Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 - Ofisi ya Waziri Mkuu

Hon. Kassim Majaliwa Majaliwa

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Ruangwa

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 - Ofisi ya Waziri Mkuu

WAZIRI MKUU: Mheshimiwa Naibu Spika, awali ya yote, nianze kwa kumshukuru Mwenyezi Mungu mwingi wa rehema kwa kuendelea kutupa afya njema na kutujalia kukutana tena kwenye Kikao hiki cha Sita cha Mkutano wa Kumi na Tano wa Bunge lako Tukufu kwa ajili ya kuhitimisha mjadala huu kuhusu hoja ya bajeti ya Ofisi ya Waziuri Mkuu, taasisi zake na Mfuko wa Bunge kwa mwaka wa fedha 2019/2020.

Mheshimiwa Naibu Spika, nitumie nafasi hii pia kutoa shukrani za dhati kwa makundi mbalimbali kama yalivyotamkwa na Mawaziri wote walionitangulia, nami sikusudii kurudia ila nitayapitia kwa makundi lakini wote waamini kuwa natambua mchango wao mkubwa katika kuwezesha Ofisi hii kutimiza wajibu wake. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, pili, natoa shukurani zangu za dhati kwa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Katiba na Sheria, Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Bajeti, Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Masuala ya UKIMWI na Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni kwa michango yao mizuri kwenye hoja ya Waziri Mkuu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, tatu, nawashukuru sana Mheshimiwa Spika, wewe Naibu Spika na Wenyeviti wote wa Bunge kwa kusimamia kwa umahiri mkubwa mwenendo mzima wa majadiliano ya hoja ya bajeti ya Ofisi ya Waziri Mkuu, taasisi zake na Mfuko wa Bunge pia kwa mwaka wa fedha 2019/2020.

Mheshimiwa Naibu Spika, nne, nawashukuru Waheshimiwa Mawaziri waliochangia hoja pamoja na Naibu Mawaziri, Ofisi ya Waziri Mkuu; Makatibu Wakuu; Naibu Makatibu Wakuu; Wakuu wa Idara; Mashirika; Wakala na Taasisi zote za Serikali pamoja na watumishi wengine katika Ofisi ya Waziri Mkuu kwa kazi kubwa waliyoifanya na ushrikiano walionipa katika kipindi chote cha mjadala wa bajeti hii ya Ofisi ya Waziri Mkuu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, pia nawashukuru sana Waheshimiwa Wabunge wenzangu kwa pongezi zenu kwa Serikali na kwa michango yenu yenye dhamira ya dhati kabisa, michango yenye hoja za kuboresha mipango na kazi zilizokusudiwa kutekelezwa na Serikali kwa mwaka wa fedha mwaka 2019/2020. Mjadala huu umeendelea kuthibitisha uimara na umakini wa Bunge katika kutekeleza wajibu wake wa Kikatiba na kuishauri na kuisimamia Serikali kikamilifu.

Mheshimiwa Naibu Spika, wakati wa mjadala huu Waheshimiwa Wabunge 142 walichangia hoja Ofisi ya Waziri Mkuu. Kati ya hao, Waheshimiwa Wabunge 98 walichangia kwa kuzungumza moja kwa moja hapa Bungeni na Waheshimiwa 44 walichangia kwa maandishi. Ninawashukuru sana Waheshimiwa Wabunge wote waliochangia hoja ya Waziri Mkuu. Hata hivyo kutokana na ufinyu wa muda, naomba uridhie nisiwataje, aidha, majina yao yote yaingingizwe katika Hansard. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali imejibu hoja zilizowasilishwa na Waheshimiwa Wabunge kupitia Waheshimiwa Mawaziri na Naibu Mawaziri, halikadhalika hoja zilizosalia zitajibiwa kwa maandishi. Vilevile baadhi ya hoja zenu zitatolewa ufafanuzi wa kina na Waheshimiwa Mawaziri ambao watajipanga vizuri kuzitolea ufafanuzi wa kutosha wakati wa kuwasilisha bajeti zao za kisekta.

Mheshimiwa Naibu Spika, sote tunatambua kuwa kuna msuala muhimu yameibuliwa wakati wa majadiliano haya. Kadhalika mtakubaliana nami kwamba mjadala ulikuwa wa kina na wa kiwango cha juu na umakini unaostahili. Ninakiri kuwa michango ya Waheshimiwa Wabunge na hoja zao zilizoibuliwa zina uhusiano wa moja kwa moja na utendaji wa kazi za Serikali. Aidha, masuala muhimu hususan usafiri wa anga, utalii, bandari, maji, makusanyo ya kodi na uwekezaji ndiyo ambayo kwa kiasi kikubwa yamekuwa ni kitovu cha mjadala mzima wa michango ya Waheshimiwa Wabunge.

Mheshimiwa Naibu Spika, hata hivyo, kabla ya kuingia moja kwa moja katika kujibu hoja za Waheshimiwa Wabunge, naomba nitolee ufafanuzi baadhi ya masuala muhimu yaliyoibuliwa na Waheshimiwa Wabunge kwenye hoja hii ya Waziri Mkuu:-

Mheshimiwa Naibu Spika, moja ilikuwa suala la bniashara na uwekezaji. Serikali imeendelea kujenga mazingira wezeshi na rahisi ya kufanya biashara na uwekezaji bila kuathiri ubora na viwango, sambasamba na kufuata sheria, kanuni na miongozo iliyopo. Hata hivyo, licha ya azma hiyo nzuri ya Serikali, bado kumekuwapo na malalamiko kutoka kwa wafanyabiashara na wawekezaji kama walivyoeleza Waheshimiwa Wabunge wakati wa kuchangia hoja hii.

