Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) na Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020

Hon. Omari Mohamed Kigua

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Kilindi

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) na Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020

MHE. OMARI M. KIGUA: Mheshimiwa Mwenyekiti, awali ya yote nimshukuru Mwenyezi Mngu kwa kuweza kusimama leo tena leo jioni hii katika Bunge lako Tukufu niweze kuchangia kwenye hotuba mbili za Waheshimiwa Mawaziri waliopo. Nichukue fursa hii kwanza kuwapongeza Mawaziri wote wawili, nimpongeze Waziriwa Nchi, Ofisi ya Rais, TAMISEMI, kaka yangu Jafo, lakini nimpongezee Mheshimiwa Mzee Mkuchika na Manaibu Waziri wote kwa kazi ambayo mnaifanya. (Makofi/)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimesimama hapa kwanza nianze eneo la TARURA, watu wamezungumza sana kuhusu TARURA. Natambua umuhimu waTARURA na katika Bunge hilihili ndipo tulipopitisha TARURA, lakini wapo ambao wanasimama hapa kusema kwamba TARURA sasa irudi tena kwa Madiwani. Naomba niseme kwamba TARURA ibaki kama ilivyo; pamoja na changamoto nyingi sana kuhusu TARURA, lakini ni ukweli usiopingika kwamba TARURA ikirudi kwa Waheshimiwa Madiwani kutakuwa kuna vurugu nyingi sana. Ushauri wangu ni nini kuhusu TARURA, ni kwamba wanakosa usimamizi wa kutosha, Meneja wa TARURA anasimamia barabara za halmashauri.(Makofi/)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ni nani anasimamia ubora wa kazi ya TARURA, hatuna chombo ambacho kinasimamia kazi za TARURA, namshauri Mheshimiwa Waziri na timu yake waangalie namna ambavyo TARURA wanaweza kusimamiwa. Nalisema hili kuna changamoto nyingi sana pamoja na upungufu wa bajeti, mathalani nizungumzie katika Jimbo langu la Kilindi, ambalo lina idadi ya barabara 139, kilometa 844, pesa ambayo tumetengewa ni shilingi bilioni moja na milioni mia moja sitini na tisa. Kiasi hiki hakitoshi, hebu fikiria barabara 139 unaweza kuzigawa vipi kwa kiasi hiki cha pesa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa wazungumzaji wa mwanzo wamezungumzia kwamba tuongeze bajeti nami niungane nao kwamba tuchukue ile asilimia kumi kwenye TANROADS tuiongeze kwenye asilimia 30 iwe asilimia 40. Hii itasaidia kupunguza changamoto za TARURA. Nalisema hili kwa sababu Wabunge wanasimama hapa wanalalamika na niseme ukweli tu, kiasi hiki ambacho kimetengwa kwa ajili ya Jimbo la Kilindi hakitoshi. Tunamlaumu sana Meneja wa TARURA; lakini ukiangalia uhalisia wa pesa zilizotengwa ni ndogo sana. Hali halisi ya Jimbo langu la Kilindi ni mabonde na milima.

