Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Male
Party
CUF
Constituent
Mtwara Mjini
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
0
Ministries
nil
MHE. MAFTAHA A. NACHUMA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana. Nianze kumshukuru Mwenyezi Mungu Subhanahu wataala kwa sababu tangu tumemaliza kufanya Uchaguzi Mkuu ndani ya chama, uchaguzi ambao ulimweka Prof. Ibrahim Lipumba kuwa Mwenyekiti wa Chama Taifa, lakini mimi ninayezungumza hapa Maftah Nachuma kuwa Makamu Mwenyekiti Bara. Tunamshukuru Mwenyezi Mungu kwa kuweza kutusimamia na sasa chama chetu kimesimama imara. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nianze kwa maneno ambayo alisema Mwanafalsafa Mtume Muhammad (S.A.W.) karne ya sita alizungumza maneno yafuatayo, kwamba man laa yashkur kaliila, laa yashkur kathiira. Kwamba yeyote ambaye hashukuru kidogo alichopewa, basi hata akipewa kingi hawezi kushukuru.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kwa dhati kabisa nishukuru Wizara hii ya TAMISEMI kwa bajeti ambayo mwaka 2018 tulipigania sana zikaletwa Mtwara shilingi bilioni 21 kwa ajili ya ujenzi wa miundombinu pale Mtwara Mjini, kujenga mifereji, kujenga shopping mall. Tunaishukuru sana TAMISEMI kwa sababu imeweza kutusikiliza kilio cha wana Mtwara na sasa tunajenga mifereji ya kupeleka maji baharini ili Mtwara sasa tuondokane na mafuriko.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sambamba na shukrani hizo, bado kuna makandokando mengi katika zile fedha ambazo zimeletwa shilingi bilioni 21. Wale ambao walipewa dhamana ya kupitia na kusaini mikataba, kuna makandokando mengi sana. Mikataba ile ilisainiwa kwa namna ambayo haieleweki, haikuwa na uwazi. Kwamba watu waliitwa kutoka Mtwara Mjini, akaitwa Mkurugenzi, akaitwa aliyekuwa Meya kwenda Dar es Salaam, baadaye wakarudishwa pale Mtwara wakiwa wamesaini mikataba. Kwa hiyo, kuna malalamiko mengi sana.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna Madiwani ambao wanazungumza mambo mazito sana, kwamba mikataba yule Mkandarasi aliyepewa ule mradi wa kujenga miundombinu Mtwara Mjini mkataba wake umesainiwa kimazingara mazingara. Tunaomba Wizara ya TAMISEMI ifanye uchunguzi haraka iwezekanavyo, wale wote waliohusika kwamba wamepewa kiasi kidogo ili wampe yule Mkandarasi kutoka China, kufanyike uchunguzi wa kina, waweze kuchukuliwa hatua. Kwa sababu kiasi kinachotajwa kwamba kimetolewa ni kiasi kingi sana kitu ambacho zile fedha zingeweza kusaidia kuboresha miundombinu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, hivi ninavyozungumza ni kwamba mpaka hivi sasa ule mradi unasuasua. Fedha zipo, Mkandarasi anasuasua kwa sababu mazingira ya ule mkataba ni mazingira ya ajabu ajabu. Tunaomba uchunguzi ufanyike. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la pili, nizungumzie suala la Hospitali ya Mtwara. Hospitali zetu za Mtwara hasa ile Hospitali ya Wilaya lakini pia ni ya Mkoa ya Mtwara, tunaomba ipelekewe vifaa. Hospitali ile haina X-Ray, haina vifaa vya kupimia, haina CIT-Scan. Wananchi pale wanapotaka kupimiwa au wanavyotaka kupimwa, pale ambapo wanaambiwa waende waende Hospitali ya Mkoa ambapo imezukuwa Hospitali ya Rufaa hivi sasa, wakifika pale vile vipimo vyote havipo, wanaambiwa waende Dar es Salaam. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, tunaomba sana, tumekuwa tunazungumza kwa muda mrefu sana kwamba hospitali hii ipelekewe vifaa, vifaa tiba, hata dawa nayo pia hakuna.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna jambo lingine la ajabu sana. Ukienda kwenye hospitali hii hivi sasa kuna walinzi ambao wamewekwa wa SUMA JKT wanaoangalia wagonjwa wanavyoenda pale kutibiwa. Nimepata malalamiko mengi kama Mbunge kwamba walinzi wanawapiga wagonjwa wanavyoenda kuingia hospitali pale eti kwa sababu wanapita mlango ambao hauko sawa sawa. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekit, sasa naiomba Serikali, pamoja na kwamba tunahitaji ulinzi uwepo katika hospitali zetu, lakini lazima wagonjwa waweze kuheshimiwa, Wana- Mtwara waweze kuheshimiwa, wasipigwe na hapa Mapolisi na SUMA JKT ambao wamewekwa pale.
Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine ambalo naomba kuzungumza ni suala hili la demokrasia; Katiba katikaIbara ya 146 inaeleza kwamba: TAMISEMI imepewa mamlaka ya kusimamia chaguzi. Mheshimiwa Waziri hapa kazungumza kwamba mwaka huu tutakuwa na uchaguzi wa mitaa, lakini kuna mambo ya ajabu sana tumekuwa tuna- experience ndani ya nchi yetu tangu chaguzi hizi zinafanyika hasa hasa hizi chaguzi za marudio.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tunachoomba kuelekea katika uchaguzi huu jambo la kwanza kuwe na Tume Huru ya Uchaguzi; tunahitaji kuwe na Tume Huru ya Uchaguzi ili iweze kusimamia sawasawa kwa sababu kuna mambo mengi ambayo yamekuwa yakijitokeza katika usimamizi wa hizi chaguzi. Kwa mfano, suala hili la kutafuta wagombea vyama vya siasa vinateua wagombeakwa mujibu wa sheria lakini wakipelekwa kwa wale wanaosimamia, wale wanaoteua, wale watendaji wakata wanawaengua wagombea kutoka upinzani.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tunazungumza haya tuna ushahidi sana, kwa mfano, pale Kata ya Nanguruwe kuna wagombea walishawishiwa wakahamia Chama cha Mapinduzi, lakini sisi Chama cha Wananchi - CUFtukasimamia uchaguzi na mchakato ndani ya chama. Wagombea wetu walivyokwenda kutakana kuteuliwa wakaenguliwa bila sababu za msingi, wakaenguliwa bila utaratibu, wakati tunasema nchi yetu niya kidemokrasia na ni nchi ya vyama vingi. Nami nilienda pale Nanguruwe kuzungumza naMtendaji wa Kata nikamwambia kwa nini unamwengua mgombea wa CUF akanieleza kwamba hajatimiza vigezo, hali ya kuwa kila ya kitu tumefanya,form kajaza sawasawa na alivyojaza mgombea wa CUF, ndivyo alivyojaza mgombe wa CCM lakini mgombe wa CUF amaenguliwa. Sasa haya ni mambo ya ajabu sana, kwa hiyo tunaiomba TAMISEMI tunavyokwenda kusimamia uchaguzi wa Serikali za Mitaa, haya mambo yaweze kufanyika sawasawa. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, eneo lingine pia pale Kata ya Tangazo, Mtwara Vijijini napo, pia kulikuwa na mazingira hayo hayo kwamba wagombea wa Chama cha Wananchi - CUF wanaenguliwa bila kufuata taratibu za kisheria na Watendaji Kata na ukimuuliza Mtendaji Kata anasema nimepata maelekezo kwamba huyu mtu hafai na kweli tumemwondoa. Kwa hiyo, mazingira hayo tunanyima demokrasia ndani ya nchi yetu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine kwenye hizi chaguzi, sisi tumeshiriki chaguzi zote za marudio Chama cha Wananchi - CUF,hasa kule kwetu Kusini kwa mfano,kuna kata moja, Kata ya Nalingu pale Mtwara Vijijini chama cha Wananchi - CUF kilipambana, mgombea wetu alikuwa makini, wananchi wakampenda, wananchi wakamchagua, tulivyokuja kwenye kuhesabu kura chama tawala kinaleta polisi ndani ya masanduku na wakawaambia kwamba bwana tunachotaka hapa sisi kama polisi, sisi ndio tunahesabu hizi kura. Kwa hiyo hiki ni kinyume kabisa cha demokrasia nchini, kwamba tunapoingia kwenye chaguzi tusiruhusu Jeshi Polisi kwenda kuhesabu, kwenda