Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) na Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020

Hon. Julius Kalanga Laizer

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Monduli

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) na Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020

MHE. JULIUS K. LAIZER: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza nakushukuru kwa kunipa nafasi ya kuchangia jioni ya leo. Nianze kwa kuunga mkono hoja, lakini niseme, namshukuru Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, kwa kazi kubwa anayoifanya ya kulijenga Taifa letu na kujenga uchumi wa nchi yetu kwa kipindi chake. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia naomba nimshukuru sana Mheshimiwa Waziri wa Nchi, TAMISEMI, kwa kazi kubwa ya kizalendo anayoendelea kuifanya, waendelee kufanya kazi Watanzania wanaona huduma ambayo Wizara yake inafanya kwa Watanzania. Katika wanaopiga kelele hakuna jimbo hata moja la kwao ambalo hajafika na kuweka alama ya utumishi katika miradi mbalimbali ya maeneo yao. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, ukiangalia wakati mwingine hawasemi, wale wananchi, wanyonge wa Taifa hili wanaohitaji afya, wanaohitaji elimu uliowahudumia ni shukrani mbele za Mungu na wao wanakushukuru. Kwa hiyo, msikatishwe tamaa na maneno ya watu waliokata tamaa wenyewe. (Makofi/Kicheko/Vigelegele)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ukimkuta binadamu asiyeshukuru hata moja jema, ujue binadamu huyo aidha amekata tamaa mwenyewe, au hajui hata anachotakiwa kushukuru au kukipinga. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ni ngumu sana kuamini kwamba wapinzani wote kwenye Bunge hili wana akili sawa, kwamba wote…..

MHE. PASCAL Y. HAONGA: Mheshimiwa Mwenyekiti, taarifa.

MWENYEKITI: Eee, taarifa!

T A A R I F A

MHE. PASCAL Y. HAONGA: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kumpa taarifa mzungumzaji wa sasa kwamba, anaposema kuna watu wamekata tamaa, ni kwamba yeye ndiye amekata tamaa kwa sababu alikimbia mapambano amekwenda kujisalimisha upande wa pili.

MWENYEKITI: Hiyo siyo taarifa, endelea.

MHE. JULIUS K. LAIZER: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba niseme mambo machache kuhusu eneo la jimbo langu, kwamba Mheshimiwa Waziri nakushukuru kwa sababu umetupa milioni 800 kwa ajili ya vituo vya afya. Hata hivyo, Mheshimiwa Waziri akumbuke ana deni la kituo cha Naalarami, alienda mwenyewe alifika, lakini ana deni kubwa la soko la Mto Mbu, ambalo yeye aliahidi lakini sijaona kwenye kitabu, kwa hiyo, wakati anajibu, naomba anisaidie kwamba ni lini soko hilo tutalijenga.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nataka niseme mambo machache, nimemsikiliza Mheshimiwa Msigwa, kaka yangu, amezungumza akasema, Rais amefanya uamuzi na lazima tuangalie uamuzi tunaofanya na matokeo ya uamuzi huo. Naomba nimtajie mambo kumi aliyofanya Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa miaka hii michache na matokeo yake kwa Taifa hili, kwa sasa na vizazi vijavyo. Halafu mwisho wapime na Watanzania wapime, kama wao hawakubaliani na haya ambayo anafanya, Watanzania watapima mwaka 2020 na watafanya uamuzi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, uamuzi wa kwanza wa Serikali hii…

MHE. FRANK G. MWAKAJOKA: Mheshimiwa Mwenyekiti, taarifa.

MWENYEKITI: Mheshimiwa Frank kaa, muda wetu umekwisha, Mheshimiwa muda wetu umekwisha kaa, taarifa nilishafunga, kaa Mheshimwa Frank kaa chini.