Mheshimiwa Naibu Spika, napenda kutoa ufafanuzi kwa yale masuala yaliyogusa vyombo vya udhibiti kama vile Mamlaka ya Chakula na Dawa (TFDA), Shirika la Viwango Tanzania (TBS), Mkemia Mkuu wa Serikali, Mamlaka nyingine za udhibiti pamoja na Mamlaka ya Mapato Tanzania TRA, OSHA, BRELA, Taasisi ya Mionzi na kadhalika.

Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali imekuwa ikipokea malalamiko mengi kutoka kwa wafanyabiashara kuhusu Mamlaka hizi na namna ya utendaji kazi wake, miongoni mwa kero hizo ni mchakato wa muda mrefu wa kupata leseni za biashara, gharama za usajiri wa bidhaa zinazotozwa na TFDA, suala la viwango vya TBS, madai ya kuwepo kwa unyanyasaji unaofanywa na TRA kwa kushirikiana na Jeshi la Polisi dhidi ya wafanyabiashara, umbali wa Makao Makuu wa Maabara za Taasisi za Mionzi na eneo wanalofanyia kazi kama vile bandari, viwanja vya ndege na kadhalika.

Mheshimiwa Naibu Spika, ikiwa ni hatua ya kuondoa kero hizo, katika nyakati tofauti Viongozi wetu wa Kitaifa wamekuwa wakichukua hatua za makusudi kuzungumza na wafanyabiashara pamoja na wawekezaji. Mazungumzo haya yamekuwa yakijielekeza zaidi katika kupokea kero na kuzitafutia ufumbuzi kero hizo. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, Mheshimiwa Rais wetu Dkt. John Pombe Magufuli ameweza kukutana na wadau mbalimbali wa biashara na uwekezaji zikiwemo taasisi za Serikali, wafanyabiashara wakubwa na wadogo, wachimbaji wa madini na wakulima katika nyakati tofauti. Aidha, nami nimekutana na wawakilishi wa wafanyabiashara wadogo na wafanyabiashara wa kati tarehe 28 Februari, 2019 Jijini Dar es Salaam. Kadhalika tarehe 6 Machi, 2019 nilitembelea Shirika la Viwango vya Taifa Tanzania na Mamlaka ya Chakula na Dawa na kufanya mazungumzo na viongozi na watendaji wa taasisi hizo akiwemo Mkemia Mkuu wa Serikali na baadaye tarehe 16 Machi 2019 tulikutana tena kwa pamoja na TRA.

Mheshimiwa Naibu Spika, katika mazungumzo hayo, nilielekeza viongozi na watendaji wa mamlaka hizo za udhibiti kutekeleza majukumu yao kwa uaminifu, uadilifu na weledi wa hali juu huku wakijiepusha na vitendo vya rushwa, kuhamisha mafaili ya ofisi, ofisi za wafanyabiashara na kukusanya komputa na kuondoka nazo. Badala yake watumie nafasi hiyo kuwaelimisha wafanyabiashara ili kuwafahamisha nini kinabadilika? Nini kinatakiwa? Hasa katika kufuata utaratibu, kanuni na sheria na miongozo mbalimbali inayohusu biashara na uwekezaji na kuondoa urasimu na mianya ya rushwa katika kutekeleza majukumu ya taasisi hizo kwa kuimarisha matumizi ya mifumo ya kielektroniki. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, changamoto nyingine ambayo imeonekana kuwa kikwazo cha biashara na uwekezaji ni mwingiliano wa majukumu ya taasisi hizo. Kwa mfano, uwepo wa majukumu yenye kufanana kwa TFDA na TBS na Mkemia Mkuu, Bodi ya Maziwa, Bodi ya Nyama, Baraza la Mifugo, EWURA, SUMATRA na TANROADS ni kikwazo kikubwa katika kurahisisha mazingira ya kufanya biashara. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tayari nimeshatoa maelekezo na yameanza kufanyiwa kazi kwa Waheshimiwa Mawaziri wa Sekta hizo zote chini ya Mheshimiwa Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu Sera na Uratibu, kwamba wakae pamoja kupitia sheria na mganyo wa majukumu yao kwenye taasisi zao za udhibiti ili kuondoa mkanganyiko uliopo sasa. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusu Mamlaka ya Mapato na Taasisi zake, nawaelekeza tena Mawaziri husika kuhakikisha kuwa wakuu wa taasisi hizo wanaendelea kutekeleza majukumu yao kwa weledi na kuzingatia sheria bila kuwabughuzi wafanyabiashara na wawekezaji hapa nchini. Kwa upande wa wawekezaji, nao pia natoa rai wahakikishe kuwa wanazingatia sheria na kanuni ili pande zote ziweze kunufaika. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, niendelee kuzisisitiza mamlaka hizi za udhibiti kupanua wigo wa shughuli zao hususan maeneo ya mipakani, kuimarisha matumizi ya kielektroniki ili kuondoa urasimu kukabiliana na mianya ya rushwa na hasa katika utoaji huduma zake. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, liko jambo limezungumza upande wa Uhamiaji. Kama ambavyo nimeeleza kwenye hotuba yangu, Serikali pia imeendelea kuboresha taratibu za Idara ya Uhamiaji kwa kutekeleza awamu ya pili ya mradi wahamiaji wa mtandao. Mradi huo wenye kuhusisha utoaji wa VISA na vibali vya ukazi vya kielektroniki utarahisisha zaidi shughuli za utalii, biashara na uwekezaji hapa nchini kwa kuondoa urasimu hususan muda mrefu unaotumika kufanya maombi hayo ili kupata vibali hivyo kwa wakati.

