Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) na Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020

Hon. Ester Alexander Mahawe

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) na Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020

MHE. ESTER A. MAHAWE: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana. Nami nimshukuru Mungu kwa kupata nafasi ya kuchangia hoja zilizopo mbele yetu za Wizara zote mbili.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nichukue nafasi hii pale alipoishia kaka yangu Papian na mimi nichukue nafasi hii kumpongeza Rais Dkt. John Pombe Magufuli, Rais wa Awamu ya Tano ambaye ndiye aliyependwa na Watanzania kuinadi Ilani ya Uchaguzi ya mwaka 2015 - 2020. Huwezi kusimama katika Bunge hili ukashindwa kusema habari za Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli, vinginevyo wewe hautakuwa mzalendo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, mambo mengi yamefanyika katika nchi hii. Kabla sijaenda mbali, nielekeze pia pongezi hizo kwa Waziri wa TAMISEMI, kaka yangu Mheshimiwa Jafo na Naibu wako, nielekeze pongezi hizi kwa ndugu yetu Mheshimiwa Mkuchika na Naibu Waziri Mheshimiwa Dkt. Mwanjelwa, Mungu awabariki sana kwa utendaji wenu uliotukuka. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nianze na nukuu hii inasema: “A good leader is not measured by how long he/she stayed in a particular position, it is measured by how many positive changes you brought over there.” Tangu Rais Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli mambo makubwa yamefanyika katika nchi hii na ni kazi yetu sisi Wabunge wa Chama cha Mapinduzi kuzitafsiri kazi hizo kwa wananchi wetu kupitia Bunge lako tukufu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ukienda kwenye suala zima la afya, niipongeze Wizara ya Afya pamoja na hii Wizara ya TAMISEMI kwa upande wa miundombinu. Tangu mwaka 1961 mpaka leo tulikuwa na vituo vya afya visivyozidi 695 lakini ndani ya miaka mitatu kutokana na utendaji uliotukuka wa Serikali ya Awamu ya Tano tumejengewa vituo vya afya zaidi ya 300. Unaanzaje kubeza juhudi kama hizi? Msema kweli ni mpenzi wa Mungu, wanasema mnyonge mnyongeni, haki yake mpeni. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Rais na Wizara ya TAMISEMI, hongereni sana, kazi yenu ni nzuri sana, mnaokoa vifo vya akina mama na huduma za afya zinapatikana. Ni kweli changamoto ndogo ndogo bado zipo, wanasema hata Roma haikujengwa siku moja, hatuwezi kumaliza changamoto kwa siku moja. Hii nchi ni kubwa, wananchi wake ni wengi na mambo yanayotakiwa kufanyika ni mengi lakini lazima tu-recognize juhudi zilizofanywa na Serikali ya Awamu ya Tano tangu 2015 to date. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nizungumzie na suala la elimu. Ni kweli kwamba kuna changamoto lakini lazima tuseme yale mazuri makubwa yaliyofanyika. Changamoto ya ukosefu wa miundombinu ni kwa sababu ya elimu bure ambayo imetolewa katika kipindi hiki cha Awamu ya Tano. Usajili umekuwa ni mkubwa sana katika shule zetu ambao umepelekea kupungua kwa matundu ya vyoo, madarasa na kadhalika lakini bado kazi kubwa imefanywa na maboma mengi yamejengwa. Sisi tu Mkoa wa Manyara tumeletewa fedha za EPforR zaidi ya shilingi bilioni saba kwa ajili ya kumalizia maboma katika Mkoa wa Manyara, naishukuru sana Serikali hii ya CCM. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, yamejengwa matundu mengi ya vyoo lakini bado kuna changamoto. Niendelee kuiomba Wizara ya TAMISEMI waweze kuzingatia hitaji hili kwa sababu kwa asilimia kubwa lina-affect watoto wa kike wanapokuwa kwenye mizunguko yao ile ya mwezi wanashindwa kuhudhuria shule kwa sababu ya mazingira mazuri ya maeneo hayo ya kujisitiri.

Mheshimiwa Mwenyekiti, masula mazima ya upungufu wa walimu wa sayansi ni kilio kikubwa. Tumejenga maabara za kutosha na tunatengeneza nchi ya viwanda, ni lazima tuwekeze kwenye elimu na walimu wa sayansi. Upungufu wa walimu wa sayansi ni mkubwa, upungufu huu ni janga la kitaifa. Tuwa-motivate watoto wetu kuanzia kwenye level za primary school kupenda sayansi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli walimu wa sayansi huwa ni wakali na wakati mwingine watoto wasipoelewa ukali unapozidi basi unakuta wanatoa adhabu mbalimbali na watoto hao wanajikuta wamechukia masomo hayo ya sayansi na hisabati. Niwaombe walimu wenzangu twende taratibu, tunahitaji kuwajenga wanasayansi ili nchi yetu iweze kupata wataalam.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nizungumzie kwa uchache suala zima…

T A A R I F A

MHE. SALOME W. MAKAMBA: Mheshimiwa Mwenyekiti, taarifa.