kung’ang’ania masanduku ya watu waliofanya maamuzi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tunaomba sanakwamba, kama kweli tunahitaji amani ya kweli, ni lazima chaguzi hizi tuzisimie sawasawa tufuate sheria, tufuate Katiba namna inavyosema,Tume ya Uchaguzi iweze kuwa huru, wale askari wakae mbali kwa mujibu wa sheria inavyosema, lakini hivi sasa chaguzi zote za marudio tumeona, tumeweza kujiridhisha kabisa kwamba polisi wanaingia ndani kwenda kuhesabu kura. Je hii ni kazi ya polisi? Tunaomba sana haya mambo yaweze kuzingatiwa.(Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine, Mheshimiwa Nkamia hapa ameezungumza mambo mengi yanayohusu Chemba, lakini sisi pia kama Chama cha Wananchi - CUF kule Chemba yule DC wake niliwahi kuzungumza kwenye Bunge hili, niliwahi kuzungumza hapa kwamba, balada ya kusimamia miongozo ya Serikali, badala ya kusimamia taratibu za nchi hii,yeye kazi yake kubwa amekuwa anafanya kazi ya kuwafukuza Wenyeviti wa Mitaa wa Chama cha Wananchi - CUF. Hivi ninavyozungumza zaidi ya Wenyeviti tisa amewafukuza, yaani anaeenda sehemu anaitisha mkutano, anawaambia hawa mimi nawafukuza. Hafukuzi Wenyeviti wa CCM, hafukuzi Wenyeviti wa chama kingine, yeye anafukuza Wenyeviti wa Chama cha Wananchi - CUF.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa hili naomba kujua,utawala bora tunaozunguza hapa ni utawala bora wa aina gani, demokrasi tunayozungumza ni demokrasia ipi, kama DC yupo pale kuangalia upinzani, pale waliposhinda anawafukuzafukuza. Wakati tunasema kwamba demokrasia uwaache wananchi wafanye wanayotaka, wamchague kiongozi wanayemtaka, wananchi wamechagua viongozi, wamechagua Wenyeviti waCUF,DC anaenda anawafukuza Wenyeviti tisa, ni mambo ya ajabu sana. Tunaomba sana Serikali kwa kweli kama tunahitaji tuwe na amani na utulivu ndani ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania tunahitaji hawa Ma-DC wafanye kazi zao walizopangiwa na mteule wao.
T A A R I F A
MWENYEKITI: Mheshimiwa Agnes, taarifa.
MHE. AGNESS M. MARWA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nampataarifa mzungumzaji kwa kifungu cha 68(7), yeye angelikuwa anaona Tanzania haina demokrasia, leo hii imekuaje yeye kutoka upinzani amekuwa Mbunge?
MWENYEKITI: Mheshimiwa Maftaha.
MHE. MAFTAHA A. NACHUMA: Mheshimiwa Mwenyekiti, namheshimusana kwa sababu anachokizungumza hakifahamu. Hapa tunachozungumza,ni kuhusu uchaguzi wa Serikali za Mitaa, na ipo kwenye taarifa ya Waziri wa TAMISEMI ukurasa wa 12kwamba, mwaka huu kuna uchaguzi wa Serikali za mitaa tunazungumza yanayojiri, yanayojitokeza katika chaguzi hizi ambazo tumekuwa tukizifanya kwa muda wa miaka mitatuhivi sasa, kwamba Wapinzani wanaong’olewa, wapinzani wanaondolewa lakini Ma-DC waliochaguliwa kusimamia maendeleo ya wananchi wao wanafanya kazi ya kuhujumu upinzani na kuwafukuza Wenyeviti waliochaguliwa wa Chama cha Wananchi - CUF na wa vyama vingine, sasa hapa tunasema hakuna demokrasia ya kweli.
