Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Female
Party
CCM
Constituent
Kigoma Kusini
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
0
Ministries
nil
MHE. HASNA S. K. MWILIMA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nami nianze kwa kumpongeza Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kazi nzuri anazofanya za kutekeleza Ilani yetu ya Chama cha Mapinduzi 2015 – 2020. Pia nimpongeze Waziri wa TAMISEMI, Naibu Mawaziri, Katibu Mkuu pamoja na Naibu Katibu Mkuu. Vilevile nimpongeze ndugu yangu Mheshimiwa Mkuchika, Waziri wa Utumishi na Utawala Bora, pamoja na Naibu wake kwa kazi nzuri wanazozifanya. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti baada ya pongezi, nitoe shukrani kwa Serikali, naishukuru Serikali kwa kutupatia shilingi bilioni 1.5 kwa ajili ya ujenzi wa Hospitali yetu ya Wilaya pale Lugufu. Naishukuru pia Wizara hii ya TAMISEMI kwa kutupatia shilingi milioni 800 kwa maana shilingi milioni 400 kwa ajili ya Kituo cha Afya cha Kalya na shilingi milioni 400 kwa ajili ya Kituo cha Afya cha Uvinza. Mheshimiwa Waziri nakushukuru sana. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, sambasamba hilo, bado nina ombi kwenye sekta hii ya afya. Tuna ahadi alipokuja Waziri Mkuu, tarehe 29 Julai, 2019, alituahidi kwamba TAMISEMI mtatupatia shilingi milioni 800 kwa ajili ya Kituo cha Afya cha Kazuramimba na Kituo cha Afya cha Kabeba. Mheshimiwa Waziri natambua kwamba mahitaji ni makubwa ndani ya nchi lakini unaweza ukatupatia nusu yake, unaweza ukatupa shilingi milioni 400 tukazigawanya shilingi milioni 200 zikaenda Kituo cha Afya cha Kabeba na shilingi milioni 200 nyingine zikaenda Kituo cha Afya cha Kazuramimba. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, niishukuru pia Serikali, nakumbuka nilichangia hapa kuhusiana na maboma, kilio chetu mmekisia kwenye zile shilingi bilioni 253 sisi kama Halmashauri ya Uvinza tumepokea shilingi milioni 375 kwenye shule kumi za sekondari. Tunakushukuru sana Mheshimiwa Waziri na Mheshimiwa Rais kwa sababu makusanyo yanakusanywa na ndiyo maana miradi ya maendeleo inaweza kutekelezeka. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema hayo, niende sasa kwenye ukurasa wa 125(ix) katika kitabu cha Mheshimiwa Waziri. Mheshimiwa Waziri umezungumzia kuhusu ununuzi wa magari kwamba magari kumi yatanunuliwa kwenda kwenye Halmashauri za Nyang’hwale, Buhigwe na nyinginezo. Mheshimiwa Waziri umefanya ziara kwenye Jimbo langu kwenye ile Timu iliyoteuliwa na Mheshimiwa Rais kwenda kuangalia migogoro ya ardhi na mipaka na umeona Jimbo langu ni kubwa sana na ulikuwa shahidi na Mawaziri wenzako, Mheshimiwa Dkt. Hussein Mwinyi, Mheshimiwa Lukuvi mliona ni jinsi gani mama natawala Jimbo ambalo hata ninyi wanaume limewagusa. (Makofi/Vigelegele)
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa nashangaa kuona kwenye ukurasa huu wa 125, Halmashauri yangu ya Uvinza hamjatenga ipatiwe gari. Mkurugenzi na Wakuu wa Idara hawana magari na hizi Halmashauri ulizozizungumza ukurasa wa 125 ni Halmashauri mpya ambazo ndiyo mnatakiwa muwapelekee Wakurugenzi magari.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi ni Mjumbe wa Kamati ya Bajeti kwenye Vote 21 ya Hazina wametenga shilingi bilioni 20 kwa ajili ya ununuzi wa haya magari, magari ya Wakurugenzi, Wakuu wa Mikoa na Wakuu wa Wilaya. Nimelizungumza jambo hili na Waziri wa Fedha, Naibu Waziri na yuko hapa, Katibu Mkuu (Ndugu Doto), Naibu Katibu Mkuu pia na mwanamke mwenzangu Kamishna wa Bajeti ili kwenye hii shilingi bilioni 20 mliyoitenga ya ununuzi wa magari, naomba gari la Halmashauri ya Uvinza kaka yangu Mheshimiwa Jafo tulipate kwenye hizi pesa, usiponiletea mimi nitaona kuna upendeleo. Namtambua kaka yangu Mheshimiwa Dkt. Mpango amezaliwa kule Buhigwe lakini walianzaanza Uvinza ndiyo wakaenda kuhamia Buhigwe basi na mimi Uvinza niletewe gari la Mkurugenzi, kaka yangu Mheshimiwa Jafo naomba hilo ulipokee. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ukienda kwenye ukurasa wa 19 – 24, Mheshimiwa Waziri amezungumzia pia kuhusu majengo ya utawala ya Wakuu wa Wilaya na Wakurugenzi. Nimwombe pia kaka yangu Mheshimiwa Jafo, hivi kuna nini, mbona Uvinza haijazungumzwa na unajua fika kwamba tunayo majengo yanayosimamiwa na TBA lakini kwenye bajeti hii ya 2019/2020 tumeomba shilingi milioni 550 kwa ajili ya ujenzi wa majengo ya Buhigwe, Uvinza na Kasulu lakini kwenye ukurasa huu wa 19 – 24, nasikitika Uvinza haijazungumzwa. Kaka yangu Mheshimiwa Jafo, naomba upokee, najua utanisikia.