Mheshimiwa Naibu Spika, kutokana na hatua thabiti za kuvutia uwekezaji zinazochukuliwa na Serikali, haikunishangaza kwa Tanzania kuibuka kinara katika kuvutia uwekezaji miongoni mwa nchi za Afrika Mashariki ambapo tulivutia mitaji yenye thamani ya Dola za Marekani bilioni 1.18. Hii ni kwa mujibu wa report ya mwaka 2018 ya Shirika la Umoja wa Mataifa linaloshughulikia masuala ya biashara na maendeleo. Tunaendelea kuvutia mitaji zaidi ya uwekezaji na ninaamini tutafikia malengo tunayokusudia. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali itaendelea kuwavutia wawekezaji kujenga viwanda nchini hususan vyenye kutumia nguvu kazi kubwa na malighafi zinazozalishwa hapa nchini kwa lengo la kutengeneza ajira, kuongeza tija kwenye uzalishaji wa bidhaa na huduma na kuipatia Serikali fedha nyingi za kigeni.

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba nizungumzie Sekta ya Utalii. Baadhi ya Waheshimiwa Wabunge pamoja na kuipongeza Serikali kwa hatua za kuboresha Sekta ya Utalii hususan ununuzi wa ndege mpya, pia wametoa mapendekezo ya ndege hizo kufanya safari katika nchi za ukanda wa Maziwa Makuu na maeneo ya kimkakati.

Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kutumia fursa hii kuwafamisha Waheshimiwa Wabunge wenzangu kuwa katika mwaka wa fedha 2019/2020 Serikali itaendelea kuipa kipaumbele Sekta ya Utalii. Uboreshaji wa usafiri wa anga unakwenda sambamba na utangazaji na utajiri mkubwa kwa vivutio vya utalii tulivyonavyo kama vile, uoto wa asili, wanyama, fukwe, malikale, tamaduni za makabila yetu yasiyopungua 120 na vinginevyo. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali itaendelea kutoa msukumo kufungua kanda za Kusini katika maendeleo ya utalii kwa kuviendeleza vivutio vya utalii vilivyopo kwenye ukanda huo ili vichangie kukamilisha ukuaji wa uchumi na ustawi wa wananchi. (Makofi)

Aidha, Serikali inaendelea na mkakati wa kuunganisha na kufungua ukanda wa ziwa kwa kuendeleza Mapori ya Akiba maarufu kama BBK, yaani Biharamulo, Burigi na Kimisi pamoja na Ibanda na Rumanyika kuwa Hifadhi za Taifa. Mpaka sasa takribani shilingi bilioni nne zimeshatumika kuimarisha ulinzi, kuainisha mipaka, kujenga miundombinu ya utalii, kuweka mifumo ya kielektroniki ya utawala na ya kukusanya mapato pamoja na kuendeleza vivutio vya utalii vinavyopatikana kwenye maeneo hayo.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa upande mwingine, kuimarika kwa usafiri wa anga nako kumeendelea kuchangia vyema ukuaji wa Sekta ya Utalii nchini. Mathalan baada ya kuwasili kwa ndege zetu kubwa tatu zinazojumuisha Boing 787 Dreamliner na nyingine mbili aina ya Air Bus A220-300. Shirika la Ndege la Tanzania sasa limeanza safari za kwenda nchi jirani za Zambia na Zimbabwe. Halikadhalika, muda siyo mrefu shirika hilo litaanza safari za masafa ya mbali zitakazohusisha nchi za China, India na Thailand. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nitumie fursa hii pia kuipongeza Bodi ya Utalii nchini ambayo mwezi Novemba, 2018 iliingia makubaliano na kampuni ya Touch Road International Holding Group kwa ajili ya kutekeleza mradi huo uitwao Tour Africa the New Horizon. Mradi huo utasaidia kuongeza idadi ya watalii kutoka China ambapo kwa kuanzia tunatarajia kupokea watalii 10,000 kwa mwaka 2019. Aidha, mwezi Mei mwaka huu Tanzania inategemea kupokea watalii wasiopungua 300 kutoka nchini humo na tayari tumeshapokea watalii 336 kutoka nchi mbalimbali walioingia wiki iliyopita kwa njia ya meli. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kampuni ya Touch Road inayo nia pia ya kufanya uwekezaji mpya kwenye ujenzi wa hoteli, maeneo ya viwanda na kanda maalum ya uchumi wa makazi. Napenda kutoa wito kwa mamlaka na wadau mbalimbali wanaojihusisha na sekta hii muhimu ya utalii, kuliangalia vyema suala la viwango vya gharama za malazi kwenye mahoteli ya kitalii pamoja na tozo mbalimbali za kuingia kwenye maeneo yenye vivutio vya utalii. Kumekuwepo na malalamiko kuwa gharama zetu kwenye maeneo hayo ziko juu na kwa hiyo, zinasababisha utalii wa ndani kupungua kwa kiasi kikubwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, niendelee kusisitiza pia kwa Waheshimiwa Wabunge wenzangu na Watanzania wote kwa ujumla kuenzi utalii wa ndani. Aidha, Mamlaka za Utalii zote zitoe vivutio mbalimbali kwa watalii wa ndani ili nao wapate fursa kujionea utajiri wa maliasili tulizonazo hasa uoto wa asili, wanyama, fukwe, malikale na kadhalika. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, Waheshimiwa Wabunge wenzangu wamezungumzia upatikanaji wa maji katika maeneo mbalimbali nchini sambamba na kuipongeza Serikali, lakini pia walikosoa utekelezaji na ubora wa baadhi ya miradi ya maji na vilevile wameonesha kutorodhishwa sana kwa baadhi ya maeneo kwa sababu hayajafikiwa na miradi hiyo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali inaendelea na usambazaji wa maji licha ya changamoto hizi. Hata hivyo, Serikali inachukua hatua stahiki kuhakikisha kuwa miradi yote ya maji inayotekelezwa inatoa matokeo yanayokusudiwa. Kwa kuanzia Mheshimiwa Rais aliunda Tume Maalum ili kupitia, kufanya tathmini na kutoa mapendekezo juu ya hatua za haraka zinazostahili kuchukuliwa. Hatua hizo zitalenga hasa kuhakikisha kuwa thamani ya fedha ya miradi hiyo inayosambazwa mikoani kote na Wilayani inapatikana na kuleta tija kwenye maeneo miradi hiyo inapotekelezwa.

