Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) na Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020

Hon. Prof. Jumanne Abdallah Maghembe

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Mwanga

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) na Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020

MHE. PROF. JUMANNE A. MAGHEMBE: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana kwa kunipa nafasi nami nichangie katika Wizara hizi mbili ambazo zote kiongozi wake ni Rais Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli. Napenda nipongeze sana kwa kazi nzuri ambazo zinafanywa katika Wizara zote hizi mbili. Pia ningependa niwashukuru sana Waheshimiwa Suleiman Jafo, Mheshimiwa George Mkuchika na Waheshimiwa Manaibu Waziri wote kwa kazi nzuri ambayo wameifanya katika kuendeleza Wizara hizi. Unaweza kuseka chochote lakini Wizara hizi zinafanya kazi nzuri sana na ni vizuri tuzipongeze, tuzipe moyo ili waendelee kuwaletewa Watanzania maendeleo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kuwa muda wenyewe wa kuongea ni mchache nitapenda sana nizingatie maendeleo kule kwenye Jimbo langu. Nikianza na sekta ya afya; napenda sana niipongeze tena Wizara hii ya TAMISEMI kwa kuvipangia ujenzi vituo hivi 95 katika bajeti hii ambayo tunaijadili sasa. Hata hivyo, Mheshimiwa Suleiman Jafo atakumbuka kwamba nilimletea rasmi kabisa matatizo niliyonayo katika Wilaya ya Mwanga katika hospitali yetu ya Wilaya ambayo awali ilikuwa ni kituo cha afya na kupandishwa kuwa hospitali ya Wilaya, Mwanga ilipokuwa Wilaya, kwamba tangu mwaka 1979 hadi leo hakuna kitu kingine kilichofanywa juu ya kituo cha afya kubadilishwa kuwa hospitali ya Wilaya. Hivi sasa majengo yamechakaa, theatre zimechakaa, vitendeakazi vimechakaa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, namshukuru Mheshimiwa Jafo kwa kutuma timu ambayo ilikwenda ikafanya tathmini ya hospitali ile na kuona matatizo yaliyopo, lakini katika orodha hi ya hospitali 95 siioni hospitali ya Wilaya ya Mwanga. Namwomba sana Mheshimiwa Waziri tafadhali ikiwezekana twende sisi wawili tukaangalie pamoja ili uone shida kubwa ambayo ipo. Hivi sasa theatre karibu inafungwa kwa sababu hakuna vitendeakazi, hakuna vifaa tiba, mortuary jengo limeanguka na majengo kwa ajili ya kuwapa uhifadhi wafanyakazi, nyumba za wafanyakazi hakuna.

Mheshimiwa Mwenyekiti, namwomba sana Mheshimiwa Waziri atusaidie kama anavyosaidia kwenye Wilaya zingine ili hospitali hii iweze kutumika vizuri. Aidha, naendelea kushukuru na kupongeza sana katika hatua kubwa zilizofanywa za kujenga na kuboresha vituo vya afya na sisi katika Wilaya ya Mwanga awali tumepata shilingi bilioni 1.4 kwa ajili ya Kituo cha Afya cha Kisangara na Kituo cha Afya cha Kigonigoni. Tunaendelea kushukuru na fedha ambazo zimepangwa katika bajeti hapa kwa ajili ya kukamilisha Kituo cha Afya cha Kifaru. Hata hivyo, bado wananchi wa Mwanga wamejenga vituo vingine viwili ambavyo ni karibu kumalizia kama hicho cha Kifaru, Kituo cha Afya cha Mwaniko na cha Kileo ambapo tunawaomba sana fedha zikipatikana basi tuwasaidie wananchi kukamilisha. Wameshajenga, wamebakiza vitu vidogo sana ambavyo wangetupatia shilingi milioni 400 hivi, basi maneno yote yangekuwa tayari.

Mheshimiwa Mwenyekiti, aidha katika sekta hi ya afya, wananchi wa vijiji sita katika Wilaya ya Mwanga wanaendelea kujenga zahanati na karibu zinakamilika. Zahanati hizi za Kituri, Mrigeni, Lembeni, Nyabinda, Lang’atabora na Vanywa ziko karibu kabisa kukamilika, wananchi wamejenga mpaka wamepaua lakini wamechoka. Tunawaomba sana katika huu utaratibu wa kumalizia maboma, ya kwao siyo maboma wameshapaua, basi watusaidie kukamilisha zahanati hizi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la pili kubwa ambalo nataka niliongelee ni suala la elimu. Katika Wilaya ya Mwanga na hasa katika elimu ya msingi nimesema hapa mara nyingi shule zetu hazina Walimu kabisa. Kati ya shule 117, shule 50 zina Walimu wawili, wawili peke yake na shule zingine 40 zina Walimu watatu, watatu, sasa utapiga hesabu mwenyewe uone ni ngapi ambazo zina Walimu wanne. Hakuna shule ambayo ina zaidi ya hapo labda zile ambazo ni za watoto wa mahitaji maalum.

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika Wilaya ya Mwanga hatuhitaji Walimu wapya. Tunachoomba Serikali itupe ni Walimu ambao watachukua nafasi za Walimu waliostaafu, wale ambao wamefariki au wale ambao wamehamishwa na Serikali kwenda maeneo mengine kufanya kazi. Kwa hivyo, sioni sababu ya kuchukua mwaka na nusu kulishughulikia jambo hili. Watoto wanateketea, wanapotea, hawana Mwalimu wa kuwafundisha, Walimu wawili wakiingia kwenye madarasa saba, watoto wa madarasa matano wanabadilisha shule inakuwa soko. Kwa hivyo, tunawaomba sana, hatuombi Walimu wapya, mishahara yao ipo kwa sababu wale waliokuwepo walikuwa na mishahara na hakuna sababu yoyote ya kutotupa Ealimu kwa sababu Ealimu wako barabarani hawana kazi. Kwahiyo nawaomba tena…

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

MWENYEKITI: Ahsante sana Profesa kwa mchango wako mzuri.

MHE. PROF. JUMANNE A. MAGHEMBE: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante na naunga mkono hoja. (Makofi)