MHE. JULIUS K. LAIZER: Mheshimiwa Mwenyekiti, muda wangu. Rais amefanya uamuzi wa kulifufua Shirika la Ndege, ili kusaidia usafiri wa ndani na nje ya nchi kwa ajili ya utalii na kupata mapato ya Taifa hili. Nataka mmoja asimame aseme ndege haina faida kwenye nchi hii ili Watanzania wapime ni nani anayesema ukweli na nani mchawi wa maendeleo yetu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Taifa hili ili liwe na uhakika wa uendelezaji wa viwanda na uchumi endelevu, lazima tuwe na umeme wa uhakika. Rais amefanya uamuzi ili tutafute umeme wa maji kwa ajili ya uchumi wa Taifa hili na hao na wao kama wajasiriamali watatumia umeme huo, nataka atuambie, ni nani kati yenu ambaye hataki umeme kwa ajili ya maendeleo ya nchi yetu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Rais na Serikali imefanya uamuzi wa kujenga miundombinu ya Standard Gauge kwa ajili ya kusafirisha mazao na kusafirisha na kujenga uchumi wa nchi yetu. Nani kati yao ambaye hakubaliani na miundombinu salama kwa ajili ya uchumi wa nchi yetu na uwekezaji wa taifa hili.

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la tano, Mheshimiwa Rais wa nchi hii amefanya uamuzi wa kutengeneza taifa la watu wenye afya njema, kwa kuamua kujenga vituo vya afya 300 na zaidi ya hospitali za wilaya zaidi ya 60 ili Watanzania wapate afya njema, afanye kazi kwa ajili ya uchumi wa nchi yetu. Nani hataki afya ya Taifa hili iweze kutengemaa. (Makofi)

WABUNGE FULANI: Oyeee. (Makofi)

MHE. JULIUS K. LAIZER: Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la sita, Katiba ya nchi yetu inasema, elimu ni haki ya msingi ya kila Mtanzania. Mheshimiwa Rais amefuta ada watoto wetu wanasoma elimu bure ili kupata haki kwa aliye na fedha na asiye na fedha. (Makofi)

MHE. MCH. PETER S. MSIGWA: Mheshimiwa Mwenyekiti, taarifa.

MHE. JULIUS K. LAIZER: Mheshimiwa Mwenyekiti, na sisi Waheshimiwa Wabunge…

MWENYEKITI: Muda wetu umekwisha, Mheshimiwa Msigwa, nilishatoa taarifa tatu huku na huku nne.

(Hapa baadhi ya Wabunge walizungumza bila kufuata utaratibu)

MWENYEKITI: Don’t question me.

MHE. JULIUS K. LAIZER: Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Rais amefanya uamuzi wa elimu bure ili Mtanzania asiye na fedha na mwenye fedha waweze kupata haki yao ya Kikatiba ya kupata elimu. Tusijilinganishe tulioko ndani tunaweza kulipa ada kuna Watanzania walioko vijijini ambao hata Sh.5,000 kwa siku ni tabu kwake, hivi leo tubeze uamuzi ambao ukienda kwenye kitabu hiki, ukurasa wa 198, Mheshimiwa Mwakajoka anajua ni kiasi gani cha fedha cha elimu bure kimeenda katika Jimbo lake. Kama ninyi ni waungwana simameni waambieni wapiga kura wetu wakatae elimu bure, wakatae fedha zinazopelekwa kwenye Majimbo yenu ili irudi tuamini kwamba hamthamini elimu bure. (Makofi)

MBUNGE FULANI: Yes.

MHE. JULIUS K. LAIZER: Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la saba, moja ya tatizo lililopo kwenye nchi yetu ni uchumi wetu haukulindwa na rasilimali zetu zilitumika vibaya. Tumetunga sheria hapa ya kulinda rasilimali za Taifa, leo husikii habari ya utoroshaji wa madini, husikii habari ya ujangili kwa wanyama wetu, halafu ninyi mnataka kuona siyo uamuzi? Nataka tupime matokeo kwa kupata wanyama wazuri pamoja na utalii kwa ajili ya uchumi wa Taifa letu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, uamuzi wa kutunga Sheria ya Kudhibiti Madawa ya Kulevya na uamuzi kutoa ardhi kwa ajili ya wakulima na mimi nasema Taifa hili liko salama… (Makofi/Vigelegele)

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)