Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017- Wizara ya Viwanda, Biashara na Uwekezaji

Hon. Emmanuel Adamson Mwakasaka

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Tabora Mjini

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017- Wizara ya Viwanda, Biashara na Uwekezaji

MHE. EMMANUEL A. MWAKASAKA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Mimi naomba kwanza nianze kwa kuipongeza Serikali yetu ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania chini ya Mheshimiwa Dkt. John Pombe Joseph Magufuli pamoja na timu yake yote ya watendaji wakiwemo Mawaziri wote kwa kazi nzuri ambayo wameendelea kuifanya.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nianze kwa kuunga mkono hoja ili nisije nikasahau ya Waziri wa Viwanda, Biashara na Uwekezaji, Mheshimiwa Charles Mwijage na nampongeza kwa hotuba yake na uwasilishaji wake mzuri wa Makadirio ya Mapato na Matumizi kwa mwaka wa fedha wa 2016/2017. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kuanza na utangulizi huo, nianze kuchangia kuhusiana na wafanyabiashara wadogo. Wafanyabiashara wadogo kama ambavyo Mheshimiwa Mwijage, Waziri wa Viwanda, Biashara na Uwekezaji alivyooanisha kwenye kitabu chake kwamba nchi kama Korea Kusini, Singapore na Malaysia wakati sisi tunapata uhuru nchi hizi tulikuwa tunalingana kiuchumi, sasa leo wenzetu wako mbali mno, sijui sisi tatizo letu ni wapi. Moja ya tatizo ninaloliona ni urasimu kwa wafanyabiashara hawa wadogo ambao tumekuwa tukiimba kwamba kwetu wako karibu asilimia 99 na hata nchi zingine ambao kwa kiasi kikubwa ndiyo wanachangia pato kubwa la Taifa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nikisema mfanyabiashara mdogo mdogo, tunaanzia na wale wanaopata leseni za kawaida, mtu ana mtaji wake wa shilingi laki mbili, tatu mpaka milioni moja. Kwa urasimu ambao tunao kwenye biashara, kwa mfano, mfanyabiashara anakata leseni ya kawaida shilingi elfu themanini, anataka kuja kuomba tender ya Serikali, kuna viainishi vingine anatakiwa kuwa navyo. Kwa mfano, awe na cheti kutoka Mamlaka ya Chakula na Dawa (TFDA) wakati anataka kuomba tender hapo hajapata, hii nayo ina gharama yake. Kwenye Sheria ya Manunuzi (PPRA) kuna GPSA, ukitaka kujisajili GPSA kununua kitabu chao tu kile cha kuomba kujisajili siyo kupata biashara ni shilingi laki moja. Mimi nina mashaka makubwa mfanyabiashara wa mtaji wa shilingi laki mbili mpaka tano au milioni moja ataweza kufanikisha milolongo hii yote. Pia huwa kunakuwa na mwingiliano wa kazi kati ya PPRA na TFDA (Mamlaka ya Chakula na Dawa). Unaweza ukakuta hawa PPRA nao wanakagua chakula, sijui kwa mamlaka yapi, mimi nashindwa kuelewa kwa sababu TFDA na hawa PPRA wanachanganyana. Kwa hiyo, ile Sheria ya Manunuzi kama walivyosema wenzangu nadhani sasa imepitwa na wakati. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini pia nichangie suala la gharama ambayo wafanyabiashara wanakutana nayo hasa pale bandarini. Kuna ushuru wa uzembe unaofanyika zile damage charges, ule uzembe unaofanyika pale haumhusu mteja. Vitu vinavyoendelea pale kwa mfano wengine waliongelea mambo ya magari lakini kuna mizigo pia, mteja unafuatilia toka siku ya kwanza unajua meli imeingia na ina gari lako, sijui wengine lakini mimi nimetoa magari mara nyingi pale, haijawahi kutokea zile siku wanazokupa kama free ukaweza kutoa gari. Wao wana kisingizio, wakati wewe unataka kwenda kulipia wanakuambia system iko down.
Mheshimiwa Mwenyekiti, wapo wasafirishaji kwa mfano wa mabasi na reli, tunaona kabisa kwamba kama gari kwa mfano limekwama njiani wataleta basi lingine kwa gharama zao kwa sababu siyo kosa la msafiri. Vivyo hivyo hata kwenye reli tumeona reli ya kati hapa ikitokea matatizo wanakodisha magari kwa gharama zao.
Sasa hawa TRA mitandao yao inapokuwa iko down kwa nini gharama zile aingie mteja? Mimi nadhani gharama zile zilikuwa zinapaswa kubaki TRA. Hili ni jipu kwa sababu kama kweli kila siku mitandao iko down, mtu anataka kwenda kulipia pesa wanasema kuna tatizo la mitandao sasa hivi huwezi kulipia, ni mapato ya Serikali yanachelewa kukusanywa. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nichangie kwenye suala la Sera hii ya Viwanda. Kama alivyoainisha Mheshimiwa Rais wakati wa kampeni kwamba nchi yetu itakuwa ya viwanda kwa asilimia zisizopungua 40, hapa nirudi kwenye Mkoa wangu wa Tabora, mimi ni Mbunge wa Tabora Mjini, nimeshasema mara nyingi mwamba ngoma anavutia kwake.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Tabora ni mkoa wa kihistoria hata kura zile za uhuru tatu zilifanyika Tabora. Tabora inalima tumbaku kwa wingi kuliko sehemu yoyote Tanzania hii. Tabora ilikuwa na kiwanda cha nyuzi lakini Kiwanda hiki cha Nyuzi, siku moja Mheshimiwa Mwijage wakati anajibu swali moja hapa alisema kwamba wame-respond vizuri wale watu kwamba wanasema nyuzi hazina soko. Siyo kweli Mheshimiwa Mwijage, naomba siku ukipata nafasi katembelee Tabora pale na mimi nikiwepo, kimefungwa na mitambo iliyopo mle ndani inasadikiwa imeuzwa kama chuma chakavu kama walivyosema wengine na huwa hawakufungulii unapokwenda pale. Kwa hiyo, Mheshimiwa Mwijage hii sababu wanayotoa si kweli, kile kiwanda aliyebinafsishiwa siyo. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini si hivyo tu kuna asali Tabora. Naomba Mheshimiwa Mwijage hata kama viwanda itashindikana kama niko sahihi hapa Tanzania hatuna maabara ya kupima ubora wa asali kwa maana ya maabara. Naomba basi hata tutakapojenga maabara tujenge Tabora ili wale wanafunzi ambapo vyuo viko vingi pale waweze kupata hiyo ajira ambayo tunasema sasa tutakuwa watu wa viwanda na biashara. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini pia naomba nimalize kwa hizi taasisi ambazo ni za utafiti kama TIRDO, TEMDO na CARMATEC. Naomba wanapofanya utafiti waikumbuke na Tabora. Kwa mfano, wanapotengeneza matofali ya saruji ambayo yamechanganyika na udongo, wanatoa matofali ambayo unajenga nyumba za kisasa, mafunzo yale yakifanyika Tabora yatawawezesha pia vijana kupata ujasiriamali kwa kutumia taasisi hizi za utafiti.
Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema haya machache, narudia kuunga mkono hoja na ahsante kwa kunipa nafasi.