Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) na Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020

Hon. Desderius John Mipata

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Nkasi Kusini

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) na Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020

MHE. DESDERIUS J. MIPATA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana kwa kunipa nafasi. Pia nichukue nafasi hii kumshukuru Mwenyezi Mungu kutujaalia uzima. Vilevile nimpongeze sana Mheshimiwa Rais kwa kazi nzuri anazozifanya na kujitoa kwa moyo kutumikia Watanzania. Kazi anayoifanya tunaiona, tuko nyuma yake na kila mwenye macho anaona. Kwa hiyo tunamuunga mkono, hayuko peke yake.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nawapongeza pia Mawaziri wote wawili mzee wangu Mheshimiwa Mkuchika na Mheshimiwa Jafo, pamoja na Manaibu Waziri Mheshimiwa Kandege, Mheshimiwa Waitara na Mheshimiwa Mwanjelwa Machuche. Wamekuwa wakitusaidia sana na siku zote wanatusikiliza na mara tunapofikishia hoja zetu wanatusaidia vizuri kabisa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nianze na miradi ya afya. Kazi nzuri sana imefanywa na Wizara hii ya TAMISEMI hasa katika eneo hili la afya, sisi kwetu tumefanikiwa kupata vituo vya afya vitatu na sasa wanatuongezea kimoja lakini pia tumepata Hospitali ya Wilaya tumepata hela za kutosha bilioni moja na milioni mia tano mwaka jana na mwaka huu wametuongezea milioni mia tano, jambo hili ni zuri sana. Kwangu mimi nimeweza kupata pia kituo cha afya cha Wampembe ambacho Mheshimiwa Jafo aliweza kutembelea alipotushauri, tunamshukuru sana sana, kazi pale imefanyika vizuri na ushauri aliotupa tunaendelea nao vizuri.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hata hivyo, niseme changamoto moja, vituo hivi vinapokamilika kuna jambo bado linabaki kuwa ni tatizo kwa akinamama wetu hata wale wa vijiji vya jirani. Ningeshauri wazo hili liendelee kwenye vituo vyote vinavyokamilika, tuwe tunaweza kujenga jengo la kuwafanya akinamama wajisubirie pale, maternity waiting home, itatusaidia kufanya wale ambao wako mbali kidogo wasogee na waweze kujisaidia vizuri zaidi na kupata huduma inayotakiwa. Vinginevyo habari ya kujifungulia nyumbani itaendelea hata kama vituo vipo kwa sababu gharama zile wanashindwa kujimudu kwenda kukaa pale na kukaa kwa ndugu ni ngumu kidogo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunajenga vituo vya afya vingine Ninde, tunajenga kituo cha afya na wananchi wamejenga majengo mazuri, vyumba kumi wamekamilisha lakini King’ombe tunajenga kituo cha afya, Kate pia wanajenga kituo cha afya, Kasu wanajenga kituo cha afya, tunaomba wanapopata nguvu tena waweze kutusaidia kwenye maeneo hayo. Hata hivyo, Kata ya Kala iko mbali sana na akipatikana mgonjwa kule anapata shida kufika kwenye kituo cha afya hasa akinamama na watoto, naomba tupate gari ya wagonjwa ili isaidie katika kuhudumia katika eneo hilo. Tumejenga zahanati nyingi zipatazo 10, zote zimefikia mtambaa panya, hatujapata uwezo wa kuweza kuezeka, lakini tunahamasisha wananchi ili tujenge. Naomba mtusaidie ziko zahanati ya Kisambala, Kantawa, Kipande, Kalundi, Nkomachindo, Ifundwa, Tundu, Kilambo, Ntuchi na Nchenje zimeezekwa, ni pesa kidogo tu zinatakiwa ili kuzikamilisha wananchi waanze kupata huduma. Naomba Serikali itusaidie na kama haiwezi kutusaidia itusaidie hata kuibana Halmashauri zaidi ili watusaidie katika zahanati hizi ambazo karibu zinakamilika.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba vilevile nizungumzie kuhusu Bima ya Afya. Bima ya Afya nzuri na inasaidia sana wananchi na mara nyingi watumishi wa taasisi mbalimbali na wa Serikali ndio wanaosaidiwa zaidi. Mpango wa kuwezesha wananchi wote kwa ujumla Watanzania wapate huduma ya Bima ya Afya umefikia wapi? Naomba nihimize Serikali ione umuhimu wa kufanya hivyo. Sambamba na hilo niwaombe, nichukue nafasi hii kuwashukuru sana watumishi wa Bima ya Afya hasa waliojipanga kuhudumia Wabunge yupo Flora Mtabwa na Felister Mabula, hawa watu wakipata dharura wanachukua kwa haraka sana na wanatusaidia na wanajipanga vizuri. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile niseme kuhusu hospitali ya Muhimbili, Muhimbili sasa hivi huduma zimejipanga vizuri, watu wanafanya kazi kama mchwa, ukipata dharura ndio unaweza ukajua kumbe sasa tuna hospitali ya Taifa yenye kiwango na inahudumia vizuri sana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunaomba Waganga hatuna, tunaomba Wauguzi kwetu kule Nkasi hatuna hasa pembezoni. Mheshimiwa Kandege na Mheshimiwa Jafo watusikilize na Mheshimiwa Waziri anapajua, bahati nzuri umeshafika.

