratiba maalum ili kukamilisha maboma haya ya wananchi hatua kwa hatua.

Mheshimiwa Mwenyekiti, miradi mingi ya visima vya maji imekwama kutokana na miundombinu. Visima vimechimbwa lakini baadhi ya maeneo ya Mkoa wa Dodoma pump na mitambo hakuna. Ni budi Serikali ikayabaini maeneo yote nchini yenye kadhia hii na kuona jinsi ya kurekebisha ili wananchi waweze kufaidika na upatikanaji maji.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hivi karibuni tumepitisha sheria inayoitaka kila Halmashauri itoe asilimia 10 ya mapato kwa makundi ya wanawake, vijana na walemavu. Nashauri Serikali ifanye ufuatiliaji wa karibu kuhakikisha kila Halmashauri inatekeleza pia urejeshwaji wa pesa hizo. Aidha, ifanyike tathmini mwishoni mwa mwaka wa fedha kuona wananchi waliofaidika wamebadilika vipi kupambana na umaskini.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ni budi uwekwe utaratibu wa utoaji taarifa kuhusiana na asilimia 10, ikiwezekana kila Halmashauri iwe inatoa taarifa ya maendeleo ya utoaji na urejeshaji fedha kila baada ya miezi sita au jinsi Serikali itakavyoona inafaa. Hali kadhalika Maendeleo ya Jamii wapitie Halmashauri zote zisizofanya vizuri ili zichukuliwe hatua.

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika michezo kuanzia ukurasa wa 71-73 imezungumzia soka, je, timu za soka la wanawake hawakushiriki katika michezo? Michezo ya mpira wa pete na mingine inayochezwa na wanawake nayo ipewe kipaumbele ili kuonyesha pia wanawake wanashiriki soka na michezo mbalimbali.

Mheshimiwa Mwenyekiti, napongeza uwepo wa ziada ya chakula ya tani milioni 3.32 za mazao yetu. Aidha, kipindi hiki mvua si nzuri na ukame umeathiri maeneo mengi, hivyo suala kilimo cha umwagiliaji bado inabidi Serikali ilisisitize kwani kutegemea mvua bado si salama kwa usalama wa chakula.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante, naunga mkono hoja.