Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 - Ofisi ya Waziri Mkuu

Hon. Mwita Mwikwabe Waitara

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Tarime Vijijini

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 - Ofisi ya Waziri Mkuu

NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. MWITA M. WAITARA): Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru. Naomba nimpongeze Mheshimiwa Waziri Mkuu kwa kazi kubwa anayofanya pamoja na Waziri Mheshimiwa Angellah Kairuki, Mheshimiwa Jenista Mhagama; Manaibu, ndugu yangu Mheshimiwa Mavunde na Mheshimiwa Stella Ikupa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nawapongeza Mheshimiwa Rais, Mawaziri wote na Wabunge wote wa Chama cha Mapinduzi kwa kuendelea kusaidia kusimamia utekelezaji mzuri na murua wa Ilani ya Uchaguzi wa mwaka 2015 - 2020.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nitajibu yale maswali ya jumla sana kwa sababu ya muda, yako mengi lakini nitajitahidi. La kwanza, imezungumzwa hoja hapa ya TARURA. Tumefurahi sana kama Wizara kwamba kila Mbunge aliyesimama kuchangia humu alipongeza kazi kubwa na nzuri ambayo inafanywa na Wakala wa Barabara wa Mjini na Vijijini ya TARURA. Ila changamoto iliyokuwepo ni upatikanaji wa fedha.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nitoe tu taarifa kwamba tayari imeshaundwa timu ya Kitaifa ya kutambua barabara, itafanya kazi yake baada ya kuleta mrejesho wa kitaalamu. Sasa tutapitia upya kuangalia mgao ule wa asilimia 70 ya TANROADS na asilimia 30 ya TARURA ili hawa watu waweze kuongezewa fedha na waendelee kuimarisha barabara zetu za mjini na vijijini.

