Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Mbulu Vijijini
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
2
Ministries
nil
MHE. FLATEI G. MASSAY: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza nishukuru sana kwa kupata nafasi ya kuongea jioni hii ya leo. Kwanza naomba nianze na kumpongeza kabisa Mheshimiwa Rais na Serikali yake kwa jinsi ambavyo anachapa kazi na kuwaletea maendeleo wananchi wa Tanzania. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, pia nitakuwa mchoyo wa fadhila kama sijampongeza na kuwapongeza hasa Mawaziri ambao kimsingi leo tunajadili hotuba zao. Mheshimiwa Waziri Jafo nampongeza sana kwa kufanya kazi kubwa ndani ya Ofisi ya Rais, TAMISEMI, lakini pia nampongeza sasa baba yangu Mheshimiwa Mkuchika, ambaye alishakuwa Mkuu wa Wilaya ya Mbulu kwa miaka kadhaa, hongera sana mzee wangu, chapa kazi, akazie uzi hapohapo; lakini nawapongeza pia, Naibu Mawaziri katika Wizara zote mbili, ili kuokoa muda, pia na Makatibu Wakuu kwenye Wizara zote hizi mbili. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, natoa shukrani pia, kwa kututengea fedha za kujenga Kituo cha Afya cha Dongobesh, Mheshimiwa Waziri nampa hongera sana. Wakati naingia jimboni nilikuwa sina kituo kabisa cha afya, lakini leo tunajenga kituo cha afya ametupatia milioni 700, Mungu awabariki sana, lakini pia wametupatia bilioni moja na milioni 500 tukajenga Hospitali ya Wilaya pale Dongobesh. Mheshimiwa Waziri namshukuru sana na nashukuru sana kwa ajili ya wananchi wa Jimbo la Mbulu Vijijini.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pia, nashukuru juzi wametupatia fedha za maboma. Tumepata milioni 230 kwa kujenga maboma kwenye shule za sekondari tisa. Biblia inasema ni bora kushukuru nami naishukuru sana Serikali yangu kwa kweli, kwa kutujalia na kutupatia fedha nyingi kiasi hiki, hizi ni pongezi kwa Serikali.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Biblia inasema kwa Waefeso 5:4, naomba niwakumbushe wachangiaji wenzangu. Waefeso 5:4 anasema: “Wala aibu wala maneno ya upuuzi si vema na hata ubishi hayampendezi Mungu, ni afadhali kushukuru.” (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nimetazama bajeti hii. Nimetazama na kusoma Wizara zote mbili, kuna mahali pa kupongeza Serikali na kumshukuru sana Mheshimiwa Rais kwa jinsi anavyofanya kazi usiku na mchana. Kwa nini? Ukiangalia leo hospitali za wilaya zimejengwa na maeneo mengi tunapata huduma. Vituo vya afya viko vingi na sasahivi naona 57 vinakwenda kujengwa. Tusiposhukuru tutakuwa na hali ya kutorudisha fadhila na shukrani. Mimi nashukuru sana Serikali na niko kifua mbele nimetumwa humu kuwashukuru kwa ajili ya hili.
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini pili ninao ushauri, ukiangalia TARURA bajeti yake kwa miaka miwili iliyopita imeanza kupungua. Mwaka 2017/2018 imepungua kwa asilimia nane, lakini mwaka jana kwa asilimia 16 na mwaka huu imezidi kupungua. Nimwombe Mheshimiwa Waziri, tumeanzisha TARURA ili ikasaidie kujenga barabara za vijijini na mijini, lakini ukiangalia kwa jinsi ambavyo bajeti ya TARURA inapungua, tutashindwa kujenga barabara ambazo amesema mwenyewe hapa kuna kilometa 108,000; kwa kweli kwa pesa hii itakuwa shida sana kuisaidia TARURA. Hivyo, naungana na Wabunge wenzangu waliosema kwamba, TARURA iongezewe fedha. Hii asilimia ya kugawana, mgawanyo wa kwake TARURA na TANROADS kwa kweli uangaliwe.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kuwa TARURA inakwenda mbali na mzunguko wake ni mkubwa na vijijini, niombe basi tuone namna ya kufanya, tuiongezee fedha na fedha hizi tupange asilimia. Sasa hivi inaonekana ni asilimia 30, ni ndogo sana, tuongeze basi asilimia hizi angalau ziende 40 au 50. Nashukuru TARURA kwa mwaka huu wamenisaidia, wamejenga madaraja mawili na nimeona kwenye bajeti hapa kuna Daraja la Qambasiro na calvat ya Gidimadoy.