Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 - Ofisi ya Waziri Mkuu

Hon. Hasna Sudi Katunda Mwilima

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Kigoma Kusini

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 - Ofisi ya Waziri Mkuu

MHE. HASNA S. K. MWILIMA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nianze kwa kumpongeza Mheshimiwa Waziri Mkuu kwa kazi kubwa ya kusimamia utekelezaji wa Ilani yetu ya CCM ya 2015-2020, sambamba na Waheshimiwa Mawaziri Mheshimiwa Jenista na Manaibu wote.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nijielekeze kwanza kwenye hoja ya uwekezaji. Tunatambua Mheshimiwa Waziri Mkuu ameanzisha kampeni ya kufufua zao la michikichi katika Mkoa wa Kigoma, Tabora, Katavi, Rukwa Mbeya Wilaya ya Kyela. Zao hili la michikichi asili yake hapa Tanzania ni Mkoa wa Kigoma na sote tunatambua kuwa zao hili ndilo linalowapa kipato wananchi wa Kigoma likifuatiwa na zao la muhogo na maharage.

Mheshimiwa Mwenyekiti, miaka ya nyuma nchi ya Malaysia walikuja kuchukua miche na kupeleka kwao, leo hii Malaysia ndiyo nchi inayoongoza duniani kwa uzalishaji wa palm oil. Kwa kuwa Mheshimiwa Waziri Mkuu ametoa tamko la kuwa Chuo cha Kihinga kuwa kituo cha uzalishaji mbegu au miche, tunaomba bajeti itengwe kwa ajili ya uzalishaji na ununuzi wa miche ili basi Serikali iweze kuwapa wananchi wake ili dhamira ya kuwa na viwanda vya mafuta ya mawese iweze kutimia.

Mheshimiwa Mwenyekiti, la pili, kwa kuwa Mheshimiwa Waziri Mkuu alikutana na wadau mbalimbali tarehe 28 Julai, 2018 akaja na Bank ya TIB na TADB, tuiombe Serikali masharti yawe mepesi ili wakulima wengi wa zao la michikichi wapewe mikopo kununua miche ya michikichi. Tumuombe pia Mheshimiwa Waziri Mkuu atuletee wawekezaji wa kununua mazao hayo na kuanzisha viwanda vya mafuta haya ya mawese ili kununua zao hili la michikichi. Nimezungumzia sana zao la michikichi kwa sababu ni zao muhimu sana Tanzania na ulimwenguni kote wanatumia palm oil.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nizungumzie zao la muhogo. Tunatambua hivi karibuni Serikali ilipokea wawekezaji wanaotoka China wanaohitaji kununua mihogo tani kwa tani kupitia Wizara ya Kilimo. Tunacho Chuo cha Naliendelea kina mbegu nzuri sana za mihogo, swali langu wananchi wanaotoka kwenye mikoa inayolima zao hili wanapataje mbegu ili wawekezaji waweze kununua mihogo yenye tija?

Mheshimiwa Mwenyekiti, sambamba na hili, Wizara ya Uwekezaji isimamie uanzishwaji wa viwanda vya kutengeneza karatasi na mifuko ya karatasi ili tuondokane na uharibifu wa mifuko ya plastic inayotuchafulia mazingira yetu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nizungumzie uwekezaji wa kwenye sekta ya uvuvi. Sekta hii tumeiacha sana lakini kama tutaiangalia vizuri inaweza kutuingizia pato kubwa katika taifa letu. Mfano tunaweza kununua meli za uvuvi katika maziwa yetu ya Victoria, Nyasa, Tanganyika na kadhalika. Kwenye bajeti ya 2018/2019, Mheshimiwa Waziri wa Fedha alionyesha kuweka fedha za ununuzi wa meli za uvuvi, hata bajeti ya mwaka huu 2019/2020 kwenye mpango wa maendeleo tumeendelea kuonyesha kuwa Serikali imepanga kununua meli hizo za uvuvi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, siku za nyuma Mkoa wa Kigoma tuliwahi kupata mwekezaji toka Ugiriki alikuwa na meli ya uvuvi iliyoitwa YOROGWE. Meli hii ilikuwa inavua samaki wengi sana. Kigoma watu wengi wanajua tuna samaki aitwae mgebuka lakini tunao samaki aina nyingi kwa utafiti uliofanywa na Wachina wakagundua tunao aina za samaki 250. Kwa mfano, ninaowajua mimi na kuwala ni mgebuka, kohe, ngenge, sangara, monzi, singa, karongwe, mbaga, mneke, kabare, mbisu, mrombo ndubu na kadhalika. Natambua sekta ya uvuvi, mifugo na kilimo inachangia zaidi ya asilimia 40 ya pato la Taifa. Hivyo ni wakati muafaka sasa Serikali yetu ikajikita kwenye sekta ya uvuvi, kilimo na mifugo ili pato letu la Taifa likue zaidi kwa sekta hizi tatu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya mchango wangu huo, naomba niendelee kumpongeza Mheshimiwa Waziri Mkuu kwa kazi kubwa anayofanya kwenye Taifa hili. Sote tunamuona jinsi anavyofanya ziara mikoani na ndani ya wilaya zote kufuatilia utekelezaji wa Ilani ya CCM ya 2015- 2020 inatekelezwa ipasavyo. Nimpongeze Waziri, Mheshimiwa Jenista, Waziri, Mheshimiwa Kairuki na Manaibu wote wawili kwa kufanya kazi nzuri ya kumsaidia Mheshimiwa Waziri Mkuu na Mheshimiwa Rais wetu Dkt. John Pombe Magufuli.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naunga mkono hoja kwa asilimia mia moja. Ahsante.