Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) na Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020

Hon. Mussa Bakari Mbarouk

Sex

Male

Party

CUF

Constituent

Tanga Mjini

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) na Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020

MHE. MUSSA B. MBAROUK: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Kwanza nianze kwa kumshukuru Mwenyezi Mungu ambaye ametuwezesha kuwa na afya njema na kuweza kukutana katika kikao chetu hiki cha Bunge na kuzungumzia mambo mbalimbali ya nchi yetu. Pia nishukuru wapiga kura wangu wa Jimbo la Tanga bila kukusahau wewe kwa kunipa nafasi hii. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nitaanza kuchangia TAMISEMI, labda nami niwe miongoni mwa wale ambao tunashukuru kwa ule mpango wa kujenga vituo vya afya 300. Kwenye Jimbo langu la Tanga tumepata vituo vya Makorola, Mikanjuni na Ngamiani. Tumepata takribani shilingi bilioni moja na milioni mia nne. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile pia nisisahau kwamba tulikuwa mgogoro wa Hospali ya Wilaya ijengwe sehemu gani. Baada ya kuwasiliana na Mheshimiwa Waziri hapo mambo yamewekwa sawa na sasa ujenzi unaendelea. Nishukuru kwa hilo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nije sasa kwenye suala la elimu hususani elimu bure. Elimu bure mimi niseme imepigiwa debe sana lakini wananchi na wazazi bado hawajaielewa vizuri na hata badhi ya Wabunge nafikiri hawajaielewa vizuri kwa saabu unaposema kitu bure ni ile free no charge sasa wazazi kufuatia suala hilo wamekuwa wazito kuchangia masuala ya umeme na maji, fedha ya mlinzi na hata akuchangia vifaa. Unapowahoji wanakwambia kwamba tumeambiwa elimu bure na ndiyo maana watoto wameongezeka sana katika shule zetu za msingi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, niitake Serikali sasa, kwa sababu watoto tumekuwa kama tunawaadhibu katika baadhi ya shule maji yamekatwa kwa sababu kufuatia kauli ya Mheshimiwa Rais ile anayosema maneno ni mawili ‘Kata’ kwamba panapodaiwa maji na umeme kata. TANESCO na Mamlaka za Maji sasa hivi hazitoi huduma zinafanya biashara matokeo yake umeme na maji katika shule yamekatwa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, matokeo yake tunawaadhibu watoto. Wanafunzi hawa masikini ya Mungu, malaika wa Mungu hawana hata maji ya kunywa shuleni wanalazimika ama kubeba chupa za maji katika mabegi yao wanayoweka madaftari au kama wako shule basi pana nyumba ya jirani karibu waende wakaombe maji ya kunywa katika nyumba za jirani. Naiona hii ni hatari kwa sababu katika baadhi ya nyumba kuna watu wengine siyo wema, mathalani watoto wa kike tunaweza kuwahatarisha maisha yao kwa kubakwa na kupata maradhi ya UKIMWI.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa nini Serikali isiongeze fedha katika ule mpango wa kupeleka capitation na fedha za matumizi katika shule tukaweza kulipia maji na umeme kwenye shule zetu? Au kwa nini Serikali isisamahe kwenye shule za msingi na sekondari lakini nifike mbali zaidi hata kwenye Misikiti na Makanisa kule ambako Mwenyezi Mungu tunamwomba nchi iendelee kuwa amani tuweke huduma ya maji na umeme iwe bure? Kwa hiyo, naishauri Serikali lifanyiwe kazi suala hilo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine kwa nini pia tusiwape umeme wanafunzi wakaweza kutuumia katika kujifunza kwa sababu kuna mambo mengi. Sote tumepitia elimu ya msingi panakuwa na umeme mnajifundisha mambo mengi, sote tumeyaona haya. Kwa hiyo, naiomba Serikali hilo walifanyie kazi na tuliambiwa kwenye bajeti ya mwaka jana kwenye Wizara ya Nishati na Madini kwamba kwenye huu umeme wa REA watahakikisha kuwa shule zote nchini zinawekwa umeme, naliomba suala hilo liharakishwe. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine nalotaka kulizungumzia ni suala la dawa. Tumeona dawa zilitengewa takribani shilingi bilioni 531 lakini fedha iliyopokelewa ilikuwa ni shilingi milioni 81, pana tofauti ya takribani shilingi bilioni 450. Kama ikiwa tunatenga fedha kubwa halafu fedha tunayopeleka ni kidogo hatuwasaidii wananchi wetu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nafikiri hakuna haja ya kuweka kasma kubwa halafu tunapelekea asilimia ndogo ya fedha. Kama tumepanga shilingi milioni 5312 basi angalau kungepelekwa shilingi milioni 400 hapo ingekuwa tumewasaidia lakini katika shilingi bilioni 531 kupeleka shilingi milioni 81 tu tunawakwaza ama madaktari na watumishi wetu wa Idara ya Afya. Kwa hiyo, naiomba Serikali pale inapopanga bajeti ihakikishe fedha inapatikana na inapelekwa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile kwenye Mfuko wa Maji, Tanga tunayo miradi ya maji ya ile vijiji 10 kila Halmashauri lakini kwa masikitiko makubwa niseme upande wa Kusini tulifanikiwa, maji yanatoka kuelekea upande wa Marungu, Kirare, Tongoni na wananchi sasa hivi wanaomba huduma ya maji ipelekwe mpaka kwenye nyumba zao.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hata hivyo, katika mradi wa Kaskazini wa Mabokweni, Kibafuta, Mpirani na Chongoleani mpaka leo kuna kizungumkuti, maji hayatoki na wananchi wana shida ya maji na mimi mwenyewe nimefika nikashuhudia. Nitamwomba tu Mheshimiwa Waziri wa Maji au Naibu wake mara baada ya Bunge hili tutembelee ili tujue kikwazo kwa nini maji hayatoki. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile katika mradi huohuo wa maji, Kamati PAC ambayo nipo tumetembelea mradi wa maji ule wa Chalinze na maeneo mengine naona kuna hitilafu kidogo kwa sababu fedha zilizoahidiwa katika mkopo ilikuwa ni takribani shilingi bilioni 158 mpaka sasa hivi zimetumika shilingi bilioni 93 lakini kuna shilingi bilioni 65 bado hazijatumika. Hata hivyo, kuna masharti ambayo katika miradi ile vifaa vyote hadi bolt lazima itoke kwa yule mtu ambaye mmeingia naye mkataba kwamba awakopeshe.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa mfano, ule mradi unafadhiliwa na India sasa basi hata mipira, bolt, nati za kwenye mradi lazima zitoke India! Tunasema tunalinda viwanda vya ndani, tunalindaje viwanda vya ndani kwa miaktaba mibovu kiasi hiki? Ina maana watumishi sasa baadhi ya ma-expert ambao wapo hata Watanzania wanashindwa kulipwa sawasawa na wale ma-expert wa Kihindi, naona hiyo ni dosari. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa nizungumzie utawala bora. Ukitazama Katiba, Ibara ya 146(1)(2)(c) kinaeleza hapa kwamba, madhumuni ya kuwepo Serikali za Mitaa ni kupeleka madaraka kwa wananchi na vyombo vya Serikali za Mitaa vitakuwa na haki na mamlaka ya kushiriki na kuwashirikisha wananchi katika mipango na shughuli za utekelezaji wa maendeleo katika sehemu zao na nchini kote kwa ujumla. Ukienda kwenye kipengele (c) inasema…

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

MWENYEKITI: Ahsante sana Mheshimiwa Mbarouk.

MHE. MUSSA B. MBAROUK: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. (Makofi)