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la pili ambalo limezungumzwa ilikuwa ni hoja juu ya maboma ya afya. Kwenye bajeti ya mwaka 2017/2018 tulikamilisha maboma 207 na vituo 552 vimeendelea kuimarishwa. Kwenye bajeti hii ambayo imeletwa, nadhani kuanzia kesho, tumetenga fedha zaidi ya shilingi bilioni 10 kujenga Vituo vya Afya vingine vipya 52, lakini mbali na hizo hospitali 67 za mwanzo za mwaka huu ambazo tunamalizia, hapa pia tumetenga bajeti ya hospitali nyingine mpya 27. Kwa hiyo, kazi ile inaendelea kufanyika.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kama nilivyojibu leo swali la msingi hapa ni kwamba kuna maboma mengine ambayo wananchi wameendelea kujenga bado Serikali hii ya Awamu ya Tano ina nia njema kabisa kuendelea kusaidia kuyakamilsha ili huduma ya afya iendelee kuimarika katika Taifa letu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, amejibu Mheshimiwa Waziri wa Elimu kwamba kuna maboma ambayo yamekamilishwa lakini ile ni bajeti ya 2016/2017. 2018/2019 tunapeleka vifaa vya maabara kwenye Shule za Sekondari 1,250; lakini kama ambavyo inajulikana pia mwezi wa Kwanza Wizara ya TAMISEMI kwa kushirikiana na Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia kupitia mradi wa EPFR tumeshapeleka fedha, shilingi bilioni 56 kwenye Elimu ya Msingi na Sekondari.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mwezi wa Pili pia tumepeleka fedha shilingi bilioni 29.9 ili kukamilisha maboma. Hapa ninapozungumza tupo kwenye mchakato pia kupeleka fedha nyingine kumalizia maboma ya Shule za Msingi, Walimu na watumishi wengine wa Serikali. Kazi kubwa inaendelea kufanyika.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kulikuwa na hoja ya asilimia 10. Naomba nitumie nafasi hii kuwapongeza sana Kamati ya Utawala na TAMISEMI ya Bunge hili Tukufu. Katika bajeti hii ambayo imewasilishwa ya mafungu ya Wizara ya TAMISEMI kila Mkoa Wakurugenzi wote walilazimika kutoa maelezo ya ziada, kila mtu aeleze mpango aliyonao wa kukusanya asilimia 10 kwa vijana, akina mama na watu wenye elemavu, pia kuonyesha ameshafikisha asilimia ngapi na adhabu mbalimbali zimetolewa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, naomba nilitaarifu Bunge kwamba katika kipindi hiki baada ya Bunge hili Tukufu kufanya mabadiliko makubwa ya sheria kifungu Na. 35, kwa kweli usimamizi umeimarika zaidi. Mwaka 2016/2017 fedha za mikopo zilizoenda kwenye makundi haya matatu maalum, tulipeleka shilingi 8,917,700,164/=.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mwaka 2017/2018 ile asilimia 10 ilipelekwa kwenye vikundi, shilingi 27,402,737.81. Kwenye vikundi 10,000 imeenda 72, lakini niseme tu, bahati nzuri sana naomba niwapongeze akina mama wa Taifa hili wamekuwa waaminifu sana na wamekopa sana kuliko vijana na watu wengine wote. Namba yao ilikuwa kubwa. Pia hata kwenye marejesho akina mama wamekuwa waaminifu, wamerejesha sehemu kubwa. Tunaomba waendelee kuhimizwa, waelimishwe kwa weledi, wakope ili waweze kujikwamua kiuchumi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, mpaka mwezi Februari mwaka huu, 2019 tumeshakusanya fedha, zinapelekwa kwenye vikundi, shilingi 21,423,619,000/= zimeshaenda kwenye makundi hayo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunashukuru sana kwamba sasa, baada ya maelekezo ya Kamati ya Utawala na Bunge hili Tukufu, kanuni za kazi hii zimeshaandaliwa, zipo kwenye hatua ya mwisho, lakini maelekezo yametoka kwamba sasa kutakuwa na akaunti maalum ambayo fedha hizi zikikusanywa ni lazima ziingizwe pale. Kwa hiyo, kuna ujanja unafanyika wakipeleka fedha kwenye vikundi, fedha za marejesho wanajumlisha wanakwambia ni asilimia zaidi ya 100. Tukasema hapana, ili tutenganishe, kutakuwa na akaunti mahususi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, fedha zinazokusanywa ziingizwe kwenye akaunti hiyo, zikipelekwa kwenye vikundi zipelekwe hivyo na zikirejeshwa zionekane ili tuweze ku- control. Kwa hiyo, kazi inamalizika na watapewa maelekezo mahususi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kulikuwa na hoja hapa ya posho ya Wenyeviti wa Mitaa na Madiwani. Naomba nijibu hoja hizo mbili kwa mkupuo. Juzi niliulizwa swali hapa, nirudie kwamba Wenyeviti wa Serikali za Mitaa, Vijiji na Vitongoji na Wajumbe wao, kabla ya kufanya uamuzi wa kugombea ni lazima wakidhi sifa na vigezo vilivyo kwenye kanuni za uchaguzi wa Serikali za Mitaa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, inaelekezwa kwamba mgombea au Mwenyekiti wa Kijiji, Mwenyekiti wa Kitongoji, Wajumbe wa Serikali za Mitaa na Wahumbe wa Halmashauri za Vijiji ni lazima wawe na kipato ambacho kinawawezesha kuishi. Kwa hiyo, ni lazima mtu apime uwezo wa kuhudumia. Kazi hii kimsingi ni kazi ya kuijtolea. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, tunatarajia pamoja na hoja mbalimbali zilizopo kwamba waongezwe posho, cha kwanza ajue kwamba ni kazi ya kujitolea na apimwe kwa uwezo wake wa kusimamia ili pia kuepuka hata ubadhirifu mbalimbali ambao unaendelea kwenye maeneo yetu ya Serikali za Mitaa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, hoja ya posho ya Madiwani ni kweli. Posho ya Diwani kwa mwezi ni shilingi 350,000/=. Kwa Wenyeviti na Mameya ni mpaka Shilingi 400,000/= ukomo. Kila Halmashauri imejipangia utaratibu wa posho mbalimbali kwenye vikao vyao. Tumetoa maelekezo kwamba imeonekana kwamba kuna Halmashauri nyingine wanalipa fedha kubwa sana, nyingine ndogo, kama ilivyo kwa Wabunge. Hata kama utaenda mahali gani, lakini ile per- diem unayolipwa na sitting inatambulika. Kwa hiyo, ikawekwa flat rate. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, hayo ni maelekezo ya Mheshimiwa Waziri kwamba kuwe na flat rate kwenye Halmashauri zetu. Kuna malalamiko, kuna barua tumepata, lakini ni kwamba ile posho ya kawaida Diwani atapewa; hizi posho za vikao na kulala, iwe standard. Kwa sababu kikao wanachokaa Dar es Salaam na sehemu nyingine ni ile ile, ukumbi ni ule ule. Kwa hiyo, kumekuwa na double standard ile. Kwa hiyo ndiyo maelekezo. Haki zao nyingine zile zipo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, posho za Wenyeviti wa Mitaa zinatofautiana. Kwa mfano, mimi ni Mbunge wa Ukonga, Ilala. Kule tulikuwa tunalipwa posho shilingi 40,000/=, lakini kwa sababu ya mapato ya Halmashauri ya Ilala tumepandisha mpaka shilingi 100,000/=. Kwa hiyo, kuwalipa Wenyeviti wa Mitaa inategemea na Halmashauri inapata kiasi gani? Hao hao inabidi wasaidie pia katika kukusanya kodi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna maeneo mengine wakitumwa kusimamia kodi hawasimamii, lakini ukweli ni kwamba Watanzania wote wanapaswa kulipa kodi ili miradi ya maendeleo iweze kukamilishwa. Hawa nao wasaidie kukusanya kodi, kuibua vyanzo, wakaangalie watu walinde miundombinu, fedha zitapatikana, watalipwa zaidi ya hiyo ambayo ipo katika eneo hilo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, hoja nyingine ambayo imezungumzwa hapa, kulikuwa na hoja ya nyumba za wakuu wa Wilaya na Wakuu wa Mikoa. Kwenye bajeti ya mwaka 2019/2020 tumetenga zaidi ya shilingi 4,626,000,000/= kwa ajili ya kujenga nyumba mpya na kukarabati. Kulikuwa na hoja hapa nadhani eneo la Liwale, wametengewa fedha zaidi ya shilingi milioni 330 kwa kazi hiyo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, vile vile kuna hoja ya magari ya Ma-DC, Wakurugenzi na Wakuu wa Mikoa. Naomba nitoe taarifa kwamba jambo hili tunalitambua na Serikali inaendelea kuhimiza, tutakuwa tunanunua magari kulingana na uwezo Serikali kadri muda unavyoenda. Vile vile viongozi hawa wamepewa dhamana kubwa katika maeneo yote ya Serikali za Mitaa, hawatakwama kufanya kazi zao. Tutafanya kila linalowezekana ili waweze kufanya kazi na waweze kufika maeneo mbalimbali. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tumetoa ushauri, kuna Wilaya nyingine ni kubwa sana kulingana na jiografia yake na mazingira ya miundombinu ile. Kwa hiyo, tunatakiwa tuangalie vipaumbele kulingana na uwezo kadri ambavyo itakuwa inawezekana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hoja nyingine ambayo ilijtokeza hapa walizungumzia ahadi za viongozi mbalimbali. Naomba tuwahakikishie kwa kasi hii ya Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli na Serikali ya Awamu ya Tano na ushirikiano mzuri wa Wabunge wa Chama cha Mapinduzi ahadi zote za viongozi na Mheshimiwa Rais, Makamu wa Rais, Waziri Mkuu na Mawaziri wote zitatekelezwa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, mwisho, nilikuwa nataka nizungumzie hoja ambayo imejitokeza hapa. Kumekuwa na hoja kwamba nikiwa nazungumza wananiambia ongea kama Naibu Waziri, lakini nimeambiwa hapa kwamba inawezekana nafasi hizi tumehongwa. Nadhani nijibu hii hoja.