Mheshimiwa Naibu Spika, hadi sasa tumehakiki madai ya Wakandarasi waliotekeleza miradi hiyo na kulipa shilingi bilioni 138. Aidha, hivi karibuni tutapata fedha nyingine kiasi cha shilingi bilioni 44. Sasa naielekeza Wizara husika ihakikishe kuwa Wakandarasi na Watendaji wa Serikali kufuatilia ufanisi wao kuwa unakuwa wa kiwango cha kuridhisha wakati wote.

Waheshimiwa Wabunge endeleeni kutoa ushauri kwenye Sekta ya Maji. Malengo yetu ni kuhakikisha kwamba tunafikia mpaka ngazi ya vijiji ili wananchi wote waweze kunufaika kwa kupata maji safi na safi na salama. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba nizungumzie maji na usafi wa mazingira. Changamoto nyingine katika eneo la maji ni uharibifu wa mazingira ambao umeshika kasi kubwa. Ni lazima hatua za haraka zichukuliwe ili kuiepusha nchi yetu na janga hili. Katika kuhakikisha kuwa tunaondokana na janga hili, Bunge lilipitisha Sheria ya Huduma za Maji na Usafi wa Mazingira ya mwaka 2019 yenye lengo la kuimarisha mfumo wa utoaji huduma za maji na usafi wa mazingira nchini.

Mheshimiwa Naibu Spika, pamoja na mambo mengine, sheria hiyo itaongeza uwajibikaji katika utoaji wa huduma ya maji, utaimarisha ujenzi, usimamizi na uendeshaji wa miradi ya maji. Kufuatia kuundwa kwa Wakala wa Maji na Usafi wa Mazingira Vijijini (RUWASA) na kuleta uendelevu kwa miradi ya maji vijijini, nawaagiza viongozi wote kuanzia ngazi ya vijiji kuchukua hatua za makusudi katika kusimamia utunzaji wa vyanzo vya maji na kudhibiti vitendo vya uharibifu wa mazingira. (Makofi)

Aidha, viongozi na watendaji watakaobainika kutosimamia ipasavyo sheria husika, hatua kali za kisheria zichukuliwe dhidi yao. Nawaomba sana Waheshimiwa Wabunge tuunge mkono jitihada hizi za Serikali ili kuweza kudhibiti uhalibifu wa mazingira. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, itakumbukwa kwamba mnamo tarehe 5 Mei, mwaka 2016 Serikali ilitoa kauli ndani ya Bunge lako Tukufu kuhusu dhamira ya kupiga marufuku matumizi ya mifuko ya plastiki hapa nchini. Kuanzia wakati huo hadi sasa Serikali imekuwa ikifanya maandalizi ya kutimiza dhamira hiyo. Hivi karibuni nimemwagiza Mheshimiwa Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais, anayesimamia masuala ya Mazingira ikiwemo kuzungumza na wadau mbalimbali, ikiwemo wenye viwanda vya kutengeneza mifuko ya plastiki kwa ajili ya kuhakikisha kwamba jambo hili linatekelezwa kwa haraka. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, matumizi ya plastiki nchini yameendelea kuleta madhara makubwa ikiwemo vifo vya mifugo kwa kula plastiki, kuziba kwa mifereji mingi nchini, uchafuzi wa mazingira na kushindikana kwa kuozesha taka kwenye vituo vya kukusanya taka. Kuanzia tarehe 1 Juni, 2019 itakuwa ni marufuku kutengeneza, kuingiza, kuuza na kutumia mifuko ya plastiki kwa ajili ya kubebea bidhaa za aina yoyote. (Makofi)

(Hapa Mheshimiwa Waziri Mkuu Alikohoa)

WAZIRI MKUU: Na washindwe! (Kicheko/Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nirudie tena. Kuanzia taehe 1 Juni, 2019 itakuwa ni marufuku kutengeneza, kuingiza, kuuza na kutumia mifuko ya plastiki kwa ajili ya kubebea bidhaa za aina yoyote. Aidha, ifikapo tarehe 31 mwezi Mei mwaka huu 2019 itakuwa ni mwisho wa kutumia mifuko ya plastiki kwa ajili ya kubebea bidhaa mbalimbali. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kuanzia sasa tunatoa fursa ya viwanda kubadilisha teknolojia yao, wauzaji kuondoa mizigo yao au kumaliza kuiuza yote na kadhalika. Ofisi ya Waziri wa Nchi, Makamu wa Rais, itajiandaa kutumia kanuni chini ya Sheria ya Mazingira ili kulifanya katazo hili kuwa na nguvu ya kisheria. Tunachukua hatua hii ili kulinda afya ya jamii, wanyama, mazingira na miundombinu dhidi ya athari kubwa zinazotokana na taka za plastiki.

