Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Male
Party
NCCR-Mageuzi
Constituent
Vunjo
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
0
Ministries
nil
MHE. JAMES F. MBATIA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru sana kwa kunipatia nafasi na mimi nitoe mawazo yangu kwenye hoja iliyoko mbele yetu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza kabisa leo ni Sokoine Day, alikuwa kiongozi mashuhuri kwa Taifa letu, ni siku ya kumkumbuka miaka 35. Mwenyezi Mungu amrehemu na tutekeleze yale mema aliyofanya kwa Taifa la Tanzania. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa haraharaka nianze na TARURA. Nimpongeze Mtendaji Mkuu wa TARURA kwa kazi nzuri kubwa anyoifanya kwa Taifa letu na TARURA Halmashauri ya Wilaya ya Moshi wanafanya kazi nzuri. Nachowakumbusha tu ni ahadi za Mheshimiwa Rais kwa barabara za Himo Mjini pamoja na barabara ya Kilema.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Jimbo la Vunjo lina barabara zenye kilometa 389.3, TARURA walifanya kazi hii ya kupima, nawapongeza sana, wakishirikiana na Vunjo Development Foundation (VDF) na barabara hizi zitagharimu shilingi bilioni 12.7, wananchi wameanza kuchanga wenyewe, Mbunge nimenunua mashine, Serikali imeahidi kutoa shilingi milioni 200 kwenye mradi huu kwenye barabara walizoweka kwenye kitabu, naipongeza Serikali. Hata hivyo, shilingi milioni 200 kati ya shilingi bilioni 12.7, naomba waongeze fedha hizi. Waliotengewa shilingi milioni 200 ni barabara ya Chekereni - Kahe ambayo tunashukuru lakini ni kidogo. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, lingine ni elimu msingi, nimeuliza swali asubuhi, naomba tu kujua na tulitendee Taifa haki, hapa tuna Sera ya Elimu na inafafanua vizuri maudhui ya Sera ya Elimu na elimu msingi ni ipi na elimu sekondari ni ipi. Je, Taifa hili leo hii linaongozwa na Sera ipi ya Elimu kuandaa Taifa kwa miaka 30, 40 au 50 ijayo? Nitazungumzia zaidi wakati wa bajeti ya elimu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, niongele kuhusu ikama ya watumishi. Halmashauri ya Wilaya ya Moshi kuna upungufu wa walimu 379, shule zingine zina walimu wawili, watatu na sekta ya afya pia ina matatizo makubwa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hapa tuko na wenzetu wenye albinism, niwapongeze kwa kazi nzuri wanayoifanya na mwaka huu ni wa kudumisha, kutetea na kulinda utu, heshima na mahitaji msingi ya watu wenye ulemavu. Nikiangalia bajeti iliyoletwa hapa bado walemavu wetu hatujaweza kuwaweka kwenye hali ya utu wao, heshima yao na mahitaji msingi yao ili na wao wajione ni binadamu. Sisi ambao tunajiona tuna akili nzuri na tumekamilika tunawaita walemavu lakini kwa kiasi kikubwa ukiangalia sisi tunaowaita walemavu ulemavu wetu wa fikra ni mkubwa kuliko ulemavu wao wa viungo vya nje. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nimponge sana Dkt. Reginald Mengi na Taasisi yake ya kutetea na kukuza utu wa walemavu. Dkt. Mengi anafanya kazi nzuri sana na niiombe Serikali imuunge mkono. Tulikuwa na Mheshimiwa Makamu wa Rais tarehe 17 mwezi uliopita na Naibu Waziri, dada yangu Mheshimiwa Stella Ikupa katika shughuli ya kuwajengea utu walemavu, kwa hiyo wapewe nafasi hiyo. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nilikuwa kwenye mkutano wa Dkt. Martin Fatael Shao, Askofu Mstaafu naye amefanya utafiti kwenye sekta ya afya na watoto na imeonekana shule zetu haziko vizuri. Kwa kuwa nina ripoti yake hapa, nampongeza Askofu huyu kwa kazi nzuri anayofanya kwa walemavu, shule za msingi, elimu ya afya na kitabu hiki nitakiweka Mezani. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa haraka haraka niingie kwenye utawala bora. Ndugu Isaac Newton anasema katika kila kanimkabala kuna kani iliyo mrejeo sawa na kinyume. Viongozi wowote wale hawaokotwi kwenye majalala viongozi huandaliwa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mwaka 1995 wewe ulikuwepo Bungeni, alikuwepo Mheshimiwa Mzee Lubeleje, Mheshimiwa Ndassa na Mheshimiwa James Mbatia kati ya Wabunge wote waliopo sasa, tulikuwa wanne. Wakati huo tulivyokuwa Bungeni ukiwa Mwanasheria Mkuu viongozi waliandaliwa kwa kupewa semina na kuelezwa jukumu la kwanza la Mbunge ni kwa Taifa lake; la pili kwa Jimbo lake la Uchaguzi; la tatu kwa chama chake cha siasa; na la nne kwa dhamira yake binafsi. Sasa hapa Bungeni leo hii watu wanachukulia mambo personal kana kwamba issues ni personal, sisi tunapita tu, tuijenge nchi yetu, wanasema great minds discuss ideas, Taifa hili ni letu sote. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nilibahatika kuongea na Mheshimiwa Rais kwa mapana sana tu tukakubaliana Taifa hili likiharibika au likienda mrama tunaangamia sisi sote, halichagui huyu ni wa chama gani, kwa hivyo, tuitazame nchi yetu. Let us think positive and big, let us think big yaani tufikiri kwa mapana tu, nchi yetu miaka 50 itakuwa kwenye hali gani. Kapteni Mstaafu Mheshimiwa Mkuchika unakumbuka mwaka 1992, 1995 ukiwa DC wa Ilala wakati tunaanzisha mfumo wa vyama vingi tulikuwa tunakuja ofisini kwako, tulikuwa tunaongea tuwe na Taifa gani baada ya miaka 25, miaka 30 ijayo. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa nini nimesema hayo? Nimesema hayo kwa sababu nimeisoma hotuba ya Mheshimiwa Kapteni Mheshimiwa Mkuchika, ukiangalia Taasisi ya Kupambana na Rushwa kazi walizonazo hapa ni zaidi ya 10 au 15 kama sijakosea lakini ukiangalia bajeti yao ni ndogo kweli kuweza kuzama mpaka chini. Kauli mbiu ya taasisi hii nilikuwa nao wiki iliyopita kwenye semina na dada yangu Mheshimiwa Dkt. Mary Mwanjelwa, Naibu Waziri pale TAKUKURU, tulitoa rai, huwezi ukasema unazuia, unapambana halafu ndiyo unaelimisha, hapana. Nilitoa rai siku ile kwamba tuanze na kuelimisha kwanza madhara ya rushwa. Tukishaelimisha ndiyo tutaenda sasa na hayo mengine ya kuzuia na kupambana, tuelimishe. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, tusiseme hapa kwamba kesi ziko 476 na nyingine zinaongezeka tujenge mazingira kesi zipungue zaidi kwa sababu ya watu kujua madhara na kujielimisha zaidi badala ya kufikiri kwamba zitaongezeka.tuwekeze kwenye kuondoa maovu zaidi kwenye jamii badala ya kufikiria maovu yataongezeka kwenye jamii. Hii ni namna ya jamii kujitambua na kwa moyo wa dhati kabisa nimpongeze CP Diwani Athumani na timu yake kwa kazi nzuri wanayoifanya ya kuweza kupambana na rushwa katika Taifa letu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika hali hii ukiangalia kwenye uongozi baada ya rushwa, unaona wamepewa majukumu nane ambako tungewekeza zaidi kwenye taasisi ukurasa ule wa 80, tulishakubaliana tangu mwaka 2002 na Komredi Mangula, Katibu Mkuu wa CCM, wakati huo tuko kwenye TDC, nimpongeze sana Nsanzugwanko waanzilishi wa TDC (Tanzania center for Democracy) tulikubaliana Taifa liandae viongozi. Ukiangalia ma-RC, ma-DAS na ma-DED wetu wanaibukaje, vetting yao ikoje katika utumishi wa umma wa Tanzania ili waweze kuwa ni endelevu katika kutekeleza majukumu yao? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, tukienda kwa ma-DC na Ma-RC wetu, tumpongeze Kapteni Mheshimiwa Mkuchika uliwahi kuzungumza hapa, wanaandaliwaje, wanapikwaje ili waweze kutekeleza majukumu ipasavyo? Kwa hiyo, wasiibuke tu kila mtu na mambo yake, huyu anasema hili, yule anasema lile, kwa kweli tukiangalia kama wataendelea kufanya wanavyofanya tutakuwa hatulitendei Taifa letu haki. Mheshimiwa Mwenyekiti,
Mheshimiwa Mwenyekiti, rasilimali kubwa kuliko zote duniani leo hii ni rasilimali watu (umoja) na utawala bora is a collective approach inaanzia kwangu, kwako, kwa jamii nzima, kwa familia baadaye kwa Taifa. Mwalimu alikuwa anajua kwamba Taifa analipeleka wapi ndiyo wanafunzi tukawa tunaimbishwa kama kasuku ahadi za mwana-TANU, unaambiwa binadamu wote ni ndugu zangu, unajua kuwa huyu ni ndugu yangu; unambiwa rushwa ni adui wa haki, sitapokea wala sitatoa rushwa, tulikuwa tunapata Taifa ambalo linaendelea, ni shirikishi, la wote kwa kuwa nchi hii ni yetu sote. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kujitambua ni jambo muhimu sana na inatupasa sisi sote kwa pamoja kujua utawala bora ni wa pande mbili; anayeongoza na anayeongozwa, is a collective approach. Huwezi ukauchukulia utawala bora kwa yule tu anayeongoza. Ukikubali mawazo mbadala ukawa na utulivu; nimeona hata hapa Bungeni, unakuta Mbunge anaongea, mwingine amemwingilia, mwingine amefanya hivi. Hata Maandiko Matakatifu yanasema kujibu kabla ya kusikiliza ni upumbavu na aibu kwako ambaye hujataka kusikiliza. (Makofi)
Tusikilizane, tuvumiliane, tuwe na lugha ya staha. Taifa hili ni letu sote. Tukiwa na mawazo mapana namna hiyo, ninaamini hapa tulipo leo hii tutatoka na Tanzania ya leo, nani mwenye kujua kesho?
Mheshimiwa Mwenyekiti, tunahitaji Taifa endelevu kwa maslahi mapana ya mama Tanzania. (Makofi)
(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)