Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) na Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020

Hon. John Wegesa Heche

Sex

Male

Party

CHADEMA

Constituent

Tarime Vijijini

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) na Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020

MHE. JOHN W. HECHE: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana kwa kunipa nafasi nami leo niweze kuchangia kwenye hizi bajeti mbili za TAMISEMI na Utawala Bora.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza nianze kwa kumpongeza sana CAG Prof. Assad, kwa kweli Prof. Assad ameitendea haki na ametendea haki uprofesa wake na ameonyesha ni kwa nini hasa kulikuwa na wingu la kutaka kumchomoa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nilifikiri Serikali yenu ambayo kwa miaka miwili imekuwa ikijitangaza kwamba inapiga vita ufisadi. Mtu ambaye alitakiwa kukumbatiwa na Serikali na kulindwa kwa gharama zote ni huyu Prof. Assad ambaye ameleta taarifa ambayo mpaka mama yangu kule Kijijini anasema sasa nimejua kwa nini CAG yupo na CAG anafanya kazi gani. Kwa hiyo, ningependa nianze na hilo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, la pili, nimnukuu kidogo Mwalimu Nyerere kwenye kitabu chetu cha TANU na Watu Wetu. Anasema, “Viongozi wa TANU hawana budi watokane na watu, kwa sababu TANU ni chama cha watu na sababu ya pili ni kwamba kazi ya TANU ni kuwatumikia watu. Sitaki kueleza mambo yanayofanywa na Serikali kama vile kujenga shule, hospitali, barabara na kadhalika. Nataka kusema juu ya shida za watu za kila siku.” Mwisho wa kunukuu. Mengine tuendelee. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, sehemu ambayo Serikali inakutana na shida za watu za kila siku ni kwenye Halmashauri zetu. Halmashauri ndizo zinasozimamia shule ambazo watoto wa wananchi masikini wanasoma; sio watoto wetu hapa. Hakuna Mbunge hata mmoja humu anasimama aseme mtoto wake anasoma kwenye shule za msingi za Serikali, hayupo hata mmoja. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwenye hospitali, ndiyo kwenye watu wetu, wanakwenda kutafuta madawa kule na kutibiwa…

MHE. HUSSEIN N. AMAR: Taarifa.

MHE. JOHN W. HECHE: Akina mama wanajifungua kule.

MHE. HUSSEIN N. AMAR: Taarifa.

MWENYEKITI: Taarifa Mheshimiwa Heche

T A A R I F A

MHE. HUSSEIN N. AMAR: Mheshimiwa Mwenyekiti, nataka nimpe taarifa mdogo wangu hapo, asiseme kwamba hakuna Mbunge ambaye anasomesha. Mimi kuna wajukuu zangu wanasoma kwenye hizo shule. (Makofi)

(Hapa baadhi ya Wabunge walizungumza bila kufuata utaratibu)

MWENYEKITI: Mheshimiwa Heche, naomba uendelee.

MHE. JOHN W. HECHE: Mheshimiwa Mwenyekiti, unilindie muda wangu ni kidogo nizungumze matatizo ya nchi, tafadhali.

MWENYEKITI: Endelea Mheshimiwa

MHE. JOHN W. HECHE: Mheshimiwa Mwenyekiti, kaka yangu sina sababu ya kumjibu kwa sababu…

Mheshimiwa Mwenyekiti, shule za msingi na shule za sekondari zipo kwenye Halmashauri, hospitali zinasimamiwa na Halmashauri, matatizo ya kila siku ya watu ambayo Mwalimu Nyerere aliyasema kwenye kitabu cha TANU yapo kwenye Halmashauri. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nianze kwanza na Halmashauri yetu ya Tarime, Kwa masikitiko makubwa; na nimpongeze Mheshimiwa Jafo kwa kazi kubwa ambayo amekuwa akiifanya na aangalie hili. Halmashauri yetu ya Tarime, huu ni mwezi wa Nne vikao vimesimamishwa kinyume cha utaratibu wa kisheria. Hili suala la utawala bora la kudhibiti Wakuu wa Mikoa na Wakuu wa Wilaya wanajifanyia vitu vyovyote ambavyo wanaamua, eti kwa kisingizo kwamba kuna ufisadi umefanyika. Fine!