Mheshimiwa Mwenyekiti, wenye kusema wamesema kwamba,ni heri uone mara moja kuliko kusikia mara 20. Mheshimiwa Naibu Waziri dada yangu Dkt. Mary Mwanjelwa amefika pale Kilindi, hata Mheshimiwa Waziri wa TAMISEMIamefika ameiona Kilindi ilivyo, nyakati za mvua, magari hayapiti kule, mvua ni nyingi, lakini na barabara pia hazipitiki. Sasa tuone dhamira hii ya Serikali ya kuanzisha TARURA, basi iendane sambamba na maeneo husika, huwezi ukampa mtu mwenye barabara 139 na barabara zenye urefu wa kilometa 844 na mtu mwenye kilometa chache unakuwa hutendi haki.(Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti,niiombe Serikali sana kwenye eneo hili watazame, wanao wataalam, wasikae maofisini, tunasimama hapa Waheshimiwa Wabunge kuyazungumza haya,wawe wanawatuma Maafisa wao waje kutembelea na kuona hali halisi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, eneo ambalo pengine nataka kulizungumzia pia ni eneo la huduma ya afya. Nimpongeze Waziri wa TAMISEMIna timu yakewamefanya kazi kubwa sana. Nitoe mfano mmoja tu kwenye Jimbo langu la Kilindi, Mheshimiwa Waziri ameweza kutoa pesa ya vituo vitatu vya afya; hili ni jambo kubwa sana sana. Eneo la Kilindi ni eneo pana, tuna vijiji 102, kata 21 bado vituo vya afya hivi ambavyo tumepata havitoshelezi; lakini wanasema asiyeshukuru kwa kidogo hata kikubwa hawezi kushukuru. Namshukuru sana Mheshimiwa Waziri katika hilo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, vile vile nizungumzie suala la utawala bora, mzee wangu Mheshimiwa Mzee Mkuchika, nimpongeze sana baaada ya kuchaguliwa katika eneo hilo. Kulikuwa kuna kelele sana sana juu ya ugomvi wa Wenyeviti, Wabunge na Wakuu wa Wilaya, Wakurugenzi, lakini naona hali imetulia. Sasa naomba nijielekeze kwa mtazamo wangu mimi nini maana ya utawala bora, Serikali hii imejikita kuwaletea maendeleo wananchi, imeamua kujenga vituo vya afya 352, huo ni utawala bora. Unapoamua kujenga mradi kama wa Stiegler’s Gorge maana yake huo ni utawala bora, SGR ni utawala bora kwa sababu ungeweza kuchukua pesa hizo ukapeleka maeneo mengine, lakini Mheshimiwa Rais kwa sababu ana dhamira nzuri ya kuwapenda Watanzania ameamua kuwekeza kwenye miradi na hii lazima tukubaliane nao tu huu ni utawala bora, ni lazima tumsifie na tumpongeze Mheshimiwa Rais katika hili. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kila mmoja ana mtazamo wake katika hili; lakini naamini kabisa dhamira ya Serikali hii ya kuwekeza katika miradi mikubwa, dhamira ya Serikali hii ya kupeleka umeme vijijini ni utawala bora, kwa hiyo ni lazima tuipongeze Serikali katika hili na naamini ipo siku Watanzania watakumbuka dhamira ya Mheshimiwa kwamba atakuwa ni Rais anayesimamia utawala bora na sisi kama Wabunge wa Chama cha Mapinduzi tuko pamoja na yeye.(Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine ambalo ningependa kulizungumzia kwenye utawala bora ni suala la eneo la utawala. Mzee wetu Mkuchika ameshawahi kuwa Mkuu wa Mkoa wa Tanga, Mkoa wa Tanga ni mkoa pekee ambao una halmashauri 11, Mkoa wa Tanga una shule za msingi 1028, lakini ipo baadhi ya mikoa ina halmashauri chache sana. Nimemsikia Mheshimiwa Rais juzi akisema kwamba hawezi kuongeza maeneo ya utawala, lakini sasa lazima tutazame,kama hatuongezi eneo la utawala, tufanye nini ili kwenda sambamba na maeneo makubwa kama haya? Lazima tuhakikishe kwamba resources zile ambazo ni chache tupeleke kwenye maeneo haya ambayo ni makubwa sana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hebu leo tuchukulie mfano, Afisa Elimu wa Mkoa wa Tanga ambaye shule za msingi tu ni 1,022, lakini baadhi ya Mkoa wana shule za msingi 177, unawezaje kufanya tathmini kwa watu hawa wawili, hapo hakuna usawa hata kidogo. Nashauri tuangalie namna ambavyo maeneo ambayo ni mapana kwa utawala tuhakikishe kwamba resourceszinakuwa za kutosha.(Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, eneo lingine ambalo ningependa kusema nikuhusu watumishi kukaimu. Hili kwa kweli halijakaa vizuri sana. Mimi kama Mjumbe wa Kamati ya PAC mara nyingi tumekutana na Wakurugenzi, wanakaimu mwaka mzima, miezi sita, hivi unawezaje kufanya upekuzi kwa miezi sita, nchi hii hii, Tanzania hii hii. Namwomba Mheshimiwa Waziri, najua watu hawa wako chini ya Ofisi yake Mheshimiwa Mzee Mkuchika, hebu tuangalie kamahawana weledi katika hili, tuangalie namna ya kuwapa mafunzo ili suala la kukaimu lisichukue muda mrefu sana. Kuna umuhimu wa mtu kukaimu kwa muda mfupi, unapomkaimisha mtu kwa muda mrefu, kwanza unampotezea confidence, uwezo wa kufanya kazi unakuwa haupo kwa sababu hana uhakika na nafasi aliyopo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti,nishauri katika dhana ya utawala bora ni pamoja na mtu kutokaimu muda mrefu. Hii nadhani nilikwishazungumza awali kwamba zamani tulikuwa na utaratibu wa succession plan, yaani leo Mkurugenzi anastaafu tayari tunajua nani atachukua nafasi yake. Sasa haiwezekani unastaafu leo, miezi sita ijayo ndiyo unaanza kumtafuta mbadala wake. Ningependa kusema kwamba hebu tuliangalie hili kwa sura nyingine. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema maneno hayo, naomba kusema kwamba naunga mkono hoja zote za Waheshimiwa Mawaziri wawili. Ahsante sana.(Makofi)