Mheshimiwa Naibu Spika, katika kuchukua hatua hizi, tumetambua kwamba kuna baadhi ya bidhaa lazima zifungwe kwenye vifungashio vya plastiki. Vifungashio kwa bidhaa hizo havitapigwa marufuku kwa sasa. Kwa msingi huo, katika hotuba ya bajeti ya Ofisi ya Makamu wa Rais yatatolewa maelekezo ya kina kuhusu katazo la vifungashio la aina hii hasa katika maeneo ya uzalishaji wa viwanda, Sekta ya Afya na Kilimo.

Mheshimiwa Naibu Spika, ni matumaini yetu kuwa utaratibu huu pamoja na kutunza mazingira, utatoa fursa kutengeneza ajira nyingi, hususan za watu wa chini kupitia utengenezaji wa mifuko mbadala ya plastiki pamoja na kutumia kikamilifu fursa ya viwanda vya karatasi vilivyopo nchini kikiwemo kiwanda cha Mgololo. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kuzungumzia makusanyo ya kodi na Mamlaka ya Mapato Tanzania. Waheshimiwa Wabunge wameainisha maeneo kadhaa ambayo yanalenga kuboresha utendaji wa Mamlaka ya Mapato Tanzania. Maeneo hayo ni pamoja na Mamlaka ya Mapato Tanzania kuongeza wigo wa kulipa kodi na maeneo haya kuweka viwango himilivu ili kuchochea walipa kodi wengine wengi zaidi kulipa kwa hiyari na kujenga mazingira rafiki kwa walipa kodi. Serikali imepokea ushauri huo na itaufanyia kazi, ili kuondoa kero kwa walipa kodi nchini. Mheshimiwa Rais Dkt. John Pombe Magufuli amefanya mabadiliko makubwa na kutoa maelekezo mahususi, hivyo nawaelekeza watendaji wote kuzingatia maelekezo wanayopewa na kuacha tabia ya kutoa visingizio vinavyokwamisha utekelezaji mzuri.

Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya kuwa nimetoa maelezo haya ya msingi, sasa nijielekeze kwenye baadhi ya hoja ambazo zimetolewa. Ziko hoja ambazo tayari zimeelezwa na Waheshimiwa Mawaziri na Waziri wa Nchi alipokuja hapa mbele, hivyo nitapitia kwa haraka kwenye maeneo yale ya kimkakati.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa mujibu wa Kanuni ya 99(13) ya Kanuni za Kudumu za Bunge, Toleo la Januari 2016, naomba nitumie nafasi hii kujibu na kufafanua baadhi ya hoja za Waheshimiwa Wabunge, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, hoja ya kwanza, Ofisi ya Waziri Mkuu ihakikishe kwamba, vipaumbele vyake vinalenga kuboresha na kuimarisha mazingira wezeshi ya uwekezaji kwa lengo la kuvutia wawekezaji wa hapa ndani na nje ya nchi. Hatua ambayo itatengeneza ajira kwa wananchi wengi na kuongeza fursa za biashara na mapato kwa wananchi na Taifa kwa ujumla wake. Serikali imepokea ushauri wa Kamati. Aidha, moja ya vipaumbele vya mpango wa pili wa maendeleo wa miaka mitano ni kuimarisha mazingira ya biashara ya uwekezaji, ili kuwezesha uanzishaji na ukuaji wa biashara hapa nchini.

Mheshimiwa Naibu Spika, katika kutekeleza hilo Serikali itaendelea kuweka kipaumbele kwenye kuimarisha miundombinu wezeshi kama vile usafiri kwenye maeneo ya ujenzi wa reli, barabara, viwanja vya ndege, bandari, lakini pia huduma za umeme na maji ili kupunguza gharama za uendeshaji wa biashara na uwekezaji kwa wawekezaji kwa ujumla. Aidha, Serikali itaimarisha upatikanaji wa ardhi, kuendeleza maeneo maalum ya uwekezaji (Special Economic Zones) na kutekeleza programs za kuboresha mazingira ya uwekezaji, ikiwa ni pamoja na mpango wa kuboresha mfumo wa udhibiti wa mazingira ya biashara nchini (Blue Print for Regulatory Reforms to Improve Business Environments). Vilevile Serikali itaendelea kuimarisha ushirikiano na majadiliano na sekta binafsi kupitia Baraza la Biashara la Taifa pamoja na mikutano ya wadau wa sekta mbalimbali wa ngazi za Kitaifa, mikoa na wilaya ambapo changamoto zinazobainishwa kwenye vikao hivyo ziweze kupatiwa ufumbuzi.

Mheshimiwa Naibu Spika, kulikuwa na hoja ya pili ya Serikali ilete Bungeni haraka iwezekanavyo Marekebisho ya Sheria ya Uchaguzi ya Mwaka 1985 na marekebisho yake ambapo kwa mambo mengine itawezesha, moja kuunda Tume Huru ya Uchaguzi (Tanzania Independent Electoral Commission) na yale yote ambayo pia yanaingia kwenye eneo hili.