Mheshimiwa Mwenyekiti, kama ufisadi umefanyika, kuna watu waliofanya huo ufisadi. Mkuu wa Mkoa achukue hatua kwa hao watu waliofanya ufisadi. Sasa leo unazuia vikao vya Halmashauri; Finance Committee haikai, Baraza la Madiwani halikai.

Mheshimiwa Mwenyekiti, leo tulikuwa na watoto 1,030 wameshindwa kwenda sekondari tangu mwezi wa Kwanza, hakuna vyumba vya madarasa, tukatenga zaidi ya shilingi milioni 250 kwenda kujenga madarasa. Hizi pesa tunazo, ni pesa za wananchi wa Tarime ambao wamekusanya wenyewe kwenye nyanya na vitunguu, tunazo zipo kwenye akaunti. Mkuu wa Mkoa amezuia kwamba vikao havikai, anataka sisi tuwe tunamwandikia barua yeye kumwomba pesa kinyume cha utaratibu wa sheria. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, utaratibu wa kisheria, watu wenye mamlaka ya kugawa pesa ni hili Bunge na Bunge la wananchi ambalo ni la Halmashauri pale Wilayani. Sasa Mkuu wa Mkoa anataka kujigeuza Pay Master General wa Mkoa. Yeye ndio anataka sisi tuwe tunamwomba. Nimesema hakuna siku tutamwomba hizo pesa. Mwangalie kama hizi hujuma mnazowafanyia wananchi wa Tarime kwa kuwabagua kwa makusudi ni sawa sawa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa nini kama wateule wa Rais; leo hapa Assad amezungumza kuhusu upotevu wa zaidi ya shilingi bilioni 16 kwenye uniforms za Askari, mbona hamjazuia Jeshi la Polisi lisifanye kazi? Jana Gilles Muroto alikuwa anasema hapa atapiga watu mpaka wachakae, mbona hamjawazuia wasifanye kazi kwa sababu kuna ufisadi kwenye Jeshi la Polisi. Amezungumza mambo mengi hapa, mbona hamjazuia hao watu wasifanye kazi? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi simtetei mwizi na nipo clear; na Mwenyekiti wa Halmashauri yangu katika kupigania hili aliwekwa ndani siku 11 kwa sababu ya kupigania ufisadi uliofanywa na wateule walioteuliwa na Mheshimiwa Rais. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa Mheshimiwa Jafo naomba atengue agizo batili hili, wananchi wa Tarime wapate haki ya Baraza lao la Madiwani ku-deliberate kwenye issue na wafanyiwe maendeleo. Hilo la mwanzo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, la pili, nije kwenye ajira. Tumeona hapa vijana wetu wako vyuoni wanasoma. Hawa vijana wanahitaji ajira. Kila siku nyie mnazungumza humu. Nyie mmeajiriwa na wananchi, mnalipwa mamilioni ya pesa, wanahitaji ajira hao. Watoke mwatengenezee mazingira mazuri kama ni kujiajiri, wajiajiri na mikopo iwepo. Kama ni ajira za Serikali, zitoke; kama ni private sector, iajiri.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa miaka minne mfululizo Serikali hii inayotudanganya inakusanya kuliko wote haijaajiri wananchi. Juzi mmetangaza ajira 4,000 za Walimu, vijana walio-apply ni 11,300. Mnaweza kuona crisis iliyopo. Mnatangaza ajira 4,000 wanajitokeza vijana 11,300 na nyie mpo hapa mnasema kila kitu kinaenda sawa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwenye afya. Bajeti iliyopita tulitenga shilingi bilioni 561, pesa ambazo mmepeleka mpaka sasa ni shilingi bilioni 89 peke yake. Hakuna madawa, hakuna gloves wala nyuzi. Serikali yenu inayokusanya kuliko zote, kwenye madawa mmetoka hapa na rhetoric za kisiasa mmepeleka chini ya asilimia 15. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, mnasema ninyi ni Serikali ya viwanda; kwenye viwanda mlitenga shilingi bilioni 90, pesa ambazo zimekwenda zimetolewa na Serikali kwa ajili ya maendeleo ya viwanda ni shilingi bilioni 5.4, asilimia sita peke yake. No wonder mnasema cherehani tano ni viwanda, kwa sababu kama shilingi bilioni 90 mmetenga, mnapeleka shilingi bilioni 5.4 kwa nini msiseme kiwanda cha cherehani ni kiwanda na gongo ni kiwanda. Kwa nini msiseme hivyo? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kilimo kinaajiri Watanzania asilimia 70, kinatoa chakula kwa Watanzania asilimia 100, kinatoa malighafi za viwandani asilimia 80; mmetenga shilingi bilioni 98.1, zimekwenda shilingi bilioni 42. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwenye maji ambayo mmesema mnamtua mama ndoo kichwani, Mfuko wa Maji tulipitisha hapa kwa mbwembwe mkapigiana makofi, shilingi bilioni 299, pesa zilizokwenda kutoka kwenye Mfuko wa Maji ni shilingi bilioni 1.62… (Makofi)