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pia niombe, kuna barabara mbili ambazo kwa kweli, hazipitiki sasa hivi. Barabara ya Masieda kwenda Mongo wa Mono kufika mpaka Yaeda Chini, wako Wahdzabe kule sijawahi kuwafikia, barabara haipitiki kabisa. Niombe Ndugu yangu aangalie kwenye bajeti hii tupate barabara ile, lakini kuna barabara nyingine kutoka Masieda kupitia Laghangesh kwenda Yaeda Chini, naomba barabara ile aiangalie vizuri, iwekewe fedha ili walau hata sisi tuwe na namna ya kutembea. Nami napigania na ku-support uongezaji wa asilimia za barabara katika TARURA ili basi barabara hizi ziweze kujengwa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, lingine nimeangalia, ndugu zangu wapinzani au upande wa Gaza wanasema, kwa nini nimesoma mstari wa Biblia, nimetaka hata washukuru. Nimeangalia kuna mzungumzaji mmoja hapa kabla yangu ame-quote maneno ya mtu anayeitwa mwanazuoni na amesema yeye mwenyewe uzalendo kwanza na nini maana ya uzalendo ku-support nchi yako.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa nimeangalia kwenye mpango wa bajeti ya mwaka huu, ukiangalia Rombo kwa Mheshimiwa Selasini pale, kapewa hospitali. Sasa sijaona kwa nini watu hawa hawashukuru mara nyingi? Nami nawaza humu kwa nini shukrani zisitokee?
Mheshimiwa Mwenyekiti, vile vile ukienda Kilombero kumepewa milioni 500, lakini ukienda Arusha AICC pale kumepewa milioni 500, ukienda Ubungo wana fedha pale, ukienda Kigoma wanayo. Sasa huwa nawaza humu ndani, jamani hata shukrani kidogo tu hakuna? Nadhani wakati fulani yako mambo ambayo hayaendi vizuri tuseme, lakini mambo ambayo yanaenda vizuri tushukuru, hata kwa jambo moja tu. Ndio maana mara nyingi ni lazima kushukuru, tusiposhukuru ndugu zangu hata Mheshimiwa Waziri na wanaofanya kazi chini yao wataona kama vile hakuna kinachoendelea.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kubwa pamoja na shukurani hizi naomba nielezee ahadi za Mheshimiwa Rais. Mheshimiwa Rais wakati anapita aliahidi kilometa tano pale Hydom na kilometa mbili Dongobesh na Mheshimiwa Waziri nina hakika amefika Dongobesh na Hydom, ili Rais wetu asionekane kwamba, ameahidi na hajatekeleza, niombe basi katika bajeti ya mwaka huu atenge hata kilometa tatu au mbili, ili walau tuonekane tunaanza kujenga barabara zile.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kiukweli barabara zetu hazina lami, nami nashukuru Mungu walau naona mpango wa Serikali wa kuweka lami katika wakati ujao, lakini naomba basi kipindi hiki cha mwaka huu wa 2019 kwenda 2020 kwa kweli, tuione lami ya Hydom ikiwekwa kwenye bajeti hii. Mheshimiwa Waziri nimempelekea maombi na naomba maombi haya ayachukue, aniwekee lami kilometa zile zilizoahidiwa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kubwa zaidi naomba kuna shule ya sekondari ambayo wananchi wanaijenga kule Maretadu, wanajenga kidato cha tano na cha sita kwa fedha zao. Tumejenga madarasa manne na tumejenga bwalo, sasa naomba tu fedha za kumalizia ili mambo yaende vizuri. Kwa nini nashukuru? Principle ya kushukuru ni hivi unaposhukuru maana yake unaomba mara ya pili. Niombe ndugu yangu fedha atuwekee pale.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ushauri wangu pia katika ugawaji wa vijiji na kata. Inawezekana kweli kukawa hakuna bajeti ya namna hii, lakini waangalie kuna vijiji ambavyo vimeshakuwa vikubwa na vingine vitongoji vina shule ya msingi na wanahitaji kuona kwamba, wanapata uongozi wao. Katika hili wafikirie, nina kata mbili za Maretadu kule na Haidereri wameanza kujenga shule zao za vitongoji na wako vizuri na wanaendelea kufanya kazi hii ya kui-support Serikali.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru sana na naunga hoja mkono. (Makofi)