Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) na Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020

Hon. Munde Abdallah Tambwe

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

2

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) na Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020

MHE. MUNDE T. ABDALLAH: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa fursa hii nami niweze kuchangia. Nilikuwa na mambo mengi ya kuchangia kuhusu Tabora, lakini nimeona muda wangu kidogo nichukue kumjibu kaka yangu Mheshimiwa Mnyika.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Mnyika amesema Mheshimiwa Rais kwa sababu ana nafasi ya kufanya uzinduzi wa miradi, angechukua nafasi ile akafanya Sala ya Kitaifa kuiombea nchi hii. Mimi nadhani Mheshimiwa Rais anafanya kazi kubwa na ndiyo maana kuna miradi mingi ya kuzindua. Hiyo ni kazi, tena kubwa ya kuwaonesha Watanzania ni nini Serikali yao inafanya? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nchi hii ina dini; ina Wakristo, Waislam na dini tofauti tofauti. Kila siku tunasali kumwomba Mwenyezi Mungu. Hapa leo ni Ijumaa, nikitoka hapa naende Msikitini kusali, kumwomba Mwenyezi Mungu kwa ajili yangu na familia na nchi yangu. Nadhani watu wote wanafanya hivyo.

Mheshimiwa Rais ameweza kuita viongozi wa dini mara kadhaa, anaongea nao kutaka maoni yao na kuwaomba waendelee kuiombea nchi yao. Mimi nadhani Mheshimiwa Mnyika labda ana stress. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Mnyika ameongea kuhusu Katiba mpya. Ni hao walijiunga UKAWA mara ya kwanza kwa ajili ya kwenda kuipinga Katiba iliyopendekezwa. Namshangaa leo anaidai Katiba hiyo ambayo wao kwa mara ya kwanza waliungana kwenda kupinga nchi nzima watu wasiiunge mkono Katiba iliyopendekezwa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa leo namshangaa ndiyo niseme ndimi mbili, ndiyo niseme mna stress kwamba hamtapata Ubunge tena, yaani nachanganyikiwa kwa kweli. Mliikataa Katiba, leo mnaitaka Katiba. Yote hiyo ni kui- frustrate Serikali ishindwe kufanya kazi yake, tukae na Katiba tushindwe kuendeleza miradi iliyopo ili pesa yetu tuimalizie kwenye Katiba mje mseme kwamba Mheshimiwa Rais aliahidi maendeleo, ameshindwa kufanya maendeleo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nirudie kusema tena Mheshimiwa Rais fanya kazi yako kama inavyostahili, achana na mambo ya Katiba, hukuwaahidi Watanzania Katiba, uliwaahidi maendeleo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, niongee tena kidogo kwamba wamekuwa wanasema sana kwamba Wakurugenzi, Ma-DC, ni wana CCM ni nani anaweza kufanya kazi na mtu ambaye hamwamini. Hata leo nikifungua duka, nitamweka ndugu yangu, nitamweka mtu ninayemwamini aliye karibu name. Ni nani anaweza kuwa Rais kati yao wao akachukua Mbunge wa CCM Munde akampa Ukuu wa Mkoa? Hatuwezi kufanya hivyo. Mheshimiwa Rais angalia watu unaowaamini, uliowachuja, wakakuridhisha kufanya kazi na wewe kama vile wao ambavyo wanabebana, wanasaidiana wao kwa wao kwenye nafasi zao chungu nzima ikiwepo Ubunge. (Makofi/Kicheko)

MBUNGE FULANI: Wape dozi. (Kicheko)

MHE. MUNDE T. ABDALLAH: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba niendelee na Bajeti Wizara. Naipongeza Wizara ya TAMISEMI kwa kazi nzuri wanayoifanya. TAMISEMI wamefanya kitu kizuri sana, wameboresha ukusanyaji wa mapato. Leo hii ukiwa popote, viongozi wa TAMISEMI wanaweza kuangalia Halmashauri gani imekusanya shilingi ngapi, imetumia shilingi ngapi na imefanya nini? Hii ni hatua kubwa sana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nawapongeza sana kaka yangu Mheshimiwa Jafo na Manaibu Waziri pamoja na Menejimenti nzima ya TAMISEMI. Vile vile naipongeza Wizara ya Utawala Bora, mzee wetu Mheshimiwa Mkuchika, mpenzi wetu Naibu Waziri, Mheshimiwa Dkt. Mary Mwanjelwa tunakupongeza sana, mnafanya kazi kubwa mno tunawaona. Tunawaombea kwa Mwenyezi Mungu mwendelee kufanya kazi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, hii system waliyoiweka ni nzuri sana. Kwa kweli mimi nimefanya kazi Halmashauri, naomba ni-declare. Hakuna tena mtu atakayeweza kuiba revenue ya Halmashauri. Watu wataiba kwenye matumizi hewa, kwenye ten percent, kuagiza vitu ambavyo siyo vya kweli. Kwenye revenue kwa kweli mmedhibiti na mtaacha legacy, hii kazi mmeifanya ni kubwa sana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, niongee kuhusu vitambulisho. Wenzetu hawa wamekuwa wanaongea sana kuhusu vitambulisho vya 20,000 wakiviponda na kuvibeza. Kama nilivyosema, nimefanya kazi Halmashauri. Zamani akina Mama Lishe, Wamachinga walikuwa wanatozwa shilingi 500 kwa siku. Anapewa risiti ya shilingi 500/=, kesho anapewa risiti ya shilingi 500, analipia shilingi 500.