MWENYEKITI: Taarifa, Mheshimiwa Ester subiri.

MHE. SALOME W. MAKAMBA: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba uwasihi Wabunge wamsikilize kwa makini Mbunge ajaye wa Jimbo wa Babati Mjini. Ahsante. (Kicheko/Makofi)

MWENYEKITI: Mheshimiwa Ester Mahawe, naomba uendelee.

MHE. ESTER A. MAHAWE: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa ruhusa hii ya kuendelea.

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika suala la elimu, mimi natokea Mkoa wa Manyara ambako wenyeji wetu wengi ni wafugaji na shule zetu nyingi za sekondari hazina mabweni na hosteli za kutosha. Nishukuru tumepata hosteli kadhaa, siyo chini ya 10 katika Mkoa wetu wa Manyara lakini hazitoshi hasa Wilaya ya Kiteto na Simanjiro, wale watoto wanatembea umbali mrefu mno. Kama unavyofahamu sisi wafugaji watoto wa kike wanaolewa haraka sana, naomba ili ku-rescue watoto hawa, shule hizi ziweze kupata hostels ili watoto wale waweze kumaliza masomo yao. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba niende kwenye suala la afya. Nishukuru sana kwa ajili ya mambo mengi yanayoendelea kufanywa na Serikali hii lakini nina ombi la dhati kabisa kwa ajili ya magari ya wagonjwa katika maeneo mbalimbali katika Mkoa wa Manyara. Hospitali ya Mbulu haina gari la wagonjwa, lililopo ni chakavu na Kituo cha Afya cha Ngusero hakina gari la wagonjwa, tunaomba sana kusaidiwa. Niliwahi kuomba gari la wagonjwa kwa ajili ya Kituo cha Afya Orkesmet mbele ya Makamu wa Rais, nina hakika ombi hili linaendelea kufanyiwa kazi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika Mkoa wa Manyara, jiografia za Kiteto na Simanjiro zimekaa vibaya kuliko mahali pengine popote nchi hii. Akina mama wakati mwingine wanapata tabu wanapopelekwa hospitali kujifungua. Naomba tena gari kwa ajili ya Orkesmet na Kituo cha Afya cha Ngusero, Kiteto. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile naomba gari kwa ajili ya Hospitali ya Mrara, Babati Mjini, gari ni moja na ni chakavu. Kama hiyo haitoshi, Hospitali ya Wilaya ya Babati Mjini ilianza kama zahanati miaka ya 1956, imeongezwa jengo moja moja baadaye ikawa kituo cha afya, leo imekuwa Hospitali ya Wilaya, majengo yapo scattered hayana mpangilio, wodi ya wazazi ipo mita 100 kutoka theatre. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, wewe unafahamu ukiingia kwenye kile chumba ama miguu itangulie kaburini au wewe mwenyewe mzima mzima. Sasa imagine theatre ipo 100 metres kutoka kwenye labor ward. Hili jambo nakuomba sana Mheshimiwa Jafo ulitazame kwa macho ya huruma. Naomba sana suala la Hospitali ya Mrara litazwamwe vizuri. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tuna upungufu wa watumishi wa kada ya afya katika Mkoa mzima. Tunajua juzi TAMISEMI wamejitahidi sana, wameachilia ajira lakini bado tuna upungufu kadhaa. Kada ya afya ni muhimu sana, ndiyo inayo-save maisha ya wananchi wetu. Ikitokea tu bajeti kidogo ya kuweza kuruhusu kuongeza watumishi wa kada ya afya tunaomba Manyara tukumbukwe kwa namna ya tofauti.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kabla sijamaliza nilikuwa naomba nizungumzie suala la lishe. Ni kweli kwamba tuna tatizo la lishe…

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

MWENYEKITI: Mheshimiwa Ester malizia, muda wako umeisha.

MHE. ESTER A. MAHAWE: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Naomba niseme tu udumavu ulipo Mkoa wa Manyara ni asilimia 36 na hili linachagizwa na ukosefu mkubwa wa maji; akina mama wengi wanatoka asubuhi wanarudi usiku hawana hata muda wa kuwaandalia watoto wao chakula kizuri hata kama kipo. Naiomba sana Serikali yangu, Ofisi hii ya TAMISEMI itusaidie kutazama namna ambavyo tutamalizana na changamoto ya miundombinu ya maji ili hatimaye tuweze kupata vijana wazuri watakaolilea taifa hili. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kuunga mkono hoja, Mungu akubariki sana. (Makofi)