Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Female
Party
CUF
Constituent
Special Seats
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
0
Ministries
nil
MHE. KIZA H. MAYEYE: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa nafasi ili niweze kuchangia katika hotuba hii ya TAMISEMI na Utawala Bora.
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini nimshukuru Mwenyezi Mungu ambaye amenipa afya nimeweza kusimama jioni hii ya leo. Kwa kipekee kabisa nimpongeze Fulbright Prof. Ibrahim Haruna Lipumba kwa kuwa Mwenyekiti wa Chama cha Wananchi CUF. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nimepitia hotuba hizi za Wizara hizi mbili, natambua Serikali inapambana kuhakikisha inaleta huduma bora kwa wananchi. Kwanza nianze na suala la TARURA. Barabara za vijijini ni muhimu sana katika maeneo yetu. Wote tunafahamu kwamba wakulima wote wako vijijini lakini barabara hizi ndizo ambazo zinaweza kuwasaidia kutoa mazao mashambani na kuleta mijini kutafuta masoko lakini hali ya barabara hizi kiukweli ni changamoto kubwa. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na kazi kubwa ambayo TARURA wanaifanya, moja ya changamoto ambayo inawakabili ni suala zima la bajeti. Niiombe Serikali katika bajeti hii tunayokwenda nayo tuweze kuwasaidia TARURA wapate bajeti ya kutosha ili waweze kufanya kazi yao na kumaliza miradi hii ya barabara zetu huko vijijini. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika suala la bajeti tumeona TARURA wanapata asilimia 30 na TANROADS wanapata asilimia 70. Naelewa Serikali mmeunda Kamati Maalum kwa ajili ya suala hili na mimi nichangie na kuiomba Serikali kwamba at least sasa TARURA wabaki na 40 na TANROADS wapewe 60 kwa sababu ya barabara za viwango vya lami na madaraja kama ya Mfugale. Kwa hiyo, tuwasaidie watu wa TARURA, naamini wanafanya kazi na kama watapata bajeti ambayo inatosha wataweza kutusaidia barabara zetu hizi kumalizika kwa wakati. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, hapo hapo kwenye TARURA changamoto nyingine ni vitendeakazi, watu hawa hawana magari ya kuweza kutoka sehemu moja na kwenda site. Mfano Mkoa wangu wa Kigoma takribani wilaya zote, kuanzia Kigoma DC, Buhigwe, Kasulu, watu wa TARURA hawana magari na imekuwa ni usumbufu mkubwa katika utendaji wao wa kazi. Nikuombe sana Mheshimiwa Waziri muangalie ni jinsi gani Kigoma wilaya zote tunaweza tukapata magari kwa watu hawa wa TARURA ili wafanye kazi kwa ufanisi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nijielekeze katika suala la afya. Natambua Serikali mnajituma na mnafanya kazi kuhakikisha mnaboresha vituo vya afya na kutuletea wauguzi. Niwashukuru kwamba Kigoma mwaka jana tuliomba, mmetuletea Kigoma nzima watumishi 402 lakini kiukweli bado changamoto ni kubwa. Maeneo mengi ukienda hospitali za Kigoma na hata maeneo mengine ya Tanzania bado hatuna wauguzi wa kutosha. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, mpaka kufikia Novemba, 2018 Kigoma tulikuwa na wafanyakazi 2,004, kiukweli bado idadi ya wafanyakazi ni ndogo ukizingatia Kigoma tuko zaidi ya watu milioni mbili lakini ni mkoa ambao tuko mpakani tunahudumia mpaka wakimbizi kutoka Kongo na Burundi. Kwa hiyo, niiombe sana Serikali, pamoja na jitihada ambazo mnafanya lakini mtuangalie kwa jicho la pili mtuongezee wauguzi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, hapo hapo katika afya, Kigoma tuna Hospitali hii ya Mkoa ambayo inaitwa Maweni. Mpaka sasa hatuna vifaa kama CT Scan na x-ray machines za kutosha hali inayosababisha usumbufu mkubwa sana kwa wananchi watu wanakwenda kutibiwa pale wanahitaji huduma hii ya CT Scan wanapewa rufaa kwenda Mwanza (Bugando) au kwenda Muhimbili. Kulingana na hali ya maisha ilivyo, siyo watu wote wataweza kwenda Muhimbili au Bugando kwa wakati. Sasa kama tunataka kuwasaidia wananchi ili tupunguze vifo, niombe sana Serikali muweze kutusaidia vifaa hivi vya CT Scan. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, bado niko katika hospitali ya mkoa; hospitali hii kama nilivyosema inahudumia watu wengi sana lakini mpaka sasa hatuna ma-specialist wa kutosha, tuna specialist mmoja wa akina mama na mmoja wa watoto. Kuna magonjwa mengine kama haya ya kisukari hatuna ma-specialist. Niombe sana Serikali mtusaidie hospitali hii tuweze kupata ma-specialist wa kutosha, mtakuwa mmetusaidia watu wa Kigoma na maeneo mengine Tanzania ambayo hakuna ma-specialist katika hospitali zao muweze kuwasaidia. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nigusie tena suala la miundombinu hospitalini na kwenye shule zetu. Sote tunajua kwamba walimu, madaktari na wauguzi ni watu muhimu sana katika maisha yetu, lakini watu hawa wamekuwa wakiishi maisha magumu kwa maana ya kwamba hata nyumba bora za kukaa hawana. Niombe sana Wizara muweze kuangalia suala hilo, muwajengee nyumba wauguzi na walimu ili nao waweze kukaa katika mazingira bora. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna suala hili la moboma, kuna majengo ambayo wananchi wamejitoa, niseme tu kwamba wananchi wanaunga mkono Serikali kwa kufanya vitu mbalimbali kama ujenzi wa zahanati, kujenga shule na hostels za wanafunzi lakini inafika muda na wao wanakwama. Niombe sana Serikali muwasaidie wananchi muweze kumalizia majengo haya ambayo yameishia kwenye lenta.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mfano tu katika Mkoa wangu wa Kigoma, Awamu ya Nne Rais aliyepita aliahidi kujenga hospitali katika eneo la Nyarubanda na Mahembe na wananchi waliitikia wakaanza kujenga lakini sasa imesimama na hakuna mwendelezo wowote. Niombe sana Serikali muwasaidie watu hawa waweze kumalizia majengo haya. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, niende kwenye suala la vitambulisho. Niseme tu kwamba mimi ni mdau wa maendeleo na naunga mkono jitihada za Serikali katika ukusanyaji wa kodi lakini tuwe wakweli; pamoja na kwamba Mheshimiwa Rais alisema hawa wajasiriamali wadogo wakate vitambulisho lakini tuwaangalie hawa wajasiriamali wadogo ni wa aina gani. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, leo katika Mkoa wangu wa Kigoma, mimi natokea Kijiji cha Mwandiga, baada ya Bunge kuisha kuna akina mama nilikwenda kuwatembelea sokoni. Kuna mama ambaye anauza ndizi kwa sababu tu nyumbani kwake amepanda ndizi, anaona ndizi zimeiva anasema nipeleke sokoni nikapange chini ili wanangu waweze kupata daftari na kupata mafuta ya taa. Sasa hawa ambao wanakwenda kutoa vitambulisho hivi unakwenda kumtoza mama kama huyu Sh.20,000 anaitoa wapi wakati biashara anayofanya haikutani mzunguko wake kupata Sh.20,000? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, kiukweli malalamiko ni mengi. Kama tunasema ni Serikali ya wanyonge, wanyonge ndiyo hawa akina mama na vijana…
(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)
MHE. KIZA H. MAYEYE: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. (Makofi)