Mheshimiwa Mwenyekiti, TARURA, ukurasa wa 83, nimeona kwenye bajeti ya 2018/2019 tuliidhinisha shilingi bilioni 243.29 lakini hadi mwaka huu Februari TARURA wamepokea shilingi bilioni 136.02 sawa na asilimia 56. Kwenye hili naomba nizungumzie kwenye barabara zangu, mtandao wangu wa barabara ni Km.1230. Bajeti tuliyopangiwa mwaka jana ni shilingi milioni 490, bajeti ya ukomo tuliyopangiwa kwenye TARURA mwaka huu ni shilingi milioni 490, mtandao wa barabara ni Km.1230, nimwombe kaka yangu Mheshimiwa Jafo hebu mtuongezee pesa TARURA ili tuweze kuchapa kazi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema hayo, naomba nizungumzie kidogo mapato ya Halmashauri. Nilikuwa naangalia ukurasa wa 139, Halmashauri ya Uvinza ilipangiwa kukusanya shilingi bilioni 1.709 kwa bajeti inayoishia tarehe 30, tumekusanya shilingi milioni 850, tatizo ni nini, naomba nizungumzie kidogo vitambulisho.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hivu vitambulisho vya wajasiriamali naviunga mkono, utaratibu ni mzuri, lakini kwenye utekelezaji kuna shida. Vitambulisho wamepewa Wakuu wa Wilaya ambao siyo Maafisa Masuuli, Maafisa Masuuli ni Wakurugenzi. Hebu sisi tushauri kama Wabunge, kule chini hivi vitambulisho tumeuliza, mimi niko Kamati ya Bajeti, tumemuuliza Waziri, hivi hizi pesa zinazokusanywa zinakwenda wapi? Tukaambiwa zinaingizwa kwenye Mfuko Mkuu wa Serikali.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa haya mapato mnayachukua kwa wale wajasiriamali wadogowadogo ndani ya Halmashauri zetu, kwa nini hizi pesa zisiingie kwenye mapato ya ndani ya Halmashauri zetu? Kwa nini hizi pesa ziende kwenye Mfuko Mkuu wa Serikali wakati mkitambua fika kwamba hiki ni chanzo cha mapato cha Halmashauri. Tunaomba Mheshimiwa Waziri mkae chini na Wizara ya Fedha mlizungumzie hili. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nimalizie kidogo kwenye suala la watumishi wetu. Watumishi wengi hawajapandishwa madaraja kwa sababu wamekaimu miaka tisa, wanatakiwa wawe Wakuu wa Idara, wanashindwa kupandishwa vyeo kwa sababu wanaambiwa sio Maafisa Waandamizi. Hebu mliangalie hili, muwaruhusu wapandishwe vyeo yaani wathibitishwe kwenye nafasi za Ukuu wa Idara huku bado hawajawa Maafisa Waandamizi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sambasamba na hili, naomba nizungumzie suala la watumishi ambao walikuwa Kigoma Vijijini wakahamia Uvinza hawajalipwa pesa zao mpaka leo. Niliona kwenye Fungu la Hazina kuna kama shilingi bilioni 350 kwa ajili ya kulipa madeni ya watumishi mbalimbali. Naomba na watumishi wangu wa Uvinza waweze kufikiriwa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mwisho kabisa nimpongeze sana Mheshimiwa Rais kwa kazi nzuri anayoifanya ndani ya nchi yetu. Leo mdogo Mheshimiwa Heche alizungumza kwamba kwenye Jimbo lake afya, elimu hali ni mbaya, lakini mimi kwa taarifa nilizonazo Serikali hii inayoongozwa na Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli imepeleka shilingi milioni 400 kwenye Kituo cha Afya cha Mkende kwenye Jimbo la Mheshimiwa Heche, imepeleka shilingi milioni 400 kwenye Kituo cha Sirari, imepeleka pesa za ujenzi wa jengo la Halmashauri kwenye Jimbo la mdogo wangu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini pia nikamsikia kaka yangu Japhary anazungumzia kwamba, unajua ninyi mnaweza mkaenda huku na sisi tukaenda huku, hivi mnazungumzia utawala bora, utawala bora kweli mnaufahamu ndugu zangu Wapinzani? Tumeona juzi Maalim Seif amehama CUF ameenda ACT, anaangalia tumbo lake haangalii chama. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, tumeona humu ndani tulikuwa na CUF A na CUF B, leo nimemsikia Bwege anasema wote ni CUF moja. Sasa najiuliza huo ni utawala bora upi? Mlikuwa CUF A na B, kwa nini msiende ACT? Kwa hiyo, nini kinachoonekana hapa ni kwamba mmebaki CUF hii hii ya Lipumba kwa ajili ya matumbo yenu. Sasa mnapokuwa mnaisema Serikali ya Chama cha Mapinduzi muwe mnajiangalia na ninyi. (Makofi)
MHE. KHATIB SAID HAJI: Mheshimiwa Mwenyekiti, taarifa.
MHE. HASNA S.K. MWILIMA: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwenye suala la utawala bora...
(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)
MWENYEKITI: Ahsante sana Mheshimiwa Hasna, muda wako umemalizika. (Makofi)
MHE. HASNA S. K. MWILIMA: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kuunga mkono hoja. (Makofi)