Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Chilonwa
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
0
Ministries
nil
MHE. JOEL M. MAKANYAGA: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza kabisa naomba kushukuru kupata nafasi hii ya kuweza kuchangia katika hotuba zilizotolewa na Mawaziri wa Wizara hizi mbili ambazo zipo chini ya Ofisi ya Rais. Pili, nimpongeze sana Mheshimiwa Rais wetu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kazi kubwa na nzuri anayoifanya. Sisi wote tunaona na tunashuhudia yale yanayoendelea katika Awamu hii ya Tano. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, niwapongeze sana Mawaziri wetu wawili, Mheshimiwa Jafo pamoja na Naibu wake lakini pia Mheshimiwa Mkuchika pamoja na Naibu wake katika Wizara zetu hizi mbili kwa taarifa zao walizoziwasilisha hapa jana ambazo zimezihidhirisha kabisa nia na kusudi zima la Serikali ya Awamu ya Tano katika kuhakikisha kwamba Tanzania hii inavuka kutoka hapa ilipo kuingia katika Tanzania ya uchumi wa kati ifikapo mwaka 2025. Nawapongeza sana. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa sababu hiyo nianze kwa kuunga mkono hoja za Wizara zote hizi mbili kwa asilimia mia. Kwanza kabisa, niseme kwamba kupanga ni kuchagua, Serikali yetu ya Awamu ya Tano ilipanga na ikachagua kwamba tunataka kufika mwaka 2025 nchi yetu iwe imeingia kwenye uchumi wa kati na njia tutakayoichukua ni hii ambayo tunaiona sasa, tunaziona bajeti zetu zilivyo makini kabisa kuhakikisha kwamba tunafika huko.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ipo mipango mikubwa, midogo na ya kati ambayo lazima yote iende kwa pamoja katika kuhakikisha kwamba tunaweza kuvuka na kufika kule tunapotaka. Tuna mipango mikubwa ambayo tunaiona, mipango ya Stiegler’s Gorge, SGR na kununua ndege ni mipango mikubwa. Mipango hii wakati mwingine watu wanashindwa kuoanisha, tunahitaji macho haya ya usoni, ya kwenye ubongo na ya rohoni tuweze kuona kwa ujumla wake tukajumlisha kwamba kweli mipango hii inawalenga Watanzania wote na hasa wa kipato cha chini. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, mipango hii ndiyo inaweza kutuwezesha sisi kutekeleza mipango mingine midogomidogo iliyo muhimu kwa ajili ya wananchi wa kati. Ukizungumzia elimu, ili tuweze kuingia katika Tanzania ya uchumi wa kati, tunahitaji wananchi wetu wawe na elimu bora. Tunaiona mipango ya Serikali ya elimu bila malipo lakini tunaiona mipango ya Serikali hii, tumekuwa tukilia walimu lakini sasa ajira zimetoka kwa walimu elfu nne na mia saba. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, huwezi ukatekeleza matakwa yako yote kwa wakati mmoja hata siku moja. Kila jambo ni mchakato, utaangalia kwenye elimu, afya na kadhalika, kwa hiyo, lazima twende kidogo kidogo. Walimu hawa wachache ambao Serikali imetoa ni mpango kamili na mwaka kesho na mwaka kesho kutwa lakini mwisho wa siku tutakuwa na uwanja mzuri wa kutoa elimu iliyo bora kwa vijana wetu. Mbagala Zachiem
Mheshimiwa Mwenyekiti, maji ni muhimu pia, tunahitaji wananchi wetu wawe na afya bora. Afya bora siyo suala la kwenda zahanati au kwenye kituo cha afya tu bali unaishi vipi nyumbani, mazingira yako yakoje? Bila maji mazingira majumbani yanakuwa ni shida tupu na tunaweza kuhatarisha afya zetu kutoka nyumbani moja kwa moja. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali imejitahidi sana kuhakikisha kwamba wananchi wanapata maji na sisi Wabunge wenyewe kupitia Mifuko yetu ya Majimbo tumejitahidi sana. Mimi jimboni kwangu toka nimeingia 2015 hadi leo nimekwishachimba visima kumi na mbili, lakini juzi Serikali imenisaidia nimepewa visima nane. Kama watu hawayaoni haya hawataona kitu. Nachoiomba Serikali ni kuongeza kasi, visima hivi vikichimbwa basi viweze kuwekewa miundombinu ili watu waweze kuyafaidi maji hayo na yaweze kuwasaidia. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, tunazungumzia vituo vya afya 352 katika Halmashauri zetu, katika hivyo viwili vinatoka Halmashauri ya Chamwino; kimoja Jimbo la Chilonwa na kingine Jimbo la Mtera. Tunaishukuru sana Serikali kwa kazi kubwa wanayoifanya. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini hospitali za wilaya 67, katika hizo moja ipo Halmashauri ya Chamwino, tunaipongeza sana Serikali. Kama hiyo haitoshi, nakushukuru sana Mheshimiwa Jafo na namshukuru sana Mheshimiwa Rais kwa kutuletea Hospitali ya Uhuru katika Wilaya yetu ya Chamwino. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ili mambo yote haya yaweze kwenda lazima kuwe na mawasiliano mazuri baina ya maeneo yetu mbalimbali. Barabara na madaraja yanaendelea kujengwa awamu kwa awamu, kama nilivyosema hatuwezi kufanya mambo yote kwa wakati mmoja. Jimboni kwangu tumetengeneza madaraja mengi, Daraja la Manyemba, daraja la kutoka Mlebe kuja Chinangali II na sasa tunashughulikia daraja la kutoka Makoja kuja Mwengamile, ni kazi kubwa inayofanywa. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, suala la TARURA na TANROADS, watu wanazungumzia kujaribu ku-balance, ni jambo jema lakini n kuangalia wapi kuna jukumu gani la kufanya na wapi kuna jukumu gani la kufanya. Mimi naiomba Serikali angalau basi kutoka asilimia 30 TARURA iende kwenye asilimia 40 hata tusipofika 50 ili nayo iweze kuboresha kazi zake nzuri ambazo inaendelea kuzifanya. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, MKURABITA ni jambo jem,a tunataka wananchi hawa wajiletee maendeleo yao wenyewe, wanyanyuke kiuchimi. Mtu mmoja mmoja ili aweze kunyanyuka kiuchumi anahitaji kuwezeshwa na Serikali na Serikali imeleta MKURABITA ili watu waweze kurasimisha maeneo yao, wakapata hati miliki za kimila, hati hizi zikatambuliwa na mabenki ili waweze kukopa na kujiletea maendeleo. Ninachokiomba Serikali isimamie kwa dhati mabenki kuhakikisha kwamba wanazitambua hizo hati na wananchi wanapata mikopo kadri inavyostahili. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, TASAF sasa tunaingia awamu ya tatu. Naiomba sana Serikali maeneo yale ambayo yalikuwa haijafika sasa ikafike maana ndiyo mpango kamili wa TASAF III. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nimalize kwa ombi mahsusi la maboma ya shule, nyumba za walimu, zahanati na maabara ambapo wananchi wetu wameweka nguvu zao nyingi sana, wamejitolea kujenga na wamefika mahali wamekwamba. Sawa Serikali imeweka nguvu lakini naiomba iongeze nguvu zaidi ili maboma haya yaweze kumalizika na wananchi waweze kuyafaidi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, namalizia kwa kuunga mkono hoja hii asilimia mia, ahsante sana. (Makofi)