Mheshimiwa Naibu Spika, Tume ya Taifa ya Uchaguzi ni Idara huru inayojitegemea na inatekeleza majukumu yake kwa mujibu wa Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya mwaka 1977. Tume hiyo inatekeleza majukumu yake kwa uhuru bila kuingiliwa na mtu au chombo chochote kwa mujibu wa Ibara ya 74(7) na Ibara ya 74(11) ya Katiba. Aidha, ni vema ikafahamika kuwa uteuzi wa Wajumbe wa Tume hufanywa kwa kuzingatia matakwa ya Katiba. Hivyo, njia inayotumika kuwateua Wajumbe au Mkurugenzi wa Uchaguzi haiathiri uhuru wa tume.

Mheshimiwa Naibu Spika, iko hoja ambayo pia, imezungumzwa na Mheshimiwa Waziri wa Nchi alipokuja hapa, uchaguzi wa Serikali za mitaa kwamba, uchaguzi wa Serikali za Mitaa usisimamiwe na Ofisi ya Rais, TAMISEMI na badala yake usimamiwe na Tume ya Taifa ya Uchaguzi. Serikali ishughulikie jambo hili mapema ili kuepuka usumbufu unaoweza kutokea.

Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali inawashukuru sana Waheshimiwa Wabunge kwa imani kubwa mnayoonesha kwa Tume ya Taifa ya Uchaguzi ambayo ni huru juu ya utekelezaji wa majukumu yake na kuona umuhimu wa kuiongezea jukumu la kusimamia uchaguzi wa Serikali za mitaa.

Hata hivyo, majukumu ya tume yameainishwa katika Ibara ya 74(6) ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ikiwa ni pamoja na kusimamia uchaguzi wa Rais, Wabunge na Madiwani katika Jamhuri ya Muungano wa Tanzania hivyo, jukumu la kusimamia uchaguzi wa Serikali za Mitaa si miongoni mwa majukumu ya tume kwa mujibu wa Katiba.

Mheshimiwa Naibu Spika, kulikuwa na hoja ya nne ambayo pia imezungumzwa kwa upana wake juu ya Sheria ya Vyama vya Siasa ambayo imeharamisha shughuli za siasa nchini na kuzifanya kuwa kosa la jinai. Hii inadhihirika kutokana na sheria hii kuwa na vifungu vingi vinavyotoa adhabu ya jamii, kifungo au vyote kwa pamoja kwa wanasiasa ili msajili na Serikali na vyombo vyake hakuna kifungu hata kimoja ambacho kinawagusa kama wakikiuka utekelezwaji wa sheria ya namna hii.

Mheshimiwa Naibu Spika, Ibara ya 3 ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania imeruhusu uwepo wa vyama vingi vya siasa hapa nchini, hivyo hakuna sheria ya nchi inayoweza kufanya siasa kuwa kosa la jinai. Adhabu zilizopo katika Sheria ya Vyama vya Siasa zinaendana na aina ya kosa linalotolewa kwa mujibu wa sheria iliyopitishwa na Bunge. Aidha, Kifungu cha 20(2) cha Sheria ya Vyama vya Siasa kinamruhusu mtu yeyote ambaye anadhani Msajili wa Vyama vya Siasa amekiuka Sheria ya Vyama vya Siasa kwenda Mahakamani kupata haki yake. Serikali inavitaka vyama vya siasa na taasisi mbalimbali kuzingatia sheria pale zinapotekeleza majukumu yake.

Mheshimiwa Naibu Spika, hoja ya tano ilikuwa ni kilimo cha zao la pamba nchini kwamba, bado hatujatumia zao la pamba vizuri katika kuongeza pato la Taifa na kuinua maisha ya Watanzania. Serikali ijizatiti kusimamia uwekezaji kwenye kilimo cha zao la pamba kwa ajili ya kufanikisha utekelezaji wa mkakati wa viwanda vya nguo hapa nchini ili kufikia malengo na kuwa na Taifa lenye uchumi wa kati.

Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali imepokea ushauri wa Waheshimiwa Wabunge. Sekta ya pamba na mnyororo wake wote wa thamani ni sekta ya kipaumbele ambayo pamoja na kuwahakikishia soko wakulima na kuongeza kipato chao uwekezaji katika viwanda vya nguo unatengeneza ajira nyingi kwa vijana, hivyo kuinua kipato chao na kuboresha maisha ya watu walio wengi. Kwa kutumia mkakati wa kuzalisha nguo na mavazi mbalimbali (cotton to clothing) Serikali itaendelea kuhamasisha uwekezaji wa viwanda kwa kutumia teknolojia za kisasa na kutengeneza nguo kuanzia kuchakata pamba hadi nguo kwa kuhakikisha kuwa taratibu zote zinafanyika nchini na msisitizo uwe ni utengenezaji wa nyuzi. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, hoja ya sita, Serikali itumie fursa ya uwepo wa mifugo mingi nchini kwa kuwekeza katika viwanda vya kuchakata nyama ili rasilimali ya mifugo iweze kunufaisha Taifa badala ya nchi jirani kunufaika na mazao ya mifugo inayotoka hapa nchini kwetu. Serikali inaendelea na jitihada za kuvutia uwekezaji katika mzao ya mifugo kwa ushirikiano na wawekezaji binafsi wa ndani na nje kwa ranchi za Taifa. Mfano ni uendelezaji wa ranchi ya Taifa ya Ruvu ambapo Serikali imeingia makubaliano ya awali ya kujenga machinjio makubwa ya kisasa, unenepeshaji wa mifugo na ufungashaji wa nyama. Aidha, kupitia Sheria ya Fedha ya Mwaka 2018 Serikali imeweka vivutio vya kikodi kwa kupunguza kodi ya makampuni kutoka asilimia 30 mpaka asilimia 20 kwa viwanda na bidhaa za ngozi, pamoja na kuondolewa kwa kodi ya ongezeko la thamani kwa mitambo na vifaa vya viwanda hivyo.

