Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) na Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020

Hon. Stanslaus Shing'oma Mabula

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Nyamagana

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) na Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020

MHE. STANSLAUS S. MABULA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nami nakushukuru kwa kupata nafasi ya kuweza kuchangia walau maneno machache ya kazi kubwa inayofanywa na Serikali ya Awamu ya Tano chini ya Chama cha Mapinduzi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nianze kutoa shukurani zangu za ujumla kwa Mheshimiwa Jafo pamoja na watendaji wenzake wote kwenye Wizara kwa namna ambavyo wamekuwa wakifanya kazi kubwa sana katika kuhudumia Wizara hii nyeti kabisa kwenye nchi hii. Mimi nilitegemea sana kwa sababu TAMISEMI ndiyo kiini au injini ya maendeleo kwenye nchi hii hata Wabunge wenzetu wote wangeendelea kuona umuhimu wa kukupa moyo na kuendelea kukushawishi na kuendelea kukueleza maeneo ambayo wanadhani yanatakiwa kufanyiwa kazi badala ya kuendelea kulalamika. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nianze kuzungumzia sekta ya afya. Nafahamu Serikali ya Awamu ya Tano imefanya kazi kubwa sana. Mimi natoka Jimbo la Nyamagana. Naposema Nyamagana unafahamu ndiyo kitovu cha Mkoa wa Mwanza. Tunashukuru sana kwa mgao wa vituo vingi vya afya na Nyamagana tunacho kituo kimoja cha afya chenye sifa ambacho umetupa sasa hivi kimeshakamilika. Nikushukuru tena kwa kutuongezea kituo cha pili kule Fumagira. Imani yangu ni kwamba kituo hiki kikikamilika tutakuwa tumeendelea kupunguza sana tatizo la vifo vya mama na watoto ambao kiukweli wanahitaji huduma za karibu sana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na jitihada hizi Halmashauri peke yake, nimpongeze sana Mkurugenzi wangu pamoja na watendaji wote, Madiwani na Meya kwa kuhakikisha tunajenga zahanati sita mpya kwa fedha za mapato ya ndani. Hii ni hatua kubwa sana na tunaposema Hapa Kazi Tu, hii ndiyo tafsiri yake sahihi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tatizo moja kubwa ambalo Mheshimiwa Waziri inabidi sasa hivi ukimbie nalo, baada ya ujenzi wa hivi vituo vya afya vyote na hospitali za wilaya, jambo kubwa tulilonalo sasa ni upatikanaji wa vifaa. Tunafahamu vinatoka kwa awamu, sasa hivi vimeanza kwa awamu ya kwanza lakini umekwenda karibia phase nne ya ujenzi wa vituo vya afya. Kwa hiyo, ni jambo zuri sana tukifanya haya mambo kwa haraka ili wananchi waone matokeo tunayoyasema kwa vitendo kama ambavyo umeshaanza kupeleka vifaa kwenye vituo vingi vya afya. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, la pili kwa sababu ya muda nizungumze juu ya TARURA. Mheshimiwa Waziri katika jambo ambalo naendelea kukupongeza sana kila siku ni uamuzi wako wa kutoa mawazo na Baraza likaazimia na Mheshimiwa Rais akaidhinisha kuwa na chombo kinachoitwa TARURA. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nataka kusema mimi ni muumini mkubwa wa TARURA kwa sababu nimeona matokeo yake lakini najua namna ambavyo TARURA inaweza kuja kuwa mkombozi wa miundombinu ya barabara kwenye nchi hii hasa kwenye maeneo ya vijijini na mjini. Juzi nimesikia wakati unazungumzia hapa ripoti ya CAG, TARURA wamepata hati safi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimpongeze sana Mkurugenzi/CEO wa TARURA Ndugu yangu Seif pamoja na Mhasibu Mkuu Ndugu yangu Nyaulinga kwa namna ambavyo wamekuwa wakishirikiana vizuri na watendaji wao wote hata kupata hati safi. Endelea kuwawekea mkazo, zaidi ni kuhakikisha fedha zinapatikana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Nyamagana napata shilingi bilioni 3.5 lakini fedha hizi ukilinganisha ukubwa wa mji na sifa ya mji na miundombinu iliyopo hatujawahi kupata fedha kwa ajili ya ujenzi wa barabara za lami. Hatuwezi kuendelea kujenga au kuboresha barabara za vumbi. Kwa hiyo, niwaombe sana Watendaji wa TARURA waangalie kwenye kitengo cha barabara za lami kwenye Jiji la Mwanza tutakapoongeza barabara za lami walau kutoka Igoma - Buhongwa, kutoka Mkuyuni kwenda Mandu kupitia Mahina, kutoka Buhongwa kwenda Nyakagwe na kule Bulale tutakuwa tumefungua mji huu na sifa yake itaonekana. Mimi sishangai sana kwa sababu haya mazuri tusipoyasema leo tutayasema lini? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nizungumzie suala la Madiwani, nimekuwa Diwani na nakubaliana na suala la posho zile za mwisho wa mwezi, Serikali inaendelea kulifanyia kazi. Hata hivyo, Mheshimiwa Waziri umetoka Waraka unaosisitiza sitting allowance, Mheshimiwa Diwani anayetoka kilometa 18 anakuja kulipwa Sh.10,000 ya nauli, hii siyo sawa. Maelekezo kwenye Waraka yako wazi kwamba Diwani apewe malipo haya kulingana na uwezo wa Halmashauri inavyokusanya mapato. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, hivi leo kwenye Halmashauri kama ya Jiji la Mwanza na Mkurugenzi wangu hawezi kutumia nguvu kwa sababu Waraka umemuelekeza kutumia Sh.40,000 na Sh.10,000. Mheshimiwa Waziri, fungua sasa kwamba Halmashauri itoe posho ya kikao kwa siku kulingana na uwezo wake wa mapato ya ndani. Ukifanya hivi, mwanzo walikuwa wanalipwa Sh.100,000 na mimi nilikuwepo pale tunalipwa Sh.100,000 ukija kwenye kikao, nauli na kadhalika angalau unaweza kuhudumiwa hata wapiga kura wako. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nizungumze kidogo, najua bado nina dakika tano baada ya kengele hii, yako maneno mengi yanaenea kwenye hii nyumba. Mimi niwasihi Waheshimiwa Madiwani yako maneno yanasema ashindwaye haishi maneno lakini sote tunafahamu hapa tunapokuja kujadili bajeti na bajeti tunayokwenda kuijadili tunafanya makisio. Hivi leo ukikisia kupata Sh.10,000 ukaishia kupata Sh.8, unamlaumu nani? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunaishia kulaumu bajeti tunayoipata, hatuoni mambo ambayo Serikali imefanya. Kila mtu akisimama wanabeza Stiegler’s Gorge na ndege lakini wanasahau Serikali ya Awamu ya Tano kutoka wanafunzi wa vyuo vikuu 30,000 mpaka 42,000, zaidi ya shilingi bilioni 420 zimetoka hapa. Hili siyo jambo jema la kushukuru ndugu Waheshimiwa wa upande wa kule? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, niulize, tunasema hivi kutoka miundombinu kwenye zaidi ya shule 500, zaidi ya shilingi bilioni 100 zilizofanyiwa ukarabati na kujengwa hili siyo bora kuliko yale mengine tunayoyasema? Tumezungumza hapa tunasema, hivi leo unapozungumzia ujenzi wa vituo vya afya zaisdi ya 300, hospitali za wilaya zaidi ya 67, unabeza hata hili? Hatuoni haya? Tunajadili mipango ya kufikirika…