Mheshimiwa Mwenyekiti, bahati nzuri nina uzoefu wa pande zote mbili; upande wa Upinzani na upande wa Chama cha Mapinduzi. Naomba niwapongeze Wabunge wa Chama cha Mapinduzi kwa kazi kubwa mnayofanya. Naomba niwaambie, kwa uzoefu ambao nimekaa miaka kumi upande huo, upinzani wa nchi hii bado sana. Bado sana kwa kweli wanapaswa kujipanga. Kwa kasi hii iliyoko sasa ya kuweka miradi kila mahali, hii kasi nadhani wanatakiwa kujipanga zaidi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, niseme tu kwamba ni kweli, kunaweza kuwa na hoja pinzani lakini wali wa kushiba unaonekana kwenye sahani. Nani hamjui Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli? Nani anaweza kupambana naye? (Makofi)

MBUNGE FULANI: Mheshimiwa Mwenyekiti, taarifa.

NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. MWITA M. WAITARA): Mheshimiwa Mwenyekiti, katika mazingira haya, sisi tuchape kazi.

MBUNGE FULANI: Mheshimiwa Mwenyekiti, taarifa.

NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. MWITA M. WAITARA): Mheshimiwa Mwenyekiti, niwaambie Wabunge wa Viti Maalum wa Chama cha Mapinduzi. Nilikuwa nafuatilia trend ya Wabunge wa Upinzani hasa wa CHADEMA wale na Wabunge wa CCM, big up sana Wabunge wa Chama cha Mapinduzi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kila Mbunge wa CCM akienda kwenye mkoa, mara amechangia cement, amepeleka mabati, amewezesha vikundi, ametoa elimu ya uraia, akisimama hapa anachangia vizuri. Kwa hiyo, hii ndiyo tofauti kubwa kati ya nyie akina mama wa hapa na Wabunge wa Viti Maalum kule. (Makofi/Vigelegele)

Mheshimiwa Mwenyekiti, la mwisho, unajua wale watu wana msongo wa mawazo, siyo mikopo tu, hatima yao ya mwaka kesho. Hali ni mbaya! Kwa sababu kuna Wabunge hapa walishaanza kuaga kwenye Majimbo yao. Mbunge wa Tanga alizungumza juzi kwamba ni Mbunge wa kwanza wa Upinzani, akashindwa kumalizia kwamba Mbunge wa kwanza wa Upinzani na wa mwisho anaaga pale Tanga. Kwa sababu tunafanya replacement, wala siyo kunyang’anywa. Hawatanyang’anywa Ubunge, lakini watu wanaangalia, Watanzania wanaona kwa kazi ya Mheshimiwa Rais, miradi mikubwa inayofanyika.

Mheshimiwa Mwenyekiti, leo nani anaweza akasimama akaponda ndege kweli? Nani anaweza akaponda? Unaponda ndege halafu unaenda unapiga selfie unaturushia tuangalie. Unaponda reli, Mbunge unatoka Morogoro pale, ikianza ile maana yake hata mabasi yale na nini havitakuwepo. Speed ndogo, unalala Morogoro, unafanya kazi Dar es Salaam. Ikianza Dodoma, unalala Dodoma unafanya kazi mahali popote pale. Haya ni mambo ambayo yanapaswa kuungwa mkono. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, la kwangu tu ni kumwambia Mheshimiwa Rais aendelee na kazi hii, Waheshimiwa Mawaziri na Waziri Mkuu, Makamu wa Rais, Wabunge wa Chama cha Mapinduzi, nyie ndio wenye dhamana ya nchi hii, Watanzania wamewaamini, wamewapa kura za kutosha. Kelele za chura hazimzuii ng’ombe kunywa maji na kelele za mlango hazimzuii mwenye mji kulala. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, nafikiri muwe na amani sana. Sisi tunazunguka, tumeenda. Leo wanasema ooh, sisi tunapishana kila mahali.

MHE. PAULINE P. GEKUL: Mheshimiwa Mwenyekiti, taarifa.

NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. MWITA M. WAITARA): Tunafanya ziara kila mahali, lakini haya ni maelekezo, kama Rais halali, Waziri atalalaje? Mbunge wa CCM analalaje na watanzania wanataka maendeleo?

MHE. PAULINE P. GEKUL: Mheshimiwa Mwenyekiti, taarifa.

NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. MWITA M. WAITARA): Fedha zinakuja na zinasimamiwa. Watanzania nawaomba sana chonde chonde lipeni kodi. Fuata utaratibu, tii sheria bila shuruti, maandamano hayatakiwi. (Makofi)

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

MWENYEKITI: Ahsante sana.

NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. MWITA M. WAITARA): Mheshimiwa Mwenyekiti, maandamano kama unataka, chumbani kwako, hutaki utachakazwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana (Makofi/ Kicheko/Vigelegele)