Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Female
Party
CCM
Constituent
Special Seats
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
1
Ministries
nil
MHE. ESTER L. MIDIMU: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana kwa kunipa nafasi ili niweze kuchangia. Kwanza kabisa, nampongeza Mheshimiwa Rais kwa kazi nzuri anazozifanya, Mwenyezi Mungu ambariki sana. Pili, nampongeze Makamu wa Rais kwa kazi nzuri anazozifanya, Mwenyezi Mungu ambariki. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nampogeza Waziri Mkuu kwa kazi nzuri anazozifanya, Mwenyezi Mungu ambariki sana. Nampongeze Mheshimiwa Waziri wa TAMISEMI pamoja na Manaibu Waziri na Makatibu Wakuu kwa hotuba nzuri waliyoisoma, inaridhisha, imesheheni mambo mazuri. Pia nampongeza Mheshimiwa Mkuchika, Waziri wa Utawala Bora. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba sasa nianze kuchangia. Naipongeza Serikali yangu ya Chama cha Mapinduzi kwa kutujengea Hospitali ya Rufaa Mkoa wa Simiyu, ambayo imezinduliwa na Mheshimiwa Rais juzi, inafanya kazi vizuri. Hata hivyo, kuna changamoto katika hospitali ya mkoa. Changamoto ya kwanza, hatuna genereta ya dharura umeme ukikatika; hospitali hiyo haina uzio na ina upungufu wa vifaa tiba. Naiomba Serikali iliangalie hilo. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, naipongeza Serikali yangu ya Chama cha Mapinduzi kwa kazi nzuri inazozifanya, imetuletea shilingi bilioni 4.5 kwa ajili ya ujenzi wa Hospitali za Wilaya; Wilaya ya Itilima, Busega na Bariadi DC mchanganuo wake, kila Wilaya inapata shilingi bilioni 1.5. Hospitali hizo zikikamilika, nina imani matatizo yatapungua hususan katika wilaya hizo nilizozitaja; huduma itakuwa karibu; na vifo vya akina mama na watoto havitatokea tena. Vikitokea ni bahati mbaya, siyo kwamba vinatokea kwa kukosa matibabu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, naiomba Serikali yangu katika hospitali yetu teule ya Mkoa wa Simiyu haina Madaktari Bingwa wa magonjwa ya akina mama; na hospitali hiyo ina msongamano sana. Inahudumia wilaya tatu; Busega, Bariadi na Itilima. Msongamano unakuwa mkubwa sana, akina mama wakienda pale, inachukua siku mbili au tatu kupata matibabu. Tunaiomba Serikali itusaidie kutuletea daktari wa magonjwa ya akina mama kwa vile akina mama tuna maradhi mengi. Kuna maradhi mengine yanahitaji kumwona Daktari Bingwa wa Magonjwa ya Akina Mama. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, naendelea kuipongeza Serikali yangu ya Chama cha Mapinduzi kwa kuboresha Hospitali ya Wilaya ya Maswa. Imetujengea genereta nzuri, imetujengea x-ray nzuri, inafanya vizuri. Vilevile imetujengea wodi ya akina mama na watoto, tunapongeza sana. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, naenda sasa Wizara ya Maji. Naipongeza sana Serikali yangu ya Chama cha Mapinduzi kwa kutuletea mradi wa maji wa Ziwa Victoria. Mradi huo ukifika utatusaidia wananchi wa Mkoa wa Simiyu hususan akina mama kwa sababu muda mwingi wanaupoteza kutafuta maji kuliko kufanya kazi za maendeleo. Nina imani mradi huo ukifika, tutafanya kazi za maendeleo, tutalima mboga mboga, tuta-supply Dodoma na Dar es Salaam mpaka nje ya nchi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na pongezi hizo kuna changamoto Wilaya ya Maswa kata ya Zanzuni. Kuna mradi wa chujio ambao umechukua muda mrefu sana. Kila kandarasi akiongezewa muda mradi huo umeshindwa kukamilika. Nashindwa kuelewa tatizo ni nini, huku wananchi wa Maswa wakiendelea kunywa maji ambayo siyo safi na salama. Fedha zipo ila mradi haukamiliki. Naiomba Serikali iangalie hilo kwa mapana yake. Kila siku nikisimama hapa hilo nalipigia kelele. Naomba sasa Serikali yangu kwa vile ni sikivu, iweze kunisikia.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba pia niipongeze Serikli kwa mradi mkubwa wa maji wa Busega ambao upo kata ya Ramaji. Niliuliza swali juzi juzi hapa Bunge lililoisha. Mheshimiwa Naibu Waziri alinipa majibu mazuri sana, akasema, mradi huo utaanza kufanya kazi mwezi wa Nane. Nami nimeenda kufanya ziara, nimewaambia akina mama, mradi huo utaanza kufanya kazi mwezi wa Nane. Kwa hiyo, wananchi wa Busega wanasubiria hiyo neema ya maji. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, niendelee kumpongeza Mheshimiwa Rais Dkt. Magufuli kwa kazi nzuri anazozifanya, Mwenyezi Mungu ambariki sana, tunamwombea, atabaki kuwa juu, atabaki kuwa mawinguni. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, naunga mkono hoja (Makofi)