Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) na Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020

Hon. Maryam Salum Msabaha

Sex

Female

Party

CHADEMA

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) na Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020

MHE. MARYAM SALUM MSABAHA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana. Awali ya yote namshukuru Mwenyezi Mungu kwa uzima na kwa pumzi hii. Pia naishukuru Ofisi ya Spika na Katibu wa Bunge na wafanyakazi kwa kuhakikisha napata matibabu na kurudi katika hali yangu ya kawaida; na Wabunge wenzangu wote walioniombea. Sasa hivi nimeimarika na nimesimama katika Bunge lako hili Tukufu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, awali ya yote, napongeza hotuba hizi mbili zote zilizowasilishwa na Mawaziri Kivuli kwa upande wa pili. Naiomba Serikali yale yote mazuri wayachukue wayafanyie kazi. Kuna mambo mazuri sana yamezungumzwa humu ndani na yataleta tija na changamoto kwa nchi yetu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nitajielekeza kwenye haki za binadamu. Haki za binadamu kwa kweli zinakiukwa. Tuangalie msongamano ulivyojaa kwenye magereza. Nenda Keko, Segerea, Tanzania nzima; zunguka mpaka Korogwe uende mpaka Arusha, kuna mahabusu wengi sana ambao wako magerezani. Kesi zinachukua muda mrefu. Kibaya zaidi, wengine wanaumwa, wengine wamepata majeraha, wengine wamepigwa labda wamevunjwa vunjwa miguu, miguu inaoza mpaka wengine wanafika hata karibia kukatwa miguu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tuangalie hii kweli ni haki au ni utawala bora? Tuangalie sasa hizi kesi ni kwa nini zinachukua muda mrefu? Kwanza wale wanachanganywa; kuna watoto mle ndani, kuna wendawazimu na kila mchanganyiko ndani ya mahabusu. Sasa kuna haki au kuna utawala bora katika haki za binadamu? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tuangalie sasa zile kesi ambazo ni ndogo ndogo au ni kwa nini zinachukua muda mrefu? Zifanyiwe maamuzi ili wapate kutoka mle ndani na mzigo utoke kwa Serikali. Kwa sababu mnavyolundika watu kule, kwanza wale wanataka kula, miundombinu siyo rafiki, wamejazana, wengine wanaumwa TB, wengine wanaumwa maradhi ya UKIMWI, wengine wanaumwa maradhi nyemelezi. Kwa hiyo, sasa tunatafuta matatizo na tunaipa Serikali mzigo mzito sana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tuhakikishe Mahakama nayo inafanya kazi kwa kufuata sheria na haki. Pia tuhakikishe vyombo vya ulinzi na usalama vinavyowakamata raia wasiokuwa na hatia wasiwapige wakawaumiza wakawavunja vunja miguu, kwa sababu huwezi kumvunja vunja raia, ukawa ulishamuumiza halafu tena unamweka mahabusu huku hajapata huduma za huduma za afya. Kwa hiyo, pale kutakuwa hakuna utawala bora. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tumeona kwenye utawala huu kuna watu wengi sana, sijui tunaambiwa wahujumu uchumi, tunaambiwa TAKUKURU wamewachukua, lakini vielelezo viko wapi? Vile vielelezo vinatakiwa vifuatiliwe sasa, kama kweli wamefanya makosa wasikae muda mrefu bila kuhukumiwa. Unakuta mtu anakaa hata miaka sita hata miaka kumi yupo tu mahabusu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, lingine, tuangalie sheria ambazo tunazipitisha humu ndani. Hizi sheria, kwa mfano, Sheria za Vyama vya Siasa. Vyama vya Siasa, Waasisi wa Taifa hili walivyoleta vyama vingi hawakuwa wagonjwa. Hawakukurupuka! Hivi vyama vimeletwa kwa mujibu wa sheria. Chama ni mtu kuwa na uhuru wako binafsi, unaamua mimi niende chama gani? Chama siyo ugomvi, siyo kuhasimiana. Tumeletewa vyama ili tupate siasa bora, tupate maendeleo, tuosoane pale mnapokosea. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa unakuta sasa hivi tumeleta sheria ya kukandamiza vyama vya siasa. Ninyi mnacheka, lakini msichekelee. Mwalimu Nyerere hakuwa mjinga, wala Mwasisi wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar naye hakuwa mjinga. Ni kwa nini alileta vyama vingi? Wengi ambao walikuja kutengeneza hivi vyama vingi pia walitoka upande wa pili wakaja huku tukatengeneza vyama. Sasa mbona mnakandamiza hivi vyama? Kwa nini mnaogopa kivuli chenu wenyewe mlichokitengeneza? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, vyama vipewe uhuru, vitangaze sera zao. Upinzani siyo ugomvi, sio chuki, kwa hiyo, Wapinzani wapewe fursa kama Chama Tawala kinavyopewa fursa ya kufanya mikutano, kujieleza, kutoa sera zao, hata pale panapokuwa na uchaguzi, kuwe na uchaguzi wa haki bila kudhulumiana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, leo mnachekelea, mnaona hii mipasuko ya vyama vya siasa, lakini tunajenga matabaka yasiyokuwa na sababu. Tunajenga matabaka kwa baadaye ambayo tutapelekea nchi yetu kutokusikilizana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, msome history, kwa mfano, vyama vya siasa kwa upande wa Zanzibar. Tuseme ile CUF ya Zanzibar na Chama cha Mapinduzi, mmetoka mbali. Kulikuwa na migogoro mpaka mkaunda Serikali ya Umoja wa Kitaifa. Serikali ile iliundwa ili msikilizane, mfanye kazi kwa pamoja turudi kwa pamoja na tupate muungano safi ili anayetoka Tanzania Bara anakwenda kule anakuwa yuko huru, anayetoka visiwani anakuja huku anakuwa yuko huru. Kujenga ni kazi, lakini kubomoa tunabomoa kwa siku moja.. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tuangalie, hawa washauri wa Mheshimiwa Rais, mshaurini na mpeleke taarifa za ukweli, msipeleke taarifa za uongo za kujipendekeza. Mumpe mustakabali wa siasa inavyokwenda, hasa siasa ya Zanzibar. Mumpe ukweli siasa ya Zanzibar iko vipi? Msione Wazanzibari wamenyamaza, wananyamaza lakini siasa ya Zanzibar ina wenyewe. Siasa ya Zanzibar siyo kama siasa ya Tanzania Bara. Ni kwa nini mnajenga chuki zisizokuwa na sababu? Ni kwa nini wengine mnafanya kazi kwa utashi wenu, kwa kujipendekeza ili kumgombanisha Mheshimiwa Rais na wananchi? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nyie kama ni wateuliwa wa Mheshimiwa Rais, mfanye kazi kwa mujibu wa sheria, pale penye haki mfanye haki. Leo unakuta hata wengine mnabambikia watu kesi za kisiasa, mnawaweka ndani ili kutaka kupandishwa vyeo. Hiyo haitakiwi, mnamharibia Mheshimiwa Rais. Kwa hiyo, mnatakiwa kila mtu anayepewa nafasi yake, aisimamie na kila mtu anayeteuliwa aisimamie ile nafasi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika mipaka yetu tuangalie sasa tumeingiza migogoro ya kisiasa isiyokuwa na maana. Mipaka yetu, usalama wa raia uko vipi? Kwa sababu tunajenga chuki, tunajenga makundi yasiyokuwa na sababu. Tuangalie haya makundi tunayoyajenga tutanufaika na nini? Tuangalie hizi chuki za kuchukua wapinzani tukawasweka ndani tutafaidika na nini? Tuangalie wawekezaji kwa nini wanakimbia? Tuangalie kwa nini watu hawataki tena kuja Tanzania? Sekta ya Utalii, kwa nini watalii wanapungua? Hii yote ni kwa kuwa tunajenga siasa ni ya chuki. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa mfano, Zanzibar ni kisiwa. Kuna visiwa viwili; Kisiwa cha Pemba na Kisiwa cha Unguja, vimezungukwa na bahari. Hii mipaka mmeilinda vipi? Hizi chuki mnazozipalilia, mnajilinda vipi? Kwa hiyo, naomba mrudi mezani, make, msifanye siasa za ubabe. Fanyeni siasa za mustakabali wa nchi hii, tuangalie Muungano unakuwa vipi? Tuangalie vyama vya siasa vinapata uhuru wa kutosha wa kujieleza na wagombea wanakwenda kwenye kugombea bila bughudha. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna Wabunge wengine wanakuja hapa hata hawasaidii wananchi wao wale waliowapigia kura. Mtu anaweza kukaa hapa Bungeni miaka mitano hajawahi kuuliza swali, hajawahi kufika Jimboni, hajawahi kufanya kitu chochote. Kwa hiyo, mwananchi ana uhuru wa kumchagua mtu anayemtaka. Kwa hiyo, sasa Serikali ijitafakari. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, turudi kwa watumishi. Mlikuwa na zoezi lile la kuondoa watumishi hewa. Watumishi hewa waliondolewa, lakini kuna taasisi ambazo sasa hivi zinafanya vizuri. Hata Taasisi ya Bunge, Watumishi wa Bunge wanafanya kazi vizuri tu, mishahara iko wapi? Wapeni stahiki zao za mishahara. Mkienda Muhimbili, pia huko Madaktari sasa hivi wanafanya kazi vizuri. Wapeni mishahara. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, mmesema mmeboresha shule kongwe. Zile shule kongwe mlizoziboresha, bado kuna changamoto ya Walimu wa Sayansi. Kwa hiyo, sasa tuhakikishe shule zile nazo zinapata Walimu wa Sayansi na wale Walimu wapandishwe madaraja. Hata wale walimu wengine wanaostahili kupandishwa madaraja wapandishwe, wale wanaostahili kupandishiwa mishahara wapandishiwe. Kuongezwa vyeo… (Makofi)

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)