Mheshimiwa Naibu Spika, hoja ya saba, Serikali iangalie namna ya kuondokana na urasimu katika kuwezesha jitihada za wawekezaji, hasa kwa wageni wanaokuja na mitaji yao kuja kuwekeza hapa nchini. Ili kuondokana na urasimu, Sheria ya Uwekezaji ya Mwaka 1977 iliunda kituo cha uwekezaji hapa Tanzania kiitwacho TIC ambapo huduma mbalimbali ikiwemo usajili, utoaji wa vibali mbalimbali na leseni na kwa ajili ya uwekezaji unafanyika katika eneo moja (One Stop Facilitation Centre) ambapo taasisi zilizokuwepo awali ni pamoja na TRA, Ardhi, Brela, Uhamiaji na Kazi, ndizo pekee zilikuwa zinapatikana kwenye kituo hicho. Kwa sasa Serikali imeongeza taasisi nyingine ikiwemo OSHA, NEMC, TFDA, TBS, TANESCO na NIDA, hivyo vyote vinafanya jumla ya taasisi 11 kutoa huduma katika eneo moja pale kwenye kituo chetu cha uwekezaji.

Mheshimiwa Naibu Spika, aidha, Serikali imeendelea kuboresha utoaji wa huduma kwa njia ya mtandao ili kupunguza muda na gharama katika kupata huduma kwa wawekezaji wetu hapa nchini. Vilevile Serikali imeunda Kamati ya Taifa inayojumuisha wakuu wote wa taasisi zinazotoa huduma kwa wawekezaji kwa lengo la kujadili maeneo ya kuboresha na urahisishaji wa upatikanaji wa vibali na leseni. Serikali imeongeza huduma za uwekezaji kwa kuanzisha Ofisi za TIC katika kanda zote hapa nchini.

Mheshimiwa Naibu Spika, hoja ya nane ilikuwa Serikali ifanye tathmini na kuangalia vikwazo vinavyokwamisha harakati za uwekezaji nchini, ikiwa ni pamoja na kutunga sheria mpya, kurekebisha baadhi ya sheria, ili kuendana na mahitaji ya Blue Print. Serikali kwa kushirikiana na sekta binafsi mwaka 2017 ilifanya tathmini ya kina na kuandaa Blue Print ambayo imebainisha masuala yote muhimu yanayokwamisha uwekezaji na kuainisha maeneo yote muhimu yanayohitaji kurekebishwa ikiwemo sheria, kanuni na taratibu zinazosimamia uwekezaji hapa nchini na kwa kila taasisi.

Mheshimiwa Naibu Spika, sambamba na hatua hiyo huduma zimeainishwa kwa kuanzisha mifumo ya kielektroniki ambapo wawekezaji sasa wataweza kufanya maombi ya vibali mbalimbali wakiwa popote bila kulazimika kufika kituoni kwetu. Mifumo hii itaondoa urasimu na kuhakikisha utoaji wa vyeti vya uwekezaji, leseni na vibali mbalimbali na hatua hizi zitapunguza gharama na muda wa mwekezaji kufuatilia vibali na leseni kupitia katika kila taasisi na badala yake anavipata kwenye eneo moja. Aidha, Kituo cha Uwekezaji Tanzania hivi sasa kina ofisi saba za kanda, Mwanza, Dodoma, Moshi, Kigoma, Mtwara, Mbeya na Dar-es-Salaam, lengo ni kuendelea kusogeza huduma karibu kwa wawekezaji.

Mheshimiwa Naibu Spika, hoja ya tisa, ni juu ya hali ya chakula kwa wananchi na wakulima wa Musoma kwamba, sio nzuri kutokana na mvua kutonyesha za kutosha na Serikali ijiandae kuwapelekea chakula na msaada wa njaa. Serikali inatambua uwepo wa mabadiliko ya tabianchi yanayosababisha upungufu wa mvua katika maeneo mbalimbali nchini. Hali hii ilitabiriwa na Mamlaka ya Hali ya Hewa kwa kipindi kilichoanza mwezi Novemba, 2018 hadi Juni mpaka mwaka 2019.

Mheshimiwa Naibu Spika, kufuatia utabiri huo mamlaka za mikoa na wilaya husika zimeelekezwa kuchukua hatua za tahadhari, ikiwemo utunzani wa chakula, upandaji wa mazao ya muda mfupi na yanayostahamili ukame. Hivyo, nitoe wito kwa maeneo yanayopata mvua kwa sasa ni vyema kutumia vizuri mvua hizi zinazopatikana kwa kulima mazao yanayostahili, yasiyohitaji kiasi kikubwa cha mvua ili kuyawezesha mazao hayo kuweza kuiva na hatimaye kujihakikishia kuwa tunakuwa na kiwango kizuri ha chakula hapa nchini.

Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya kuwa nimetoa hoja hizi, naomba kuhitimisha hoja yangu kwa kueleza kuwa nimesikiliza na kufuatilia kwa umakini sana mjadala kuhusu Hotuba ya Waziri Mkuu. Napenda niwahakikishie Waheshimiwa Wabunge na wananchi kwa ujumla kuwa Ilani ya Uchaguzi ya Chama cha Mapinduzi ya Mwaka 2015 mpaka Mwaka 2020 inatekelezeka vema chini ya jemadari Rais wetu mpendwa, Dkt. John Pombe Joseph Magufuli. Mwelekeo wetu ni mzuri, suala la msingi lililopo mbele yetu ni kuongeza umakini na kasi kwa malengo yote tuliyojiwekea ambayo dhamira ni kuwaletea maendeleo wananchi wote kwa Taifa na kwa ujumla yaweze kufikiwa na yaweze kuwafikia wananchi wote popote walipo. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, tarehe 7 Aprili, mwaka huu wa 2019 tuliadhimisha miaka 47 ya kumbukumbu ya kifo cha Hayati Sheikh Abeid Amani Karume, Rais wa kwanza wa Zanzibar na terehe 12 mwezi huu, kwa maana ya keshokutwa tutaadhimisha miaka 35 ya kumbukumbu ya kifo cha aliyekuwa Waziri Mkuu, hayati Edward Moringe Sokoine. Watanzania tutaendelea kuwakumbuka viongozi hao kwa mchango wao mkubwa katika kuleta mabadiliko chanya hapa nchini, kutetea wanyonge na kudumisha misingi ya amani, mshikamano na umoja wa Kitaifa. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kutokana na misingi imara iliyoachwa na viongozi tunaoendelea kuwakumbuka, Tanzania imeendelea kung’ara duniani katika eneo la amani na usalama. Kwa mfano, report ya The Global Peace Index 2018, inaonesha kuwa Tanzania imeendelea kuwa kinara wa amani kwenye ukanda wa Afrika Mashariki na pia tunayapiku pia hata mataifa makubwa ambayo pia yenyewe yanasimamia amani kwa nchi changa. Amani tuliyonayo ni hazina kubwa tuliyoachiwa na viongozi wetu hawa. Wito wangu ni kuwa tuienzi na kuilinda amani ya nchi yetu ikiwa ni sehemu ya kuenzi jitihada za waasisi wa nchi yetu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nawakumbusha Waheshimiwa Mawaziri, viongozi wateule wa Serikali na watendaji wote kuwa, wananchi wamejenga imani nasi baada ya Rais kutupa majukumu ya kumsaidia, hivyo kila mmoja wetu hana budi kutekeleza wajibu wake ipasavyo. Tufanye kazi kwa bidii, tuache mazoea ya kiurasimu, tuchape kazi kwa maslahi ya Taifa na kwa maslahi ya wananchi wetu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nikiwa namalizia kufafanua hoja zangu napenda kuwakumbusha tena Waheshimiwa Wabunge na Watanzania wote kuwa zimebaki siku tano tu kufikia tarehe 14 Aprili, mwaka 2019, siku ambayo Taifa letu litaweka historia kupitia timu yetu ya vijana, Serengeti Boys, itakayozindua mashindano ya mpira wa miguu, maarufu AFCON Under 17, dhidi ya timu ya Nigeria ikitafuta tiketi ya kucheza Fainali za Kombe la Dunia. Uzinduzi wa michezo hiyo utakaofanyika Uwanja wa Taifa tarehe 14 Aprili, siku ya Jumapili ni muhimu kwetu Waheshimiwa Wabunge na Watanzania wote kwenda Uwanja wa Taifa kushuhudia na kuwashangilia vijana wetu ili waweze kushinda vizuri. Timu yetu imeandaliwa vizuri, tunahitaji kushinda michezo miwili tu ili tuweze kucheza Kombe la Dunia, sasa ni zamu yetu, Mungu ibariki Serengeti Boys, Mungu ibariki Tanzania. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba niseme haya mawili yafuatayo: Wakristo duniani kote wanaendelea na kipindi cha toba ambacho ni muhimu katika imani kuelekea siku ya sikukuu ya pasaka. Niwasihi kuwa maisha mnayoishi katika kipindi hiki yalingane na maisha yetu ya kila siku. Kadhalika, kuelekea kumalizika kwa kipindi hicho niwatakie Watanzania wote heri na baraka ya Pasaka. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, la pili; mfungo wa Mwezi Mtukufu wa Ramadhani nao unatarajiwa kuanza mwanzoni mwa mwezi Mei mwaka huu wa 2019. Napenda kutumia fursa hii pia, kuwatakia Waislam wote nchini mfungo mwema na wenye mafanikio, ili kila atakayefanya ibada hiyo aifanye kikamilifu na kama inavyoagizwa katika Quran Tukufu ili tuweze kufuata misingi yake.

Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya maelezo hayo, sasa naomba Bunge lako Tukufu liridhie na kupitisha Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Ofisi ya Waziri Mkuu, Taasisi zilizo chini yake na Mfuko wa Bunge, kama nilivyowasilisha katika hoja yangu ya tarehe 4 mwezi huu wa Aprili, 2019.

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kutoa hoja. (Makofi)

WAZIRI WA ULINZI NA JESHI LA KUJENGA TAIFA: Mheshimiwa Naibu Spika, naafiki.