Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 - Ofisi ya Waziri Mkuu

Hon. Dr. Faustine Engelbert Ndugulile

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Kigamboni

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 - Ofisi ya Waziri Mkuu

NAIBU WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kuchangia katika maeneo mawili ambayo yaligusiwa na wachangiaji katika hotuba ya Mheshimiwa Waziri Mkuu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, la kwanza ni mabadiliko ya kisheria, kuna sheria mbili ambazo tunatarajia kuzileta Bungeni kwa mara ya kwanza. Tunatambua kumekuwa na changamoto katika ugharamiaji wa matibabu na hivyo kama Serikali tunakusudia kuleta Muswada wa Bima ya Afya kwa wananchi wote.

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini la pili, tunatambua vilevile katika kufikia malengo ya 90-90-90 kwa maana ya asilimia 90 ya watu wote ambao wanaishi na Virusi vya UKIMWI tuweze kuwafikia na kuwapima, asilimia 90 ya wale ambao wamepimwa waweze kupata matibabu na asilimia 90 ya wale ambao watapata matibabu tuweze kufubaza kabisa Virusi vya UKIMWI, tumeona kwamba kumekuwa na changamoto hususani katika kundi la vijana na wanaume, hivyo tunataka kuja na mabadiliko ya sheria ili kuruhusu upimaji binafsi lakini vilevile kushusha umri wa upimaji kufikia miaka 15. Taratibu zote za mabadiliko haya ya sheria yako katika ngazi mbalimbali ndani ya Serikali na pindi taratibu hizi zitakapokamilika Miswada hii italetwa Bungeni. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, eneo la pili ambalo liligusiwa na wachangiaji ni kuhusiana na hali ya magonjwa nchini. Kwa muda mrefu tumekuwa tunapambana na magonjwa ya kuambukiza lakini sasa hivi tumeanza kuona ongezeko kubwa sana la magonjwa yasiyoambukizwa kwa maana ya kisukari, pressure, kiharusi na magonjwa ya figo. Sisi kama Serikali tumeona tunahitaji tuanze kujipanga upya, hivyo tunataka tuangalie mtiririko mzima wa huduma za afya kama alivyokuwa ameongelea Mheshimiwa Mukasa kuangalia masuala ya elimu, kinga, tiba na huduma ya utengamao. Awali tulikuwa tumejikita sana katika masuala ya tiba tukaacha haya maeneo mengine. Ili sasa tuweze kupambana vizuri na magonjwa yasiyoambukiza tunahitaji tuhakikishe kwamba huu mtiririko mzima tunauzingatia. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali kupitia Wizara ya Afya tuko katika hatua za mwisho kuanzisha Mpango wa Taifa wa Magonjwa Yasiyoambukiza kama ilivyo kwa magonjwa ya UKIMWI, TB na Malaria. Tunataka tuje na Mpango wa Magonjwa Yasiyoambukiza ili tuweze kuwa na utaratibu mzuri wa kudhibiti magonjwa haya. Tutaweka utaratibu ambao utaanzia katika ngazi ya Taifa mpaka ngazi za kata.

Mheshimiwa Mwenyekiti, yangu yalikuwa ni hayo, naunga mkono hoja. (Makofi)