Mheshimiwa Mwenyekiti, suala la pili ni kuhusu TARURA. TARURA kama wenzangu wanavyosema naunga mkono tuwape asilimia 50 kwa 50, lakini sisi leo hii kutokana na TARURA hatuwezi kufikika kwenye vijiji kadhaa, Kijiji cha Kisula siweze kufika kwa sababu barabara imekatika na mvua na hakuna fedha za dharura. Kwa hiyo TARURA haina hata uwezo wa kukabili dharura yoyote inayotokea mpaka waombe. Sasa jambo hili sio zuri sana, kwa hiyo naomba sana Serikali itusaidie kuhakikisha kwamba TARURA wanapata pesa za kutosha.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna daraja la Ninde, Kata nzima haiwezi kufikika kwa sababu ina barabara moja, daraja limevunjika hakuna pesa na tumeshatuma maombi, lakini bado hatujapata pesa, sababu hawana pesa, kwa hiyo tunaomba. TARURA pia hawana watumishi, watumishi wake wako kwa mkataba, naomba waajiriwe, kama ni kujaribiwa wamejaribiwa muda wa kutosha ili watu waweze kujiamini. Sasa hivi wanafanya kazi kwa mikataba ya miezi mitano mitano au sita sita haiwezekani! Wapeni uwezo full mandate waweze kufanya kazi vizuri itasaidia. Vilevile hawana magari ya supervision hasa kule wilayani, lakini vilevile hata huku hawana pesa za kutosha, naomba watusaidie.

Mheshimiwa Mwenyekiti, niendee katika eneo la maji. Kuna miradi ya maji ambayo inatekelezwa ya vijiji kumi hivi vya Benki ya Dunia. Miradi mingi imefanya kazi bila utafiti wa kutosha, usanifu wake haukuwa mzuri, Kijiji cha Nkundi kina mradi umegharimu zaidi ya bilioni mbili, lakini maji hayatoki. Naomba Serikali ione utaratibu wa kuwezesha vijiji kama hivi viweze kupata wataalam wa kutosha au kuona vikwazo gani vinafanya maji yasitoke katika gharama yote hii.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Kijiji cha Kisula vilevile maji bado ingawaje wao wanaendelea na mradi. Miradi wa Mpasa, mradi wa Isale una zaidi ya bilioni tano katika Jimbo langu, lakini unaendelea vizuri, tumeshafanya kazi za kutosha, mkandarasi anaendelea vizuri, ila certificate tuliyoomba bado haijarudi ili kazi iweze kuendelea vizuri zaidi. Kwa hiyo, naomba Serikali itupe hela ambayo tulishaomba ili Mkandarasi aendelee na kazi vizuri. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, suala la umeme, kuna vijiji vilirukwa katika awamu ya kwanza na ya pili, nikienda kule naonekana kama kichekesho; Kijiji cha Katani, Kijiji cha Malongwe, Kijiji cha Nkana, Kijiji cha Sintali, Kijiji cha Nkomachindo, ni vijiji ambavyo vinanitesa, nashindwa hata namna gani niweze kwenda. Naomba nitumie hadhara hii Mheshimiwa Waziri wa Nishati anisikie, vijiji hivi ni kero, nikienda jimboni, sina raha hasa kwa sababu wamezungukwa na vijiji vyote vyenye umeme. Ingawaje bado kuna vijiji vingi kabisa ambavyo havina umeme, lakini hivi ndio zaidi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la mwisho kama nitapata muda ni kilimo, kilimo kikiboresha ndio halmashauri zinaweza kupata mapato ya kutosha. Kwa sasa hivi natoa ushauri kwamba ruzuku iliyokuwa imewekwa kwenye kilimo, irudi kwa sababu ilikuwa inabeba watu wa chini zaidi. Ruzuku iliyoko sasa hivi inawabeba wakubwa wakubwa tu, wenye uwezo wa kwenda kununua pembejeo madukani, lakini wale wenzangu na mimi inakuwa ni ngumu sana kupatikana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia masoko ya mazao ya wakulima, Mkoa wa Rukwa bila kuwa na masoko ya kutosha, wataalam mko wapi? Tutafutieni masoko ya wakulima kwa sababu tunawahimiza wakulima walime, wanatupa sayansi za kuvuna vizuri zaid, sasa tukishavuna tunaweka vyakula vinaharibika na vinauzwa kwa bei ya chini, watu wanakufa moyo. Kwa hiyo naomba sana…

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

MWENYEKITI: Ahsante sana Mheshimiwa.

MHE. DESDERIUS J. MIPATA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana na naunga mkono hoja. Natambua sana kwamba Serikali ya Mitaa zinafanya kazi vizuri. (Makofi)