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini nizungumze jambo moja hawa Ma-DC na Ma-RC kwa sababu wamekuwa na utamaduni, kwa mfano, pale kwangu Mtwara,juzi Mheshimiwa Rais kaja Mtwara, katika jimbo la Maftaha Nachuma ambaye ndiye, Mbunge wa Jimbo la Mtwara Mjini, RC tunamuuliza kwamba katika ratiba umemweka Mbunge wa jimbo ili aweze kusalimia wananchi wake. RC anasema wewe hatuwezi kukuweka kwa sababu wewe ni mpinzani. Sasa haya ni mambo ya ajabu sana.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hata hivyo,kule kote alikopita ambapo Wabunge ni wa Chama cha Mapinduzi wamepewa nafasi Mkoa ule ule lakini mimiwa Mtwara Mjini nauliza pale mbona hujaniweka kwenye ratiba, ananijibu wewe ni mpinzani. Sasa hii ni demokrasia ya wapi, lakini niwaambie, naomba niwaambie kwamba hawa Ma-DC na Ma-RCna viongozi wengine wanapimwa na Mheshimiwa Rais kwa kazi wanazofanya, sio kazi ya kuwahujumu wapinzani ndani ya nchi hii. Mheshimiwa Rais atawapima atawapandisha vyeo kwa kazi wanazozifanya.(Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa tunaomba sana Serikali, kwa sababu hawa watu wanafahamika, nilishawahi kuzungumza hapa ndani ya Bunge hili kwenye Briefingnikamweleza Waziri Mkuu wakati Fulani, akasema hakuna maagizo yoyote wanayotuma hawa Ma-DC na Ma- RC waweze kuwahujumu upinzani na hasa pale ambapo Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania au Kiongozi yoyote wa Kiserikali anavyokwenda kutembelea kwenye maeneo yetu kwamba ni Mbunge lazima upewe nafasi. RC anayetoka Mtwara Mjini anamnyima nafasi Maftaha eti kwa sababu ametokea Chama cha Wananchi CUF, anaenda Nanyumbu, anaenda kule wapi, anaenda kuwapa wale Wabunge wa CCM, Mkoa mmoja ule ni ubaguzi na sisi tunasema kwamba kama tunahitaji nchi hii iwe na amani ili amani yetu iweze kuendelezwa tuheshimu msingi ya kidemokrasia, ni lazima tuheshimu misingi ya utawala bora hatuwezi kuwa na ubaguzi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali hii tunasema inafuata good governance kwamba utawala bora na utawala wa kisheria na miongoni mwa misingi ya utawala bora ni kuwa na inclusive, watu lazima tushirikishwe, nilichaguliwa na wananchi wa Jimbo la Mtwara Mjini na kwa kuthibisha hilo juzi Mheshimiwa Rais ameondoka, lakini nilivyoitisha mkutano wa hadhara mafuriko yamekuwa ni makubwa kweli kweli kwa sababu wananchi wanamwamini Mbunge wao waliyemchagua. Serikali lazima ishirikiane na Mbunge husika sio kumtenga Mbunge, sio misingi ya kidemokrasia. Kwa hiyo kwa sababu Waziri ananisikia Mheshimiwa Mkuchika alikuwepo ameshuhudia hilo na Waheshimiwa Mawaziri walikuwepo wameshuhudia.
Mheshimiwa Mwenyekiti,jambo lingine la ajabu ambalo nasikitika sana baadhi ya Wabunge wenzetu wanashadidia Wabunge wa Chama cha Mapinduzi wanashadidia kwamba Mbunge wa CUF amenyimwa nafasi halafu. Naomba haya mambo yaweze kurekebishwa ilituweze kuwa na maendeleo sawasawa ya nchi hii. (Makofi)