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya wiki mbili anaenda kufurumuliwa, masufuria ya wali yanamwagwa, maharagwe yanamwagwa, mboga zao zinatupwa. Leo Mheshimiwa Rais amewatambua kwenye Sekta Rasmi ya Wamachinga kwa kuwapa vitambulisho wa shilingi 20,000. Nilidhani tutafurahi, tutaridhika wamama hawa, Wamachinga, vijana wetu hawatanyang’anywa tena vitu vyao, watafanya kazi wakiwa na confidence zao na wameambiwa wasiguswe wafanye kazi popote. Mnaka nini? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, zamani shilingi 500/= ukiizidisha mara siku 365 za mwaka walikuwa wanalipa shilingi 182,000/=. Leo shilingi 20,000/= ukiigawa kwa siku 365, wanalipa shilingi 55/= kwa siku. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi nimetoka Tabora. Sisi ni maarufu sana wa kupika vitumbua. Mama anayepika vitumbua; kitumbua kimoja shilingi 500/=, akiuza vitumbua 40 ana shilingi 20,000/=. Mwaka mmoja una wiki 52. Kila wiki mama huyu aweke hela ya kitumbua kimoja tu 500, ndani ya wiki 40 amefikisha 20,000/=. Hivi mnataka nini jamani? Au mmezoea kupinga tu? Mlipinga reli, mmepinga Stiegler’s, mnapinga ndege. Tumewazoea! (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, niwaambie Serikali, nimwambie Mheshimiwa Jafo, vitambulisho hivi viendelee, ni kitu kizuri sana, kinawatambua Wamachinga wetu, Mama Lishe wetu, hawafukuzwi tena, hawamwagiwi vitu vyao, lakini 20,000 ni reasonable price. Wale watu ilikuwa vikishachukuliwa vile vitu vikamwagwa na Mgambo wao wanawachukua wanawatumia kwenye maandamano. Safari hii mmewakosa. Safari hii mtoto wake ambaye yuko India, yuko Marekani, amlete aandamane. Wamachinga tena hamwapati. (Kicheko/Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nichangie haraka haraka. Niseme tu, ni lazima kila Mtanzania achangie pato la Taifa. Tuache kujidanganya. Hamna nchi yoyote duniani watu hawalipi kodi; hamna nchi yoyote duniani watu wanafanya kazi bila kulipa ushuru; tusidanganyane. Hawa watu wenye sekta ambazo siyo rasmi, ndogo ndogo ndio walio wengi. Kwani wanapita barabara zipi? Hospitali wanatibiwa ipi? Kwa nini wasichangie pato la Taifa? Kwa hiyo, tusitake kuivuga Serikali na kuitoa kwenye msimamo wake thabiti. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nichangie kuhusu Jimbo la Ulyankulu. Jimbo hili lina wakimbizi wengi sana. Wakimbizi hao wamekubaliwa kupiga kura ya Mbunge na kura ya Mheshimiwa Rais. Wakimbizi hawa wamekataliwa kuchagua Diwani kwenye maeneo yao, hawachagui viongozi wa Serikali za Mitaa, jambo linalotushangaza kabisa. Kwa sababu huu ni uadui mkubwa. Huwezi kukaa na mtoto wa ndugu yako ukambagua, hiki fanya, hiki usifanye. Kama walikuwa hawatakiwi, wasingepewa uraia.

Mheshimiwa Mwenyekiti, watu hawa wameshakuwa raia sasa, Watanzania, kwa nini mnawazuia wasichague Madiwani? Kwa nini mnawazuia wasifanye uchaguzi wa Serikali za Mitaa? Ukiangalia ni double standard. Kwa sababu kwa yangu Mheshimiwa Kakoso kule kuna wakimbizi, lakini wanachagua Madiwani, wanachagua Serikali za Mitaa, wanachagua Wabunge, wanachagua Rais. Sasa huku ninyi mmetuwekea wachague Wabunge na Rais tu. Sasa kama anamchagua Rais, anamchagua Mbunge, kwa nini unamkatilia asichague Diwani na umeshampa urai? Huyu ni raia. Kwa hiyo, naomba mwatendee haki, wapate nafasi, wapate fursa nao wachague na wajichague. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, imeenda mbali zaidi, hawapati chochote cha Kiserikali wakati tumeshawapa urai. Juzi nilikuwa kule Kaliua, wamana hawo wanakataliwa kupata mikopo ya Halmashauri na wakati vikundi vyao na wakati tumeshawapa uraia: Je hii ni sahihi jamani?

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, tunatengeza bomu ndani ya nchi yetu. Hawa tumekuwa kama tumewapa uraia, lakini tunawabagua. Basi kama ni hivyo, tuwanyime uraia, tuwanyang’anye. Kwa sababu tumeshawapa, naomba pia wakubaliwe kufanya kila kama wanavyofanya wengine. Kule kwa Mheshimiwa Kakoso, kwa kaka yangu Mbogo kuna wakimbizi, lakini wanafanya kila tu. Kwa nini isiwepo na Ulyankulu hivyo hivyo?

Mheshimiwa Mwenyekiti, je, ni lini Kambi za wakimbizi zitafungwa? (Makofi)

(Hapa kengele ya pili ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)