MHE. FRANK G. MWAKAJOKA: Mheshimiwa Mwenyekiti, taarifa.

MHE. STANSLAUS S. MABULA: Mheshimiwa Mwenyekiti, Mwakajoka kaa nitakushukia jumla jumla.

MHE. FRANK G. MWAKAJOKA: Mheshimiwa Mwenyekiti, taarifa.

MHE. STANSLAUS S. MABULA: Mheshimiwa Mwenyekiti, tunapojadili habari ya bajeti, bajeti ni matarajio. Kama tulipanga kufikisha shilingi bilioni 1 tukaishia shilingi bilioni 2.

MHE. FRANK G. MWAKAJOKA: Mheshimiwa Mwenyekiti, taarifa.

MHE. STANSLAUS S. MABULA: Mheshimiwa Mwenyekiti, mwaka 1992 vyama vya upinzani viliundwa, malengo yao ni kuchukua dola. Kama ingekuwa ukifikiri unatenda, leo wangekuwa wamechukua dola wale.

MHE. FRANK G. MWAKAJOKA: Mheshimiwa Mwenyekiti, taarifa.

MHE. STANSLAUS S. MABULA: Mheshimiwa Mwenyekiti, Tanzania siyo kijiji. Tanzania ni duara, ni nchi kubwa na wanakosea sana kuilinganisha Tanzania na vijiji. Wanakosea sana kuilinganisha Tanzania na mtaa. Hii ni nchi, ina wilaya, mikoa na ardhi kubwa na watu zaidi ya milioni 50, inataka mipango na mipango hii inayofanywa na Serikali ya Awamu ya Tano, tunaamini kuja mpaka mtukamate hapa tulipo ni kazi ya ziada sana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana lakini waendelee kujifunza. Kwa mfano, kwa kumalizia, tumesema hivi toka nchi hii umeundwa kwa mara ya kwanza maamuzi ya ujenzi wa Bwawa la Stiegler’s Gorge tunataka wananchi watoke kwenye kulipa senti 11 ya umeme tunayolipa leo waje walipe senti 5 au 6. Mtu mwingine anasema hapana, huyu mwananchi unayetaka aendelee …

MHE. FRANK G. MWAKAJOKA: Mheshimiwa Mwenyekiti, taarifa.

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)