NAIBU WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI: Mheshimiwa Mwenyekiti, taarifa.

MHE. JOHN W. HECHE: Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa…

NAIBU WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI: Mheshimiwa Mwenyekiti, taarifa.

MHE. JOHN W. HECHE: Tulia Mheshimiwa Waziri utapata nafasi ya kujibu, subiria.

MWENYEKITI: Mheshimiwa Heche, taarifa.

MHE. JOHN W. HECHE: Tulia.

NAIBU WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI: Mheshimiwa Mwenyekiti, taarifa.

T A A R I F A

NAIBU WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nimpe taarifa kaka yangu Mheshimiwa Heche, katika bajeti ya mwaka 2018 tulitengewa shilingi bilioni 100,058 katika Mfuko wa Maji. Mpaka mwezi Februari tumepokea zaidi ya shilingi bilioni 93. Kwa hiyo, namwombe tu ajiridhishe katika kuhakikisha halipotoshi Bunge letu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana. (Makofi)

MWENYEKITI: Mheshimiwa Heche taarifa hiyo.

MHE. JOHN W. HECHE: Mheshimiwa Mwenyekiti, sources za maji zipo tatu…

MHE. GOODLUCK A. MLINGA: Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu utaratibu.

MHE. JOHN W. HECHE: Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi sizungumzii pesa za wahisani za kutoka India. Mimi nazungumzia…

MHE. GOODLUCK A. MLINGA: Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu utaratibu.

MHE. JOHN W. HECHE: Mimi nazungumzia pesa za Mfuko wa Maji na Mheshimiwa Waziri anajua ninachokizungumza.

Mheshimiwa Mwenyekiti, bajeti ambayo tunakuja kupitisha hapa kila mwaka, ina maana tuna matatizo ya wananchi tunataka kwenda kuyatatua. Kama tutakuja hapa watu watalipwa pesa, halafu utekelezaji ni zero; general budget utekelezaji ni chini ya asilimia 30. Leo tunakwenda kupitisha bajeti nyingine kwa sababu gani? Hapa Mawaziri wamejua kila siku wakisimama… (Makofi)

MBUNGE FULANI: Mheshimiwa Mwenyekiti, taarifa.

MHE. JOHN W. HECHE: …ni kutukana CHADEMA mnapiga makofi mnasahau matatizo yaliyowaleta hapa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, elimu. Tangu kuwepo na elimu bure, enrollment kwenye shule ni asilimia 17…

MBUNGE FULANI: Mheshimiwa Mwenyekiti, taarifa.

MHE. JOHN W. HECHE: …lakini miundombinu ni asilimia moja peke yake mme-improve. Matundu ya vyoo zaidi ya asilimia 63. Kwa wasichana hakuna, vyoo wanajisaidia vichakani… (Makofi)

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

MWENYEKITI: Mheshimiwa Heche muda wako umemalizika.

MHE. JOHN W. HECHE: Matundu ya vyoo kwa wavulana hakuna; hakuna mabweni… (Makofi)

MWENYEKITI: Umemalizika muda wako Mheshimiwa Heche.

MBUNGE FULANI: Taarifa.

MHE. JOHN W. HECHE: Je, mnapaswa kuchaguliwa tena au mwondolewe kwa... (Makofi)

MWENYEKITI: Mheshimiwa Heche muda umeisha.